Mshitakiwa ajali ya Wangwe ajitetea
Aupinga ushahidi wa Serikali
na Rahel Chizoza, Dodoma
MFANYABIASHARA, Deus Mallya, anayekabiliwa na kesi ya kusababisha kifo cha Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, ameupinga ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka.
Akitoa utetezi wake jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Thomas Simba, Mallya alidai ushahidi uliotolewa mahakamani hapo dhidi yake unakinzana, hali inayomfanya ajione kuwa hana hatia.
Alidai katika mashahidi wote wa upande wa mashitaka, hakuna hata shahidi aliyethibitisha kumuona akiendesha gari wakati ajali inatokea na kueleza kushangazwa na kitendo cha kutoshitakiwa kwa fundi Israel Nyali, ambaye alitoa ushahidi kuwa ndiye aliyetengeneza gari kabla ya safari.
Mallya ambaye alidai kuwa yeye ni mfanyabiashara na mtaalamu wa kutengeneza picha za fulana, kofia, bendera na vitabu, alidai hana utaalamu wa udereva na hajawahi kuomba kazi ya kumwendesha mtu yeyote, hivyo ushahidi uliodai alikuwa akiendesha gari si sahihi.
Alidai ushahidi uliotolewa na shahidi huyo ambaye ni fundi unapaswa kutiliwa mashaka, kwani fundi huyo aliithibitishia mahakama kuwa hana cheti cha ufundi, hajui kama gereji anayofanyia kazi imesajiliwa na hakumbuki alisoma katika chuo gani.
Mheshimiwa hakimu upo uwezekano kuwa ubovu uliosababisha ajali, ulisababishwa na fundi ambaye hajui hata alisoma wapi? Hivyo nashangaa kushitakiwa peke yangu huku fundi huyo akiwa huru wakati inawezekana kabisa kuwa yeye ndiye aliyesababisha ajali, alidai Mallya.
Kuhusu shahidi aliyesema kuwa alikuwa wa kwanza kufika katika eneo la ajali na kumtoa marehemu katika gari baada ya kumfungua mkanda, alidai ushahidi huo unaonyesha kuwa Wangwe alikuwa akiendesha gari, kwani shahidi huyo alisema alimfungua mkanda marehemu Wangwe ukiwa umefungwa kutoka kulia kuelekea kushoto.
Gari la marehemu lilikuwa na usukani upande wa kulia, hivyo shahidi alivyosema marehemu alifungwa na mkanda kutoka kulia kwenda kushoto ina maana yeye ndiye alikuwa kwenye kiti cha udereva, alidai.
Deus ambaye alionekana kuwa mwenye furaha mahakamani hapo alidai kuwa taarifa iliyotolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali imeeleza kuwa mkemia alikiri kupokea boksi lenye vipande vya figo na ini la marehemu kwa ajili ya uchunguzi na kudai kuwa Januari mosi mwaka jana, ajali ilikuwa haijatokea.
Kuhusu ushahidi uliotolewa na mtoto wa marehemu Wangwe, Zakayo Wangwe, ambaye alikuwa shahidi namba moja wa upande wa mashtaka, alisema si wa kweli, kwani hakuwepo eneo la ajali.
Alidai licha ya kutokuwepo katika eneo hilo la tukio, shahidi huyo kwa namna yoyote ile ni lazima atamlinda marehemu Wangwe kwa kuwa ni mzazi wake na hakuweza kuithibitishia mahakama kwa kuonyesha cheti cha daktari kama baba yeke alikuwa mgonjwa kama alivyodai.
Pia Mallya alidai gari walilopata nalo ajali na marehemu Wangwe si mali yake, bali ni mali ya Halfan Bakari, ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam, ingawa ushahidi wa polisi ulisema kuwa walipata ajali na gari la marehemu.
Aidha, ushahidi wa picha uliotolewa kupitia ramani iliyochorwa katika eneo la tukio, alidai kuwa unaonyesha kuwepo kwa miti bila makazi, ingawa ilidaiwa mahakamani hapo kuwa eneo ilipotokea ajali hiyo ni eneo la makazi.
Mallya alikiri kufahamiana na marehemu Wangwe tangu mwaka 2005 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambapo kwa mara ya kwanza alimtengenezea vipeperushi vya kampeni za uchaguzi vilivyosomeka Mfahamu Chacha Zakayo Wangwe.
Alidai urafiki wake na Wangwe ulianzia hapo na kuendelea kumpa kazi mbalimbali ikiwemo kumtengenezea fulana zilizosomeka kwa maneno ya Changia Jimbo la Tarime kwa maendeleo ya Jimbo.
Baada ya kumaliza utetezi wake, wakili wa Mallya, Godfrey Wasonga, aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kufanya majumuisho ya kesi na kusubiri siku ya hukumu.
Hakimu Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo watafanya majumuisho ya kesi na kusubiri hukumu.
Ajali hiyo ilitokea Julai 28 mwaka jana katika Kijiji cha Pandambili, wilayani Kongwa, ambapo marehemu Wangwe na Deus Mallya, walikuwa njiani kuelekea jijini Dar es Salaam kwa gari T 865 AMR Toyota Corolla.
Source:
Mshitakiwa ajali ya Wangwe ajitetea