Kitabu: Maisha ya Malcom X

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Jan 31, 2021
7,232
12,733
Tafsiri ya kitabu The Autobiography of Malcom X. Unaweza kukisoma ndani ya Maktaba app.
Malcom x cover.png


Muandishi: Malcom X(Alex Haley), 1965.

Mtafsiri: Pictus Publishers ltd

Email: pictuspublishers@gmail.com.

Whatsapp: 0715278384

©Pictus Publishers Ltd2023.

Sura ya kwanza
JINAMIZI​
Mama yangu alinisimulia kuwa alipokuwa na mimba yangu, usiku mmoja kundi la wabaguzi wa rangi la Ku Klux Klan lilifika kwa farasi nyumbani kwetu huko Omaha, Nebraska. Waliizingira nyumba yetu huku wakionyesha bunduki zao, walipiga kelele wakimtaka baba yangu atoke nje. Mama yangu alienda mlangoni na kufungua.

Akisimama sehemu ambayo waliweza kuona hali yake ya ujauzito, aliwaambia kuwa alikuwa peke yake na wanawe watatu wadogo, na kuwa baba yangu alikuwa amesafiri, ameenda kuhubiri huko Milwaukee. Watu wale walitoa vitisho na onyo wakisema ni vyema tukahama mji haraka kwa sababu “Wakristo wema wa Kizungu” hawatavumilia kuona baba yangu “akifanya uchochezi” kati ya Manegro “wema” wa Omaha kwa kutumia mahubiri ya “kurudi Africa” ya Marcus Garvey.

Baba yangu, mchungaji Earl Little alikuwa ni mchungaji wa kanisa la Baptist, mfuasi mtiifu wa chama cha Marcus Aurelius Garvey, U.N.I.A(Universal Negro Improvement Association(Chama cha Kuwainua Watu Weusi Duniani)). Kwa msaada wa mitume kama baba yangu, Garvey kutoka katika makao yake makuu huko Harlem, New York-alikuwa akitoa mwito juu ya ubora wa watu weusi na akiuhimiza umma wa watu weusi kurudi Afrika, nyumbani kwa mababu zao-kampeni iliyomfanya Marcus Garvey kuwa mtu mweusi mtata zaidi dunaini.

Huku wakiendelea kutoa vitisho, wabaguzi wale waliamrisha farasi wao kukimbia kuizunguka nyumba huku wao wakivunja vioo vyote vya madirishani kwa vitako vya bunduki. Kisha wakaenda zao, mioto yao iking’aa gizani kama walivyokuja.

Baba yangu aliporudi alikasirika sana. Aliamua kusubiri mpaka nitakapozaliwa-na wakati ulikuwa karibu, kisha ahamishe familia yake. Sijajua kwa nini alifanya uamuzi huu maana hakuwa Mnegro muoga kama ambavyo wengi walikuwa nyakati hizo, na bado wengi wako hivyo hadi hii leo.

Baba yangu alikuwa na mwili mkubwa, urefu wa futi sita na nchi nne na mweusi ti. Alikuwa na jicho moja tu zima. Mpaka leo sijajua nini kililipata lile lingine. Alikuwa ni mzaliwa wa Reynolds, Georgia ambako aliacha shule baada ya darasa la tatu au la nne. Aliamini-kama alivyoamini Marcus Garvey, kuwa mtu mweusi hawezi kupata uhuru, kujitegemea na kujiheshimu ndani ya Marekani, hivyo inampasa mtu mweusi kumuachia mtu mweupe Marekani na yeye kurudi Afrika alikotokea. Moja ya sababu iliyofanya baba yangu kutumia muda wake na kuhatarisha maisha yake kusambaza falsafa hii kati ya watu wake ni kuwa alikuwa ameshuhudia kaka zake wanne kati ya sita wakiuawa kikatili. Watatu kati yao wakiuawa na wazungu, akiwemo mmoja kwa kuuliwa na umati. Kitu ambacho baba yangu hakujua wakati ule ni kuwa, kati ya watatu waliobaki, yeye akiwemo, ni mmoja tu-mjomba Jim ndiye atakufa kifo cha kawaida kitandani.

Baadaye, polisi wa kizungu wa kaskazini ya Marekani walimpiga risasi mjomba wangu Oscar. Na mwishowe baba yangu mwenyewe alikufa kwa mikono ya wazungu.

Siku zote imekuwa ni imani yangu kuwa mimi pia nitakufa kikatili. Nimefanya kila niwezalo kujiandaa.

Nilikuwa mtoto wa saba kwa baba yangu. Alikuwa na watoto wengine watatu kutoka kwenye ndoa yake ya kwanza, Ella, Earl na Mary walioishi Boston.

Alikutana na kumuoa mama yangu huko Philadelphia, na huko ndiko mtoto wao wa kwanza, kaka yangu mkubwa Wilfred alizaliwa. Walihama kutoka Philadelphia kwenda Omaha ambako Hilda na Philbert walizaliwa.

Kisha nikafuata. Mama yangu alikuwa na miaka ishirini na nane nilipozaliwa tarehe 19/5/1925, kwenye hospitali huko Omaha. Kisha tukahamia Milwaukee ambako Reginald alizaliwa.

Toka uchanga wake amekuwa na aina fulani ya ugonjwa wa ngiri ambao ulimsumbua maisha yake yote.

Mama yangu, Louise Little alizaliwa huko Grenada, British West Indies. Mama yangu alionekana kama mwanamke wa kizungu. Baba yake alikuwa ni mzungu.

Alikuwa na nywele ndefu nyeusi, na ongea yake haikuwa kama ya mtu mweusi. Sijui chochote juu ya baba yake mzungu zaidi ya kuwa alijisikia aibu kuzaliwa naye. Nakumbuka kumsikia akisema kwamba hajawahi kumuona. Na ni kwa sababu yake ndiyo maana nina rangi hii ya ngozi na nywele.

Nilikuwa ndiye mtoto mweupe zaidi katika familia yetu(Baadaye maishani nilipokuwa huko Boston na New York, nilikuwa kati ya mamilioni ya watu weusi ambao walikuwa wehu hadi kufikiri kuwa ilikuwa ni aina fulani ya hadhi kuwa na weupe-na kuwa mtu alikuwa na bahati kuzaliwa hivyo. Lakini badaye zaidi nilikuja kuchukia kila tone la damu ya mzungu yule mbakaji ndani yangu).

Familia yetu haikukaa sana huko Milwaukee maana baba yangu alitaka kuishi sehemu ambayo tungepanda vyakula vyetu wenyewe na ambako angeweza kuanzisha biashara, na kuishi kulingana na mafundisho ya Marcus Garvey ya kutotegemea wazungu. Kwa sababu fulani, tulienda Lansing, Michigan.

Baba yangu alinunua nyumba, na ndani ya muda mfupi, kama kawaida yake, akaanza kujitolea kuhubiri kwenye makanisa ya kibapstisti ya watu weusi yaliyokuwepo eneo letu, na siku za juma alikuwa akizunguka akitangaza maneno ya Marcus Garvey.

Alikuwa ameanza kutunza pesa kwa ajili ya duka ambalo siku zote alikuwa ametamani kumiliki, kisha, kama kawaida, watu weusi fulani wapumbavu wa jamii ya Uncle Tom(Vibaraka) wakaanza kupeleka maneno kwa wazungu juu ya muelekeo wake wa kimapinduzi. Safari hii kitisho cha kutakiwa kuhama mji kilitoka kwa kikundi cha wabaguzi kilichoitwa the Black Legion, hawa walivaa kanzu nyeusi badala ya nyeupe. Haikuchukua muda ikawa kila mahali ambako baba yangu alikwenda, wanachama wa Black Legion walikuwa wakimfuata ili kumuumbua kama mnegro “mwenye kujifanya” kwa sababu ya kutaka kwake kufungua duka, kwa kuishi nje ya eneo la Lansing lililotengwa kwa ajili ya watu weusi na kwa kuchochea vurugu na uasi kati ya watu “weusi wema.”

Kama ilivyokuwa Omaha, wakati huu mama yangu alikuwa mjamzito tena, wakati huu ilikuwa mimba ya dada yangu mdogo. Muda mfupi baada ya Yvonne kuzaliwa, ulifika usiku wa kutisha wa mwaka 1929, kumbukumbu yangu ya kwanza ambayo bado ipo. Nakumbuka ghafla kubebwa juu juu katikati ya vurugu za milio ya bastola, kelele, moshi na moto. Baba yangu alikuwa akifoka na kupiga risasi kuelekea wazungu wawili waliokuwa wamewasha moto na sasa wakikimbia. Nyumba yetu ilikuwa ikiungua.

Tulikuwa tukikanyagana na kugongana tukijaribu kujiokoa. Nusura nyumba imuangukie mama yangu akiwa na mtoto mkononi, alikimbia kupitia mlango wa uani huku nyuma yake nyumba ikianguka na kurusha cheche huku na kule. Nakumbuka tukiwa nje usiku tukiwa na nguo zetu za ndani, tukilia na kupiga kelele. Polisi na askari wa zimamoto wa kizungu walifika na kusimama wakiangalia nyumba ikiteketea hadi chini.

Marafiki kadhaa walimsaidia baba yangu kutupa hifadhi na nguo kwa muda; kisha akatuhamishia kwenye nyumba fulani pembezoni mwa Mashariki ya Lansing. Wakati huo watu weusi hawakuruhusiwa kuwepo katikati ya Lansing Mashariki baada ya giza kuingia.

Huko ndiko ambako chuo kikuu cha Jimbo la Michigan kilikuwepo: nilisimulia haya yote nilipozungumza na wanafunzi wa chuo hicho mwezi wa kwanza mwaka 1963(Na nilikutana na mdogo wangu Robert baada ya kipindi kirefu cha kutoonana, alikuwa pale akichukua masomo ya juu ya saikolojia).

Niliwaeleza jinsi ambavyo Lansing Mashariki ilitunyanyasa hadi tukalazimika kuhama tena, wakati huu tukienda maili mbili nje ya mji. Huko ndiko ambako baba yetu kwa mikono yake mwenyewe alitujengea nyumba ya vyumba vinne.

Huko ndiko nilikoanza kukumbuka mambo, hiyo ndiyo nyumba niliyokulia.

Nakumbuka baada ya tukio la moto, baba yangu aliitwa na kuhojiwa juu ya kibali cha bastola ambayo alifyatulia wazungu wawili waliowasha moto.

Nakumbuka mara nyingi polisi walikuwa wakifika nyumbani kwetu na kurusha vitu huku na kule, wakitafuta bastola. Bastola waliyokuwa wakiitafuta, ambayo hawakuwahi kuipata, na ambayo hawangeweza kumpa baba yangu kibali cha kuimiliki-ilikuwa imeshonewa ndani ya mto.

Lakini bunduki ya baba yangu na gobole lake vilikuwa peupe tu; kila mtu alikuwa navyo kwa ajili ya kuwindia ndege, sungura na wanyama wengine.

Baada ya hapo, kumbukumbu zangu ni juu ya mizozo kati ya baba na mama yangu.

Ilionekana kama walizozana muda wote. Wakati mwingine baba yangu alimpiga mama. Pengine ilitokana na kuwa mama yangu alikuwa na elimu nzuri.

Sijui alikoipata, lakini nafikiri mwanamke mwenye elimu hawezi zuia kishawishi cha kumsahihisha mwanaume asiye na elimu. Mara moja moja alikuwa akimsahihisha naye baba hakusita kumkunja.

Baba yangu alikuwa pia mkali sana kwa watoto wake wote isipokuwa mimi. Ndugu zangu wakubwa walipigwa kikatili kila walipovunja sheria zake-na alikuwa na sheria nyingi hivyo haikuwa rahisi kuzifahamu zote.

Karibu vipigo vyangu vyote vilitoka kwa mama yangu. Nimejiuliza sana kwa nini? Naamini kabisa kuwa, pamoja na kuwa baba yangu alikuwa mpinga wazungu, lakini kwenye akili yake alikuwa ameathirika na mtazamo wa wazungu kiasi kwamba alipendelea watoto weupe, na kati ya watoto wake mimi ndiye niliyekuwa mweupe zaidi.

Wazazi wengi weusi wa wakati huo walikuwa wakiwatendea watoto weupe kwa upendeleo kuliko wale weusi. Hii ilitoka moja kwa moja wenye utamaduni wa wakati wa utumwa kuwa “chotara” kwa sababu alikuwa anafanana na mtu mweupe kwa karibu, basi alikuwa bora.

Kumbukumbu zangu nyingine mbili juu ya baba yangu ni nje ya nyumbani. Moja ni juu ya kazi yake kama mhubiri wa Kibapstisti. Hakuwahi kuwa mchungaji mwenye kanisa lake mwenyewe; siku zote alikuwa ni “mhubiri mualikwa” nakumbuka mahubiri yake maarufu aliyopendelea sana, “treni ndogo nyeusi inakuja. . . na ni vyema ukaweka mambo yako yote sawa!” Nadhani kuwa hili lilihusiana na kampeni ya Marcus Garvey ya kurudi Afrika, ikiwa na kaulimbiu, “Treni nyeusi kuelekea nyumbani.” Philbert, kaka yangu ambaye alikuwa amenipita umri kidogo tu, alipenda sana habari za kanisa, lakini mimi zilinichanganya na kunishangaza.

Nilikuwa nikikaa nimemtumbulia macho baba yangu akiruka na kufoka alipokuwa akihubiri huku kanisa zima likiruka na kupiga kelele nyuma yake, likiwa limejitoa roho na mwili kwenye kuimba na kusali.

Hata katika umri huo mdogo, sikuweza kuamini dhana ya Wakristo kuwa Yesu ana uungu. Na hakuna mtu yeyote wa kidini, hadi nilipokuwa mtu mzima wa miaka ishirini-na baadaye nikiwa gerezani, aliyeweza kunieleza chochote.

Niliwaheshimu kidogo sana watu waliowakilisha dini.

Ni kupitia kazi yake hii ya uhubiri ndipo baba yangu aliweza kukutana na watu wengi weusi walioishi Lansing.

Niamini ninapokuambia kuwa Manegro wale walikuwa na hali mbaya sana wakati huo. Bado hata sasa wana hali mbaya-japo ni kwa namna nyingine. Kwa kusema hivyo, namaanisha kuwa sijawahi kuona mji ambayo una asilimia kubwa zaidi ya watu weusi wanaoitwa wa “daraja la kati” walioridhika na waliopotoshwa –watu weusi watafuta hadhi na kuchangamana.

Hivi karibuni nilikuwa nimesimama kwenye sehemu ya mapokezi ya Umoja wa Mataifa nikiongea na balozi kutoka nchi ya Afrika na Mke wake. Mtu mweusi mmoja alinifuata na kusema, “Unanifahamu?”

nillifedheheka kidogo sababu nilifikiri labda ni mtu ninayepaswa kumfahamu. Kumbe ni mmoja wa wale Manegro wa “daraja la kati” wanaojisifu na kuridhika kutoka Lansing. Sikujisikia vizuri.

Alikuwa ni aina ya mtu mweusi ambaye kamwe hangeweza kujihusisha na Afrika hadi pale kitendo cha kuwa na rafiki wa kiafrika kilipokuwa kama fasheni kati ya watu weusi wa “daraja la kati.”

Zamani nilipokuwa nakua, watu weusi wa Lansing waliokuwa na “mafanikio” walikuwa ni wahudumu na wang’arisha viatu.

Kuwa mfanya usafi kwenye duka fulani mjini ilifanya mtu aheshimike sana. Watu wa “maana,” “wakuu,” “wasemaji wa watu weusi,” walikuwa ni wahudumu wa Lansing Country Club na wang’arisha viatu kwenye makao makuu ya jimbo.

Watu weusi pekee waliokuwa na pesa kiukweli walikuwa ni wachezesha kamari au ambao kwa namna fulani waliishi kwa kunyonya masikini zaidi, na masikini walikuwa wengi sana. Wakati ule hakuna mtu mweusi aliyeajiriwa na kiwanda cha magari cha Lansing au kiwanda cha Reo. (Unakumbuka magari ya Reo? Yalitengenezwa Lansing na R. E. Olds, mtu ambaye yaliitwa jina lake, aliishi Lansing. Vita ilipoingia, waliajiri wafanya usafi kadhaa weusi.) Sehemu kubwa ya watu weusi ilitegemea msaada wa serikali, au W.P.A(Works Projects Adminstration)., au iliteseka kwa njaa.

Siku ilifika ambayo familia yetu ilikuwa masikini hadi tulikula tundu la donati; lakini wakati huo tulikuwa na hali nzuri kidogo kulinganisha na watu weusi wengine. Sababu kubwa ni kuwa tulizalisha sehemu kubwa ya chakula chetu wenyewe huko nje ya mji tulikokuwa.

Tulikuwa na afadhali kuliko watu weusi wa mjini ambao walipiga kelele, kama baba yangu alivyosema kwenye mahubiri yake, juu ya keki angani na mbingu yao baadaye wakati mzungu anayo yake hapahapa duniani.

Nilifahamu kuwa michango ambayo baba yangu alipata kwenye kazi yake ya kuhubiri ndiyo hasa ilitulisha na kutuvisha, na pia alifanya kazi zingine za ajabu, lakini picha yake inayofanya nijivunie zaidi ni harakati na upambanaji wake juu ya maneno ya Marcus Garvey.

Pamoja na udogo wangu niliokuwa nao, nilifahamu kutokana na niliyosikia kwamba baba yangu alikuwa akiongea mambo yaliyomfanya awe “shupavu.” Nakumbuka mwanamke mzee mmoja akitabasamu na kumwambia baba yangu, ‘Unawaogopesha wazungu, wako karibu kufa.’

Moja ya sababu zinazofanya nihisi kuwa baba yangu alikuwa akinipendelea ni kuwa, kulingana na kumbukumbu zangu, ilikuwa ni mimi tu ndiye aliyenichukua kwenda naye kwenye mikutano ya chama cha Garvey, U. N. I. A ambayo aliifanya kwa siri kwenye nyumba za watu tofautitofauti. Mikutano hiyo haikuwa na watu wengi, hawakuzidi ishirini.

Lakini hao walikuwa ni wengi sana kwenye sebule ya mtu. Nilitambua walivyokuwa tofauti wakati wa mikutano hii japo ni watu walewale waliokuwa wakiruka na kupiga kelele kanisani. Kwenye mikutano hii, wote-kutia ndani baba yangu, walikuwa makini sana, wenye akili zaidi na wanyenyekevu. Hili lilinifanya nami nijihisi namna hiyohiyo.

Nakumbuka kusikia, “Adam alifukuzwa kwenye bustani ya Eden kwenda kwenye mapango ya Ulaya,” “Afrika kwa waafrika,” ‘Waethiopia amkeni!” Kisha baba yangu angeongea kwamba haitachukua muda mrefu Afrika yote itaongozwa na mtu mweusi. Alipendelea kutumia neno “mtu mweusi” badala ya Negro.

“Hakuna anayejua wakati ambao saa ya ukombozi wa afrika itafika. Ipo kwenye upepo inakuja. Siku moja, kama tufani itafika.”

Nakumbuka kuona picha kubwa za kung’aa za Marcus Garvey zikipitishwa kwa kupasiana mikononi. Baba alikuwa na bahasha kubwa ya kuzihifadhi ambayo mara zote aliibeba kwenye mikutano hii. Kwenye picha zile, niliona kama mamilioni ya watu weusi wakiwa wamesongamana nyuma ya Marcus Garvey aliyekuwa amepanda gari zuri sana.

Mtu mweusi mkubwa akiwa amevalia sare nadhifu iliyokuwa na mapambo ya dhahabu, na pia alivalia kofia nzuri ikiwa na manyoya marefu. Nakumbuka nilisikia kuwa ana wafuasi weusi si tu katika Marekani bali duniani kote, na nakumbuka jinsi mikutano ilivyoisha mara nyingi kwa baba yangu kusema, huku watu wakimfuatisha; “Simama ewe mtu mkuu, utatimiza unachotaka!”

Sijawahi elewa kwanini baada ya kusikia mambo haya, kwa namna fulani, wakati huo; sikufikiria juu ya watu weusi wa Afrika. Picha yangu juu ya Afrika wakati huo ilikuwa ni washenzi walio uchi, wala watu, nyani, simba na misitu yenye joto.

Kwenye ziara zake baba yangu alitumia gari yake kuukuu iliyokuwa na rangi nyeusi, wakati mwingine alinichukua na tukaenda wote kwenye maeneo mbalimbali yaliyozunguka Lansing. Nakumbuka mkutano mmoja wa mchana(Mikutano mingi ilifanyika usiku) kwenye mji wa Owosso, umbali wa maili arobaini kutoka Lansing, mji ambao watu weusi waliuita “Mji mweupe” (Jambo kubwa ambalo Owosso ilijivunia ni kuwa mji wa Thomas. E. Dewey).

Kama ilivyokuwa East Lansing, watu weusi hawakuruhusiwa kutembea usiku, ndiyo sababu ya kufanya mkutano mchana. Na ukweli ni kuwa, miji mingi ya Michigan ilikuwa hivyo wakati huo. Kila mji ulikuwa na watu weusi wachache walioishi hapo. Wakati mwingine ilikuwa ni familia moja tu, kama ilivyokuwa kwenye makao makuu ya county, Mason. Huko kulikuwa na familia moja tu ya watu weusi, familia ya Lyon. Bwana Lyon alikuwa ni mcheza mpira maarufu wa shule ya sekondari ya Mason, aliheshimika sana huko Mason. Sa sasa alikuwa akiishi mjini humo akifanya vibarua vya hapa na pale.

Wakati huo mama yangu alionekana kama vile muda wote alikuwa akifanya kazi, akipika, akifua, akipiga pasi, akisafisha nyumba na kupigishana kelele na sisi watoto wake nane, na kawaida alikuwa akibishana au amenuniana na baba yangu. Moja ya chanzo cha mizozo yao ilikuwa ni mama yangu kuwa na msimamo mkali juu ya vitu ambavyo hataki kula, na wala hataki sisi tule, mfano nguruwe na sungura, vitu ambavyo baba yangu alivipenda sana.

Alikuwa ni mtu mweusi kutoka Georgia na aliamini katika kula vya kutosha chakula ambacho hapa Harlem tunaita “Chakula cha roho.”

Nimesema kuwa mama yangu ndiye aliyekuwa akinichapa-Lakini ilimbidi kufanya hivyo wakati ambao angeepuka aibu kutoka kwa majirani ambao wangeweza dhani kuwa alikuwa akitaka kuniua.

Kila alipojaribu kuinua mkono kunichapa, nilifungua mdomo na kupiga kelele za kufanya dunia yote ijue. Kama kuna mtu alikuwa anapita barabarani, basi angehairisha au angenichapa fimbo chache tu.

Nikiwaza kuhusu hilo leo, nahisi kuwa, kama ambavyo baba yangu alinipendelea kwa kuwa mweupe kuzidi wengine, mama yangu aliniadhibu vikali kwa sababu hiyohiyo.

Yeye mwenyewe alikuwa mweupe lakini aliwapendelea watoto waliokuwa weusi zaidi. Nafahamu kuwa kipenzi chake alikuwa ni Wilfred.

Nakumbuka alikuwa akiniambia nitoke ndani na “Acha miale ya jua ikupige ili upate rangi kidogo.”

Bidii yake katika kunifanya nisijihisi bora kutokana na rangi yangu ilivuka mipaka. Nina hakika alinitendea hivi kutokana na jinsi yeye mwenyewe alivyopata kuwa mweupe.

Nilijifunza mapema maishani kuwa kupiga kelele kunaweza kusaidia. Kaka zangu wakubwa na dada yangu walikuwa wameanza shule, wakati mwingine walikuwa wakirudi toka shule na kuomba biskuti zenye siagi au kitu fulani, kwa mkato mama yangu aliwajibu hapana. Lakini mimi nikikataliwa nililia na kufanya fujo mpaka nipate ninachotaka. Nakumbuka vizuri mama yangu akiniuliza kwa nini siwi mtoto mwema kama Wilfred; lakini nilijiambia mwenyewe, Wilfred kwa kuwa mwema na mkimya kulimfanya ashinde njaa mara nyingi. Hivyo basi, ingali bado mdogo sana nilijifunza kuwa kama unataka kitu fulani ni vyema ukapiga kelele.

Hatukuwa tu na bustani kubwa, bali pia tulifuga kuku. Baba yangu alinunua vifaranga na mama alivilea. Sote tulipenda kuku. Hicho ndicho chakula pekee ambacho hakukuwa na ubishani kati ya mama na baba. Kitu kimoja ambacho kinanifanya nimshukuru mama yangu ni hiki, siku moja nilimfuata na kumuomba niwe na bustani yangu na akaniruhusu kuwa na kitalu changu mwenyewe.

Nilikipenda na nilikihudumia vizuri sana. Nilipenda zaidi kupanda njegere. Nilijivuna sana tulipozila mezani petu. Niling’oa magugu kwenye bustani yangu kwa mikono mara tu yalipochomoza.

Nilikagua matuta nikiwa nimepiga magoti kuangalia minyoo na wadudu. Niliwaua na kuwazika. Wakati mwingine ambapo kila kitu kilikuwa safi na sina cha kupanda, nililala katikati ya matuta na kuangalia anga la bluu na mawingu yanayosafiri huku nikiwaza mambo mbalimbali.

Baada ya kufikisha miaka mitano nami pia nikaanza shule, nikiondoka nyumbani asubuhi pamoja na Wilfred, Hilda na Philbert. Shule yetu ilianzia chekechea hadi darasa la nane.

Ilikuwa umbali wa maili mbili kutoka mjini, nafikiri hakukuwa na shida sisi kusoma pale kwa sababu tulikuwa ndiyo watu weusi pekee kwenye eneo lile.

Kipindi hicho wazungu wa kaskazini walikuwa na kawaida ya”kuasili” watu weusi wachache kwenye jamii yao; hawakuwaona kama kitisho. Watoto wa kizungu hawakutufanyia ubaguzi mkubwa. Walituita “nigger” “weusi” na “Rastus” mara nyingi kiasi kwamba tulidhani hayo ndiyo majina yetu ya asili. Lakini hawakusema hivyo wakiwa na lengo la kututusi, ni namna tu waliyofikiria kutuhusu.
***​
 
Sura ya kwanza inaendelea.

Mchana mmoja wa mwaka 1931; mimi, Wilfred, Hilda na Philbert tuliporudi nyumbani, tulikuta baba na mama wako kwenye moja ya mizozo yao. Siku hizo hali nyumbani ilikuwa tata sana sababu ya vitisho vya wafuasi wa Black Legion. Siku hiyo baba alikuwa amemchukua mmoja wa sungura tuliowafuga na kumwambia mama ampike. Tulifuga sungura lakini ilikuwa kwa ajili ya kuwauzia wazungu, baba alikuwa amemchukua sungura bandani na kumng’oa kichwa. Alikuwa na nguvu sana hivyo hakuhitaji kisu kutoa kichwa cha kuku au sungura. Kwa kutumia mikono yake, alinyonga na kunyofoa kichwa na kisha kutupa kiwiliwili chenye shingo inayovuja damu miguuni mwa mama.

Mama yangu alikuwa akilia. Alimchukua sungura na kuanza kumchuna, kumuandaa kwa ajili ya kumpika. Wakati huo baba naye alikuwa na hasira sana, alibamiza mlango, akatoka nje na kuanza kutembea kuelekea mjini.

Ni wakati huu ndiyo mama yangu alipata maono. Siku zote likuwa na maajabu hayo, alikuwa na uwezo wa kuhisi ujio wa jambo fulani. Na karibu watoto wake wote wako namna hiyo. Ninauwezo wa kuhisi vitu. Sikumbuki kitu kilichowahi nitokea na nisikihisi ujio wake hata kidogo-isipokuwa mara moja tu, na hiyo ilitokea miaka mingi baadaye, pale nilipogundua ukweli kumhusu mtu ambaye kabla ya kugundua ukweli huo, nilikuwa tayari kufa kwa ajili yake.

Baba yangu alikuwa ameishafika mbali mama yangu alipotoka ndani akiita. “Earl! Earl!” aliita kwa sauti kubwa. Alikunja aproni yake na kuanza kukimbia kuelekea barabarani. Baba aligeuka. Na kwa sababu anazizijua yeye, ukizingatia kuwa alitoka ndani akiwa na hasira, alipunga tu mkono na kuendelea na safari.

Mama aliniambia hapo baadaye; aliniambia kuwa alipata maono ya mwisho wa baba yangu. Mchana kutwa siku hiyo hakuwa sawa, alikuwa na wasiwasi, mwenye hasira na akilia. Alimaliza kumpika sungura yule na kumuweka kwenye sehemu yenye joto ya jiko la kupikia. Baba alipokuwa hajarudi hadi wakati wa kwenda kulala, mama alitukumbatia na kutuweka pamoja, tulihisi ni kitu cha ajabu lakini hatukujua cha kufanya maana hajawahi kufanya hivyo.

Nakumbuka niliamshwa na sauti ya mama yangu akilia kwa kelele, nilipokurupuka kwenda sebuleni, nikawakuta polisi; walikuwa wanajaribu kumnyamazisha. Alikuwa ameishavaa kwa ajili ya kwenda nao. Na watoto wote, bila ya mtu yeyote kutuambia, tulitambua kuwa baba amepatwa na jambo baya.

Mama yangu aliongozana na polisi hadi hospitali, na hadi kwenye chumba ambako baba yangu alikuwa amefunikwa shuka mwili wote kitandani. Hakuangalia, aliogopa kuangalia. Pengine kutoangalia lilikuwa ni jambo la busara. Baadaye niliambiwa kuwa kichwa cha baba yangu kilikuwa kimebonyea ndani upande mmoja. Watu weusi wa Lansing mara zote walinong’ona kuwa alivamiwa na kushambuliwa na kisha kulazwa relini ili treni ya mjini impitie. Mwili wake ulikatwa karibu nusu.

Alikaa katika hali ile kwa saa mbili na nusu. Watu weusi wa wakati huo walikuwa na nguvu kuliko wa sasa, hasa hasa wa kutoka Georgia. Iliwapasa watu weusi kutoka Georgia kuwa na nguvu ili kuishi.

Ilikuwa ni asubuhi watoto tulipopata taarifa kuwa amekufa. Nilikuwa na miaka sita, nakumbuka kuona pilikapilika na vurumai nyumbani, nyumba ikijaa watu waliokuwa wakilia na kusema maneno makali kwamba mwishowe Black legion wamempata. Mama yangu alikuwa kama kachanganyikiwa. Wanawake wenzake walikuwa wakimuwekea chumvi za kunusu puani. Hata wakati wa mazishi alikuwa bado kama kachanganyikiwa.

Sina kumbukumbu nzuri ya mazishi. Lakini ajabu ni kuwa kitu ninachokumbuka ni kuwa hayakufanyika kanisani, na hilo lilinishangaza sana maana baba yangu alikuwa mhubiri, na nilihudhuria ibada za mazishi alizoendesha kanisani. Mazishi yake yalifanyika kwenye nyumba inayotoa huduma ya mazishi.

Pia nakumbuka wakati wa mazishi, nzi mkubwa mweusi alifika na kutua usoni mwa baba yangu. Wilfred alisimama haraka na kumfukuza nzi yule. Alirudi kukaa huku machozi yakimtiririka. Tulipopita mbele ya jeneza kumuaga, nakumbuka kuona uso wenye nguvu wa baba yangu ukiwa kama umepakwa unga na nilitamani wasingempaka kwa wingi kiasi kile.

Kwa juma moja au zaidi, nyumbani kwetu kulikuwa na wageni wengi sana. walikuwa ni marafiki wema wa familia yetu, kama familia ya Lyon kutoka Mason, umbali wa maili kumi na mbili, familia ya Walker, McGuire, Liscoe, Greens, Randolph, Turner na wengine wengi kutoka Lansing na miji mingine ambao nimewahi kuwaona kwenye mikutano ya kigarvey.

Watoto tuliweza kuzoea kirahisi kufiwa kule kuliko mama yetu. Hatukuweza kuona majaribu yaliyokuwa mbele yetu kama yeye. Waombolezaji walivyozidi kupungua, ndivyo wasiwasi wake juu ya malipo ya bima mbili za maisha ambazo baba yetu alikuwa amekata ulivyozidi kumuandama. Baba yetu alikuwa anajivunia sana kuwa na bima hizo, mara zote alisema kuwa familia inatakiwa kuhakikishiwa usalama iwapo atakufa. Bima moja ililipa kwa urahisi bila shida yoyote-bima ndogo. Sijui ilikuwa ni kiasi gani. Nadhani haikuwa zaidi ya dola elfu moja, pengine nusu yake.

Lakini baada ya pesa hiyo kufika na mama kulipa gharama za mazishi na zinginezo, akaanza kufunga safari kwenda mjini na kurudi akiwa amesononeka sana. Kampuni ambayo kulikuwa na bima kubwa ilikuwa inagoma kulipa. Walikuwa wanadai kuwa baba yangu alijiua. Watu walitutembelea tena na tena; na kulikuwa na maneno makali juu ya wazungu: inawezekanaje kwa baba yangu kujipiga kichwani hadi kichwa kibonyee, kisha kwenda kwenye reli na kujilaza ili treni impitie!!?

Basi tukajikuta katika hali hiyo. Wakati huo mama yangu alikuwa na umri wa miaka thelathini na nne, bila mume, mtegemezi wala mlinzi wa watoto wake nane. Lakini baadhi ya mambo ya familia yaliendelela kwenda kama kawaida. Na kadri ambavyo pesa ile ya bima ilivyokuwepo, maisha yaliendelea vizuri.

Wilfred, ambaye alikuwa mshupavu sana, akaanza kufanya mambo kuzidi umri wake. Nafikiri alikuwa na akili ya kuona mambo ambayo wengine tulishindwa kuona, mambo yanayotunyemelea. Aliacha shule kimyakimya na kwenda mjini kutafuta kazi. Alifanya kazi yoyote aliyoweza kuipata, jioni alirudi akiwa hoi kwa kuchoka, alimpatia mama chochote alichokuwa amepata.

Hilda ambaye mara zote alikuwa mkimya naye akaanza kufanya kazi ya kulea watoto. Mimi na Philbert hatukuchangia chochote. Tulipigana muda wote nyumbani, kisha shuleni tuliungana kupigana na watoto wa kizungu. Wakati mwingine ugomvi huo wa shuleni ulichukua sura ya rangi, lakini uliweza kuwa kwa sababu yeyote ile.

Baada ya Reginald kukua kidogo, mimi ndiye nikawa mlezi wake. Tukatokea kuwa karibu sana. Nadhani nilifurahia kuwa na mtu aliyekuwa akinitegemea.

Mama yangu akaanza kununua vitu kwa mkopo. Siku zote baba yangu alikuwa akipinga sana kukopa, alisema mikopo ni mwanzo wa kurudi utumwani. Baadaye naye akatafuta kazi. Alienda Lansing na kutafuta kazi tofautitofauti kwa wazungu, kazi za ndani au za kushona. Mara nyingi hawakutambua kuwa ni mtu mweusi. Wazungu wengi wa maeneo yale hawakutaka mtu mweusi kuingia kwenye nyumba zao.

Alifanya kazi bila matatizo mpaka pale ilipojulikana yeye ni nani, mjane wa nani. Hapo alifukuzwa kazi. Nakumbuka jinsi alivyokuwa akirudi nyumbani akilia kwa kupoteza kazi aliyoihitaji sana, lakini alilia kwa kificho tusigundue.

Wakati fulani, mmoja wetu-sikumbuki ni nani, kwa sababu fulani alienda mahali anakofanya kazi mama yetu. Watu walipomuona mtoto wake wakatambua kuwa ni mtu mweusi. Alifukuzwa kazi hapohapo, alirudi nyumbani akilia, siku hiyo hata hakujificha.

Watu wa ustawi wa jamii wakaanza kututembelea, wakati mwingine tulipotoka shuleni tuliwakuta wakiongea na mama yetu. Kwa jinsi walivyotenda; walivyomuangalia mama yetu, walivyotuangalia sisi na nyumba kwa ujumla, ilikuwa ni kama hatukuwa watu. Kwenye macho yao tulikuwa vitu tu.

Mama akaanza kupata malipo mawili. Moja ni kutoka ustawi wa jamii, na ya pili nafikiri yalikuwa malipo ya ujane. Lakini yalikuwa hayatoshi, maana tulikuwa wengi. Pesa hizo zilitoka mwanzoni mwa mwezi, karibu mara zote malipo ya kwanza yaliishia kulipa madeni tuliyodaiwa dukani, na bado wakati mwingine hazikuyamaliza. Pesa iliyobaki nayo haikukaa sana.

Polepole hali ya maisha ikaanza kuwa duni. Lakini kushuka kwa maisha hakukuwa kwa kasi kama kulivyokuwa kudhoofika kisaikolojia. Mama yangu alikuwa ni mwanamke anayejiheshimu sana, ilimharibu sana kisaikolojia kuona kuwa anategemea msaada. Na tuliliona jambo hilo.

Alizungumza na muuza duka kwa ukali alipokuwa akipiga hesabu, akimwambia kuwa hakuwa mjinga. Muuza duka hakupendezwa na hilo. Angeweza pia kujibizana na watu wa ustawi wa jamii, akiwaambia kuwa alikuwa ni mtu mzima anayeweza kulea watoto wake, na kuwa hakukuwa na umuhimu wa wao kuja mara kwa mara na kuingilia maisha yetu. Nao hawakupendezwa na hilo.

Lakini malipo ya msaada ya kila mwezi tuliyopata ndiyo yalikuwa tiketi yao. Walikuwa ni kama wanatumiliki, ni kama vile tulikuwa mali yao binafsi. Mama yangu alipenda sana wasije, lakini haikuwezekana. Alikuwa akichukia zaidi walipokuwa wakituchukua watoto wakubwa pembeni na kuanza kutuuliza maswali. Wakituambia vitu dhidi ya mama yetu na dhidi ya sisi kwa sisi.

Hatukufahamu ni kwa nini alionyesha kuchukia kupokea vitu kutoka serikalini, serikali ilikuwa tayari kutupatia nyama, viroba vya viazi na vyakula vingine vya kila aina. Hatukuelewa kabisa. Nilichokuja kuelewa baadaye ni kuwa mama yangu alikuwa akijitahidi awezavyo kulinda heshima yake na yetu.

Heshima ilikuwa ndiyo kitu pekee tulichobakiwa nacho maana kufikia mwaka 1934 mateso yakaanza. Mwaka huo kulikuwa na mdororo mbaya sana wa uchumi, na hakuna hata mmoja tuliyemjua aliyekuwa na chakula cha kutosha. Marafiki fulani wa familia walitutembelea hapa na pale. Mwanzoni walikuwa wakituletea chakula, japo ilikuwa ni msaada, mama yangu alipokea. Wilfred alikuwa akifanya kazi na kusaidia familia, mama naye alifanya kazi yoyote aliyopata. Lansing kulikuwa na kiwanda cha mikate. Watoto tulikuwa tukienda kununua mikate na biskuti za jana za kuweza kujaza mfuko wa unga kwa pesa chache sana, kisha tukatembea umbali wa maili mbili kurudi nyumbani kijijini. Nafikiri mama yangu alijua njia kadhaa za kupika mkate na vitu vingine. Aliweza pika chachandu ya nyanya na mkate na ukawa mlo, kifupi ni kuwa aliweza kutoa karibu kila mlo kwa kutumia mkate. Biskuti ambazo mara zote tulikuja nazo, zililiwa kama zilivyo.

Lakini kuna wakati hatukuwa hata na senti, hapo tulipigwa na njaa hadi kupatwa na kizunguzungu. Nyakati hizo mama alichemsha mboga nyingi za majani na tukala. Nakumbuka watoto na baadhi ya majirani wenye akili fupi walikuwa wakitutania kuwa tulikula nyasi za kukaanga. Nyakati nyingine tukiwa na bahati tulikula mara tatu kwa siku, hasa mlo wa shayiri au mahindi.

Mimi na Philbert tulikuwa tumekua vya kutosha kuacha kupigana, na tulikuwa warefu wa kuweza kubeba bunduki ya baba na kwenda kuwinda sungura ambao majirani zetu wazungu walinunua. Sasa ninafahamu kuwa walifanya hivyo ili kutusaidia tu maana na wao waliwinda sungura wao wa kula kama watu wengine wote. Nakumbuka mimi na Philbert tukimchukua Reginald tunapokwenda kuwinda. Hakuwa na nguvu, lakini mara zote alifurahia kuongozana nasi. Tulitega aina fulani ya panya kwenye korongo nyuma ya nyumba yetu. Pia tulikuwa tukiwinda vyura, tulijificha mpaka vyura walipotokea, hapo tuliwapiga mikuki na kisha kuwakata miguu na kuwauza kwa jirani zetu. Wazungu walionekana kutojali sana juu ya wanachokula.

Kama nakumbuka vizuri, mwishoni mwa mwaka 1934 kuna kitu kikaanza kutokea. Familia yetu ikaanza kudhoofika kisaikolojia na kujiheshimu kwetu kukaanza kuathirika. Pengine ni sababu ya ushahidi wa wazi uliokuwepo kuwa tulikuwa masikini wa kutupwa. Tulifahamu juu ya familia zingine ambazo zilienda kukinga chakula cha msaada. Kila mtu kwenye familia yetu alijivuna kwa kuwa sisi hatukwenda kukinga chakula cha bure, japo hakuna aliyesema hilo. Sasa na sisi tukaanza kwenda kukinga chakula cha msaada. Na sisi tukaanza kunyoshewa vidole shuleni kuwa tulikuwa tunakinga chakula cha msaada, na wakati mwingine tulitaniwa waziwazi.

Ilionekana kama kila kitu tulichokula nyumbani kilikuwa na mhuri uliosema Hakiuzwi. Vyakula vyote vya msaada vilikuwa na mhuri huu ili kuzuia watu kuviuza. Ni ajabu hatukuwahi kufikiria kuwa Hakiuzwi linaweza kuwa jina la bidhaa.

Wakati mwingine, badala ya kurudi nyumbani kutoka shuleni, nilitembea umbali wa maili mbili kwenda Lansing. Nilianza kushinda nje ya maduka ambako vitu kama matufaa viliwekwa, nilikaa nikiangalia nafasi ya kuiba chochote cha kula.

Pia nilianza kutembelea nyumba za watu tuliofahamiana nao wakati wa chakula cha usiku. Nilifahamu kuwa walifahamu nipo pale kwa ajili gani, lakini hawakuwahi kuniabisha kwa kusema hilo. Walinialika kupata chakula cha usiku nami nilikula nikashiba.

Hasa hasa nilipenda kwenda kwenye familia ya Gohannase. Walikuwa ni wazee wakarimu na wachamungu wazuri. Niliwahi waona wakiongoza urukaji na kupiga kelele wakati baba yangu alipokuwa akihubiri. Walikuwa wakiishi na mpwa wao ambaye tulizoea kumwita Bonge, mimi na bonge tulielewana vizuri sana. Pia waliishi na bibi mmoja aliyeitwa bibi Adcock, walihudhuria kanisani pamoja na bibi huyu. Mara zote bibi huyu alikuwa akijaribu kumsaidia mtu yeyote yule kadri alivyoweza. Alimtembelea kila mtu aliyesikia kuwa ni mgonjwa, akimbebea zawadi mbalimbali. Miaka kadhaaa baadaye aliniambia kitu ambacho nakikumbuka mpaka leo, aliniambia: “Malcom nakupendea kitu kimoja. Wewe ni mjeuri lakini haujifichi. Wewe si mnafiki.”

Kadri nilivyozidi kuwa mbali na nyumbani, nikitembelea watu na kuiba madukani, ndivyo nilivyozidi kuwa mjeuri. Sikuwa na subira juu ya kitu chochote.

Nilikuwa nakua kwa kasi sana, kimwili zaidi kuliko kiakili. Nilivyozidi kufahamika mjini, nikaanza kutambua mtazamo waliokuwa nao wazungu kunielekea. Nilihisi hilo lilihusiana kwa namna fulani na baba yangu. Walionyesha kile ambacho watoto wakizungu walikizungumza shuleni waziwaziwali au kwa kugusia, na lilionyesha kuwa wazazi wao waliongea kuwa Black Legion au KKK ndiyo walimuua baba yangu na kuwa shirika la bima lilicheza mchezo mchafu kwa kukataa kumlipa mama yangu pesa aliyostahili.

Nilipozidi kukamatwa nikiiba vitu, ndivyo watu wa ustawi wa jamii walivyozidi kunitilia maanani sana walipokuja kututembelea. Sikumbuki ni lini mara ya kwanza walipongelea juu ya kunihamisha. Ninachokumbuka ni mama yangu kuzua mzozo akisema kuwa anaweza kulea watoto wake mwenyewe. Alinichapa kutokana na wizi wangu, nami kama kawaida nilipiga kelele ili majirani wote wasikie. Kitu kimoja ninachojivunia ni kuwa sikuwahi kuinua mkono dhidi ya mama yangu.

Wakati wa majira ya joto, mbali na mambo mengine tuliyofanya, baadhi ya wavulana tulikuwa tunakwenda kuiba(ku-coon) matikiti maji. Siku zote matikiti maji yalihusianishwa na watu weusi. Wazungu waliwaita watu weusi “Coons.” Basi kitendo cha kwenda kuiba matikiti maji kiliitwa cooning. Iwapo watoto wa kizungu wangekutwa wanaibwa matikiti, wangesemwa kuwa wanafanya mambo kama watu weusi. Siku zote wazungu wameficha au wamehalalisha hatia zao kwa kuwatania au kuwasingizia watu weusi.

Nakumbuka usiku mmoja wa sikukuu ya Halloween, tulienda kupindua vile vyoo vya kizamani vilivyokuwa mashambani. Mkulima mmoja-nadhani naye ndiyo ulikuwa mchezo wake utotoni-akawa ametutegea mtego. Kawaida tulinyata kutokea nyuma ya choo, kisha kwa pamoja tunakisukuma na kukiangusha. Mkulima huyu alikuwa amesogeza choo chake na kukiweka mbela ya shimo. Basi tukatokea nyuma tukinyemelea tukiwa tumejipanga mstari, usiku wa giza nene. Wavulana wawili wa kizungu waliokuwa mbele wakatumbukia ndani ya shimo la choo, kinyesi kikiwafika shingoni. Walinuka vibaya sana, tulichoweza kuvumilia ni kuwatoa tu shimoni, na huo ukawa mwisho wa Halloween. Ilikuwa kidogo na mimi nitumbukie lakini wazungu walikuwa wanapenda sana kuongoza, wakati huu hilo liliwapeleka shimoni.

Nilijifunza vitu vingi hapa na pale, nilichuma matunda ya Strawberries sikumbuki nilipata kiasi gani kwa kreti moja, nakumbuka siku moja baada ya kufanya kazi kwa siku nzima, niliondoka na kama dola moja, kiasi ambacho kilikuwa kikubwa sana wakati huo. Nilikuwa na njaa sana hadi sikujua cha kufanya. Nilianza kutembea kuelekea mjini kwa matumaini ya kununua chakula kizuri. Njiani nikakutana na mvulana wa kizungu aliyekuwa mkubwa kidogo, nilimfahamu, alikuwa ni Richard Dixon. Alinifuata na kuniuliza iwapo nilitaka kucheza kamari, alikuwa na sarafu nyingi. Baada ya kama nusu saa akawa amenila dola yangu. Badala ya kuelekea mjini kununua kitu cha kula, nikarudi nyumbani mikono mitupu, nilihisi uchungu sana. Lakini uchungu huo haukuwa mkali kama niliopata baada ya kugundua kuwa alikuwa amedanganya. Kuna namna ya kushika sarafu na kufanya iangukie upande unaotaka. Hilo ndilo lilikuwa somo langu la kwanza kuhusu kamari: kama ukiona mtu anashinda mara zote, jua kuwa hachezi kamari, anadanganya. Baadaye maishani, kama nilikuwa ninaliwa tu kwenye kamari, nilichunguza kwa makini sana. Ni kama tu mtu mweusi wa Marekani anavyomuona mtu mweupe akishinda kila wakati. Ni nguli wa kucheza kamari; karata nzuri na ushindi wote uko upande wake huku sisi akitupatia magarasa.

Wakati huu mama yangu alianza kutembelewa na wasabato waliokuwa wamehamia nyumba iliyokuwa si mbali kutoka kwetu. Wakati mwingine walizungumza naye kwa saa kadhaa na kisha kumuachia majarida ya kusoma. Aliyasoma. Wilfred, ambaye sasa alikuwa amerudi shule baada ya kuwa tumeanza kupata chakula cha msaada, naye aliyasoma sana. Alipenda sana kusoma vitabu.

Haikuchukua muda mrefu mama yangu akawa akitumia muda mwingi pamoja na wasabato. Naamini kilichomvutia zaidi kwa wasabato ni jinsi walivyo na masharti mengi juu ya vyakula kuliko hata yeye mwenyewe aliyoyafuata na kutufundisha. Kama sisi tu; ilikuwa haramu kwao kula sungura na nguruwe; walifuata sheria za Musa kuhusu chakula. Hawakula mnyama yeyote ambaye kwato zake hazikugawanyika mara mbili au asiyecheua. Tulianza kwenda na mama kwenye mikutano ya wasabato iliyofanyika mbali kijijini. Kwa sisi watoto, kilichotuvutia zaidi ni chakula kizuri walichoandaa. Lakini tulisikiliza mafundisho pia. Kulikuwa na watu weusi kadhaa kutoka miji midogo ya karibu, lakini naweza kusema kuwa asilimia tisini na tisa ya waumini walikuwa wazungu. Wasabato waliamini kuwa tulikuwa tukiishi katika siku za mwisho, kwamba dunia itafika mwisho karibuni. Walikuwa ni wazungu wenye urafiki kuliko wote niliowahi kukutana nao. Watoto tulitambua hilo, na tulipofika nyumbani tulijadiliana kuwa kwa namna fulani walikuwa tofauti na sisi-kwa mfano vyakula vyao havikuwa na viungo vya kutosha kama vyetu na harufu yao ilikuwa tofauti na yetu.

****​
 
Wakati huohuo watu wa ustawi wa jamii walizidi kumuandama mama yangu. Kufikia wakati huo mama hakufanya siri tena kuwa anawachukia na hakuwataka nyumbani kwake. Lakini walihakikisha wanatumia haki yao ya kuja, na mara nyingi nimetafakari jinsi ambavyo kwa kuongea na sisi watoto, walikuwa wakipanda mbegu ya utengano ndani yetu. Waliuliza maswali kama vile ni nani mwenye akili kuliko wote, na waliniuliza kwa nini nilikuwa tofauti sana na wengine.

Nafikiri walihisi kuwa kuwapeleka watoto kwenye nyumba za malezi ndiyo kazi yao kuu.

Mama yangu alipopambana nao, nao walipambana naye-hasa kupitia mimi. Nilikuwa ndiye silaha yao ya kwanza. Nilikuwa mwizi, hilo lilimaanisha kuwa mama yangu hakunipa mahitaji ya kutosha.

Watoto wote tulikuwa watundu wa hapa na pale. Mimi nikiwa mtundu kuliko wote. Pia mimi na Philbert hatukuisha kugombana, na hili lilikuwa ni moja ya mambo yaliyomhangaisha sana mama yetu.

Sikumbuki ni lini na wapi wafanyakazi wa ustawi wa jamii walitoa wazo kuwa mama yangu alikuwa anapoteza uwezo wake wa akili. Lakini nakumbuka vizuri wakimwita “Kichaa” walipopata habari kuwa mkulima mmoja mweusi aliyekaa si mbali toka nyumbani kwetu, alitaka kutupatia nyama ya nguruwe-nguruwe mzima, pengine wawili lakini mama yetu alikataa. Wote tulisikia wakimwita mama yetu “kichaa” kwa kukataa nyama nzuri kabisa. Hawakuelewa kitu hata alipowaeleza kuwa hatujawahi kula nguruwe, na kwamba ilikuwa ni kinyume cha dini yake ya Kisabato.

Walikuwa wakatili kama wanyama. Hawakuwa na hisia, uelewa, huruma wala heshima kwa mama yangu. Walituambia, “Mama yenu ni kichaa kwa kukataa chakula.” Hapo ndipo familia yetu ilipoanza kuparanganyika. Tulikuwa na wakati mgumu sana, na tabia yangu ilizidisha ugumu wa mambo. Lakini pamoja na hayo tungeweza kuyashinda, tungeweza kuendelea kubaki kama familia. Nilimpenda mama yangu pamoja na ujeuri wangu na matata yote niliyomletea.

Tulikuja gundua kuwa watu wa ustawi wa jamii wameongea na familia ya Gohannase nayo ikawa imekubali kuishi nami. Mama yangu aliposikia hilo alifoka sana na wale wavunja familia wakapotea kwa muda.

Kipindi hicho ndipo mwanaume mmoja mrefu na mweusi kutoka Lansing alipoanza kututembelea mara kwa mara. Sikumbuki ni lini na wapi walikutana na mama yangu. Pengine itakuwa kupitia marafiki wao. Sikumbuki taaluma ya mtu yule. Mwaka 1935 watu weusi wa Lansing hawakuwa na chochote cha kufanya unachoweza kuita taaluma. Lakini mwanaume yule, mkubwa na mweusi, alifanana sana na baba yangu. Sikumbuki jina lake, lakini hakuna ulazima wa kulitaja hapa. Alikuwa ni mseja, na mama yangu alikuwa mjane wa miaka thelathini na sita. Mtu yule alikuwa anajiamini sana, na hilo lilimvutia mama yangu. Alikuwa na wakati mgumu sana kushughulika na tabia zetu hivyo uwepo tu wa mwanaume mwenye mwili mkubwa ungesaidia. Na kama mama akiwa na mwanaume wa kutunza familia, watu wa ustawi wa jamii hawataonekana tena.

Wote tulielewa kinachoendelea bila hata ya kukiongelea au walau hatukuwa na pingamizi. Na hata tuliongea kati yetu kuwa mwanaume yule alipofika, mama yetu alivalia nguo zake nzuri kabisa kuonyesha kuwa bado alivutia-ukweli ni kuwa alikuwa bado ni mwanamke mwenye kuvutia, pia tabia yake ilikuwa tofauti. Mpole na mwenye kicheko kuliko tulivyomzoea kwa miaka kadhaa.

Uhusiano wao ulidumu kama mwaka hivi kisha mnamo 1936 au 1937 mtu yule akamuacha mama yangu ghafla. Aliacha tu kuja kumtembelea. Kutokana na nilivyokuja kuelewa baadaye ni kuwa alikimbia majukumu ya kulisha watoto nane. Aliogopa wingi wetu. Hadi leo naona mtego ambao mama yetu alikuwemo kwa kuwa nasi. Pia naelewa kwa nini mtu yule alikimbia mzigo mzito namna ile.

Lakini jambo lile lilimshtua vibaya sana mama. Kwake ulikuwa ni mwanzo wa mwisho wa maisha halisi. Ilituogopesha sana alipoanza kukaa au kutembea huku akiongea peke yake kama vile haoni uwepo wetu.

Watu wa ustawi wa jamii waliona jinsi alivyokuwa akidhoofika. Hapo ndipo walipochukua hatua ya kunihamisha nyumbani. Walianza kuniambia jinsi itakavyokuwa vizuri nikienda kuishi na familia ya Gohannase, kuwa bibi na bwana Gohannase, Bonge na bibi Adcock wote wamesema wananipenda na wangependa niishi nao.

Nami niliwapenda wote, lakini sikutaka kutengana na Wilfred. Nilimpenda na kumtegemea kaka yangu huyo mkubwa. Sikutaka kutengana na Hilda ambaye alikuwa kama mama yangu wa pili. Hata Philbert sikutaka kutengana naye, pamoja na kupigana mara kwa mara bado kulikuwa na upendo wa kindugu kati yetu. Au kutengana na Reginald aliyekuwa dhaifu kutokana na ugonjwa wake wa ngiri, ambaye aliniangalia kama kaka yake mkubwa na alitegemea niwe mlezi wake, kama tu nilivyomtegemea Wilfred. Na niliwapenda pia wadogo zangu, Yvonne, Wesley na Robert.

Kadri mama yetu alivyozidi kuongea peke yake ndivyo alivyozidi kutokutujali na kupuuza majukumu yake. Nyumba ilianza kuwa chafu nasi pia tukaanza kuwa wachafu. Na sasa ikawa ni kawaida kwa Hilda kupika.

Watoto tulishuhudia polepole nguzo yetu ikiteketea. Ilikuwa ni kitu kibaya sana, kitu usichoweza kukishika lakini huwezi kukiepuka. Kulikuwa hisia za kuwa kuna kitu kibaya kinaenda kutokea. Tuliokuwa wadogo tukaanza kuwategemea zaidi na zaidi Wilfred na Hilda ambao walikuwa ndiyo wakubwa na walau walionekana wapo imara.

Mwishowe nilipopelekwa kwenda kuishi na familia ya Gohannase, walau kijuujuu nilifurahia. Nakumbuka nilipotoka nyumbani nikiwa na mtu wa ustawi wa jamii, mama yangu alisema kitu kimoja; “Usiwaruhusu walimshe nguruwe hata kidogo.”

Kwenye familia ya Gohannase hali yangu ilikuwa bora kwa kila Nyanja. Mimi na Bonge tulilala chumba kimoja na tulielewana sana, ni vile tu hakuwa ndugu yangu wa damu. Watu wa familia ya Gohannase walikuwa watu wa dini sana. Mimi na Bonge tulienda kanisani pamoja nao. Wakati huo walishakuwa walokole kindakindaki. Wahubiri na kanisa zima walikuwa wakipiga kelele na kuruka kuliko Wabaptisti niliowazoea. Waliimba kwa sauti yao yote, na kulia, na kuunguruma na kutingisha vichwa huku na kule.

Bwana na bibi Gohannase na bibi Adcock walipendelea sana kwenda kuvua samaki. Baadhi ya jumamosi, mimi na Bonge tuliambatana nao. Nilikuwa nimehama shule na kuhamia Lansing’s West Junior High School. Ilikuwa katikati ya makazi ya watu weusi, lakini kulikuwa na wanafunzi wachache wa kizungu. Bonge na mimi hatukujichanganya sana na wanafunzi wengine. Tulipoenda kuvua, mimi na Bonge hatukufurahia kitendo cha kukaa kusubiria samaki anase na kuvuta kamba. Nilifikiri kuwa lazima kutakuwa na njia nyingine nzuri zaidi ya kufanya uvuvi, lakini sijawahi igundua.

Bwana Gohannase alikuwa na marafiki zake ambao baadhi za jumamosi walituchukua mimi na Bonge kwenda kuwinda sungura. Nilikuwa na bunduki ya baba, mama alikuwa ameniruhusu kuondoka nayo. Wazee wale walikuwa na mbinu yao ya kuwinda sungura ambayo waliitumia siku zote. Kwa kawaida, iwapo sungura alishambuliwa na mbwa na akafanikiwa kuponyoka, basi sungura yule atakimbia na mwishowe kurudi eneo lilelile aliloshambuliwa. Basi wazee wale walijificha na kusubiria sungura arudi na kumpiga risasi. Nilifikiria hiyo mbinu yao kisha nikapata wazo. Niljitenga nao na kukaa sehemu ambayo nilijua kuwa sungura atapita wakati wa kurudi.

Ilifaa sana, nilikuwa naua sungura watatu hadi wanne kabla wao hawajapata hata mmoja. Ajabu ni kuwa hakuna aliyegundua mbinu yangu. Walinisifu sana kuwa nina shabaha. Wakati huo nilikuwa kama na miaka kumi na miwili hivi. Nilichofanya ilikuwa ni kuboresha tu mbinu yao na huo ulikuwa mwanzo wa somo zuri sana maishani-kwamba, mara zote unapomuona mtu amefanikiwa zaidi yako, hasa kama mnafanya kazi ya aina moja-basi jua kuwa kuna kitu anakifanya na wewe hukifanyi.

Nilirudi nyumbani mara nyingi kusalimia. Wakati mwingine nilikwenda na Bonge au na mmoja wa Gohannase, na wakati mwingine peke yangu. Nilifurahi nilipoambatana na mmoja wao, ilifanya hali iwe rahisi kiasi.

Haukupita muda watu wa ustawi wa jamii wakaanza mipango ya kuchukua watoto wote kutoka kwa mama yangu. Sasa alikuwa akiongea peke yake karibu wakati wote, na wazungu, wengine kabisa-wakaanza kumzonga na kuuliza maswali ya kila aina. Na wakati mwingine walinitembelea na mimi nilikoishi. Walikaa na mimi kibarazani au kwenye gari lao na kunihoji maswali.

Mwishowe mama yangu akachanganyikiwa kabisa. Na mahakama ikatoa uamuzi wa mwisho. Walimpeleka kwenye hospitali ya magonjwa ya akili ya jimbo iliyokuwa huko Kalamazoo.

Kalamazoo ilikuwa umbali wa kama maili sabini hivi kutoka Lansing, mwendo wa karibu saa moja na nusu kwa basi. Jaji McClellan wa Lansing ndiye alikuwa na mamlaka juu yangu na ndugu zangu. Tulikuwa watoto wa “serikali”. Alikuwa ndiye mwenye kauli ya mwisho kutuhusu. Mzungu kuwa msimamizi wa watoto wa mtu mweusi! Si kitu kingine bali utumwa wa kisasa uliohalalishwa kisheria-haijalishi kuwa lengo lake ni zuri.

***​
 
Mama yangu aliendelea kuishi kwenye hospitali ileile ya Kalamazoo kwa kama miaka ishirini na sita. Nilimtembelea mara nyingi nilipokuwa naendelea kukua huko Michigan. Nafikiri hakuna kitu kilichoweza kunihuzunisha kama kumuona katika hali ile. Mwaka 1963 tulimtoa mama yetu hospitali na sasa anaishi Lansing pamoja na familia ya Philbert.

Pengine ingekuwa afadhali angepatwa na ugonjwa wa kawaida ambao unajulikana chanzo chake, dawa zake zipo na kupona kunawezekana. Kila mara nilipomtembelea na kuona akirudishwa ndani, kwao akiwa si kitu bali mgonjwa kama wagonjwa wengine tu- nilijisikia vibaya sana.

Mara ya mwisho kumtembelea, na siku nilipojua kuwa sitamtembelea tena ilikuwa ni mwaka 1952. Nilikuwa na umri wa miaka ishirini na saba. Philbert alikuwa ameniambia kuwa mara ya mwisho alipomtembelea hakumtambua vizuri. Lakini mimi hakunitambua kabisa. Alinishangaa tu akiwa hajui anaongea na nani. Nilijaribu kuongea naye lakini akili yake ilikuwa mbali kabisa. Niliuliza, “Mama unafahamu leo ni siku gani?”

Alijibu huku akishangaa, “Watu wote wameondoka.”

Siwezi kueleza jinsi nilivyohisi. Mwanamke aliyenileta duniani na kunilea, na kunifundisha, na kunirekebisha na kunipenda alikuwa hanifahamu. Ilikuwa ni kama najaribu kupanda mlima wa manyonya. Nilikaa tu nikimuangalia na kusikiliza aliyosema. Kulikuwa hakuna kingine cha kufanya.

Niliamini kabisa kuwa iwapo idara ya ustawi wa jamii huharibu familia, basi imeharibu yetu. Tulitamani na tulijaribu tuwezavyo kubaki pamoja. Hakukuwa na haja ya kuvunja nyumba yetu. Lakini ustawi wa jamii, mahakama na madaktari wao hawakujali hayo. Na sisi hatukuwa wa kwanza kupatwa na hayo.

Nilifahamu kuwa sitarudi tena kumtembelea mama yangu sababu hilo lingenifanya kuwa mtu mwenye hasira na hatari sana-nikifahamu kuwa sisi tulikuwa tarakimu tu kwenye vitabu vyao, si binadamu. Na nikifahamu kuwa mama yangu alikuwa takwimu tu mle hospitali, na hakupaswa kuwa mle isipokuwa sababu ya kushindwa kwa jamii, unafiki, ulafi na ukosefu wa rehema na huruma. Matokeo yake, ndani yangu nimekosa kabisa rehema na huruma kwa jamii ambayo inakandamiza watu na kisha inawashtaki kwa kushindwa kusimama sababu ya uzito.

Ni mara chache sana huongea na watu kuhusu mama yangu, maana ninaamini kuwa nina uwezo wa kumuua bila kusita mtu yeyote ambaye atamzungumzia mama yangu kwa ubaya. Kwa hiyo naogopa kuweka shimo ambalo mpumbavu fulani ataingia.

Wakati familia yetu inasambaratishwa, mwaka 1937, Hilda na Wilfred walikuwa wamekuwa watu wazima hivyo serikali iliwaacha wabaki kwenye nyumba yetu. Philbert alipelekwa kuishi na familia moja huko Lansing, familia ya bibi Hackett. Reginald na Wesley walikwenda kuishi na familia ya William ambao walikuwa ni marafiki wa mama. Yvonne na Robert walikwenda kuishi na familia ya Wamarekani Weusi wa kutoka visiwa vya Karibeani, familia ya McGuire.

Japo tulikuwa tumetenganishwa lakini sote tuliendelea kudumisha ukaribu wetu kupitia shuleni na kwa namna yoyote tuliyoweza kukutana. Pamoja na utengano uliotengenezwa na umbali uliokuwepo kati yetu, bado tuliendelea kuwa na ukaribu wa kihisia kati yetu.
 
SURA YA PILI

KIKARAGOSI

Mnamo tarehe ishirini na saba mwezi wa sita 1937, Joe Louis alimpiga James J. Braddock na kuwa bingwa wa dunia wa uzito wa juu. Watu weusi wote wa Lansing, kama ilivyokuwa kwa watu weusi wa kila mahali, walilipuka kwa furaha na kujivunia mafanikio ya mtu mweusi mwenzao ambayo hayajawahi tokea katika kizazi chetu. Kila mtoto mweusi alitamani kuwa Joe Louis ajaye. Kaka yangu Philbert ambaye tayari alikuwa mwanamasumbwi mzuri wakati anasoma, naye alikuwa kwenye mkumbo huo(Mimi nilitaka kuwa mcheza mpira wa kikapu, nilikuwa mrefu lakini sikuwa mchezaji mzuri). Wakati wa majira ya kiangazi mwaka huo, Philbert aliingia kwenye mashindano ya vijana yaliyofanyika ukumbi wa Prudden huko Lansing.

Alifanya vizuri. Akipita michujo mingi migumu. Nilikuwa nikienda kwenye ukumbi wa mazoezi kumtazama akijifua. Ilikuwa inachangamsha sana kumuona akijifua. Pengine bila ya mimi mwenyewe kujua, nikaanza kumuonea wivu. Kitu kimoja ambacho sikutaka kuona, ni kuona mdogo wangu Reginald anaacha kunikubali na kuanza kumkubali Philbert.

Watu walikuwa wakimsifu Philbert kuwa amezaliwa kuwa mwanamasumbwi. Kwa vile tulikuwa tumezaliwa katika familia moja, niliona kuwa nami pia nimezaliwa kuwa mwanamasumbwi. Basi nami nikaingia ulingoni. Nafikiri nilikuwa na miaka kumi na tatu nilipopambana pambano langu la kwanza, urefu na mwili wangu ulinifanya niweze kudanganya kuwa nina miaka kumi na sita, umri wa chini ulioruhusiwa, na uzito wangu wa kilo 58 ulinifanya niingie uzito wa bantam.

Walinipambanisha na mvulana wa kizungu ambaye alikuwa ndiyo anaanza kama mimi, jina lake Bill Peterson. Sitakaa nimsahau. Ilipofika zamu yetu ya kupambana, kaka zangu na dada zangu wote walikuja kushuhudia, pamoja na wote niliowafahamu mjini pale. Hawakuja kwa sababu yangu, walikuwa wamekuja kumtazama Philbert ambaye tayari alikuwa ameanza kujizolea mashabiki, hivyo walitaka kuona mdogo wake naye yukoje.

Nilitembea katikati ya watu waliokaa na kuingia ulingoni. Tulitambulishwa na muamuzi na kisha akatuasa yote juu ya kanuni za mchezo. Kengele ikalia na tutatoka kwenye kona zetu. Nilikuwa naogopa, lakini sikujua, mpaka Bill aliponiambia hapo baadaye kuwa naye alikuwa akiniogopa. Alikuwa anaogopa sana kuwa nitamuumiza hivyo akajiandaa kupambana hasa.

Alinipiga kiasi kwamba nikalazimika kujificha kwa muda. Mtu mweusi hawezi kupigwa na mzungu kisha akabakia na heshima yake mtaani kwake, hasa wakati huo ambao michezo na sanaa ndizo kazi pekee ambazo mtu mweusi angeweza kufanya, wakati ambao ni ulingoni tu mtu mweusi aliweza kumpiga mzungu bila ya umati kumshukia na kumuua. Nilipoonyesha uso wangu tena, watu weusi niliofahamiana nao walinidhihaki vibaya sana, nilijua kuwa kuna kitu natakiwa kufanya.

Lakini aibu yangu kubwa zaidi ilikuwa kutokana na mtazamo wa mdogo wangu Reginald: hakuongelea hata mara moja pambano lile. Ilikuwa ni jinsi alivyoniangalia na kukwepa kuniangalia. Basi nilirudi kufanya mazoezi kwa nguvu sana, nilipiga ngumi gunia la mazoezi na kuruka kamba, nilihema na kuvuja jasho kila sehemu. Mwishowe nikajiandikisha kupigana na Bill Peterson kwa mara nyingine. Safari hii pambano lilifanyika kwenye mji wake wa Alma, Michigan.

Jambo pekee zuri katika mechi ile ya marudioano ni kuwa kulikuwa hakuna yeyote niliyemfahamu kuishuhudia. Nilifurahia zaidi kutokuwepo kwa Reginald. Mara tu kengele ilipolia niliona ngumi, na sekunde kumi baadaye nikasikia muamuzi akinihesabia “Kumi!” Pengine lilikuwa pambano fupi zaidi katika historia. Nililala nikisikiliza akihesabu hadi mwisho lakini sikuweza hata kujisogeza. Kusema ukweli sina hakika kama nilitaka kujisogeza.

Bill Peterson ndiye alikuwa mwanzo na mwisho wangu wa kuwa mwanamasumbwi. Mara nyingi tokea nimekuwa muislamu, nimefikiria juu ya pambano lile na nimeona kuwa ilikuwa ni kazi ya Allah kunizuia: pengine ningekuwa mpigwaji tu.

Muda mfupi baada ya matukio hayo nikaanza kuingia darasani nikiwa nimevaa kofia. Mwalimu wangu, ambaye alikuwa ni mzungu, aliniamuru nizunguke darasani mara nikiwa na kofia yangu hadi atakaponiambia basi. Alisema kwa kufanya hivyo,”Kila mtu ataniona. Na wao kuendelea na darasa kwa wale waliokuja kuifunza.”

Nikiwa bado naendelea kutembea kuzunguka darasa, mwalimu yule akawa amesimama na kwenda kuandika kitu fulani ubaoni. Kila mtu darasani aliona nilipopita nyuma ya dawati lake na kuchukua kipini cha kubania vitu ubaoni na kuweka kwenye kiti chake. Aliporudi kukaa, nilikuwa tayari nipo mbali na eneo la tukio, nyuma ya darasa nikiendelea kuzunguka. Akakalia kipini! Nilimsikia akipiga kelele na kuruka, wakati huo natokomea mlangoni.

Kutokana na historia ya tabia yangu, sikushtuka niliposikia kuwa nimefukuzwa shule.

Nadhani nilikuwa na wazo kuwa kama sitakuwa naenda shule basi nitaruhusiwa kuendelea kuishi na familia ya Gohannase, nikizunguka huku na kule mjini ninavyotaka, au labda kupata kazi ya kunipatia pesa ya matumizi. Lakini niliistaajabu sana mtu wa serikali ambaye sikuwahi kumuona, alipofika na kunichukua mpaka mahakamani.

Waliniambia kuwa wananipeleka shule ya watoto watukutu. Nilikuwa bado na miaka kumi na tatu.

Kwanza kabisa walinipeleka kwenye makazi ya mahabusu iliyokuwa huko Mason, Michigan. Umbali wa maili kumi na mbili kutoka Lansing. Makazi hayo ya mahabusu ndiko ambako watoto wote watukutu kutoka wilaya ya Ingham waliwekwa kabla ya kupelekwa kwenye shule za watoto watukutu.

Bwana yule wa serikali-mzungu aliyeitwa Maynard, alikuwa mkarimu kwangu kuliko mtu yeyote wa ustawi wa jamii niliyewahi kushughulika naye. Hata alijaribu kuwapooza moyo bwana na bibi Gohannase, bibi Adcock na Bonge. Wote walikuwa wanalia lakini mimi nilikuwa mkavu. Niliweka nguo chache nilizokuwa nazo kwenye sanduku, kisha nikaingia kwenye gari kuelekea Mason. Tulipokuwa kwenye gari aliniambia kuwa iwapo nitaacha utukutu, ninaweza kufika mahali. Aliniambia kuwa shule za watukutu zinaeleweka vibaya. Alisema kuwa lengo lake kuu ni kumbadilisha mtu awe bora zaidi, na kuwa ni mahali ambapo wavulana kama mimi wanaweza kukaa na kutafakari makosa yao na kuanza maisha mapya na kuwa mtu ambaye kila mtu atajivunia. Aliniambia pia kuwa, bibi ambaye alisimamia mahabusu, bibi Swerlin na mume wake walikuwa watu wazuri sana.

Ni kweli walikuwa watu wazuri. Bibi Swerlin alikuwa na mwili mkubwa na mcheshi kuliko mume wake. Bwana Swerlin yeye alikuwa ni mwembamba mwenye nywele nyeusi, sharubu nyeusi na uso mwekundu. Alikuwa mkimya na mkarimu sana, hata kwangu.

Walinipenda mara moja, bibi Swerlin alinionyesha chumba changu, mara ya kwanza maishani kuwa na chumba changu. Zilikuwa ni aina ya zile nyumba zilizokuwa kama bweni ambazo watoto waliwekwa mahabusu nyakati zile na baadhi ya sehemu leo. Nilishangazwa sana baada ya kufahamu kuwa niliruhusiwa kula na familia ile. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kula na wazungu-yaani wazungu watu wazima toka wakati wa ile mikutano ya wasabato. Si kuwa mimi tu nilieyekula nao, wote wavulana kwa wasichana tulikula nao, isipokuwa wale waliojaribu kutoroka na wakakamwatwa. Hao walifungiwa.

Walikuwa na mzungu aliyewasaidia kupika, nakumbuka aliitwa Lucille Lathrop. (Inanishangaza jinsi ambavyo majina haya yananijia maana sijayafikiria kwa zaidi ya miaka ishirini). Lucille pia alikuwa mkarimu kwangu, mume wake aliitwa Duane Lathrop. Alikuwa akifanya kazi mahali pengine, lakini mwisho wa juma alikaa pale na mke wake.

Kwa mara nyingine niliona jinsi ambavyo wazungu wana harufu tofauti na sisi, na jinsi ambavyo chakula chao kilikuwa tofauti, hakikuwa na viungo kama chakula cha watu weusi. Nilianza kufanya kazi ya kufagia na kupiga deki nyumbani pale, kama tulivyofanya na Bonge nyumbani kwa Gohannase.

Wote walipenda tabia yangu, ni kutokana na kunipenda huko ndipo wakanifanya kuwa kikaragosi, sasa ndiyo nimeelewa. Kwa mfano, waliweza kuongea jambo lolote lile bila kujali nipo pale nawasikia, kama vile tu watu wanavyoongea kwa uhuru mbele ya chiriku wao wa kufugwa. Wakati mwingine waliongea kunihusu mimi mwenyewe, au hata kuhusu “Niggers” wengine kama vile sipo au sielewi neno hilo linamaanisha nini. Mara nyingi sana kwa siku walitumia neno “Nigger” nadhani kwenye akili yao waliona ni neno la kawaida tu, na pengine hata walikuwa wanalisema kwa uzuri. Hata mpishi, Lucille na mume wako Duane walikuwa namna hiyo. Nakumbuka siku moja bwana Swerlin alitoka Lansing, na alikuwa amepita kwenye makazi ya watu weusi, alimwambia bibi Swerlin, mbele yangu-kwa uzuri tu, “siwezi kuelewa inakuwaje Ma-Nigger wanaweza kuwa na furaha namna ile na ni masikini wa kutupwa.” Aliongea jinsi ambavyo wanaishi kwenye vibanda lakini wana magari mazuri wamepaki mbele yake.

Naye bibi Swerlin alijibu, nikiwa bado nipo, “Ma-Nigger ndivyo walivyo. . . .” hadi leo nakumbuka tukio lile.

Wazungu wengi waliokuja kutembelea pale walikuwa namna hiyo, hasahasa wanasiasa. Moja ya mazungumzo waliyopendelea sana ilikuwa ni juu ya “Ma-Nigger.” Mmoja wao alikuwa ni jaji aliyenisimamia nilipokuwa Lansing. Alikuwa ni rafiki wa karibu wa familia ya Swerlin. Alipofika alikuwa akiniulizia nao waliniita, nilipofika aliniangalia juu mpaka chini huku akionyesha sura ya kuridhika-kama vile alikuwa akiangalia mtoto mzuri wa mbwa. Najua watakuwa walimwambia jinsi tabia yangu ilivyokuwa na nilivyokuwa nikifanya kazi.

Ninachotaka kusema hapa ni kuwa hawakuelewa kabisa kuwa nafahamu kuwa mimi si mnyama wa kufugwa, ni binadamu. Hawakuthamini kuwa nina uelewa na hisia kama ambavyo wangeweza kumthamini mtoto wa kizungu ambaye angekuwa katika hali yangu. Lakini kihistoria wazungu wamekuwa hivyo wanapowachukulia watu weusi. Kwamba hata kama tupo pamoja nao, hawatuchukulii kama tupo sawa nao. Japo walionekana kama wamefungua mlango, lakini bado ulikuwa umefungwa. Hivyo ukweli ni kuwa hawakutambua kabisa uwepo wangu.

Hii ndiyo aina ya dharau ambayo najaribu kuwaambia leo watu weusi wenye kiu ya kuchangamana juu ya sehemu kubwa ya rafiki zao “waliberali” wa kizungu wanaowaita “wazungu wazuri.” Sijali ni mwema kiasi gani kwako, ukweli ni kuwa, kamwe hatakuona kama anavyojiona, kama anavyoona wazungu wenzake. Atasimama na wewe kijuujuu tu mambo yanapokuwa mazuri, lakini siku zote atajiona ni bora kuliko mtu mweusi yoyote yule.

Lakini wakati huo nikiishi kwenye makazi ya mahabusu, niliyafaamu mambo hayo kijuu juu tu. Nilifanya kazi zangu na mambo yote yalikuwa sawa. Kila juma waliniruhusu kwenda Lansing mchana au jioni. Japo sikuwa na umri mkubwa, lakini nilikuwa na mwili mkubwa hivyo hakuna aliyejali kuniona nipo maeneo ya watu weusi usiku. Nilikuwa nakuwa mkubwa kuliko hata Wilfred na Philbert ambao walikuwa wameanza kupata wasichana shuleni kwenye dansi na sehemu zingine, na walikuwa wamenitambulisha kwa baadhi ya wasichana hao. Lakini walioonekana kunipenda sikuwapenda, na kinyume chake. Sikuweza kucheza dansi hata kidogo na sikuona sababu ya kupoteza pesa zangu chache kwa ajili ya wasichana. Kwa hiyo mara nyingi nilijiburudisha siku za jumamosi na jumapili kwa kutembelea baa na migahawa ya watu weusi. Maeneo hayo zilisikika nyimbo kama “Tuxedo Junction” ya Erskine Hawkin, “Flatfoot Floogie” ya Slim and Slam na nyingine kama hizo. Nyakati nyingine bendi kubwa kutoka New York zilifika Lansing na kutumbuiza. Kila mtu mwenye miguu alifika kuona wasanii wa New York. Hivyo ndivyo nilivyowafahamu watu kama Lucky Thompson na Milt Jackson ambao nilikuja kufahamiana nao hapo baadaye huko Harlem.

Vijana wengi waliokaa mahabusu, walienda kwenye shule za watukutu tarehe yao ilipofika. Lakini tarehe yangu ilipofika, kama mara mbili au tatu hivi ilipuuzwa. Niliona vijana wakija na kuondoka. Nilifurahi na kushukuru sana, nilijua ni bibi Swerlin aliyewezesha hilo, sikutaka kwenda shule ya watukutu.

Siku moja akaniambia kuwa nitajiunga na shule ya upili ya Mason. Ilikuwa ndiyo shule pekee mjini pale. Hakuna mkazi wa mahabusu aliyewahi kuhudhuria shule pale, hasa akiwa bado mahabusu. Basi nikaanza darasa la saba pale. Wanafunzi weusi pekee shuleni pale walikuwa ni watoto wa bwana Lyon, walikuwa ni wadogo kuliko mimi, wakisoma madarasa ya chini. Bwana Lyon alikuwa ni mtu mwenye akili na bidii ya kazi. Mke wake pia alikuwa ni mtu mzuri sana. Niliwahi msikia mama yangu akisema kuwa ni yeye na bibi Lyons walikuwa ni wawili kati ya watu wanne wenye asili ya visiwa vya Karibeani waliokaa pande zile za Michigan.

Nilikuja kuona kuwa baadhi ya watoto wa kizungu kwenye shule ile walikuwa ni wenye urafiki kuliko baadhi ya wale wa kule Lansing. Japo baadhi yao, wakiwemo waalimu waliniita “Nigger” lakini ilikuwa ni rahisi kuona kuwa ilikuwa si kwa ubaya, kama tu bwana na bibi Swerlin walivyoniita. Nikiwa kama “Nigger” wa darasa, nilikuwa maarufu sana na kwa sehemu ni kwa sababu nilikuwa mgeni nilikuwa natendewa kwa upendeleo. Lakini pia nilifaidika kwa kuwa na mhuri wa kukubalika kutoka kwa mwanamke muhimu sana katika Mason-bibi Swerlin. Hakuna mtu wa Mason ambaye hata aliota kumuudhi bibi Swerlin. Ilikuwa ni ngumu kwa siku kupita shuleni bila ya mtu kunifuata na kunitaka nijiunge na hiki au niwe kiongozi wa kikundi cha mijadala, timu ya mpira wa kikapu au mambo mengine yaliyofanyika nje ya masomo. Kamwe sikuwakatalia.

Si muda mrefu tokea nianze shule bibi Swerlin akawa ameona kuwa nitahitaji pesa kwa ajili ya matumizi madogomadogo. Basi akanitafutia kazi ya kuosha vyombo kwenye mgahawa uliokuwa karibu. Bosi wangu alikuwa ni baba wa mwanafunzi mwenzangu ambaye nilitumia muda mwingi sana pamoja naye. Familia yao iliishi ghorofani kwenye mgahawa ule. Nilifurahia kazi mahali pale. Kila ijumaa nilipolipwa, nilijihisi nimekuwa na urefu wa futi kumi. Nimesahau nililipwa kiasi gani lakini nilikiona kingi sana. naweza kusema ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumiliki pesa yangu mwenyewe, yote ikiwa yangu. Mara tu nilipopata pesa za kutosha, nilinunua suti ya kijani na viatu, na shuleni niliwanunulia wengine vitu vidogovidogo-kama ambavyo wao walinifanyia.

Nilipendelea zaidi masomo ya kiingereza na historia. Namkumbuka mwalimu wangu wa kiingereza, bwana Ostrowski-ambaye mara zote alikuwa akitoa ushauri wa jinsi ya kufanikiwa maishani. Kitu pekee ambacho sikukipenda katika somo la historia ni suala la mwalimu wangu, bwana Williams kupendelea sana utani uliohusu watu weusi. Siku moja, juma moja baada ya kuanza shule, nilipokuwa naingia darasani akaanza kuimba-kama utani, “Kule kusini kwenye mashamba ya pamba, kuna watu wanasema kuwa Nigger hataiba.” Inachekesha. Nilipenda somo la historia, lakini bwana Williams sikuja kumpenda. Nakumbuka kuna muda tulifika sehemu ya kitabu inayozungumzia historia ya watu weusi. Ilikuwa ni sehemu ya aya moja tu. Bwana Williams aliifundisha kwa utani ndani ya dakika chache tu. Akisoma kwa sauti jinsi ambavyo watu weusi walifanywa kuwa watumwa na baadaye kuwekwa huru, na jinsi ambavyo siku zote wamekuwa ni wavivu, wajinga na waliokosa malengo. Aliongezea kwa kutuambia kwa utani jinsi ambavyo miguu ya watu weusi ni mikubwa kiasi kwamba hawaachi alama ya unyayo bali shimo.

Nasikitika kusema kuwa somo ambalo nililichukia kuliko yote lilikuwa ni hisabati. Nimetafakari sana kuhusu hilo. Nafikiri ni kwa sababu hesabu haziachi nafasi ya kubishana. Kama umefanya kosa linakuwa hivyo, hakuna mjadala.

Mpira wa kikapu ulichukua sehemu kubwa sana ya maisha yangu. Nilikuwa kwenye timu ya shule; tulisafiri kwenda miji ya karibu kama Howell na Charlotte, nilipoonyesha tu sura yangu, mashabiki uwanjani walinitania “Nigger” au “Coon” au waliniita “Rastus.” Kocha wangu na wachezaji wenzangu hawakujali hata kidogo, na kusema ukweli mimi mwenyewe sikujali sana. Nilikuwa na saikolojia ileile ambayo hata leo inawafanya watu weusi wa leo kuwaacha wazungu wawasifie jinsi wanavyojitahidi na kupiga hatua, japo kwa ndani hilo linawakera. Wamesikia hivyo mara nyingi sana kiasi kwamba wameamini kuwa ni kweli au walau kukubaliana nalo.

Kwa kawaida kulikuwa na dansi baada ya mchezo. Kila timu yetu ya shule ilipoingia ndani ya ukumbi wa dansi, nami nikiwemo, niliona ukumbi mzima ukizizima. Ulianza kuchangamka baada ya kuona kuwa sijichanganyi kucheza bali nakaa kuongea na mmoja wa wachezaji wenzangu au nimetulia peke yangu. Nadhani nilijenga uwezo wa kufanya hilo bila kuonekana. Hata shuleni niliona hilo, pamoja na bashasha na tabasamu zote, bado kikaragosi hakutakiwa kucheza dansi na msichana yeyote wa kizungu.

Ilikuwa kama utaratibu uliokuja tu wenyewe. Nilikuwa nikisimama nikiongea na kutabasamu, nikila na kunywa. Kisha nikatunga sababu na kuondoka mapema.

Dansi zilikuwa kama zinavyokuwa kwenye shule za miji midogo. Wakati mwingine bendi ndogo ya wazungu kutoka Lansing ilikuja kutumbuiza, lakini mara nyingi ulikuwa ni muziki tu uliochezwa kwenye fonografi, sauti ikiwa imewekwa mpaka mwisho, ikipiga nyimbo kama “Moonlight Serenade” ya Glenn Miller-bendi yake ilikuwa maarufu sana wakati ule-au nyimbo za bendi ya Ink Spot ambayo nayo ilikuwa maarufu sana na wimbo wao wa “If I didn’t care.”

Nilizoea kutumia muda mrefu nikifikiri juu ya jambo fulani la tofauti sana. Wavulana wengi wa kizungu wa shule hii ya Mason, kama tu wale wa Lansing-hasa kama walinijua vizuri na nilitumia muda mwingi pamoja nao, walikuwa wakinivuta pembeni na kunihamasisha kumtongoza msichana fulani wa kizungu, wakati mwingine dada zao wenyewe. Wangeweza kuniambia kuwa wao wenyewe wameishawapata wasichana hao au wanajaribu kuwapata lakini wanashindwa. Baadaye nilikuja kuelewa kilichokuwa kinaendelea: kama wangeweza kumfanya msichana huyu kuvunja miiko na kuwa nami, basi walikuwa na jambo la kuweza kumfedhehesha msichana huyo na hivyo kumfanya awakubalie kirahisi.

Ni kama wavulana wa kizungu walinidhania kuwa-kwa kuwa nilikuwa mweusi basi nilifahamu zaidi yao juu ya masuala ya mapenzi au ngono-kwamba kiasili nafahamu nini cha kusema kwa wasichana wao. Sijawahi mwambia mtu kuwa niliwafuata baadhi ya wasichana wa kizungu na baadhi yao walinifuata. Lakini kila ilipoonekana uhusiano wetu na wasichana hao unakuwa mzuri kuna kikwazo kilikuja kati yetu. Wasichana hasa niliotaka kuwa nao ni weusi ambao Wilfred na Philbert walinitambulisha kule Lansing. Lakini sikuwa na ujasiri wa kuwafuata wasichana hawa.

Kulingana na habari nilizozisikia wakati nilipoenda maeneo ya watu weusi siku za jammosi usiku, nilifahamu kuwa kulikuwa na watu weusi wenye wapenzi wa kizungu. Lakini ajabu ni kuwa hili halikuniathiri kabisa. Nadhani manegro wote wa Lansing walijua jinsi ambavyo wanaume wa kizungu walipita na magari kwenye makazi ya weusi kuchukua wanawake weusi waliojiuza barabarani. Na kwa upande mwingine, kulikuwa na daraja lililotenganisha makazi ya manegro na wapolishi, hapo wanawake wa kizungu walifika na kukutana na wanaume weusi ambao walikaa karibu na daraja wakiwasubiria. Hata katika miaka hiyo, wanawake wa kizungu wa Lansing walikuwa maarufu kwa kuwatongoza wanaume weusi. Sipendezwi na kitendo cha wazungu wengi kuwahusisha watu weusi na uwezo mkubwa wa kingono. Kule Lansing sikuwahi kusikia tatizo lolote juu ya muingiliano huu watu rangi mbalimbali kimapenzi. Nadhani walionelea ni hali ya kawaida tu kama mimi nilivyoiona.

Pamoja na hayo, uzoefu wangu nikiwa mwanafunzi huko Lansing ulinifanya niwe mjanja sana katika kuwaepuka wasichana wa kizungu.
 
Sura ya pili inaendelea.

Katika muhula wa pili wa darasa la saba nilichaguliwa kuwa rais wa darasa. Ilinishangaza zaidi kuliko ilivyowashangaza watu wengine. Lakini sasa naelewa kwa nini darasa lilifanya vile. Alama zangu zilikuwa moja ya alama za juu kabisa shuleni pale. Kutokana na rangi yangu, nilikuwa wa tofauti sana darasani kwetu na nilikuwa najikubali sana, siwezi kudanganya kuhusu hilo. Wakati huo sikuwa na hisia sana juu ya kuwa mtu mweusi, sababu ni kuwa nilikuwa nikijitahidi niwezavyo kuwa kama mzungu. Na hiyo ndiyo sababu namwambia mtu mweusi leo kuwa anapoteza muda kwa kujitahidi kuchangamana. Nafahamu kutokana na uzoevu. Nilifanya jitihada za kutosha.

“Malcom tunajivunia sana mafanikio yako,” alisema bibi Swerlin kwa furaha aliposikia kuchaguliwa kwangu kuwa rais wa darasa. Habari ilisambaa kwa kila mtu kwenye mgahawa niliokuwa nikifanya kazi. Hata yule bwana wa serikali, Maynard Allen, ambaye bado alikuwa akinitembelea hapa na pale alinipa pongezi. Alisema hajawahi ona mtu anayetoa ushuhuda bora juu ya faida ya kazi ya kurekebisha tabia kama mimi. Kiukweli nilikuwa napendezwa na mtu huyu isipokuwa kwa kitu kimoja tu. Hapa na pale alikuwa akidokezea kwamba kwa namna fulani mama yangu alituangusha.

Mara nyingi nilikwenda kuitembelea familia ya Lyon, walifurahia kuniona kama vile nilikuwa mmoja wa watoto wao. Nilipokelewa kwa namna hiyohiyo nilipoenda Lansing kuwatembelea kaka na dada zangu au familia ya Gohannase. Nakumbuka kuna kitu kimoja kilichokuwa kinaanza kunitatiza sana wakati huo: Filamu ya “Gone with the wind.” Ilipoonyeshwa huko Mason, nilikuwa mtu mweusi pekee kwenye ukumbi wa sinema, na ilipofika sehemu ya Buttefly McQueen nilitamani kuingia chini ya zulia kujificha.

Karibu kila jumamosi nilikwenda Lansing. Wakati huo nilikuwa nakaribia miaka kumi na minne. Wilfred na Hilda bado walikuwa wakiishi kwenye nyumba ya familia. Hilda aliweka nyumba safi muda wote, ilikuwa rahisi kuliko ilivyokuwa kwa mama yangu na sisi nane tukikimbia huku na huko. Wilfred aliendelea kufanya kazi wakati wote alipoweza, na bado aliendelea kusoma kila kitabu alichoweza kupata. Philbert alizidi kupata umaarufu kama mmoja wa mabondia chipukizi bora kabisa katika maeneo yale; kila mtu alikuwa anatarajia kuwa atakuwa bondia wa kulipwa.

Uhusiano wangu na Reginald ulikuwa umeimarika tena baada ya kulegalega kutokana na ile aibu ya kupigwa. Nilifurahia kuwatembelea yeye pamoja na Wesley katika familia ya Bibi William. Mara nyingi niliwapatia dola kadhaa za kutumia. Yvonne na Robert nao walikuwa wanaendelea vyema kwenye familia ya Bibi McGuire. Niliwapatia kama senti ishirini na tano kila mmoja; nilifurahi kuona maendeleo yao.

Hakuna kati yetu aliyezungumza sana juu ya mama yetu. Na kamwe hatukumzungumzia baba yetu. Nafikiri hakuna aliyejua cha kusema. Nafikiri pia hatukutaka mtu yeyote mwingine amzungumzie mama yetu. Mara moja moja sote tulikwenda Kalamazoo kumtembelea. Mara nyingi sisi tulio wakubwa tulikwenda kila mmoja peke yake, maana halikuwa jambo ambalo ungetaka kuwa na mtu mwingine yeyote, hata kama ni kaka au dada yako.

Ziara ya kumtembelea mama ambayo naikumbuka sana ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka wa darasa la saba, wakati huo Ella, dada yetu mkubwa kutoka kwenye ndoa ya kwanza ya baba, alikuja kutoka Boston kututembela. Wilfred na Hilda walikuwa wamendikiana barua kadhaa na Ella, pia nami, kwa ushauri wa Hilda, nilimuandikia barua. Wote tulifurahi sana tulipopata barua yake akitujulisha kuwa atakuja Lansing.

Nafikiri tokea moja kubwa sana la ujio wa Ella, kwangu mimi, ni kwamba alikuwa ni mwanamke wa kwanza mweusi kumuona akijivunia weusi wake maishani mwangu. Alijivunia waziwazi rangi yake nyeusi ti. Hili lilikuwa jambo geni kabisa katika watu weusi wakati huo, hasa katika Lansing.

Sikuwa na hakika ni siku gani atafika. Siku moja mchana niliporudi kutoka shule nikamuona huyu hapa kafika. Alinikumbatia, akaniachia na kunitazama juu mpaka chini. Mwanamke anayejiamini, pengine kuliko hata Bibi Swerlin. Ella hakuwa tu mweusi, lakini kama baba yetu, alikuwa mweusi ti. Jinsi alivyokaa, alivyotembea, alivyoongea na alivyofanya mambo yake, iliashiria kuwa alikuwa ni mtu ambaye alifanya na kupata kile alichotaka. Huyu ndiye mwanamke ambaye baba yangu alijivunia sana kwa kutoa watu wengi wa familia yao Georgia na kuwapeleka Boston. Alituambia alitunza pesa na kuwekeza kwenye majengo ambayo aliyaboresha na kuyaongezea thamani, kisha akaanza kutuma pesa Georgia kwa dada, kaka, binamu na wapwa wake ili nao waende Boston. Yote niliyosimuliwa juu ya Ella niliyaona kwenye muonekano na mwenendo wake. Sikuwahi kumstaajabia mtu kama nilivyomstaajabia. Alikuwa kwenye ndoa yake ya pili; mume wake wa kwanza alikuwa ni daktari.

Ella aliniuliza maswali mengi juu ya maendeleo yangu; tayari alikuwa amesikia kutoka kwa Wilfred na Hilda juu ya kuchaguliwa kwangu kuwa rais wa darasa. Hasa hasa aliuliza juu ya maendeleo yangu katika masomo nami nikakimbia kwenda kuleta barua za matokeo yangu. Wakati huo nilikuwa kwenye tatu bora ya darasa. Ella alinipongeza sana. Nilimuuliza kuhusu kaka yake, Earl, na dada yake Mary. Alifurahia kunihabarisha kuwa Earl alikuwa muimbaji kwenye bendi huko Boston. Akitumia Jimmy Carleton kama jina lake la uimbaji. Marry naye alikuwa akiendelea vizuri.

Alinisimulia habari za ndugu wengine wa upande wa baba. Baadhi yao sikuwahi hata kuwasikia; wote alikuwa amewasaidia kuondoka Georgia. Nao pia wakasaidia wengine. “Sisi familia ya Little tunatakiwa kuwa wamoja,” alisema Ella. Niliguswa sana kumsikia akisema jambo hilo, na hasa zaidi jinsi alivyolisema. Nilikuwa nimekuwa kikaragosi; familia yetu ilivunjika vipandevipande; nilikuwa nimeshasau kuwa nami ni mwanafamilia ya Little. Aliniambia kuwa baadhi ya wanafamilia wanafanya kazi nzuri, na na hata wengine wana biashara zao ndogo. Wengi wao walikuwa na nyumba zao wenyewe.

Ella alipotoa wazo la wana-Little wote wa Lansing tuambatane naye kwenda kumuona mama yetu tulifurahi sana. Wote tulifikiri kuwa kama kuna mtu atamsaidia mama yetu-kumsaidia kurudi katika hali yake ya kawaida basi ni Ella. Kwa mara ya kwanza, wote tuliongozana na Ella kwenda Kalamazoo.

Mama yetu alikuwa akitabasamu walipomleta. Alishangaa sana alipomuona Ella. Walikuwa tofauti sana, mwanamke mwembamba aliyekaribu kufanana na mzungu alikumbatiana na na mwingine mweusi na mwenye mwili mkubwa. Sikumbuki mengi juu ya safari yetu ile isipokuwa kulikuwa na maongezi mengi na Ella alisimamia mambo yote. Tuliondoka tukijisikia vizuri kuliko tulivyowahi kuhisi juu ya hali ya mama yetu.

Siku chache baadaye, baada ya kutembelea mahali ambako kila mmoja wetu aliishi, Ella alituaga na kurejea Boston. Lakini kabla ya kuondoka aliniambia niwe nikimuandikia barua mara kwa mara. Na alipendekeza iwapo nitapenda kumtembelea huko Boston wakati wa majira ya joto nifanye hivyo, nilikubali mara moja.

***​
 
Sura ya Pili inaendelea.

Majira ya joto ya mwaka 1940 nilipanda basi la Greyhound kueleka Boston nikiwa na sanduku langu la mbao. Nilikuwa nimevaa suti yangu ya kijani. Kama mtu angening’iniza bango lenye neno “MSHAMBA”shingoni mwangu, lingefaa kabisa kunielezea. Basi lilionekana kusimama karibu kila kituo. Kutoka kwenye siti yangu, na kama ulivyokisia- siti ya nyuma kabisa-nilikodoa macho dirishani nikiangalia Marekani yaa mzungu ikirudi nyuma kwa muda ulioonekana kama ni mwezi mzima, lakini labda ilikuwa ni siku moja na nusu tu.

Tulipofika, Ella alikuja stendi ya basi kunipokea na kunipeleka nyumbani. Nyumba ilikuwa mtaa wa Waumbeck, eno la Sugar Hill huko Roxbury, Harlem ya Boston. Nilikutana na Frank, mume wa pili wa Ella ambaye alikuwa ni mwanajeshi; na kaka yake na mwanamuziki, Earl ambaye alijiita Jimmy Carleton; na Mary ambaye alikuwa tofauti sana na dada yake mkubwa. Inachekesha kwamba nilikuwa namuona Mary kama dada wa Ella badala ya kufikiri kuwa ni dada yangu kama tu alivyokuwa Ella. Pengine kwa sababu mimi na Ella tulikuwa karibu, tulikuwa ni watu wa kujiamini wakati Mary alikuwa ni mkimya na mwenye aibu.

Ella alikuwa akijishughulisha na mambo mengi. Sikumbuki alikuwa mshiriki wa vikundi vingapi, alikuwa ni mwanachama wa chama kilichoitwa, “Chama cha Watu Weusi” nilikutana na mamia ya watu weusi huko, watu ambao tabia zao na maongezi yao ya kimjini viliniacha mdomo wazi.

Nisingeweza kujidai sijali na kujidai wa mjini hata kama ningetaka kufanya hivyo. Watu walizungumza juu ya Chicago, Detroit na New York kirahisi tu. Sikujua kuwa duniani kuna watu weusi wengi kama niliowaona Roxbury mjini nyakati za usiku, hasa siku za jumamosi. Matangazo ya kuwaka, klabu za usiku, baa na magari waliyoendesha! Migahawa ilifanya mitaa inukie vizuri, jukebox zilipiga nyimbo za Erskine Hawkins, Duke Ellington, Cootie Williams na wengine wengi kwa sauti kubwa. Kama kuna mtu angeniambia wakati huo kwamba siku moja nitafahamiana nao nisingemuamini. Bendi kubwa kama hizi zilipiga muziki kwenye ukumbi wa dansi wa Roseland uliokuwa kwenye barabara ya Massachusetts-usiku mmoja kwa ajili ya watu weusi na usiku mmoja kwa ajili ya wazungu.

Kwa mara ya kwanza niliona wapenzi-mzungu na mweusi wakitembea wameshikana mikono. Jumapili, Ella, Mary au mtu yeyote alipoenda nami kanisani, niliona makanisa ya watu weusi ambayo sijawahi kuyaona hapo kabla. Yalikuwa ni mazuri kuliko kanisa mengi la wazungu nililohudhuria huko Mason, Michigan. Huko, wazungu walikaa tu na kuabudu kwa maneno; lakini watu weusi wa Boston, kama watu weusi wengine niliowahi kuwaona kanisani, waliweka mwili na nafsi yao yote katika kuabudu.

Kama mara mbili au mara tatu hivi niliandika barua kwa Wilfred nikilenga iwafikie wote kule Lansing. Niliwaambia kuwa nitajaribu kuwaelezea zaidi nitakaporudi, lakini bahati mbaya sikuweza.

Niliporudi Mason nilipatwa na wakati mgumu sana kuwa katikati ya wazungu, hali hiyo ilianza mara tu niliporudi nyumbani na kuanza darasa la nane.

Mara zote niliendelea kufikiria juu ya yale niliyoyaona kule Boston, na jinsi nilivyohisi nilipokuwa huko. Sasa nafahamu kuwa zilikuwa ni hisia zilizotokana na kuwa katikati ya umati wa watu wa jamii yangu kwa mara ya kwanza maishani.

Wazungu niliosoma nao, familia ya Swerlin na watu kwenye mgahawa niliokuwa nafanya kazi waliona mabadiliko hayo. “Umekuwa wa ajabu. Unaonekana hauko sawa Malcom. Shida nini?”

Lakini bado niliendelea kuwa kati ya wenye alama za juu darasani. Nakumbuka nafasi za juu tulipokezana mimi, msichana mmoja aliyeitwa Audrey Slaugh na mvulana aliyeitwa Jimmy Cotton. Iliendelea hivyo huku nikizidi kuwa kutatizwa akilini mwangu kadri muhula wa kwanza ulivyoendelea. Kisha ghafla siku moja, wakati ambao sisi tuliofaulu tulitakiwa kuhamia 8-A, na kisha kutoka hapo kuingia sekondari ya juu mwaka unaofuata-jambo fulani lilitokea na likawa jambo la kwanza kubadili maisha yangu kwa kiasi kikubwa.

Kwa namna fulani nilijikuta peke yangu darasani na bwana Ostrowski, mwalimu wangu wa kiingereza. Alikuwa ni mrefu, mwenye rangi nyekundu hivi na masharubu mengi. Nilikuwa nimepata baadhi ya alama zangu za juu zaidi kwenye somo lake. Na mara zote alinifanya nihisi kuwa anapendezwa nami. Kama nilivyoeleza, alikuwa na “Kipaji” cha kutoa ushauri juu ya unachotakiwa kusoma, kufanya, kufikiri na juu ya kila kitu. Tulizoea kutania kuwa kwa nini anafundisha Mason badala ya sehemu nyingine na kujipatia “mafanikio” ambayo amekuwa akituambia jinsi ya kuyapata?

Nafahamu kuwa pengine alikuwa ana nia njema kwa kile alichonishauri siku ile. Sidhani kama alikuwa na nia yoyote ovu. Ilikuwa ni asili yake akiwa kama mwanaume wa kizungu. Nilikuwa mmoja wa wanafunzi wake bora, mmoja wa wanafunzi bora shuleni pale, lakini kitu pekee alichoona ndani yangu ni kuwa natakiwa “Kubaki sehemu ninayostahili” kama ambavyo wazungu wote huona kwa watu weusi.

Aliniambia, “Malcom, unatakiwa kufikiria juu ya utakachofanya maishani. Umefikiria juu ya hilo?”

Ukweli ni kuwa sikuwahi kufikiria juu ya hilo. Sijawahi elewa ni kwa nini nilimjibu, “Ndiyo Sir, nimekuwa nafikiria kuwa mwanasheria.” Kipindi hicho hakukuwa na daktari wala mwanasheria mweusi huko Lansing kuwa kama mfano wa kitu ninachotaka kuwa. Kitu nilichojua kwa hakika ni kuwa mwanasheria haoshi vyombo kama nilivyokuwa nikifanya.

Nakumbuka bwana Ostrowski alishangazwa sana, aliegemea kiti chake na kuweka mikono nyuma ya kichwa. Alitabasamu tabasamu jembamba na kusema, “Malcom, moja ya hitaji la kwanza la maisha ni kwa sisi binadamu kuona uhalisia. Usinielewe vibaya. Sote hapa tunakupenda, unafahamu hilo. Lakini unatakiwa kuangalia uhalisia kama mtu mweusi. Hakuna uhalisia kwa mtu mweusi kuwa na lengo la kuwa mwanasheria. Unatakiwa kufikiria juu ya kitu unachoweza kuwa hasa. Upo vizuri katika kazi za mikono. Kila mtu anastaajabia kazi yako katika karakana ya useremala. Kwa nini usipange kuwa seremala. Mtu kama wewe utapata kila aina ya kazi.”

Kadri nilivyofikiri juu ya maneno yake hapo baadaye, ndivyo yalivyozidi kunihangaisha. Yaliendelea tu kuzunguka kichwani mwangu bila kukoma.

Kilichonitatiza hasa ni ushauri wa bwana Ostrowski kwa wanadarasa wenzangu-wote wazungu. Wengi wao walikuwa wamemwambia kuwa wanapanga kuwa wakulima. Wale waliomwambia kuwa walitaka kufanya kitu tofauti aliwatia moyo. Baadhi yao, hasa wasichana walitaka kuwa waalimu. Wachache walitaja taaluma zingine, mfano mvulana mmoja alitaka kuwa afisa ugani; mwingine daktari wa wanyama; na msichana mmoja alitaka kuwa muuguzi. Wote walisema kuwa bwana Ostrowski aliwatia moyo kuwa kile walichotaka. Lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyepata alama sawa na mimi.

Inashangaza kuwa sikuwahi kufikiri namna hiyo hapo kabla, lakini nilitambua kuwa, pamoja na yote bado nilikuwa na akili kuliko karibu watoto wote wale wa kizungu. Lakini machoni mwao bado sikuwa na akili za kutosha kuwa kile nilichotaka kuwa.

Hapo ndipo nilipoanza kubadilika ndani yangu.

Nilianza kujitenga na wazungu.Nilifika darasni na kutulia, nilijibu nilipoulizwa tu na kuhudhuria vipindi vya bwana Ostrowski ikawa kama mateso kwangu.

Hapo mwanzo sikujali kuitwa Nigger, lakini sasa kila nilipolisikia jina hilo nilisimama na kumuangalia aliyelisema. Nao walionekana kushangazwa na kitendo cha mimi kufanya hivyo.

Hakuna hata mmoja, kutia ndani waalimu aliyeelewa kilichonipata. Nilifahamu kuwa walikuwa wakiniongelea.

Baada ya majuma machache hali ikawa hivyo kwenye mgahawa ninaofanya kazi na nyumbani kwenye familia ya Swerlin.

***
 
Mwendelezo lini tena aise
Polepole hadi mwisho. Sehemu ya mwisho ya sura ya pili hapa chini.

Siku moja bibi Swerlin aliniita sebuleni, huko nilimkuta mtu wa serikali, bwana Maynard Allen. Kwa kuangalia sura zao nilitambua kuwa kuna jambo linakwenda kutokea. Bibi Swerlin aliniambia kuwa hakuna kati yao anayeelewa kwa nini baada ya kufanya vizuri shuleni na katika kazi yangu, na kuishi nao na baada ya kupendwa na kila mkazi wa Mason-nimeanza kuwafanya wahisi kuwa sina furaha tena kuwa nao.

Alisema kuwa haoni sababu ya mimi kuendelea kuishi kwenye nyumba ya mahabusu, na kuwa mpango umefanywa wa mimi kwenda kuishi na familia ya Lyon, watu walionipenda sana.

Alisimama na kusema huku akinipa mkono “Nadhani nimekuuliza mara mia kadhaa, Malcom, unaweza kuniambia kinachokusumbua?”

Nami nilimpa mkono na kusema, “Hakuna shida Bi Swerlin,” kisha nikaenda chumbani kubeba vitu vyangu na kurudi. Nilipokuwa natoka mlangoni nilimuona bibi Swerlin akijifuta machozi. Nilijisikia vibaya, nilimshukuru kisha nikaambatana na bwana Allen aliyenipeleka kwenye familia ya Lyon. Kwa muda wa miezi miwili niliyoishi na Bwana na bibi Lyon pamoja na watoto wao, nikimalizia darasa la nane-walijitahidi wawezavyo kuniuliza tatizo linalonisibu. Lakini hata wao sikuweza kuwaambia.

Kila jumamosi nilikwenda Lansing kuwatembelea kaka na dada zangu. Na karibu kila siku nilimuandikia Ella barua, nilimwambia kuwa ninataka kwenda kuishi Boston, lakini sikusema kwa nini.

Sijui alifanya namna gani, lakini alifanya mipango ya kiserikali iliyoniwezesha kuhama kutoka Michigan na kwenda kuishi naye Massachusetts. Juma lile lile nililomaliza darasa la nane, nilipanda basi la Greyhound kuelekea Boston.

Toka wakati huo nimekuwa nikifikiria juu ya nyakati zile mara nyingi sana. Hakuna uhamaji uliokuwa na matokeo makubwa katika maisha kama ule.

Kama ningebaki Michigan pengine ningeoa mmoja wa wale wasichana wa Lansing niliowapenda. Pengine ningekuwa mmoja wa wale vijana wang’arisha viatu kwenye makao makuu ya jimbo au mhudumu kwenye Country Club ya Lansing, au ningepata kazi za vibarua ambazo kwa wakati huo watu wa Lansing waliziona kuwa ni za maana sana-pengine hata ningekuwa seremala.

Tokea hapo, kitu chochote nilichokifanya, nimekifanya kwa bidii sana ili kufanikiwa. Nimefikiria mara nyingi kuwa iwapo bwana Ostrowski angenitia moyo kuwa mwanasheria, pengine leo ningekuwa mmoja wa mabwanyenye weusi katika mji fulani, nikinywa mvinyo na kujitokeza kama msemaji na kiongozi wa watu weusi wanaoteseka huku lengo langu kuu likiwa ni kujipatia makombo ya ziada kutoka mezani kwa wazungu wanafiki ambao wanajidai wako pamoja na watu weusi kwenye kudai “uchangamano.”

Sifa zote zimuendee Allah kwa kuhamia kwangu Boston wakati ule. Kama si hivyo, pengine bado ningekuwa Mkristo Mweusi niliyechotwa akili.
 
Back
Top Bottom