Kisa cha mwanamke wa ziwani

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,810
15,398
Mnamo August 12, 1997 majira ya Mchana Katika wilaya ya Lake nchini uingereza kundi la wazamiaji kutoka mji mdogo wa Kendal waliamua kwenda kufanya mazoezi katika mto ulioko jirani wa Caniston.

Mmoja wa wazamiaji wale alifanikiwa kwenda kina kirefu zaidi ya mita 21 na ndipo alipohisi harufu kali ya kitu kinachonuka, alipozidi kusogelea eneo lile aligundua ni mabaki ya mwili wa mwanadamu uliofungwa kwenye mfuko wa plastiki.

Mzamiaji yule pamoja na wenzie ilibidi wasitishe mazoezi yao na kuwafahamisha Polisi.Baadae mchana huo huo kikosi cha Polisi wazamiaji walifika kwenye eneo la tukio na kufanikiwa kuyatoa mabaki ya mwili ule.

Walipofungua ule mfuko wa plastiki walikuta mabaki ya mwili wa mwanamke ambae alikuwa akionekana dhahiri kwamba alikuwa na umri wa chini ya miaka 30 na ilionekana dhahiri kwamba alikaa ndani ya maji kwa miaka mingi sana kwani hata mavazi aliyokuwa ameyovaa yalionyesha hivyo.

Alikuwa amevaa vazi la usiku la miaka ya 70 na alionekana kwamba alikuwa amepigwa na kitu kizito kichwani na kisha kutupwa mtoni. Ndani ya mfuko wa plastiki uliokuwa umehifadhi ule mwili kulikutwa pia vipande vizito vya vyuma ambavyo viliwekwa kwa makusudi na muuaji ili ule mwili uzame moja kwa moja bila kuibuka.

Kwa kuanzia askari wa upepelezi walianza kuchunguza kesi zaidi ya 50 za watu walioripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwenye miaka ya 70. Ukweli ni kwamba hata vazi alilokutwa nalo Carol lilirahisisha sana kutambuliwa kwake kwani haikuwachukuwa muda mrefu Polisi kutangaza kuhusu kutambuliwa kwa mwili ule ambao ulikwisha harbika vibaya kutokana na kukaa katika maji kwa takribani miaka 21.

Mnamo August 21, 1997 ikiwa ni siku 9 baada ya kugundulika kwa ule mwili, Polisi wa upelelezi walitangaza rasmi kwamba ule mwili ulikuwa ni wa Carol Park mama wa watoto watatu na mwalimu wa shule ya msingi aliyekuwa na miaka 30 wakati huo alipotoweka.

Taarifa za Kipolisi zilionyesha kwamba Carol alitoweka nyumbani kwake mnamo July, 1976. Inasemekana kwamba mnamo tarehe hiyo Familia yao ilikubalina wafanye safari ya kwenda katika mji wa Blackpool ili kupunga upepo kwenye Hoteli za ufukweni lakini Carol alisitisha uamuzi wa kwenda huko kwa madai kwamba anajisikia vibaya, hivyo mumewe Gordon Park ambae pia ni mwalimu pamoja na watoto wao wakaamua kwenda bila ya mama yao.
Lakini waliporudi usiku hakumkuta mkewe, na ilimchukuwa wiki 6 kuripoti kutoweka kwa mkewe polisi.

Alipoulizwa sababu ya kuchelewa kutoa taarifa wakati huo aliwaambia Polisi kwamba katika miaka ya karibuni mkewe alikuwa na akitoka nje ya ndoa na wanaume tofauti tofauti tabia ya kutoweka pale nyumbani na kurejea na akiwa salama. Utokana na tabia hiyo mume huyo alidai kuwa hata maisha yao ya ndoa yalishaanza kuyumba.

Polisi walikuja kugundua baadae kupitia kwa majirani kwamba Maisha ya ndoa kati ya Gordon na mkewe Carol yalikuwa si mazuri na yaliyojaa misukosuko mingi. Majirani waliwaeleza Polisi kwamba Carol aliwahi kuwaambia kuwa alikuwa na wanaume wawili waliokuwa wakiishi katika maeneo tofauti na alikuwa akienda kuishi nao katika vipindi tofauti. Taarifa zaidi zilibainisha kwamba kuna wakati aliwahi kutoweka nyumbani kwa miezi 18.

Pia majirani hao walijenga hisia kwamba huenda Carol alikwepa safari ya kwenda Blackpool akichukulia kama ni nafasi muhimu kwake atakayoitumia ili kutoroka pale nyumbani kwake na kwenda kuanza maisha mapya mahali pengine na mwanaume mwingine. Hata hivyo kaka yake Carol aitwae Ivor Price alidai kwamba ni jambo lisiloingia akilini kuamini kwamba dada yake anaweza kuwatelekeza watoto wake watatu na kwenda kusikojulikana bila mawasiliano nao kwa kipindi chote alichopotea kwani hata kipindi cha nyuma alichowahi kutoweka alikuwa akiwasiliana nao. Pamoja na maelezo yake, Polisi hawakuonekana kuyatilia maanani kwani waliona kwamba hakuna haja sana ya kushughulika na kesi ya mtu ambae alikuwa na tabia ya kutoweka nyumbani kwake mara kwa mara.

Hata hivyo Polisi hawakuipuuza sana ile kesi, kwani waliona ni busara kuichunguza ile kesi kwa makini zaidi, hasa ikizingatiwa kwamba tukio lenyewe lilitokea zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Ili kuthibitisha hayo mwendesha mashtaka wa serikali(Detective Superintendent) aliyejulikana kwa jina la Ian Douglas ambae aliipa kesi hii jina la "mwanamke wa ziwani"(Lady of the Lake) aliwaambia waandishi wa habari kwamba Polisi wanaishughulikia kesi ya Carol kama ya mauaji ya kukusudia, kutokana na mazingira ya jinsi mwili ulivyopatikana.

Pia Msemaji huyo alitanabahisha kwamba Polisi watawahoji ndugu na watu wa karibu wa Carol akiwemo Aliyekuwa mumewe Gordon Park ambae alikuwa ameshastaafu kazi yake ya ualimu, na kwa wakati ule ambao mwili wa Carol umepatikana alikuwa ameenda Likizo nchini Ufaransa akiwa na mke wake wa tatu aitwai Jenny.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama kuna uwezekano wa Gordon Park kuchukuliwa kama nimtuhumiwa wa mauaji hayo. Msemaji huyo alisema kwamba haingekuwa vyema kwa Polisi kumtuhumu moja kwa moja Gordon, na hawezi kuwaomba Polisi wa nchini Ufaransa wamkamate kwa sababu kuna mambo mengi ya kuangaliwa kabla ya kumtia mbaroni.

Kwa maneno yake mwenyewe Douglas alisema "Bado tuna jukumu la kuwatafuta na kuwahoji watu waliokuwa wakiishi jirani na familia ya Gordon Park wakati Carol alipotoweka, na pia ndugu wa karibu wa familia husika pamoja na marafiki, ni jambo ambalo linahitaji muda na umakini wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kwamba ni siku nyingi tangu tukio hili lilipotokea, na ikumbukwe kwamba tunazungumzia tukio lililotokea miaka 21 iliyopita, ni vigumu watu kuwa na kumbukumbu za tukio zima"

Alipoulizwa kama Polisi watakwenda kuchunguza nyumba ambayo familia ya Gordon Park ilikuwa ikiishi. Msemaji huyo alisema kwamba hilo linawezekana kwa sababu teknolojia imekuwa kubwa katika miaka ya karibuni na kuna uwezekano wa mtuhumiwa kukamatwa.
Siku mbili baada ya Msemaji wa Polisi Ian Douglas kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu muenendo wa upelelezi wa kesi ya Carol Park.

Msemaji huyo pamoja na timu ya wataalamu wa kuchunguza mazingira ya eneo la tukio walikwenda kuchunguza nyumba anayoishi Gordon Park iliyoko katika eneo la Borrow-in-Furness. Pia Timu hiyo ilikwenda kuchunguza Boti ya uvuvi(Yatch) ya Gordon ambayo ilikuwa imeegeshwa kando ya ziwa Caniston. Timu hiyo iliondoka na vitu kadhaa kwa ajili ya kuvifanyia uchunguzi.

Pamoja na kuondoka na ushahidi huo lakini Douglas alionyesha wasiwasi na muonendo mzima wa maisha ya Gordon. Kwani Polisi walijenga wasiwasi kutokana na kitendo cha Gordon kuuza Boti yake ya uvuvi ya awali ambayo aliipa jina la "Lady J" muda mfupi tu baada ya Carol kutoweka.


Wakati Polisi wakiendelea kumsubiri Gordon arejee kutoka Ufaransa alipokwenda kwa likizo, waliona ni vyema wawahoji watoto wao watatu ambao ni Jeremy aliyekuwa na miaka 27 lakini wakati mama yake anatoweka alikuwa na umri wa miaka 6, mwingine ni Rachel aliyekuwa na miaka 26 na Vanessa aliyekuwa na miaka 29 wakati mwili wa mama yao ulipopatikana.
Katika mahojiano hayo, Polisi waligundua kwamba Vanessa hakuwa mtoto wa Gordon wa kuzaa, bali alikuwa ni binti wa dada yake Carol aitwae Christina ambae aliuwawa na bwana yake. namo mwaka 1969, ambapo Carol na Gordon waliamua kumuasili na kumfanya binti yao.
Hata hivyo Polisi walikanusha kuwepo kwa mahusiano kati ya kesi hizo mbili.


Ukweli ni kwamba Polisi hawakupata ushahidi wowote wa kumtia Gordon hatiani, kwani wale watoto wote watatu hawakuwa na kumbukumbu za matukio yote yaliyotokea kabla na baada ya mama yao kutoweka. Pia Polisi walitaka kutengeneza taarifa ya kumbukumbu (Profile) ya maisha ya Gordon Park na familia yake mpaka kufikia mwaka 1976.

Kazi hiyo ilikuwa ngumu kwa sababu watu waliotaka kuwahoji walikuwa aidha wamehamia katika maeneo ya mbali au wamefariki Dunia. Hata hivyo Polisi walifanikiwa kumpata mama mmoja aitwae Mary Robins aliyekuwa na umri wa miaka 61 ambae alikuwa akifanaya kazi ya uyaya kwenye familia ya Gordon Park. Mama huyo alikiri kuwa anakumbuka vizuri sana siku Carol aliyotoweka.

Akizidi kuwasimulia Polisi mama huyo alisema kwamba, hata yeye binafsi alijenga wasiwasi na namna carol alivyotoweka, na alihisi kwamba huenda kuna jambo ambalo si la kawaida limemtokea. Kwani pale mtaani kila mtu aliliona tukio la kutoweka kwa Carol kama kitu cha kushangaza, kwa mtu kuwatekeleza watoto wake ghafla kiasi kile na kutokomea kusikojulikana bila kuwasiliana na wanae kama alivyokuwa akifanya awali.

Mama Robinson aliendelea kuwaeleza Polisi kuwa, yeye alidhani labda ameamua kwenda kuanza maisha mapya huko nchi za ulaya kwa sababu hata hivyo alikuwa ni mwalimu mzuri hasa katika kufundisha lugha ya kiingereza. Mnamo August 24 1996, Gordon Park na mkewe Jenny walirejea nchini uingereza wakitokea nchini Ufaransa. Baada ya kufika nyumbani kwake katika eneo la Barrow-in-Furness ambapo alishusha mizigo kutoka kwenye gari, kisha akaondoka na kuelekea katika kituo cha Polisi kujisalimisha kwani pamoja na kwamba alikuwa nje ya Uingereza lakini alikuwa akiifuatilia ile habari ya kupatikana kwa mabaki ya mwili wa aliyekuwa mkewe kupitia vyombo vya habari na hasa Luninga.

Alipofika alishikiliwa kwa muda na kuhojiwa. Wanafamilia na marafiki pamoja na majirani zake walionyesha kusikitishwa kwao na kukamatwa kwa Gordon, akizungumzia tukio hilo mmoja wa marafiki zake aitwae Paul Shaw alisema kwamba alitokea kumfahamu Gordon kwa miaka mingi, kwani walisoma pamoja. Akizidi kumuelezea Paul kwa maneno yake mwenyewe alisema "Ni mtu anaejiheshimu, muungwana, anaeheshimu kila mtu, na katika kipindi alipokuwa mwalimu alikuwa akifanya kazi zake kwa uadilifu mkubwa na asiyependa kumkwaza mtu.

Pamoja na kuzungumziwa vizuri na marafiki na majirani zake lakini kulikuwa na wingu la mashaka lililotanda kwa upande wa familia ya Carol dhidi ya Gordon. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya misa ya kumuombea dada yake, kaka yake na Carol alisema "Bado nina mashaka dhidi yake lakini, mpaka hapo atakapokamatwa muuaji ndio atakuwa hana hatia"

Baada ya masaa 36 tangu Gordon kukamatwa, msemaji wa Polisi, akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri nje aliwaambia kwamba Gordon Park amefunguliwa mashitaka ya kuhusika na mauaji ya Carol.

Kwa maneno yake mwenyewe msemaji huyo alisema "mnamo majira ya saa mbili na nusu usiku, kuna mtu amefunguliwa mashitaka ya kuhusika mauaji ya Carol Park, na kwa taarifa yenu mtu huyo atafikishwa katika mahakama ya Barrow siku inayofuata"

Baadae msemaji huyo alibainisha kwamba mtu huyo alikuwa ni Gordon Park.
Siku inayofuata Gordon alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ambapo alikanusha kuhusika na mauaji hayo.


Kesi hiyo iliahirishwa mpaka wiki inayofuata ili kuruhusu upelelezi wa kesi hiyo ukamilike.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa Gordon aitwae Michael Graham aliiomba mahakama impe dhamana mteja wake, lakini mwendesha mashitaka katika kesi hiyo aliyejulikana kwa jina la Elizabeth Grant, alikataa Gordon kupewa dhamana na alitoa sababu zifuatazo, kwanza alidai kwamba mshitakiwa anaweza kuingilia upelelezi wa kesi hiyo, pili alisema kwamba kuna uwezekano wa wa Gordon kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na mwisho ni kutokana na usalama wake mwenyewe, Mama Grant alisema kwamba kuna uwezekano wa mtu yeyote ambae ameguswa na kifo cha Carol kujichukulia sheria mkononi na kumdhuru mshitakiwa, hivyo kutokana na kukataliwa Dhamana ilibidi aendelee kubakia Rumande.

Hata hivyo wiki mbili baadae Mwendesha mashtaka mama Grant alibatilisha uamuzi wake na kuruhusu Gordon kuachiwa kwa dhamana kwa masharti kwamba akakae kwa dada yake aishie katika mji wa Manchester, pia asalimishe Hati yake ya kusafiria na awe anaripoti Polisi kila siku na hakutakiwa kutoka nje ya mji wa Manchester.

Kesi yake iliahirishwa mpaka Januari 1998, ambapo iliwapa Polisi fursa ya miezi minne kufanya uchunguzi. Mnamo Januari 7, 1998 ikiwa imebaki wiki moja ili kesi ya Gordon kusikilizwa, msemaji wa Polisi aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi wameamua kutoendelea na kesi ya Gordon, kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi madhubuti wa kumtia mshitakiwa hatiani. Taarifa hiyo ilipokelewa kwa furaha sana na Gordon,na kusema wazi kwamba hana hatia ya kuhusika na mauaji ya Carol.

Akiongea na waandishi wa habari Gordon, kwa maneno yake mwenyewe alisema "Kwa jinsi Carol alivyonitendea katika ndoa yetu, watu wanadhani nilihusika na mauji yake, lakini ukweli ni kwamba sikuhusika na mauaji hayo, najua watu wanatilia mashaka kutokutiwa kwangu hatiani labda mpaka hapo mhusika wa mauaji hayo atapofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani ndio watu wataamini kwamba sikuhusika na mauaji hayo"

Hata hivyo Mnamo Januari 2002, Polisi walianza upelelezi wa siri kwa kuunda timu ya watu sita wakiongozwa na Detective Chief Inspector Keith Churchman. Timu hiyo ilitangaza zawadi ya paundi 5000 kwa mtu yeyote atakaye jitokeza na kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa kuuaji na pia kituo kimoja cha Luninga nchini humo cha Channel 4 kuonesha kipindi maalumu (Documentary) kuhusina na kesi hiyo iliyopewa jina marufu la Lady in the Lake wakiifananisha na jina la kitabu cha riwaya kilichotungwa na mwandishi maarufu wa vitabu vya riwaya Raymond Chandler, ambapo kilikuwa na jina kama hilo.

Hatua hiyo ilizaa matunda baada ya watu wawili ambao waliwahi kufungwa katika jela ambayo Gordons Park aliwekwa rumande watu hao walitoa taarifa Polisi kuwa Park aliwahi kukiri kumuua mkewe kwa kumpiga na kitu kizito kichwani, watu hao waliokuja kujulikana kwa majina ya Michael Wainwright na mwenzie Glen Banks walimnukuu Park akiwaambia, "anastahili kufa, kwani nilimkuta chumbani akiwa na mwanaume mwingine" Ushahidi huo maarufu kama Jailhouse Snitch ndio uliopewa uzito zaidi na Polisi katika kumtia Gordons hatiani. Walidai kuwa katika kipindi cha siku 14 alizokuwa amewekwa rumande akisubiri kusomewa masitaka ndipo alipokiri kuhusika na mauaji ya mkewe Carol Park.

Baada ya timu hiyo kukusanya ushahidi mnamo Novemba 2004, Gordons Park alifikishwa mahakamani kwa mara ya pili na kufunguliwa mashitaka ya kuhusika na mauaji ya mkewe Carol Park. Wakati wa kuendeshwa kwa kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Mheshimiwa Jaji McCombe katika mahakama ya Manchester Crown, ilielezwa kwamba Park alimpiga mkewe Carol kichwani na kitu kizito wakiwa chumbani hapo mnamo julai 1976. Baadae aliuhifadhi mwili huo kwenye Jokofu kabla ya kwenda kuutelekeza katika ziwa la Caniston wiki moja baadae.

Mahakama ilielezwa kwamba wanandoa hao hawakuwa na mahusiano mazuri katika maisha yao ya ndoa na kuwa walikuwa wakijihusisha na shajara za kubadilishana wanawake, maarufu kama ''wife-swapping' parties' ambapo katika tukio moja la shajara ya chakula cha usiku Carol Park aliondoka na kwenda kulala na rafiki wa mumewe aitwae Colin Foster, huku Gordond Park akiondoka na mke wa Colin Foster kwenda kulala naye katika chumba kingine.




Lakini hata hivyo ushahidi wote uliokusanywa dhidi ya Gordons Park ulikuwa na utata mtupu kiasi cha kuwavutia watu wengi yakiwemo Makundi mbalimbali ya watetezi wakipiga kampeni ya kutaka Gordons Park aachiwe huru kutokana na ushahidi finyu dhidi yake.

Shahidi mwingine alikuwa ni mama mmoja aitwaye Joan Young, ambaye alidai kuwa mnamo Julai 1976 yeye na mumewe wakiwa katika mapumziko katika wilaya hiyo ya Lake walikuwa wamekaa kandoni mwa eneo hilo la Caniston na ndipo walipoona boti likiwa ufukweni.

Mama huyo alidai kumuona mwanaume akisukuma kitu kilichofungwa kama furushi, ambapo alimtania mumewe kwa kumwambia ‘yawezekana huyo akawa ni mkewe' . Hata hivyo ushshidi huo ulizua utata kwa sababu kwanza, siku na muda ulioelezwa ilitofautiana na ule uliokuwa ukifahamika na Polisi.

Pili, ingawa mumewe alikumbuka kusikia ule utani, lakini alikuwa akisoma gazeti hivyo hakuona kitu chochota. Tatu umbali walipokuwa wamekaa na umbali unaosemekana boti hilo kuwepo, ni vigumu kwa mtu kuweza kuona kitu na kukitambua.

Nne, kama aliona mtu akisukumia kitu ziwani, basi haiwezekani ukawa ni mwili wa Carol Park kwa sababu mwili ulipatikana umbali mrefu kutoka katika eneo ambalo wao Joan Young na mumewe walikaa. Ikumbukwe kwamba mwili ule ulikuwa umefungwa ndani ya begi la plastik pamoja na vyuma ili kuupa uzito usiweze kuelea, sasa itawezekana vipi kusogezwa umbali wote ule.

Tano, kwa mujibu wa maelezo yake wakati akifafanua kuhusu muonekano wa boti aliyoiona ufukweni siku hiyo alidai kuwa aliona boti la uvuvi kama Cruiser. Lakini wakati mwili wa Carol ulipopatikana ilifahamika kuwa Gordons Park alikuwa akimiliki Boti kubwa ya uvuvi aina ya Yatch.

Lakini mwaka 1976 Gordon alikuwa akimiliki Boti ieandayo kwa kasi ambayo ilikuwa ikitumika kwa uvuvi pia.

Ingawa kumbukumbu hazioneshi usahihi wa madai hayo lakini kuna ukweli kwamba Boti hiyo haikuwahi kuwepo katika ufukwe wa Caniston katika kipindi hicho cha mwezi wa tano wa summer, miezi miwili kabla ya Carol hajatoweka, kwani Boti hiyo ilikuwa ikitumika kuvua samaki katika ziwa jingine la Windermere.

Kama ikichukuliwa kuwa ni yeye aliyeutelekeza mwili wa Carol, basi mwili ule usingetelekezwa katika ziwa la Canistone na badala yake mwili ule ungetelekzwa mahali ambapo Boti la Gordons lilipokuwa ambapo ni Windermere, na kama ni kuogopa kuonekana na mwili ule na watu, basi angeenda maeneo ya mbali zaidi na sio Coniston mahali ambapo katika kipindi hicho cha Summer kunakuwa na watu wengi katika eneo hilo.

Mojawapo ya kidhibiti kilichofikishwa mahakamni hapo ni jiwe, ambapo mwendesha mashtaka alidai kuwa pamoja na kuutupa mwili wa Carol mtoni pia Gordons alizitupa nguo za Carol mtoni ambapo alizitosa zikiwa zimefungwa kama furushi na ndani yake kukiwa na lile jiwe.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa kitaalamu imethibitisha kwamba madini yaliyoko katika lile jiwe yanafanana kabisa na na madini yaliyoko kwenye mawe nyumbani kwa Gordons.

Lakini ni kwa nini mpaka jiwe likahusishwa na kesi hiyo? Hata hivyo katika hali ya kushangaza askari wa kikosi cha uzamiaji ambaye ndiye aliyehusika katika kuuopoa mwili wa Carol katika ziwa la Coniston alidai kuwa hakumbuki kuopoa jiwe hilo.

Naye Profesa Kenneth Pye ambaye ndiye aliyehusika na uchunguzi wa jiwe lile na akiwa ni shahidi wa kitaalamu katika kesi hiyo, alipoulizwa kuhusiana na mazingira ya kuhusishwa kwa jiwe hilo na kesi hiyo alidai kuwa ingawa ushahidi huo haukuwa na nguvu lakini ushahidi wa wale wafungwa wawili waliokuwa wamewekwa selo moja na Park wakati alipokuwa amewekwa rumande alipokamatwa kwa mara wa kwaza ndio muhimu katika kesi hiyo.

Ilielezwa mahakamni hapo kwamba mnamo Septemba 2000 mfungwa mmoja aitwae Michael Wainwright aliwasiliana na Polisi na kutoa taarifa kuwa Gordons Park aliwahi kukiri mbele yake akiwa na mwenzie aliyetajwa kwa jina la Glen Banks ambaye ana matatizo ya kutojua kusoma (Learning Disability) kuwa ni kweli alimuua mkewe.


Hata hivyo Park alidai kutokuwa na ukakika wa kukutana na watu hao alipokuwa gerezani. Lakini Banks alionekana dhahiri kutokuwa na kumbukumbu nzuri wakati alipokuwa akitoa ushhidi wake pale mahakamani, kwani alisema, "Alituambia kuwa alimuua mkewe kwenye Boti huko Blackpool"

Naye Wainwright, katika maelezo yake wakati wa kutoa ushahidi mahakamni alinukuliwa akisema, "Park aliniambia kuwa alipopanda ghorofani katika chumba chao cha kulala alimkuta mkewe akiwa na mwanaume mwingine kitandani na ndipo alipomuua hapohapo" Kauli hiyo ilizidi kuacha maswali nyuma, Je, ni nini kilichotokea kwa yule mwanaume aliyefumaniwa?


Lakini jambo lingine ambalo liliwashangaza watu ni hili, hivi inawezekana kweli mtu kama Park ambaye amekuwa mwalimu kwa muda mrefu na ambaye amekuwa akisisitiza kwa marafiki zake, familia yake, na hata mwanasheria wake kutokuwa na hatia tangu kukamatwa kwake kwa mara ya kwanza kwa kutuhumiwa kuhusikana mauaji ya mkewe, aweze kukiri kwa urahisi hivyo kwa watu hao ambapo mmoja wapo, yaani Wainwright, anahusishwa na uvutaji wa bangi kupindukia akiwa na uwezo wa kuvuta misokoto mpaka 12.


Na kama Gordons Park hakuhusika na mauaji ya mkewe, je ni nini kilichomtokea mkewe siku hiyo wakati walipomuacha mkewe nyumbani siku hiyo ya jumamosi Julai 1976?


Kulikuwa na mambo matatu muhimu ya kuyaangalia ambayo yalitokea siku hiyo. Kwanza jirani mmoja alimuona Carol akiwa amesimama nje ya nyumba yao, pili jirani mwingine alimuona mtu akiendesha gari dogo aina ya VW Beetle hadi jirani na nyumbani kwa Gordons Park na kusimama hapo kwa takribani dakika 20.


Tatu huyu jirani aliyeliona gari hilo aina ya VW Beetle alikuwa na uhakika aliyekuwa akiendesha gari hakuwa ni Gordons, ingawa hakumuona aliyekuwa akiendesha gari hilo, kwa kuwa aliliona likipita tu. Hata hivyo uwepo wa gari hilo katika eneo la tukio haukuwahi kuzungumziwa pale mahakamani.
Pamoja na utata huo, utata mwingine ni pale mwanamke mwingine ambaye alidai kumuona Carol majira ya jioni katika eneo la Charnock Richard services. Mwanamke huyo alisema kuwa alimuona Carol akikatiza mbele yake katika mwendo wa haraka lakini akiwa ameinamisha kichwa chini.


Katika ripoti moja kutoka kituo cha ushauri, ilionyesha kuwa tangu mwaka 1975 Carol hajawahi kulalamika kuwa amewahi kupigwa au kutishiwa maisha na Gordons kwa kipindi chote alichokuwa akihudhuria hapo katika kituo hicho. Lakini hata hivyo miongoni mwa wapenzi wa Carol, wengi wao walikuwa na tabia ya ukatili na mmoja wapo alikuwa ni John Rapson ambaye ndiye aliyemuua dada yake na kufungwa gerezani.

Je Johna Rapton alikuwa gereani wakati Carol alipouawa? Hapana alikwishaachiwa tangu Disemba 1975, lakini alipohojiwa na polisi alidai kuwa alikuwa katika mji wa Barrow hapo mnamo Julai 1976, Carol alipotoweka.


Polisi hawakumtilia mashaka kuhusika na mauaji ya Carol, lakini wachunguzi wa masuala ya kiuhalifu walidai kuwa yeye John Rapton ni miongoni mwa wapenzi wa Carol wa kutiliwa mashaka kuhusika na mauaji hayo zaidi ya Gordons Park.

Kesi hiyo iliisha kusikilizwa hapo Januari 2005, ikiwa ni wiki 10 tangu ilipoanza kusikilizwa kwa mara ya pili, na ikiwa ni takribani miaka 29 tangu Carol alipotoweka.

Katika hali ya kushangaza Gordons Park alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa kosa hilo. Lakini alipewa uwezekano wa kuachiwa baada ya kutumikia kifungo cha miaka 5 kama ataonyesha tabia nzuri.

Mnamo siku ya jumatatu januari 25, 2010, ikiwa ni imebakiza mwenzi mmoja, kufikiriwa kuachiwa, Gordon Park alikutwa akiwa amejinyonga katika selo yake huko katika Gereza la HMP Garth, Leyland, Lancs.

Je ni kwa nini achukue uamuzi huo wa kujinyonga wakati kulikuwa na uwezekano wa kuachiwa huru muda mfupi ujao? Hili swali mpaka leo halijapatiwa majibu. Kwa jinsi kesi hii ilivyojaa utata, na ndivyo hata kifo cha Gordons Park kule Gerezani kilivyojaa utata pia.



 
Mchambuzi mzima?? usishangae watu wakaanza kuchangia kesho..leo wanaisoma kwanza!
 
Mchambuzi mzima?? usishangae watu wakaanza kuchangia kesho..leo wanaisoma kwanza!

Hii ni kwa maandalizi ya mapumziko ya miaka 50 ya uhuru, but it is true story and it is touching.........
 
Nitaisoma week end!!

Bora wewe umesema ukweli.......... naamini utapata muda mzuri wa kutafakari maisha ya ndoa na uhusiano pale unapo-pogoka na kuzingirwa na mikengeuko.............
 
Mhhh ndefu sana japo nimeisoma yote
Ila swali ambalo halijajibiwa nani alimuua Carol na kwa nini Gordons alijiua
 
Mhhh ndefu sana japo nimeisoma yote
Ila swali ambalo halijajibiwa nani alimuua Carol na kwa nini Gordons alijiua

Ni swali ambalo bado linawaumiza vichwa wapelelezi wa Uingereza................ bado kitambo kidogo jibu linaweza kupatikana, kwani kuna vichwa bado vinafanyia kazi jambo hilo.................
 
Nime-icopy na kudownload movie yake. Nafikiri weekend itakuwa njema kwangu. Kama kuna movies au documentaries zingine kama hizi nijulishe majina yake Mtambuzi ili weekend yangu iwe fupi sana.
 
Nime-icopy na kudownload movie yake. Nafikiri weekend itakuwa njema kwangu. Kama kuna movies au documentaries zingine kama hizi nijulishe majina yake Mtambuzi ili weekend yangu iwe fupi sana.

Zipo nyingi, nitajitahidi niziweke hapa kwa kadiri muda na muitikio kutoka kwa wana JF wengine utakavyokuwa..................
 
Babu mtambuzi shkamoo! Nafurahi kuona umepona mkono na unatyp kwa haraka now!

Marhaba mwanangu, ndio nimetoa POP jana na kutokana na kutype hii stori jana usiku, mkono wangu umevimba mbaya, lakini nimeanza kuuchua na Fastrum
 
mkuu asante kwa hilo gazeti,
naomba umruhusu binti yako cantalisia anifupishie
mimi nimeshindwa kulisoma mkuu.
Hebu ni PM namba yako ya simu nikupigie naikusimulie........... si unajua nimehamia Airtel!
Mwanangu Cantalisa yuko bize na tuition anasoma mambo ya Utambuzi hapa nyumbani................
 
Hebu ni PM namba yako ya simu nikupigie naikusimulie........... si unajua nimehamia Airtel!
Mwanangu Cantalisa yuko bize na tuition anasoma mambo ya Utambuzi hapa nyumbani................

nitafanya hivyo mkuu,
lakini ngoja nianze nayo asubuhi
nikishindwa nitaku -pm.

Kumbe una shule ya utambuzi mkuu, hongera sana kwa hilo.
je ni kwa ajili ya watu wa umri gani,
na jinsia ipi hasa, itakuwaje nikakuletea na binti yangu akasoma na cantalisa wako.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom