Kesi ya waliokuwa vigogo NIC yakwama mara ya pili mfululizo

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
Kesi ya kuchepusha fedha na kulisabishia hasara Shirika la Bima la Taifa (NIC) ya Sh 1.8 bilioni, inayowakabili washtakiwa saba akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Sam Kamanga, imeshindwa kuendelea mahakamani.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 18/2023 imeshindwa kuendelea leo Julai 5, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuleta mshtakiwa ambaye alitakiwa aongezwe katika kesi hiyo.

Mbali na Kamanga, washtakiwa wengine ni Tabu Kingu ambaye alikuwa Kaimu Mhasibu Mkuu wa shirika hilo; Victor Mleleu na Peter Nzunda ambao walikuwa wahasibu wa shirika hilo.

Washtakiwa wengine ni Kenan Mpalanguro ; Lusubilo Sambo na Mafworo Ngereji.

Wakili wa Serikali, Monica Ndakidemi ameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na walitaka kuongeza mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo, lakini mshtakiwa huyo yupo mahabusu kwa sababu anakesi nyingine ya uhujumu uchumi.

"Mheshimiwa…kesi hii iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka ulipanga kumleta mshtakiwa mwingine katika kesi hii kwa ajili ya kumsomea mashtaka, lakini tumeambiwa mshtakiwa yupo mahabusu kwa sababu anakesi nyingine ya uhujumu uchumu iliyopo mbele ya Hakimu Rhoda Ngimilanga wa Mahakama hii," amedai.

Amedai kutokana na sababu hiyo wanaomba Mahakama itoe ahirisho fupi hadi kesho ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Kutokana na hali hiyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Denis Msafiri, Hekima Mwasipu na Wema Kakomanga, walihoji sababu ya upande wa mashtaka kushindwa kumpeleka mshtakiwa huyo wakati kesi hiyo hata jana iliahirishwa kwa sababu hizo.

"Jana kesi hii iliitwa na haikuendelea ikapangwa leo na leo pia inaahirishwa, Mheshimiwa Hakimu tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi huyo mtu wamlete ili asomewe mashtaka yake kwa sababu jana wateja wangu walikuja mahakamani na leo pia amekuja mahakamani na kesi haijaendelea," amedai Wakili Mwasipu

Hakimu Kyaruzi baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa kesho wanamleta mshtakiwa huyo mahakamani ili aje asomewe mashtaka yake.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Kyaruzi aliahirisha kesi hiyo hadi kesho na ambapo mshtakiwa Maleleu, Nzunda, Mparanguro na Sambo wataendelea kubaki rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Huku mshtakiwa Kamanga, Kingu na Ngereji wako nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.

Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kuahirishwa ndani ya siku mbili kutokana na sababu hizo, kwani jana Julai 4, 2023 kesi hiyo haikuendelea baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa kuna mtu wanataka kumuunganisha katika kesi hiyo, hivyo waliomba ipangwe leo ili waweze kumsomea mashtaka.

Hata hivyo, leo pia kesi hiyo imeshindwa kuendelea kutokana na sababu hizo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka hayo 365, ambayo yapo ya kughushi nyaraka za uongo, kutakatisha fedha, kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa, kichepusha fedha, kuongoza genge la uhalifu na kulisababishia hasara shirika hilo ya Sh 1.8 bilioni.

Washtakiwa hao wanadaiwa katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili wote, inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya Januari Mosi 2013 na Desemba 31, 2018 katika maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam, Rukwa, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro na Kigoma.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom