Bismillahi naanza, wa Rehema Rahamani,
Wakili ulo muweza, Subihana Maanani,
Maliki mwenye kujaza, ya dunia na mbinguni,
Wabarakatau walid, mtetezi wa Kuduri!
Mtoto nipe kalamu, nikae chini nitunge,
Niyasema yalojimu, kwa tungo chache nipange,
Lile niloazimu, la mafisadi nilonge,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
Kikwete ataliweza, la kumfunga kengele,
Paka mwenye kujikuza, ajaye bila kelele,
Ili watu kuwajuza, hatari iliyo mbele,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
Au ndiyo imetoka, kama mabasi ya Keko!
Balali kishatimka, katuacha na mbeleko,
Mgonja akichopoka, kama kinyaa na toko,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
Mapesa wameyachota, Kikwete yu njia panda,
Ni sime atajikita, Jitu Pateli adunda,
Mwenye kupata kapata, walokonda wamekonda,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
Mramba mtapata, akaishie Maweni,
Au twacheza kalata, magelesha ni yanini,
Na wengine watanata, au ndiyo magirini,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
Beti zangu zinakoma, usingizi wanibana,
Nyani huyu twamkoma, si Ngabu hilo bayana,
Fisadi tutawazima, kama kupe kuwakana,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?