Chuki za kidini ni mbaya hata kuliko VVU/UKIMWI. Kirusi cha uchomaji makanisa (udini) kilianzia Visiwani. Sasa maambukizi yanazidi kuenea: juzi yalifika Mbagala, utasikia Kigoma, Kariakoo,Tandika na kwingineko. Huenda maambukizi haya yakaenea hadi makambini(majeshini), mashuleni, maofisini, sokoni, sehemu za kazi zingine, mitaani hadi kwenye nyumba zetu ,kwani Wakristo tunaishi pamoja na ndugu zetu Waislam. Virusi hivi vitapiga hodi Ikulu, ndani ya baraza la mawaziri, bungeni , mahospitalini na sehemu zote nyeti. Hakuna eneo au kaya itakayosalimika iwapo maambukizi hayatadhibitiwa. Ukweli ni kwamba katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, kawaida hakuna mshindi. Ila faida kubwa huwaendea wauza silaha na zana zingine. Tunahitaji viongozi jasiri wa kiserikali, kisiasa, kijeshi na kidini wa kuiepusha Tanzania yetu na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vinatunyemelea.