Kinana: Lowassa ni Rafiki yangu

technically

JF-Expert Member
Jul 3, 2016
11,975
48,843
12dcaa3ccd5011bd7001a3ebcf5c1fa5.jpg


''Ni rafiki yangu, lakini kuna urafiki na kuna nchi. Binafsi nadhani sisi bado ni marafiki. Tangu uchaguzi umekwisha tumeshakutana mara nyingi, tumeshapigiana simu mara kadhaa. Tunazungumza, sitaki kuamini kwamba ana nongwa, na hata kama ana nongwa nitamuelewa. Unajua, kama nilivyosema hapo mwanzo, kuna urafiki wangu na Lowassa na kuna nchi'' - Abdulrahmaan Kinana.
---------------
Raia Mwema: Tayari Rais Dk. John Magufuli amezungumzia mwaka wake mmoja madarakani. Kwa nyongeza, kauli zake kadhaa zinaashiria kuzisuta serikali zilizopita. Huko ndani ya CCM hamuoni hivyo?

Kinana: Niseme kwanza kwamba kwa wakati huu ni mapema mno kuanza kumhukumu Rais na serikali yake pamoja na Chama Cha Mapinduzi kwa haya ambayo tayari anafanya.

Tukianza kuorodhesha vitu ambavyo anasema au hajafanikiwa kuvifanya, hatutakuwa tukimtendea haki.

Na hizo kauli unazorejea, kila mtu amezisikia, nikuambie tu kwamba ni za nia nzuri. Ameanza vizuri na ana nia njema na nchi. Anataka kujenga matumaini mapya katika nchi.

Labda niseme hivi, mzee Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema kila zama na kitabu chake. Kila kiongozi ana namna yake ya kuongoza ukiangalia namna Mwalimu Nyerere alivyoongoza, Mwinyi, Mkapa na Jakaya Kikwete.

Zipo staili za uongozi si tu hapa Tanzania, bali duniani kote. Uzuri ni kwamba katika nchi yetu chama kilichoendelea kuchaguliwa ni CCM. Lakini viongozi wamekuwa tofauti, sasa hiki anachokifanya Magufuli tunasema nini, mimi nadhani kwanza hii ni staili tu ya uongozi na haya anayosema Rais yalikuwapo kwenye awamu zote.

Kama ni dili zilikuwapo wakati wa Baba wa Taifa. Alipambana na wakwepa kodi. Alipambana na mianya ya rushwa. Utakumbuka Mwalimu Nyerere aliunda tume nyingi za kuchunguza rushwa. Ilikuwapo ya mzee Jozeph Kaaya, hata hii Takukuru ilikuwa na mtu mzee Maftaha, baadaye akaja Jenerali Anatoly Kamazima.

Zote hizo ni juhudi za kupambana na masuala haya. Na mzee Mwinyi alipochukua nchi alikabidhiwa ufagio wa chuma. Lengo lilikuwa ni kusafisha kila aina ya uchafu. Hiyo haikuwa na maana kwamba wakati wa Mwalimu Nyeerere kulikuwa na uchafu mwingi.

Kulikuwa na kasoro kwa hiyo alichoambiwa Mwinyi ni kwamba ondoa hizo kasoro. Na Mwalimu aliwahi kusema ‘mimi nimeongoza kwa miaka 24, chukueni yale mazuri acheni mabaya’.

Mzee Mkapa alipokuja aliunda Tume ya Jaji Joseph Warioba kuziba mianya ya rushwa na masuala yote yanayoendana na uadilifu katika uendeshaji wa serikali na hata yeye aliorodhesha maeneo ambayo kumekuwa na matumizi mabaya ya madaraka na wizara zipi zinaongoza kwa vipaumbele. Na hata Jakaya Kikwete alipokuja naye alianza hivyo hivyo.

Kwa hiyo anachofanya Rais Magufuli sasa ni kuimarisha uwajibakaji ndani ya serikali na kwenye vyombo mbalimbali.

Anachofaya ni kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ndani ya serikali na taasisi mbalimbali. Anachofanya vilevile ni kutoa tahadhari.

Unamwona kila wakati anajaribu kueleza mambo yalivyo ili kutoa tahadhari kwamba mambo si mazuri katika sehemu nyingi kwa hiyo ni vizuri turekebishe.

Lakini wakati mwingine anazungumza kwa kuonya, kwamba kama msipochukua hatua hizi, mimi nitachukua hatua. Tofauti ya Magufuli na viongozi wengine labda kwanza nadhani ni mtu anayezungumza kwa uwazi.

Tupo viongozi wa aina nyingi, wengine wanaweza kuona tatizo na wakanyamaza lakini wanachukua hatua. Wengine wanaona tatizo watakemea lakini hawatachukua hatua. Lakini yeye ataona tatizo, atalikemea na atachukua hatua. Huenda labda hatua hiyo inafanya watu waone kama vile huyu bwana mbona spidi yake kali … mbona kama anakosoa mambo ya nyuma?

Sidhani kwamba anakosoa. Lakini, kuna ubaya gani kama anakosoa jambo ambalo halikuwa sawa?

Raia Mwema: Mwendo kasi huu mnauzungumza huko kwenye chama?

Kinana: Tunazungmza kwenye vikao vyetu kwenye chama. Serikalini tunazungumza, na hata bungeni watu wanazungumza. Wabunge wenyewe wanakosoa serikali yao, chama pia kinakosoa serikali yake.

Sidhani kama hili ni jambo kubwa isipokuwa tu kwamba halikuzoeleka kwa Rais kuzungumza moja kwa moja kwa uwazi kiasi hicho au kuzungumza wakati mwingine kwa ukali na kuzungumza kwa maneno ya mkato tofauti na tulivyozea.

Inawezekana wakati mwingine ikatafsiriwa isivyo lakini mimi nadhani Rais ana nia nzuri na nchi hii katika kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na maeneo anayoyatazama sana ni kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kudhibiti viongozi wanaotumia vyeo vyao vibaya, nadhani wakati mwingine kwa sababu anataka kuona matokeo ya haraka ya kuleta mabadiliko mazuri yenye nia njema huenda, wakati mwingine, ndiyo anaonekana kuwa na spidi kali na watu wengine wanajiuliza mbona anakemea sana?

Lakini lazima ukumbuke kwamba muda wenyewe ni miaka mitano tu. Ni muda mfupi na ameahidi mambo mengi sana. Sasa yeye mwenyewe akichelewachelewa atakuwa kwenye changamoto.

Mimi nina uhakika, kwa mfano, kama angekuwa anafanya mambo polepole katika kuyatekeleza, kwamba angekuwa amejikalia kimya, bila shaka watu hao hao wangesema aah Magufuli ni nguvu ya soda.

Kumbe ukifanya unaambiwa ooh unakosoa wenzako (waliotangulia Ikulu), ukikaa kimya wanakwambia nguvu ya soda. Sasa kati ya nguvu ya soda na kufanya haya anayofanya kipi bora?

Kila anachofanya (kiongozi) lazima kuna watakaopenda na watakaolaumu. Tuangalie nia yake njema na matokeo ya mambo anayoyafanya.

Ukitazama kwa mfano, wamefuta sherehe nyingi sana, fedha nyingi zimeweza kupatikana. Ni mtu anayehakikisha fedha zinazopatikana kwa njia mbalimbali kama kodi ziende katika matumizi ya wananchi, mimi nadhani tumuunge mkono, tumsaidie na tumpe moyo.

Anataka kurudisha au kuimarisha nidhamu ya utendaji serikalini, kwenye mashirika ya umma na kwenye maeneo mbalimbali.

Hivi sasa watendaji wote wa serikali wamekuwa na nidhamu ya hali ya juu, tofauti na walivyokuwa huko nyuma. Wanawahi kazini na wanawajibika vyema.

Vikao vingi vimepungua. Zamani ukienda ofisi nyingi kulikuwa na vikao vingi, lakini sasa vikao haviko na kila mmoja anachapa kazi.

Ameanza safari vizuri na ana nia njema, na safari ni ndefu, na mara nyingi mwanzo wa safari huwa mgumu. Naamini huko tuendako kila mmoja atakuja kumpongeza.

Na hatua zake hizo tayari zimeleta mafanikio. Tazama mpango wa elimu bure. Hiyo ni kati ya ahadi kubwa alizotoa.

Fedha zinatumwa wilayani na kwenye shule. Ni kweli elimu ni bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Na malipo ya madeni ya walimu, kwa kiwango kikubwa, yanakwenda vizuri.

Wote ni mashahidi, kulikuwa na tatizo kubwa la madawati. Lakini ilianzishwa nguvu kubwa ya utengenezaji wa madawati.

Sehemu kubwa kwa njia mbalimbali za kujitolea michango. Sasa tunaweza kusema bila kumung’unya maneno, kwamba tumepunguza kero ya madawati kwa kiwango kikubwa. Na sehemu nyingi nchini sasa tatizo hili haliko tena.

Lakini pia amepunguza matumizi ya serikali kwa kukata yale yasiyokuwa ya lazima na ya anasa, pamoja na kuondoa au kuahirisha sherehe zisizokuwa na ulazima.

Amechukua uamuzi mzuri kuhusu sherehe. Ni vizuri kuwa na sherehe hizi. Lakini wakati mwingine sherehe zikishakuwa nyingi zinatakiwa kupunguzwa ili kuepusha gharama, na bahati mbaya, wanaohudhuria sherehe hizi ni watu walewale wa siku zote.

Rais Magufuli amepunguza kwa kiwango kikubwa suala zima la safari za nje ya nchi ambazo huwa zinaingizia hasara kubwa serikali.

Ni kweli kutakuwa na umuhimu wa kusafiri, kama kwenda kuimarisha uhusiano na kuzungumza na marafiki zetu ambao tuko nao karibu, lakini vilevile tunatakiwa kutazama tija ya safari yenyewe na faida inayopatikana kupitia safari hiyo.

Bahati mbaya kuna watu wanapenda kusafiri bila ya kuwa na tija yoyote. Katika hotuba yake ndani ya Bunge alisema serikali inatumia zaidi ya Sh. bilioni 400 kwa safari za nje. Hizo ni fedha nyingi.

Ametekeleza miradi mikubwa ya miundombinu. Amefufua Shirika la Ndege la Tanzania na kuweka msisitizo katika kuanzisha mchakato wa ujenzi wa Reli ya Kati.

Reli hii itapita katikati ya nchi kwenye mikoa 18, ni reli yenye mchango mkubwa kwa uchumi na maendeleo ya nchi. Itakwenda katika nchi nne za Uganda, Rwanda, Burundi na DR Congo.

Ni reli muhimu na ina gharama kubwa, lakini Rais amedhamiria kila linalowezekana linafanyika kuhakikisha reli hiyo inajengwa na kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege.

Ameimarisha huduma za afya katika hospitali na hiyo imepunguza idadi kubwa ya Watanzania waliokuwa wakienda nje kwa matibabu.

Sasa, kwa tathmini hii fupi unaweza kuona Rais ni mtu wa aina gani kwa maana anasema tupunguze safari za nje na yeye mwenyewe kapunguza. Ndiyo maana unaweza kuona mpaka sasa amesafiri nchi tatu tu za Kenya, Rwanda na Uganda.

Ziara zake zinadhihirisha ya kuwa kipaumbele chake ni ujirani mwema, ushirikiano kiuchumi, kijamii, kisiasa, kibiashara na hizo ndizo nchi zilizopakana na Tanzania.

Na tusisahau kwamba haya anayoyatekeleza sasa hivi yanatokana na bajeti yake ya kwanza iliyoanza Juni mwaka huu.

Raia Mwema: Vyama vya Upinzani vinamlalamikia Rais Dk. Magufuli kwa kuzuia mikutano ya vyama hivyo?

Kinana: Nataka nijibu swali hilo kwa kurejea kwenye utafiti uliofanywa hivi karibuni na taasisi binafsi ya Twaweza.

Yapo mambo tisa muhimu yaliyojitokeza kwenye utafiti huo ambao kwa sehemu kubwa ulihusu masuala ya demokrasia na udikteta. Hapa nitazungumzia machache tu.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa Twaweza, wafuasi wa vyama vyote, saba kati ya 10 waliohojiwa, wanaikubali demokrasia kama mfumo bora wa utawala.

Asilimia 69 wanaielezea demokrasia kama mfumo unaokubalika zaidi kuliko aina nyingine za mifumo ya serikali huku asilimia 16 wakisema kuwa kuna nyakati ambazo utawala usio wa kidemokrasia unaweza ikakubalika.

Lakini pengine, jambo kubwa kabisa lililoibuliwa na utafiti huo wa Twaweza katika nyakati hizi ni la ushiriki wa vyama katika shughuli za kisiasa wakati huu ambao uchaguzi umepita.

Naomba kunukuu ripoti ya Twaweza kama ifuatavyo: “…lakini wananchi wamegawanyika kuhusu shughuli za kisiasa katika kipindi kisicho cha kampeni.

“Asilimia 80 ya wananchi wanasema kwamba baada ya uchaguzi, juhudi za kimaendeleo zipewe kipaumbele na vyama vya siasa.

“Kwa upande mwingine asilimia 86 ya wananchi wanasema Tanzania inahitaji vyama vya upinzani ili wananchi waweze kuchagua vema nani wa kuwaongoza.”

Ukiutafakari utafiti wa Twaweza, maana yake moja ni kwamba upande mmoja, watu wanapenda vyama vingi lakini pia wanapenda tukishamaliza uchaguzi mwelekeo uwe ni shughuli za maendeleo kwa sababu vyama vyote wakati wa kampeni viliahidi na kueleza katika ilani kwamba vingewaletea Watanzania maendeleo. Kwa hiyo, baada ya uchaguzi wanachotaka Watanzania ni huduma bora za kijamii kwa ajili ya maendeleo yao.

Lakini si hivyo tu, Tanzania si nchi pekee ambayo ina mfumo wa siasa za vyama vingi. Karibu nchi zote duniani, ukiondoa Cuba na Korea Kaskazini, na nchi za Falme za Kiarabu, Saudia, Kuwait, Qatar, Bahrain na kwingine, ni za vyama vingi na katika nchi hizo utaratibu ni kwamba uchaguzi ukimalizika, shughuli za siasa za majukwaani zinakwisha. Watu wanabaki kushughulika kujiletea maendeleo.

Chama kilichoshinda kinapewa nafasi ya kutekeleza ilani na ahadi zake. Vyama vingine vinajiimarisha na pengine kujiandaa lakini si kwa utaratibu huu tuliouzoea Tanzania wa kila chama kuzunguka nchi nzima kupotosha ukweli na kugombanisha wananchi, ambao walikwishakufanya uamuzi kwa njia ya upigaji kura, na serikali yao.

Juzi hapa nimesikia wenzangu wa vyama vya upinzani wanasema wanakwenda kuishitaki Serikali ya CCM kwa wananchi. Sasa unatushitaki kwa wananchi wakati wananchi hao hao ambao miezi michache iliyopita waliamua kuwakataa wapinzani na kukipa Chama cha Mapinduzi (CCM) dhamana ya kuongoza nchi?

Kwa nini mashitaka hayo yasisubiri ‘mahakama’ ya mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu? Ili kuwapa fursa Watanzania, wakati huo, waamue kama kweli tulichoahidi ndicho kilichotekelezwa.

Raia Mwema: Lakini kuna hoja kwamba kuzuia mikutano ya kisiasa kunakiathiri pia Chama Cha Mapinduzi?

Kinana: Ni kweli kwa kiwango fulani inatuathiri. Hata sisi ni lazima tupunguze shughuli za kisiasa ili kujikita zaidi katika shughuli za maendeleo. Lakini kwa upande wetu, tuna nafasi kubwa zaidi ya kusimamia serikali yetu kuhakikisha inatekeleza ahadi zake.

Kwa mfano, tuna utaratibu kwamba tunayo Ilani ya Uchaguzi ambayo inatekelezwa katika ngazi mbalimbali – vijiji, mitaa, kata, wilaya na mkoa.

Kila miezi mitatu kuna taarifa zinazotolewa katika vikao mbalimbali katika ngazi hizo kwa chama na Halmashauri Kuu ya CCM mkoa inapokea taarifa kutoka serikali ya mkoa juu ya utekelezaji wa Ilani katika sekta zote.

Halmashauri kuu za chini ya mkoa nazo zinapokea taarifa za utekelezaji. Kazi hizi lazima tuzifanye na viongozi wa CCM lazima wapite kuona kama ahadi zinatekelezwa.

Kwa hiyo, hiyo ndiyo kazi kubwa tuliyonayo, na wapinzani nao wamo katika maeneo hayo wanafuatilia kuona kama kile tulichokiahidi kimefanyika au hakijafanyika. Watakuwa na fursa itakapofika uchaguzi wa vijiji na vitongoji, uchaguzi wa serikali za mitaa na baadaye Uchaguzi Mkuu kusema hiki au kile CCM hawajafanya. Tupeni sisi ridhaa.

Lakini nenda kote duniani, nenda Marekani, Uingereza, Ufaransa, Afrika Kusini, Amerika ya Kusini na kwingineko uchaguzi ukiisha chama kilichoshinda kinapewa nafasi ya kufanya kazi na serikali ndiyo inayofanya kazi zaidi na chama kilichoshinda kinaisimamia serikali yake.

Vyama vingine vinasubiri uchaguzi ujao. Hatuwezi kuwa na mikutano ya hadhara kila siku, mwananchi badala ya kwenda shambani kwake leo anasikiliza mkutano wa Chadema, kesho mkutano wa CCM halafu mkutano wa CUF, NCCR … watu watafanya kazi za maendeleo wakati gani?

Raia Mwema: Marufuku hii ya mikutano ya siasa, imewafanya wapinzani kuunda kitu kinachoitwa Ukuta (Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania). Vinasema mambo yanasukumwa kiimla imla?

Kinana: Ukuta nitauelezea katika maeneo manne. Kwanza si jambo jipya, kabla ya Ukuta tuliwahi kusikia Operesheni Sangara. Sijui sangara aliishia wapi?

Aliliwa na mamba? Baadaye tukasikia M4C … hakuna lolote, sasa wamekuja na Ukuta.

Ukuta ni nini? Ni matokeo ya wapinzani kufedheheka kwa kushindwa kwenye uchaguzi. Mwanzo walisema wao watashinda uchaguzi. Tumekwenda kwenye uchaguzi tukanadi ilani na wagombea.

Fedheha ya kwanza, katika miaka 25 ya mfumo wa vyama vingi wamepata pigo jingine. Pili, wakasema hapana wameibiwa kura, Watanzania wakawapuuza.

Kuna siku nimemsikia Mwenyekiti wao (Chadema) Freeman Mbowe katika moja ya vikao vyao akisema hawakujipanga vizuri, hawakujiandaa vizuri na viongozi wa Chadema wakawa wanalaumu, maana yake ni kwamba alikuwa anakiri hawakujiandaa vizuri katika kukabiliana na CCM.

Sasa basi wao walitaka waendelee na ule utaratibu wa zamani wa kujipa uhai mkubwa zaidi. Baada ya uchaguzi waendelee kupiga maneno. Kupotosha wananchi. Kushutumu na kusema uongo, lakini kama takwimu zinavyosema Watanzania wanachotaka baada ya uchaguzi ni huduma za jamii kama afya, barabara na nyingine, hilo ndilo jambo kubwa kwao na muhimu zaidi.

Sasa kwa nini Ukuta ulibomoka? Walisema wangeandaa maandamano Septemba Mosi, wakapima hali ya hewa kwa wananchi na kubaini wananchi hawatawaunga mkono. Maandamano hayakuwapo.

Nimefuatilia. Mimi ni Katibu Mkuu wa CCM, kati ya kazi zangu ni kufuatilia, kwangu kunafanyika nini na kwa wenzangu kunafanyika nini?

Walichogundua ni kwamba; kwanza, wananchi wasingekwenda kwenye maandamano. Wasingeungwa mkono na maandamano yao yasingefanikiwa, kwa hiyo wangeadhirika. Wangepata aibu.

Ili kupata namna nzuri ya kuepuka aibu hiyo, waliwafuata viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali na kuwaambia jamani njooni tuzungumze mtusaidie kutoka hapa (kwenye mkwamo). Maelezo wanayotoa hadharani kwamba wamefuatwa na viongozi wa dini si ya kweli hata kidogo.

Wao ndio waliowafuata viongozi wa dini ili waingilie kati jambo hili na wao wapate mahala pa kupenyea na kuponea.

Raia Mwema: Hayo nyinyi mliyajuaje wakati ni ya wao na viongozi wa dini?

Kinana: CCM tuliyajuaje hayo? Baada ya wao kuzungumza na viongozi wa dini ambao ni pamoja na viongozi wa Kilutheri, Kiislamu, Kikatoliki na madhehebu mengine, waliwaeleza shutuma zao nyingi juu ya serikali, Rais John Magufuli na CCM.

Baadaye viongozi wa dini walituita sisi pia. Nilikwenda na maofisa wangu. Wakatuambia (viongozi wa dini) yafuatayo: jamani wenzenu (Chadema) wametuomba tuingilie kati jambo hili, wana malalamiko. Wanataka muwasikilize. Tukawaambia tupeni malalamiko yao. Wakatueleza.

Kwa hiyo kwanza tukagundua wao ndio wamewaita viongozi wa dini na wale viongozi wa dini wakasema maadam wenzenu wako tayari kuahirisha hili jambo (maandamano) na wanatafuta namna ya kuliahirisha, kwa nini nanyi msisaidiane nao ili kuahirisha?

Tukawaambia, jamani kama ninyi (viongozi wa dini) mnataka kuwasaidia kuepusha hii shari ni jambo jema, lakini ni vema nanyi muwaambie nao wawe wakweli. Kwamba wamegundua jambo hili lisingeweza kufanikiwa.

Viongozi wa dini wakatuambia jamani ni vizuri nanyi mtafute namna ya kuishauri serikali yenu ili jambo hili liweze kumalizika kwa amani. Basi, tukaeleza msimamo wetu kwamba jambo la kwanza, kilichowatoa bungeni ni hoja ambazo wangeweza kuzimaliza ndani ya Bunge.

Kanuni za Bunge zinawapa fursa kama wana hoja dhidi ya Spika au Naibu Spika. Wala wasingekuwa na haja ya kutoka nje ya Bunge.

Kanuni za kudumu za Bunge zinataja hatua za kuchukua iwapo mbunge ataona ya kuwa Spika au Naibu Spika hamtendei haki. Sehemu ya Pili ya kitabu cha Kanuni za Kudumu za Bunge, ibara ya tano kifungu cha kwanza kumetajwa jinsi ya utendaji wa Spika.

Vifungu namba nne, namba tano na namba sita, vinazungumzia hatua za kuchukua iwapo mbunge atahisi hatendewi inavyopasa na Spika au naibu wake.

Ngoja ninukuu vifungu hivyo uone; …kifungu cha nne; “…mbunge yeyote ambaye hataridhika na uamuzi wa Spika anaweza kuwasilisha sababu za kutoridhika kwake kwa Katibu wa Bunge ambaye atawasilisha malalamiko hayo kwa Spika.

Kifungu cha tano… Spika atawajibika kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge na kulijulisha Bunge kuhusu uamuzi utakotolewa na Kamati hiyo.

Kifungu cha sita… Spika au Naibu Spika hatakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge inapokaa kujadili uamuzi unaolalamikiwa, bali wajumbe watachagua Mwenyekiti wa muda kwa asilimia 50 za kura ya siri..”

Mambo hayo wanayajua, lakini walifanya kusudi. Walipojiondoa bungeni walifikiri wangepata umaarufu, lakini hawakuupata. Walifikiri wangeungwa mkono, lakini hawakuungwa mkono. Na haya ni matokeo ya kufanya mambo kwa kukurupuka. Huwa hawajipi muda wa kutafakari.

Raia Mwema: Unasema Ukuta ulikuwa ni mkakati wa kurejea bungeni?

Kinana: Unajua wamekaa nje ya Bunge kwa muda. Na hiyo ina athari kwa maisha ya wengi wao. Maana kama hushiriki shughuli za Bunge, kipato kinaathirika. Wamejiuliza sana, wanawezaje kurudi?

Wakatengeneza Ukuta. Wakaona umma hauwaungi mkono. Wakaenda kwa viongozi wa dini.

Wakatumia mgongo wa viongozi wa dini kuahirisha maandamano yao ya Septemba hadi Oktoba.

Oktoba ilipofika wakagundua maandamano hayawezi kufanyika. Wakasema wanakwenda kushitaki nje ya nchi. Sijui wamefikia wapi? Lakini kwa taarifa nilizonazo, hawakwenda.

Kwa hiyo mimi nadhani viongozi wa upinzani ni vizuri wakaacha kufanya kazi kwa vituko na matukio. Tatizo lao ni kwamba mambo yao mengi yanakwenda kwa vituko na matukio.

Utasikia Kamati Kuu ya Chadema inakutana, tutarajie mambo makubwa, baadaye hakuna lolote kubwa zaidi ya kutafuta vichwa vya habari tu. Ni vizuri wakaanza kufanya kazi kwa kuzingatia sera na kanuni. Vituko na matukio ni mambo ya kupita. Hufutika baada ya muda mfupi. Haki haitafutwi kwa maandamano na fujo.

Raia Mwema: Turudi kwenye CCM. Miezi minne imepita tangu Mwenyekiti mpya apatikane. Nawe umesema kwamba mnafanya tathmini ndani ya chama chenu. Tutarajie nini katika tathmini hii?

Kinana: Kwanza niseme kwamba kumtathmini Rais Magufuli katika miezi mitatu ya uenyekiti wake si kumtendea haki.

Ni muda mfupi sana. Lakini amechukua uenyekiti katika kipindi muhimu sana? Kwa nini?

CCM kimetoka kwenye uchaguzi mwaka jana na kila baada ya uchaguzi chama kina utaratibu wa kufanya tathmini ya kina, inayofanywa na chama pamoja na jumuia zake zote.

Lakini tathmini ya mwaka huu ni kubwa zaidi kwa sababu mwaka ujao, Februari, CCM kitakuwa kinaadhimisha kutimiza miaka 40 tangu kuzaliwa kwake.

Ni kipindi kizuri cha kutathmini chama chetu. Kuangalia muundo wake. Kuangalia ufanisi wake.

Kuangalia mafanikio yake. Kuangalia changamoto zake.

Kuangalia hali ya nchi kwa ujumla na namna watu wanavyokichukulia chama chetu. Kuangalia kukubalika kwake, lakini na kuangalia huko tunakokwenda katika miaka ijayo nini nafasi ya CCM?

La pili, tutakuwa tunaadhimisha miaka 25 ya kurejea kwa mfumo wa siasa za vyama vingi. Kwa bahati nzuri CCM kimekuwa kikipata ushindi katika chaguzi zote, katika uchaguzi wa vijiji na vitongoji na mitaa, ushindi wa ubunge na urais wakati mwingine ushindi mkubwa na wakati mwingine ushindi wa wastani. Lakini tumekuwa tukishinda katika nafasi zote.

Sasa ni wakati mzuri vilevile wa kujitathmini namna gani CCM kimeweza kufanikiwa katika chaguzi zote katika mfumo wa vyama vingi.

Kwa hiyo ni wakati ambao nasi tunapata fursa nzuri ya kujitathmini namna chama chenyewe kilivyotekeleza wajibu wake katika mfumo wa vyama vingi.

Lakini vilevile tumeongoza nchi hii kwa miongo mitano. Miaka 50 ni muda mzuri sasa wa kujitathmini juu ya namna tulivyoweza kuunda serikali, kusimamia ahadi zetu, kuwa karibu na wananchi, kusimamia shughuli za maendeleo na mambo mengine mengi.

Ni tathmini itakayoibua namna ya kuweza kuongeza ufanisi katika chama. Kuimarisha utendaji. Namna ya kupunguza matumizi. Kuimarisha uwajibikaji na uadilifu, lakini vilevile tutatizama namna gani chama chetu kinaweza kuwa imara zaidi kufanya kazi katika mazingira ya sasa ambayo bila shaka ni tofauti na mazingira ya miaka 40 iliyopita.

Raia Mwema: Bila shaka tathmini hii itazingatia pia kwamba kweli mnashinda lakini kura zenu zimekuwa mara zikipanda, mara zikishuka nyakati za uchaguzi.

Kinana: Lazima tutatilia maanani hilo. Kwa mfano, ukitazama mwaka 1995 Benjamin Mkapa alipata ushindi wa asilimia 61 baadaye akapata asilimia 72.

Mwaka 2005 Jakaya Kikwete alipata asilimia 80 baadaye akashuka akapata asilimia 61. Leo Rais John Magufuli amepata asilimia 58, haya ni mambo ambayo lazima tuyatafakari na itabidi tufanye uchambuzi wa kina.


Rai Mwema
 
Ukiona hivyo anatafuta namna ya kufuta dhambi zake asije akafa kama wenzake, hivi na yeye si yuko kwenye list ya watu waliomuita Lowasa ni mtu wa kufa??? CCM wanakana maneno yao leo! Wote hao waliomnenea Lowasa mabaya ya kifo ujue wako kwenye list, it is a matter of time tu. So far wameshaondoka kama sita hivi so who is next? Kinana mpigie magoti Lowasa
 
Ukiona hivyo anatafuta namna ya kufuta dhambi zake asije akafa kama wenzake, hivi na yeye si yuko kwenye list ya watu waliomuita Lowasa ni mtu wa kufa??? CCM wanakana maneno yao leo! Wote hao waliomnenea Lowasa mabaya ya kifo ujue wako kwenye list, it is a matter of time tu. So far wameshaondoka kama sita hivi so who is next? Kinana mpigie magoti Lowasa
Mkuu mbona mimi sikumbuki kama Mzee Kinana alinena hayo?
Zaidi nakumbuka alivyokuwa akimuonya Nape alipokuwa akimsema Mzee Lowassa ktk ile mikutano yao waliyozunguka nchi nzima kabla ya uchaguzi.
 
Lazima mjikombe kwa EL tu...
Kwa dhambi ambazo mlimfanyia... kashfa, chuki, fitina na matusi hamtasalimika kabisa.
Na kwasasa mnavyomwona Lowassa amezidi kuimarika ndio mnapagawa kabisa... kila mmoja anadai yeye ni rafiki yake...!!
The number is too long.. Let's wait and see who is next..!!
 
Naiona tamati ya Kinana kama Katibu mkuu wa CCM. Mahusiano ya karibu kwa awaye yote kwa Lowasa inaonekana kama kitu kisichompendeza mwenyekiti.
 
Ukiona hivyo anatafuta namna ya kufuta dhambi zake asije akafa kama wenzake, hivi na yeye si yuko kwenye list ya watu waliomuita Lowasa ni mtu wa kufa??? CCM wanakana maneno yao leo! Wote hao waliomnenea Lowasa mabaya ya kifo ujue wako kwenye list, it is a matter of time tu. So far wameshaondoka kama sita hivi so who is next? Kinana mpigie magoti Lowasa
Kinana ana matatizo yake sio hayo ya uswahili wa kumsemea vibaya mwenzake
Ukitaka kugombana naye wewe pita kwenye anga zake za Ndovu beer anagonga mvinyo huyo ,Tanzania nzima hakuna kwa mbali kidogo anafuatiwa na yule Mbunge wa Mbarali

Hata ile picha yake na Lowasa kwenye jubilee ya Mkapa ni jibu tosha
 
Na kwamba anajiandaa kujiunga na chama cha Lowassa baada ya kuujua ukweli na kukamilisha mipango yake ya kujiuzulu ndani ya gari bovu.
(Joke)
 
Naiona tamati ya Kinana kama Katibu mkuu wa CCM. Mahusiano ya karibu kwa awaye yote kwa Lowasa inaonekana kama kitu kisichompendeza mwenyekiti.

Nahofia mwenye kigoda asije akachukia hasira za Kihehe bure! Maana anguko kila mahali kama kimbunga cha sunami
 
Back
Top Bottom