SoC02 Kilio changu elimu yetu

Stories of Change - 2022 Competition

Alpha bartazary

New Member
Jul 5, 2022
1
1
Mara kwa mara mitaala ya elimu hufanyiwa marekebisho lakini bado haijakidhi wala kufikia robo ya matarajio kwa watanzania. Nilikaa nikatafakari nikagundua kuwa kuna mahali lazima hapako sawa.

Elimu yetu watanzania imeingiliwa sana na siasa kiasi ambacho kila kitu kinaenda kisiasa na mwisho wake tumebaki bila mwelekeo mzuri na dira hasa kwa kizazi hiki na kijacho kwani ndoto za wasomi wengi zilififishwa na nyingine kufa kabisa wakiwa bado hawajazifikia.

Kwa mfano, kwa utaratibu wa kawaida mtu anayemaliza kidato cha nne akifaulu vizuri hupelekwa sekondari za juu yaani kidato cha tano na sita kwa tahasusi mbalimbali kama vile PCM, PCB,CBGM,HGK,HKL,HGL,HGE,EGM,CBA,CBN, n.k lakini aliyepata ufaulu wa kawaida hasa daraja la tatu na la nne huweza kuchaguliwa kwenda vyuo vya kati kusoma aidha ngazi ya cheti au diploma.

Kilio changu kinaanzia hapa ambapo huyu aliyekwenda kusoma kidato cha tano na sita baada ya kumaliza masomo yake hanao Uwezo wa kusoma baadhi ya kozi kwa ngazi ya shahada ya kwanza kutokana na tahasusi yake haswa wakati anayetoka kidato cha nne kwa ufaulu wa chini D nne anaweza kusoma kozi nzuri ya ndoto yake lakini siyo aliyepita kidato cha sita.

Kozi nyingi zinazotolewa na vyuo vya Afya nchini kwa ngazi ya diploma wanahitaji ufaulu wa D kwa masomo manne na masomo hayo yasiwe ya dini. Lakini kozi nyingi za Afya kwa ngazi ya shahada ya awali humtaka mwombaji awe na ufaulu wa daraja la kwanza au la pili aliyesoma tahasusi za PCB na baadhi ya kozi chache huchukua CBG, CBN na PCM.

Masikitiko yangu na machozi yangu ni kwa huyu mtoto wa kitanzania ambaye hana uwezo wa kujilipia ada ya kusoma diploma nzuri ya ndoto yake akiwa ametoka kidato cha nne na amefaulu vizuri analazimika kwenda kidato cha tano na wakati mwingine kapangiwa tahasusi ambayo hata haipendi ila kwa kukosa fedha analazimishwa kusoma asichokipenda na hapa ndiyo mwqnzo wa kufa kwa ndoto yake ya kuwa mtu fulani.

Machozi yananitoka, sauti imekauka nashindwa hata kueleza ndugu jamaa na rafiki kwa njia ya masimulizi ya mdomo, na ninalazimika kuandika walau mtoto huyu wa kitanzania anayetoka familia duni zenye kipato cha chini aweze kutazamwa upya ili atimize ndoto zake kwani shida siyo kufaulu chida ni mfumo uliopo.

Alikuwa na ndoto ya kuwa muuguzi alipochaguliwa kwenda kidato cha tano akasoma HKL baada ya hapo ikabidi afanye shahada ya awali ya sheria, tayari huyu kapoteza dira ya ndoto ya maisha yake kielimu lakini angelikuwa na fedha angeweza kwenda kufanya diploma ya uuguzi na badaye shahada ya awali kwenye ndoto yake ya kuwa muuguzi.

Machozi yananitoka nikitazama hospitali zinakosa madaktari wa mionzi, lakini ni wale ambao walienda kidato cha tano wakasoma CBG, na CBA halafu baadaye mitaala ikawataka kufanya shahada zisizo za Afya kwa kigezo cha kwamba hawajasoma fizikia sekondari ya juu lakini wangelikuwa na fedha wangejiunga vyuo vya kati wakasoma diploma ya radiografia na badaye wangesoma shahada za ndoto zao za kuwa wataalamu wa mionzi.

Siasa ni nzuri, siasa siyo mbaya ila kwenye suala hili la elimu naona kuna haja ya kutupilia mbali siasa nyingi tupunguze siasa kwenye hili ili kilio changu hiki kikome kwani pasipo hivyo elimu yetu itakuwa haina manufaa katika kutimiza ndoto za watoto wengi wa walalahoi.

Fikiri kipato cha mtanzania wa hali ya chini, fikiri juu ya ada za vyuo vya kati ambavyo vinaweza kuwa ndiyo njia bora kwa watoto wengi wa walalahoi kufikia ndoto zao kwa kuepuka kwenda kidato cha tano ambako kumeua ndoto za wengi, nikitazama yote haya nalia nalia na ninaona hakuna mtu wa kuninyamazisha msiba huu mzito unaoliza moyo wangu kila asubuhi, mchana,, jioni na hata usiku.

Wahenga walisema "maskini akipata matako hulia mbwata" wako waliofanikiwa kutoka kwenye familia duni lakini wamekaa kimya wamesahau kilio walichokuwa nacho hapo kwanza na sasa wameshikilia mifumo na wanaona ni sawa tu kwani "Baada ya dhiki faraja" ila ni vema wajue " Ganda la muwa la Jana chungu kaona kivuno" hivyo watambue hawajafanikiwa ili wakae kimya kwenye siasa ila wamefanikiwa ili kuwatetea walalahoi na watoto wao juu ya hatima zao kielimu na nyanja nyingine zote.
 
Back
Top Bottom