Imetolewa mara ya mwisho: 28.11.2008 0146 EAT
• Uchunguzi faili la Karamagi wakamilika
*Ni kuhusu mkataba tete wa Buzwagi
*DPP Feleshi:Nimeshatoa mapendekezo
*Akina Mramba kupanda Korti Kuu leo
Na Reuben Kagaruki
Majira
IDADI ya vigogo wanaoendelea kuangukiwa na mkono mzito wa dola katika Serikali ya Awamu ya Nne huenda ikaongezeka, kufuatia kuwepo taarifa za kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma za kuliingiza taifa katika hasara kupitia mkataba wa Buzwagi uliosainiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Nazir Karamagi kwa niaba ya Serikali.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), imelithibitishia gazeti hili kukamilika kwa uchunguzi huo katika mkataba huo ambao uliibua mjadala nchini baada ya pamoja na mazingira mengine tete, mkataba huo kusainiwa nje ya nchi, mjini London, Uingereza.
Kauli hiyo ya DPP imekuja huku kukiwa kumetanda wingu zito la tetesi kuwa huenda Bw. Karamagi akafikishwa kortini muda wowote. Awali juzi iliaminika kuwa kigogo huyo angefikishwa kortini.
DPP, Bw. Eliezer Feleshi, akizungumza na Majira Dar es Salaam jana kupitia Msemaji wa Wizara ya Sheria na Katiba, Bw. Omega Ngole, alisema jalada la kesi hiyo lilikwishafanyiwa kazi na ofisi yake na kupelekwa ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) tangu Septemba 9 mwaka huu.
"Jalada la Buzwagi lilipokelewa likafanyiwa kazi na kurudishwa TAKUKURU na kimsingi uamuzi wote ulifikiwa na ofisi mbili," alisema Bw. Ngole akimaanisha ofisi za TAKUKURU na ile ya DPP zililifanyia kazi kwa pamoja suala hilo.
Alipoulizwa ni lini jalada hilo lilifikishwa kwa DPP kwa mara ya kwanza, Bw. Ngole hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Alipoulizwa ni lini jalada hilo litarejeshwa kwa DPP kutoka TAKUKURU kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani waliohusika na kashifa hiyo, Bw. Ngole alijibu:
"DPP amepewa madaraka kisheria ya kukasimisha kwa chombo chochote kinachohusika kikawa na uwezo wa kisheria wa kuendesha kesi husika yenyewe."
Kwa mujibu wa sheria inayounda TAKUKURU, The Prevention and Combating of Corruption Act, 2007, taasisi hiyo inao uwezo kisheria kufungua yenyewe mashitaka na kuyaendesha baada ya kupata kibali cha DPP.
Iwapo DPP atakuwa ametoa kibali cha kuruhusu Bw. Karamagi kushitakiwa kwa tuhuma hizo na TAKUKURU ikaamua kufuata sheria, huenda Waziri huyo wa zamani aliyelazimika kujiuzulu kwa kashifa ya Richmond, akawa kiongozi wa tatu wa ngazi za juu Serikalini kuburutwa kortini.
Tayari mawaziri wa zamani Bw. Basir Mramba na Daniel Yona hadi leo wako gereza la Keko, Dar es Salaam baada ya kukosa dhamana katika mashitaka ya kuiingizia Serikali hasara waliyofunguliwa mapema wiki hii.
Mkataba huo wa Buzwagi uliosaniwa Februari mwaka huu uliibua tafrani nchini hasa baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, kusimamishwa kuhudhuria Bunge baada ya kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka Waziri Karamagi awajibishwe kwa kile alichodai alilidanganya Bunge kuhusu namna mkataba huo ulivyoingiwa na faida ambazo Serikali inatarajiwa kuzipata.
Badala yake, Bw. Kabwe aligeuziwa kibao na kuonekana kuwa yeye ndiye aliyesema uongo na Bunge likaridhia adhabu hiyo dhidi yake, adhabu ambayo ilipingwa na wananchi mbalimbali.
Bw. Zitto pia alihoji kitendo cha Karamagi kwenda kusaini mkataba huo London kwa kutumia mfumo wa mikataba ya zamani wakati Serikali ikiwa inajadiliana na wawekezaji kurekebisha mikataba ya madini nchini.
Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu Rabia Bakari anaripoti kuwa leo Mahakama Kuu itasikiliza maombi ya Bw. Mramba na Yona ya kuitaka Mahakama Kuu iingilie kati kile watuhumiwa hao wanacholalamikia kuwa ni masharti magumu ya dhamana waliyowekewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Watuhumiwa hao kupitia mawakili wao waliwasilisha rasmi maombi yao hayo jana kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vilivyo karibu na watuhumiwa hao, rufaa hiyo itasikilizwa leo ambapo vigogo hao watawasilisha hoja za kupinga masharti ya dhamana kama yalivyotolewa na Hakimu Hezron Mwankenja wa Kisutu.
Mahakama hiyo iliwataka watuhumiwa hao kila mmoja kujidhamini kwa sh. bilioni 3.9 ambapo katika kesi ya msingi, washitakiwa hao wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 11.7.
Bw. Mramba na Bw. Yona walifikisha mahakamani hapo juzi wakikabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo matumizi mabaya ya ofisi, madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja anayesikiliza kesi hiyo.
Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Joseph Ole, aliwasomea mashitaka watuhumiwa hao mapema wiki hii alidai kuwa, kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri walitumia vibaya madaraka.
Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa kukagua kampuni za madini nchini ambapo kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba na kampuni tanzu kuzalisha madini ya dhahabu kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mramba na Yona wanadaiwa kuwa Mei 28, mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma jijini Dar es Salaam, wakiitumikia serikali katika nafasi za Uwaziri wa Fedha na Nishati na Madini, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mikataba ya kuiongezea kampuni hiyo muda wa miaka miwili wa kuendelea kuzalisha madini kuanzia Juni 2005 hadi Juni 2007 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Ole aliendelea kudai kuwa, katika shitaka la tatu wote wawili wanadaiwa kuwa kati Machi na Mei mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao kwa kumualika Dk. Enrique Segura wa M/S Alex Stewart ( ASSAYERS) Government Business Corporation kusaini mkataba wa nyongeza wa miaka miwili kabla timu ya majadiliano ya Serikali kulifanyia kazi suala hilo.
Katika shitaka la nne, kati ya Machi na Mei mwaka 2005, washitakiwa wanadaiwa kuwa walitumia nyadhifa zao vibaya kwa kukaidi kupeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali suala la kodi kama ilivyopendekezwa na Timu ya Serikali ya Majadiliano, jambo ambalo lilisababisha mkataba uongezeke kwa miaka miwili bila kupitishwa na timu ya majadiliano.
Shitaka la tano, ilidaiwa kuwa mshitakiwa Mramba Oktoba 10, mwaka 2003 akiwa Waziri wa Fedha alidharau mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kutotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.
Katika shitaka la sita, Mramba anadaiwa kati ya 18 na 19 Desemba mwaka 2003, akiwa Waziri wa fedha, alitoa kibali namba GN 423/2003 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume na mapendekezo yaliyopendekezwa na TRA.
Katika shitaka la saba, Mramba anadaiwa kuwa Desemba 19, mwaka 2003 akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka vibaya kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.
Ole, aliongeza kuwa shitaka la nane, Oktoba 15, mwaka 2004 akiwa Waziri wa Fedha alitoa kibali namba GN 497/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume na mapendekezo ya TRA.
Shitaka la tisa, Mramba anadaiwa kuwa kati 14 na 15 Oktoba 2004, akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 498/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume na mapendekezo ya TRA.
Katika shitaka la 10, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, mwaka 2005 akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 377/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume na mapendekezo ya TRA.
Katika shitaka la 11, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, 2005 akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 378/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume na mapendekezo ya TRA.
Katika shitaka la 12, Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni 2003 na Mei 2005 wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri kwa makusudi na kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi ili kuipendelea kampuni hiyo na kuisababishia Serikali hasara ya Sh. 11, 752,350,148.00.
Katika shitaka la mwisho, Mramba anadaiwa kuwa kati ya 2003 na 2007 akiwa Waziri wa Fedha kwa makusudi alishindwa kuwa makini au kutotimiza wajibu wake alisaini vibali, kuruhusu kampuni hiyo kutokulipa kodi na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 11.7.