UZUSHI Kula matango baada ya kuvuta sigara kunasaidia kupunguza athari zake

Baada ya tathmini, tumebaini kuwa taarifa hii ni ya uzushi
Salaam ndugu zangu,

Mtaani kwetu nimezungukwa na ndugu na marafiki wanaovuta sigara. Baadhi Yao hupendelea kula matango baada ya kuvuta sigara wakidai wanapunguza sumu itokanayo na sigara.

Nimejaribu kugoogle kutafuta ukweli lakini sijafanikiwa kuona.

Naomba JamiiCheck itusaidie kupata facts kwenye jambo hili.

Cigga.jpg
 
Tunachokijua
Tango ni mmea au tunda familia ya malenge (Cucurbitaceae) ambayo inazalisha matunda yenye umbo refu na rangi ya kijani. Kwa Tanzania Matunda haya mara nyingi huliwa yakiwa mabichi au hutumiwa kiungo kwenye saladi au kachumbali nk. 95% ya mmea huu inajengwa na maji na pia ina virutubisho vingine kama vile vitamini C, vitamini K, na potasiamu.

Kuvuta sigara ni kitendo cha kuingiza mwilini moshi wa tumbaku uliofungwa katika sigara. Watu hufanya hivyo kwa kuiweka sigara mdomoni na kuiwashia mwisho wake ili kuvuta moshi wa kemikali mbalimbali zilizomo ndani ya tumbaku.

Mashirika ya makubwa ya Afya Ulimwenguni ikiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Marekani (CDC) wanakubaliana kuwa uvutaji wa sigara una madhara makubwa kiafya ikiwamo kupata magonjwa katika mfumo wa upumuaji, Kupata Kansa ya Mapafu na kuwa katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.

Aidha takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Marekani (CDC) zinaonesha kuwa uvutaji wa sigara ulimwenguni umekuwa chanzo cha vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka. Mathalani, WHO wanaeleza:

"Uvutaji wa Sigara (tumbaku) ni moja ya vitisho vikubwa vya afya ya umma ambavyo dunia imekabiliana navyo. Uvutaji huu unaua zaidi ya watu milioni 8 kila mwaka duniani kote. Zaidi ya watu milioni 7 kati ya vifo hivyo ni matokeo ya matumizi ya moja kwa moja ya tumbaku wakati takriban watu milioni 1.3 ni matokeo ya watu wasiovuta sigara kufichuliwa kwa moshi wa sigara."

Kama alivyouliza mleta mada hii, kumekuwapo baadhi ya watu katika jamii wakiamini kuwa unapokula matango baada ya kuvuta sigara inasaidia kupunguza athari zake.

Zaidi ya hayo JamiiCheck imabaini andiko mtandaoni (hili) linalotaja tango kama miongoni mwa mmea unaoweza kusafisha kemikali ya sigara ndani ya mwili wa binadamu. Andiko linabainisha kwamba kula matango kwa wingi kunasaidia kupunguza uraibu wa sigara. Hata hivyo andiko hili haliweki bayana ni kwa namna gani hasa tango linaweza kupunguza athari za sigara kwa mvutaji.

Upi ukweli kuhusu madai ya kula matango na kupunguza athari za sigara?
JamiiCheck imefatilia vyanzo mbalimbali vya taarifa za afya ulimwenguni ikiwamo CDC na WHO pamoja na vyanzo vinavyofafanua faida za matango kiafya lakini hakuna chanzo kinachoelezea tango kama mmea unaopunguza athari za sigara kwa mvutaji.

Ziaidi ya hayo JamiiCheck imefanya mawasiliano na Wataalamu wa Afya Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mfumo wa Upumuaji na Hewa, Dkt. Elisha Osati ambaye amesema:

Inawezekana ni uzoefu wa mtu au imani ya mtu au baadhi ya watu lakini kitaalam hakuna uhusiano wa tango kuweza kupunguza madhara ya uvutaji sigara kama vile saratani au magonjwa ya mapafu na magonjwa ya njia hewa.
Tango ni tunda lenye faida zake kiafya lakini hakuna uhusiano wa moja kwa moja.
Hivyo, kutokana na ufafanuzi huo, JamiiCheck inaona kuwa hoja inayodai kuwa kula matango baada ya kuvuta sigara kunasaidia kupunguza athari zake ni uzushi.

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom