Kilio Miamala ya Benki chatikisa nchi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,356
8,055
Tozo zilizoanza kukatwa kwenye miamala ya kifedha kupitia benki zimetajwa kuongeza makali ya ugumu wa maisha kwa watumiaji wa huduma husika.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kupitia gazeti la Serikali No.478 lililochapishwa Julai Mosi mwaka huu, alitangaza kuanza utekelezaji wa kodi ya miamala ya fedha kupitia benki.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa hatua ya Serikali kubuni vyanzo vipya vya mapato na Julai 15 mwaka jana, watumaji fedha kupitia simu za mkononi walianza kulipa kodi iliyotafsiriwa ni ya uzalendo.

Salome Shabani, mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, alisema hatua hiyo ya Serikali inazidisha ugumu wa maisha kwa wananchi na utawafilisi.

“Kwenye simu tayari nakatwa tozo, benki tulikimbilia kukwepa maumivu makali tena na huku wamekuja kutuwekea tozo, si sawa, eneo tunalopata unafuu wa maisha ndipo Serikali inakwenda kutuminya,” alisema.

Alisema kumsukumia mwananchi mzigo wa tozo ni kuendelea kumfanya aone maisha ni magumu zaidi, akisisitiza hakuna haja ya wafanyabiashara kuweka fedha zao benki kama wanahitaji faida.

Mariam Hussein, mkazi wa Tabata alisema Serikali kuweka tozo kwenye maeneo ambayo wananchi hupata huduma kwa urahisi, ni ukosefu wa ubunifu watendaji wa umma.

“Watu hawaumizi vichwa kuangalia ni namna gani watuhudumie wananchi, pale wanapoona tunacheka ndio wanakuja kutufanya tutoe machozi.

“Kila wakati wanafikiri kupata kidogo tulichonacho, kwa nini hao watumishi wa Serikali wasiache kulipana baadhi ya posho wakazielekeza kuboresha huduma za wananchi kuliko kutukamua kidogo tulichonacho,” alisema.

Alisema tayari kupitia mshahara wake anakatwa kodi, kwenye simu anapotoa au kutuma anakatwa tozo, kupitia luku ya umeme nako anakatwa kiwango kingine, akipendekeza Serikali itafute eneo moja la kuwatoza wananchi kodi na si kila eneo linafaa kutozwa tozo.

Joel Ulomi, mfanyabiashara mkazi wa Arusha, alisema japo nia ya Serikali ni nzuri, hasa kuboresha miundombinu, lakini mwananchi kuwekewa mlolongo wa tozo ni kuzidi kumuumiza.

“Dunia nzima inakwenda kidijitali, suala la kutuma miamala kwenye simu ilikuwa ni eneo ambalo wananchi waliliona kama kimbilio na kuacha kutuma fedha kwa njia ya mabasi, sasa tozo ilipoanza kuwepo tukahamia kwenye benki ambapo hakukuwa na makato.

Herry Mkunda, mkazi wa Dar es Salaam, alisema kipato cha watu kwa sasa kipo chini, maisha yamepanda na uwezo wa watu kupata kipato kutokana na shughuli mbalimbali umeshuka, hivyo kuongezewa tozo kunawafanya wapitie maumivu kwa kila shilingi wanayotumia.

Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema uwepo wa tozo hizo tayari alishalizungumzia na hawezi kuzungumza kwa mara nyingine, akisisitiza tozo hizo hazikuanza leo (jana).

Kauli ya Tucta

Akizungumzia hatua hiyo ya Serikali, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema tayari wameanza kulifanyia kazi na watatoa kauli yao.

“Jambo hili linawaumiza wafanyakazi kwa sababu mishahara yao inapita benki, tozo za simu zinamuumiza mfanyakazi, kwahiyo hata kile kinachoongezwa kwenye mishahara hakina maana sana kama tozo zinakuwa nyingi,” alisema.

Wachumi watoa tahadhari

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana alisema tozo hiyo itakuwa na madhara kwenye taasisi za kifedha, yaani benki.

Alisema kuwepo kwa tozo hiyo kutawafanya watu kutafuta njia mbadala ya kuhifadhi fedha walizonazo na kufanya malipo, akisisitiza uwezo wa kifedha wa benki utaathirika.

“Ni sawa na kuwepo kwa tozo kwenye simu, kiwango kikubwa cha fedha kiliondoka kwenye miamala iliyokuwa ikifanyika kwenye kampuni za simu,” alisema.

Alisema kuna hatari watu hawatapeleka fedha benki, hivyo kuna hatari ya uhalifu kuongezeka kwenye jamii, akisema nia ya Serikali kuweka tozo hizo ni njema lakini imekuwa ni mapema.

“Hatua hii inaweza kuchangia benki kuongeza kiwango cha riba na kupungua kwa uwezo wa taasisi hizo kukopesha wananchi.

“Serikali inachopaswa kufanya ni kubuni vyanzo vingine vya kodi ambavyo havina madhara ya moja kwa moja kwa wananchi, kudhibiti upotevu wa mapato kwenye maeneo ya bandari, kuhimiza uzalishaji kwa wananchi, kukaribisha uwekezaji kutoka nje, kwani kutaongeza wigo mpana wa Serikali kupata mapato,” alisema.

Profesa Semboja Hajji kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar, alisema, kuna wakati mwingine sheria zinatengenezwa bila kupitia mchakato wa kuzungumza na wahusika.

Alisema tozo hizi zimewekwa kipindi ambacho bidhaa mbalimbali wanazotumia wananchi zimepanda, hivyo ugumu wa maisha unaongezeka mara mbili kutokana na hali ilivyo sasa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Emmanuel Kwayu alisema ongezeko la tozo unalenga kuchukua kidogo walichonacho wananchi.

“Kwa upande mwingine, Serikali inategemewa kuimarisha ulinzi, elimu, huduma za maji na umeme hata barabara. Canzo cha mapato ya Serikali ni kodi,”alisema.

Alisema Serikali ikiacha kuwatoza wananchi kodi na tozo mbalimbali zipo huduma nyingi zitakwama na wananchi watailaumu serikali.

Chanzo: Mwananchi
 
Hapo dawa ni kususia tu kufanya miamala yoyote ile, na isiyo na ulazima ya kibenki.

Turudi tu kwenye vibubu.
Hatua kama hiyo waingereza wameichukua hivi sasa. Juzi nimeangalia kwenye WION wamepunguza sana miamala ya benki tozo zimezidi kiwango. Sasa ni cash kwa kwenda mbele.

Nikajisemea mwenyewe mbona hawa ni kama sisi tu?
 
Mwenye mchanganuo wa tozo za benki naomba anisaidie
 
Back
Top Bottom