Kura za maoni zapandisha homa ya uchaguzi

Invisible

Robot
Feb 11, 2006
9,075
7,859
HATA kabla kampeni za uchaguzi hazijaanza rasmi, makampuni mbalimbali mjini Nairobi , yalikuwa yakiendesha kura za maoni juu ya kiongozi gani anayekubalika zaidi na Wakenya kuiongoza nchi hiyo mara baada ya uchaguzi wa Desemba 2007.

Na ugomvi ndani ya Chama cha ODM Kenya kati ya Raila Odinga na wapambe wake kwa upande mmoja na Kalonzo Musyoka na wapambe wake kwa upande mwingine, ulitoa nafasi kwa makampuni mbalimbali jijini Nairobi , kuanza kuendesha kura ya maoni juu ya ni nani hasa anakubalika na jamii ya Wakenya.

Bwana Kalonzo Musyoka:
12.jpg


Ikumbukwe kuwa Raila na Kalonzo, wakiwa washirika wakubwa wa kisiasa kwa takribani miaka mitano, wakiwa wamevuka milima na mabonde katika kipindi hicho, walianza kubishana juu ya namna bora ya kupata mgombea urais wa ODM Kenya ambaye angepambana na Rais Mwai Kibaki.

Na wakati huo, kura za maoni zilizoendeshwa na makampuni mbalimbali, ikiwamo kampuni maarufu hapa ya Steadman Group, zilipoanza kutangazwa katika vyombo vya habari, zikionyesha kuwa Kalonzo alikuwa akikubalika zaidi kuliko Raila Odinga. Kwa hakika, kura hizo zilimweka Kalonzo juu kabisa ya Rais Mwai Kibaki.

Kwa namna fulani, matokeo hayo yaliathiri uamuzi wa baraza la wazee lililoundwa na chama hicho kuangalia namna bora ya kupata mgombea wa chama hicho, ambalo katika mapendekezo yake, ambayo hata hivyo, hayakutolewa hadharani, lilisisitiza kwamba ODM Kenya ihakikishe kuwa inatumia njia yoyote kuhakikisha kuwa Kalonzo anakuwa mgombea urais kwa kuwa Raila hawezi kukubalika kutokana na kabila analotoka kutopendwa na Wakenya wengi.

Hata hivyo, Raila ambaye alitumia muda mwingi kufanya kampeni za chini kwa chini, akitafuta kuungwa mkono na makabila mengine kutoka mikoa yote ya Kenya , aliukataa uamuzi huo na baadaye akafanikiwa kumshawishi mwanasheria mmoja wa hapa ambaye alikuwa amesajili chama cha Orange Democratic Movement (ODM), mara baada ya serikali kushindwa katika kura ya maoni mwaka 2005.

Raila na kundi kubwa la wapambe wake, wakiwamo watu maarufu kama William Ruto, Musalia Mudavadi na Joseph Nyagah, wakajiengua ODM Kenya na kuhamia ODM. Ikumbukwe kuwa wazo la kuanzisha chama cha ODM, liliibuka baada ya ushindi wao katika kura ya maoni kuhusu katiba mpya, iliyotumia alama za chungwa kwa walioikataa na ndizi kwa waliokuwa wakiikubali.

Umoja ulioonyeshwa na wapinzani wa katiba hiyo mpya dhidi ya serikali waliokuwa wakitumia alama ya chungwa, ndiyo uliochochea mawazo ya kuundwa kwa chama kipya ambacho kingetumika kupambana na Rais Mwai Kibaki katika uchaguzi wa mwaka huu. Lakini walipotaka kusajili jina la Orange Democratic Movement, walikuta tayari kuna mtu alikuwa amesajili chama hicho, na kukumbana na mshtuko mkubwa.

Hata hivyo, katika kukabiliana na hali ya mambo, wakaamua kusajili chama kwa jina la Orange Democratic Movement of Kenya (yaani ODM Kenya).

Haijulikani ni nini hasa kilichotokea, lakini kuna maneno ya chini kwa chini kuwa Raila na watu wake, walimfuata aliyesajili chama cha ODM, Mungambi Imanyara na kumshawishi kwa njia wanazojua wao, hadi akaamua kukubali kuwakaribisha na kuwapa nyaraka zote za chama hicho mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Kalonzo na wapambe wake, wengi kutoka Ukambani, akiwamo mwanasheria maarufu, Mutula Kilonzo, na watu maarufu kama David Musila, wakabaki katika ODM Kenya huku Raila na kundi lake wakifunga virago kuelekea ODM.

Hivyo ndivyo kwa mara ya kwanza kura za maoni zilivyosababisha kuporomoka kwa muungano wa wanasiasa hao wawili maarufu katika siasa za Kenya .

Haraka haraka, mara baada ya kuchukua uongozi katika ODM, uchaguzi ulifanyika na Henry Kosgei kutoka Mkoa wa Bonde la Ufa , akachaguliwa kuwa Mwenyekiti, huku Profesa Anyang’ Nyong’o, mfuasi mwaminifu wa Raila, akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu.


RAILA Odinga
11.jpg


Kutokana na kampeni alizofanya Odinga, chama hicho kilipokewa kote Kenya na kupata wafuasi na wanachama wengi kwa muda mfupi na hadi Agosti 31, chama hicho kiliitisha mkutano wa kuchagua mtu atakayesimamishwa na chama kuwania urais. Wagombea walikuwa ni Raila Odinga, Musalia Mudavadi, William Ruto, Najib Balala na Joseph Nyagah.

Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya Michezo vya Kasarani, Raila aliibuka na ushindi mkubwa dhidi ya wenzake na hapo hapo akamtangaza Musalia Mudavadi kuwa mgombea Mwenza, huku akilibatiza kundi la viongozi hao watano kwa jina la The Pentagon.

Kesho yake, Septemba mosi, ODM Kenya pia walifanya uchaguzi katika uwanja huo huo na Kalonzo Musyoka akaibuka na kura nyingi dhidi ya mpinzani wake, Profesa Julia Ojiambo.

Kuanzia wakati huo, kura za maoni zilizoanza kuendeshwa na mashirika mbalimbali jijini Nairobi , zikaanza kumwonyesha Raila akiwa juu kabisa ya wenzake, akifuatiwa na Rais Mwai Kibaki na Kalonzo Musyoka akishika mkia.

Katika kura ya maoni ya kwanza iliyoendeshwa na kampuni ya Steadman, Raila alikuwa na asilimia 47, akifuatiwa na Rais Kibaki aliyekuwa na alama 38, huku Kalonzo akiambuliwa asimia 8. Hii ilikuwa na maana kuwa hata kama Kalonzo angeungana na Kibaki, bado walikuwa nyuma ya Raila kwa asilimia moja.

Ukiondoa Steadman, mashirika mengine yanayoendesha kura za maoni hadi sasa ni Infotrak Harris, Consumer Insight na Strategic Reasearch. Hata hivyo, wakati Steadman inaendesha utafiti wake huru, mashirika mengine matatu yamekuwa yakiendesha kura ya maoni kwa gharama za kampuni ya Nation Media Group (NMG) kwa ajili ya matumizi yake kwa vyombo vya habari inavyovimiliki.

Pamoja na gazeti maarufu la Daily Nation, NMG pia inamiliki magazeti mengine ya Taifa Leo, Business Daily na Daily Metro. Pia inamiliki kituo cha televisheni cha NTV na kituo cha redio cha Easy FM. Mashirika hayo ya utafiti yamekuwa yakiendesha kura za maoni kila wiki, wakati Steadman sasa inatoa matokeo ya kura ya maoni kila baada ya wiki mbili.

Wiki chache baadaye, yaani mwanzoni mwa Oktoba, kura ya maoni ya Steadman ilionyesha kuwa Raila alikuwa amepanda chati baada ya safari hii kupata asilimia 53, huku Kibaki akipata asilimia 37 na Kalonzo asilimia nane. Matokeo ya kila wiki ya mashirika mengine matatu ya NMG yalionyesha mwelekeo wa aina hiyo hiyo.

Hata hivyo, matokeo hayo hayakupokewa kimya na wanasiasa. Upande wa ODM ambao ulionekana kupendelewa na matokeo hayo, ulikuwa ukisema siku zote kwamba Wakenya wanataka mapinduzi na kwamba kura za maoni zilikuwa zikionyesha waziwazi msimamo wa Wakenya wa kutaka mabadiliko. Kibaki na wapembe wake waliyapuuza matokeo hayo, wakisema ni ya kupikwa, huku wakiituhumu Steadman na mashirika mengine kwa kukubali kununuliwa na wanasiasa badala ya kufuata matakwa halisi ya Wakenya.

Kalonzo Musyoka kwa upande wake alisema matokeo ya uchaguzi wa Desemba 27, yatamshangaza kila mtu, wakiwamo mahasimu wake wa kisiasa, kwa kuwa wakati Raila atakuwa amesimama upande mmoja na Kibaki upande mwingine, yeye na wakenya watapita katikati yao bila kuonekana na kuibuka na ushindi.

Hata katika mikutano yake ya hadhara, ambayo kwa kawaida hubeba wafuasi wengi, Kalonzo amekuwa akiilaumu Steadman kwa kuonyesha upendeleo wa waziwazi kwa wagombea ambao kwa madai yake, hawakubaliki miongoni mwa Wakenya.

Lakini watafiti na wasomi wamekuwa wakisema kwamba siku zote, wanasiasa hawakubali matokeo ya kura ya maoni ambayo yanawaonyesha kuwa wameshindwa kwa kuwa kufanya hivyo hadharani ni kuwakatisha tamaa wafuasi wao.

Ukweli wa hoja hii umeanza kuonekana katika siku za karibuni, baada ya mwenendo katika kura ya maoni kuanza kubadilika, sasa ikionekana kuwa kibaki ameanza kuvuta kasi kubwa kumkaribia Raila.

Katika kura za maoni zilizotangazwa Ijumaa, Steadman wanasema Raila bado yuko juu, akiwa na asilimia 43.6, lakini akifuatiwa kwa karibu kabisa na Kibaki aliyepata asilimia 43.3. Kalonzo ana asilimia 11.4.

Matokeo hayo yamelalamikiwa sana na viongozi katika ODM, wakidai yamefanywa kumpendeza rais Kibaki. Pia wanadai kuwa siku chache zilizopita, wakuu wa Steadman walialikwa Ikulu na Rais Kibaki ambako wanahisi njama za kuandaa matokeo hayo ziliandaliwa.

Rais Mwai Kibaki:
10.jpg


Lakini upande wa Kibaki na chama chake cha PNU unasema hiyo ndiyo hali halisi katika uwanja wa mapambano na kwamba wananchi sasa wameweza kuchambua pumba na mchele na sasa wanaelekea kuutambua mchango wa Rais Kibaki kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kalonzo kama kawaida yake anasema matokeo hayo ni ya kupikwa na kwamba kama alivyoahidi, atapita katikati ya wagombea hao wawili na hawatamwona hadi atakapoingia Ikulu baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, matokeo ya mashirika mengine yaliyotangazwa Ijumaa iliyopita ni kama ifuatavyo; Infotrak Harris Raila 44.2%, Kibaki 36.1%, Kalonzo 17.9%; Consumer Insight Raila 41.5%, Kibaki 39.1%, Kalonzo 15.8% na Strategic Research Raila 44.3%, Kibaki 36.2%, Kalonzo 17.3%.

Chanzo: Gazeti la Raia Mwema
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom