MKUU WA MKOA WA NJOMBE, MHE. ANTHONY MTAKA, ASHIRIKI KILELE CHA MAADHIMISHO YA WIKI YA AFYA KITAIFA 2025 – NJOMBE YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA
Dodoma, Aprili 8, 2025
Na. Chrispin Kalinga
Maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Afya Kitaifa mwaka 2025 yamefanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, yakibeba kaulimbiu isemayo: “Tulipotoka, Tulipo na Tunapoelekea; Tunajenga Taifa Imara Lenye Afya.” Tukio hili limehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wataalam wa afya, wadau wa maendeleo pamoja na washiriki kutoka mikoa yote ya Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ameungana na viongozi wengine wa kitaifa kushiriki tukio hili muhimu akiwa ameambatana na viongozi kutoka Njombe. Miongoni ni: Eng. Joseph Mutashubilwa – Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Mhe. Juma Sweeda – Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Dkt. Juma Mfanga – Mganga Mkuu wa Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri za Njombe Mji, Njombe DC na Makambako, Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya ya Njombe, Makambako na Njombe Mji, Waganga Wakuu wa Halmashauri, Maafisa Afya wa Halmashauri, Waganga Wafawidhi wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya, Watendaji wa Vijiji na Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa.
Ushiriki wao umeonesha dhamira ya dhati ya Mkoa wa Njombe katika kuboresha afya ya jamii na mazingira bora kwa wananchi, sambamba na kuendeleza sera ya afya inayomgusa mwananchi moja kwa moja.
Katika kilele hicho, Mkoa wa Njombe umeibuka mshindi wa jumla wa mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa mwaka huu, baada ya kung’ara katika makundi mbalimbali ya mashindano. Taasisi kutoka Njombe zimepata ushindi katika zaidi ya makundi tisa, hatua iliyosababisha mkoa huo kutunukiwa gari aina ya Toyota Landcruiser Hard Top kama zawadi ya heshima.
Miongoni mwa washindi kutoka Njombe ni:
Halmashauri ya Mji wa Njombe
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe
Mtaa wa Nazareth na Mtaa wa Sido Njombe Mjini
Kijiji cha Ikuna na Kijiji cha Kidegembye Njombe DC
Shule ya Msingi Kakora
Shule ya Sekondari ya Wasichana Njombe
Hospitali ya Wilaya ya Njombe – Kibena
Ushindi huu mkubwa ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya viongozi wa mkoa, watendaji na wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera za afya na mazingira.