Julius Mtatiro, ameendelea na ziara ya kuwasaka watoto wachache ambao hawajaripoti wilayani Tunduru

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro, ameendelea na ziara ya kuwasaka watoto wachache ambao hawajaripoti wilayani Tunduru.

Mtatiro ametekeleza wajibu kwa kuzitembelea familia tatu ikiwemo familia ya mtoto Zawadi Mustapha Chiwaulo (miaka 14) ambaye anapaswa kuripoti Shule ya Sekondari Frankweston lakini wazazi wake wakampa kazi ya kutembeza mayai na kwa hiyo amekosa masomo kwa siku 45.

DC Mtatiro alifunga safari hadi nyumbani kwa mama mzazi wa Zawadi na kubaini kuwa mama huyo ni mtu anayejiweza na hana changamoto zozote.

Kisha akafunga safari hadi maeneo anakoishi baba mzazi wa Zawadi na kukuta yuko kijiweni anacheza bao.

Baada ya ufuatiliaji, Mtatiro amebaini kuwa baba mzazi wa Zawadi ameachana na mama ya Zawadi na kila mmoja ana mwenza mwingine.

Baba mzazi wa zawadi, Mustapha Chiwaulo ni fundi Majenzi mzoefu na anafanya miradi mingi Tunduru.

Mtatiro amekubaliana na wazazi wa Zawadi kuhakikisha Zawadi anaripoti shuleni kesho Jumatano kwa ajili ya kuendelea na masomo na tayari wazazi wake wameanza manunuzi ya sare za shule na madaftari asubuhi ya leo.


Mtatiro ameeleza mwaka huu 2024 watoto 4,952 wamepangiwa kujiunga na sekondari 28 za serikali wilayani Tunduru na hadi Februari 15, 2024 asilimia 92 ya wanafunzi wameshadahiliwa na wanaendelea na masomo, jambo ambalo amesisitiza ni rekodi ya kihistoria.

Mtatiro amewataka wazazi wa Tunduru waendelee kusimamia elimu ya watoto kwa kushirikiana na serikali na kwamba hatosita kuchukua hatua za kisheria kwa wazazi ambao watachezea elimu ya watoto wao.

Ali Kibwana,
Tunduru.
 
Back
Top Bottom