SoC02 Kwa tabia hizi, Ewe Kondakta wa daladala badilika

Stories of Change - 2022 Competition

sue bae

Member
Aug 16, 2022
21
13
Habari za wakati huu wana jamii forum.

Ni siku nyingine tena ya kuelimishana ili kila mmoja wetu aweze kuwajibika kwa nafasi aliyokuwa nayo katika jamii. Leo ningependa kuongea na baadhi ya kondakta wa daladala ambao kiukweli wanapaswa kujirekebisha kwenye baadhi ya maeneo.

Kila kazi ina changamoto zake na ambapo muhusika(mwenye changamoto) anaweza kuzijua ama kutozijua na ndio maana tuko hapa kukumbushana na kuelimishana lengo likiwa ni kupata jamii bora kwa kila mmoja kuwa muwajibikaji kwenye eneo lake la kazi.

F72E2675-1E93-4F4B-BAEC-C94C5ECDB137.jpeg

Picha na magda.glod

Changamoto kubwa iliyonifanya mpaka kuandaa andiko hili kama abiria katika daladala ni hali unayomkuta nayo kondakta baada ya kupanda daladala.

Kuna siku nilipanda daladala kutoka Makumbusho kuelekea Goba na kumkuta kondakta amevaa sare ambayo imechanika balaa. Siwezi kusahau suruali yake ilivyokuwa imechanika na kusababisha vazi la ndani kuonekana muda wote. Mbaya zaidi hata hakuonesha kujali muhimu yake alikuwa makini tu kukusanya nauli za abiria.

Dereva, unashindwa kumshauri kondakta kushona sare yake? kondakta ni kweli umekosa muda wa kushona sare yako na kuamua kuonyesha nguo za ndani?

Uwajibikaji unapaswa kuwepo, kwani kwa mtu mwenye akili timamu hawezi kuvaa nguo zilizochanika kiasi kuonesha nguo za ndani ni uzembe uliopitiliza na kupitia hili mnaifanya kazi ya ukondakta kuonekana haina maana mbele za watu.

Kuna nguo kutoboka ama kuchanika kidogo ni sawa lakini si kwa hali kama niliyomkuta nayo yule Kondakta maana suruali ilichanika kuanzia pajani mpaka mguuni.

Wito wangu kwa kondakta yeyote ni kuhakikisha kuwa nguo za ndani hazionekani kwani kwa kufanya hivyo hujiongezea heshima na uthamani wa kazi aifanyayo. Badilika.

Tabia nyingine isiyofaa, utamkuta kondakta ameshikilia suruali ili isimuanguke, akianza kudai nauli anasimama na kutanua miguu yake huku na huko ili mradi suruali isimuache mwilini.

Hivi ni jinamizi gani limewakumba? kwani kuwa kondakta ndio kutojijali kiasi hiki? kwanini usipunguze kiuno hiyo suruali ili ukiivaa ikukae vizuri kuliko muda wote kuishikilia?

Wengine mpaka huanguka pale gari inapofunga breki maana hukosa usawa. Mkono kutwa umeshikilia suruali, akidaiwa chenji ndio kuweka V na kutafuta chenji huku akilinda suruali yake kutodondoka.

Siamini kama ni muda mnakosa kutengeneza vizuri sare zenu bali ni uzembe tu. Badilika.

Tabia nyingine ni uvaaji wa ndala, ni hakika yangu kuwa kila kazi ina misingi yake na kama haina basi kwa akili tu inatosha kupambanua jema na baya.

Kama abiria, hainiathiri vyovyote kwa kondakta kuvaa ndala lakini kwa usalama wake si vyema kuvaa ndala.

Waweza angukiwa na kitu chochote chenye ncha kali na kukuumiza miguuni. Kila eneo la kazi huwa na mambo ya kuzingatia ili kumlinda mfanyakazi dhidi ya changamoto fulani.

Siamini kama inashindakana kuvaa viatu vya kufunika ukiwa kazini bali ni uzembe tu. Badilika.

Tabia ya kuwaacha wanafunzi jioni. Kuna baadhi ya daladala nazipongeza kwa kuwajali sana wanafunzi kwani kila asubuhi hujitolea kuwapakiza wanafunzi tu na kuwasogeza shuleni , lakini changamoto inakuwa ni jioni, unakuta kondakta anazuia wanafunzi kupanda.

Kiuhalisia ni heri mtoto awahi kufika nyumbani kuliko mzazi kuwahi na mtoto kuchelewa, sisemi watu wazima wasipakizwe jioni, hapana, nasema na wanafunzi nao wapakizwe bila kubaguliwa.

Sio daladala zote hufanya hivi bali zipo chache nilizofanikiwa kupanda na kuona changamoto hii.

Kutowapakiza wanafunzi jioni (watokapo shuleni) kunawaweka wanafunzi kwenye changamoto zifuatazo;

Kuchelewa kufika nyumbani.
Mwanafunzi akichelewa kufika nyumbani, atafua sare zake saa ngapi?, ataziandaa saa ngapi?, atajisomea saa ngapi? maana kwa kuchelewa itampasa alale tu ili kesho awahi kuamka aende shule. Nimepitia maisha haya hivyo nina huzunika nisipoona mabadiliko yoyote hapa japo miaka inazidi kusonga.

Inawaweka wanafunzi kwenye vishawishi.
Mara nyingi nakutana na wanafunzi wakisimama barabarani ili kusimamisha magari binafsi wapewe lifti.

Dunia hii imeharibika sana mpaka binadamu tuna uzana sisi kwa sisi, usalama wao uko wapi? Dunia hii imeharibika watoto wanalawitiwa, usalama wao uko wapi? Wapo watu wazuri huwapa lifti na kuwafikisha salama, lakini je, ni wote walio wazuri?

Lakini pia watu wengi nao wenye magari binafsi huogopa kuwapa lifti wanafunzi kwa kuhofia kufikiriwa vibaya na jamii. Licha ya kusimamishwa, baadhi hayasimami. Sasa hawa wanafunzi, Taifa la kesho linavyo randa randa barabarani na kwenye vituo vya daladala tuna mpango nao gani?

011B454B-B5F4-4E8D-8E03-3818FB7311F5.jpeg

Picha na Katalii _na_masela

Kuwakoromea wanafunzi na kuwakataza kupanda gari hii sio sahihi kabisa kwani inajenga uadui kati yako (kondakta) na mwanafunzi, mwanafunzi kamwe hawezi kumwongelea vizuri kondakta pia ina waharibu kisaikolojia kwamba amekataliwa kupanda kisa tu yeye ni mwanafunzi hivyo kumbe mwanafunzi hana thamani katika jamii?

Sio wote wenye tabia zisizoridhisha ila nawaandikia wale wachache ambao hawataki kuwa sawa kama wengine.

Ukondakta ni kazi ya thamani sana, watu hujenga, hulisha familia, hununua gari na kuajiri watu kupitia kazi hii lakini yote huanzia kwa mtu kuwa na nidhamu binafsi. Kujijali yeye na wale waliopo kwenye gari.

Kuna watu hupata fursa kwa namna tu wajiwekavyo, wengine huongezewa mishahara kwa jinsi wajiwekavyo, unaweza kuwa mmoja kati ya watu hao kwani nina hakika hata bosi wako hatapendezwa kukukuta katika hali isiyofaa.

Wengi hufukuzwa kazi kwa kutojijali ama kutopewa fursa yoyote kama kuongezewa mishahara.

Kumbuka, daima huanzia kwako binafsi kisha kuwafikia wengine, ukijitengeneza vizuri wengine watakufuata na vingine vitaongezeka.

Nawapongeza kondakta wawajibikaji pia waliowazembe ni wakati wa kubadilika sasa.

Asante.
 
Back
Top Bottom