KAULI ya mwanasiasa wa zamani Kingunge Ngombale-Mwiru dhidi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye kuhusu maamuzi ya vikao ndani ya chama hicho, imeibua mjadala kutoka kwa wajumbe wa vikao hivyo wanaohoji anachokitetea mzee huyo.
Wakizungumza na FikraPevu kwa nyakati tofauti, wajumbe hao wamehoji kinachomsukuma Kingunge kupigana kufa na kupona kumtetea Lowassa bila kuzingatia maslahi ya chama na Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Nape alisema Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM kuingia katika Vyombo vya Dola, toleo la Februari 2010 hazitoi nafasi kwa Mgombea wa Nafasi ya Urais kukata rufaa.
Hata hivyo, Kingunge akizungumza na waandishi wa habari alionekana kuwa na msimamo tofauti akisema mgombea anaweza kukata rufaa bila kutoa mifano wala nukuu ya kanuni zinazoruhusu jambo hilo.
Mmoja wa wajumbe wa NEC aliyepo Dodoma, ameifahamisha FikraPevu kuwa mkakati wa baadhi ya wagombea ni kuvuruga vikao baada ya kuanza kukata tamaa.
Wapo wanachama waliwahi kukata rufaa huko nyuma, akiwemo Lowassa mwenyewe 1995 kupitia makada wengine kina Galus Abeid na Yusuf Makamba, lakini Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, wakati huo alisema kwamba kazi ya vikao vya maamuzi ni kupunguza idadi ya wagombea si kuongeza majina, anasema mjumbe huyo na kuongeza;
Mifano mingine ni mwaka 2005 ambapo Mzee Malecela (John Samwel) alikata rufaa kupinga kuenguliwa katika nafasi ya kuwania urais kupitia CCM na alipoomba kujieleza ndani ya NEC alijibiwa kwa dakika tatu tu kwa Mkapa kuzungumzia mambo mawili tu ikiwamo suala la umri kuwa mkubwa na kukumbushia kukataliwa kwa Malecela na Mwalimu Nyerere.
Alisema katika mchakato huu unaoendelea, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alipoingizwa katika kundi la wataka urais sita waliosimamishwa na CCM mwaka 2014, aliamua kukata rufaa kupinga kuhukumiwa bila kuzingatia uzito wa makosa anayotuhumiwa nayo, lakini hadi sasa hakuwahi kujibiwa wala kujadiliwa na badala yake CCM iliendelea na mchakato wake.
Mjumbe huyo mkongwe anasema katika hali ya kawaida, vikao vya maamuzi vinakuwa na ratiba ambayo wakiruhusu kukata rufaa, italazimika kusitisha shughuli zote kwa muda usiojulikana.
Kinachofanywa na Kingunge ni kutafuta uhalali wa kutata rufaa ili kuvuruga mchakato, ili vikao vya NEC na Mkutano Mkuu usifanyike wakati Kanuni ya tano imekaa kimya kuhusu rufaa katika vikao vya uchujaji na uteuzi, anasema.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mzee Kingunge akionekana kumtetea Lowassa alitoa mfano wa Mzee Malecela bila kueleza jinsi Mkapa alivyozima hoja ya Malecela alipopewa nafasi ya kuzungumza (si kukata rufaa) ndani ya NEC.
Tayari wafuasi wa Lowassa wanadaiwa kuanza kueneza taarifa kwamba Nape amefukuzwa uongozi na kuvuliwa uanachama kwa kumzibia nafasi mgombea wao na kwamba mapendekezo hayo yametolewa na Kingunge.
FikraPevu imeelezwa kwamba hasira na visasi vya Kingunge vinatokana na migogoro katika kampuni zake za ujenzi na ukusanyaji ushuru katika Kituo cha Mabasi na Maegesho anakodaiwa kuwa alikuwa anainyonya serikali fedha ambazo zingeweza kutumika kulipia mishahara na huduma za hospitali.
Source: FikraPevu
Kauli ya Kingunge yaibua mjadala CCM, wadau wahoji anachokitetea | Fikra Pevu