Jinsi Ya Kufokasi Katika Uwekezaji Wa Viwanja/Mashamba/Majengo

Aliko Musa

Senior Member
Aug 25, 2018
156
240
Kufokasi ni msingi mojawapo muhimu sana sana kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo. Bila kufokasi kwenye maeneo nitakayoainisha hivi punde haiwezekani kujenga himaya ya utajiri kwa wakati muafaka.

Fokasi ni kuchagua njia/mbinu moja ya kuwekeza kwenye ardhi na majengo mpaka kupata mafanikio ya kuweza kukuza njia nyingine ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

Fokasi ni kuchagua aina ya vigezo fulani vya kupata kiwanja au nyumba inayolipa bila kutamani viwanja vingine ambavyo havina vigezo vyako vya kiuwekezaji.

Fokasi ni kutokubali kumiliki viwanja au majengo nje na mpango biashara ulioandaliwa na timu yako ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

Fokasi ni kutumia ardhi na majengo kujitajirisha na kuacha njia nyingine zitumiwe na watu wengine. Mpaka uwekezaji wako uwe na uzao mkubwa sana wa kiuwekezaji.

Fokasi ni kuchagua na kulisimamia jambo moja mpaka likamilike bila kuacha. Fokasi ni kudumu kwenye mchakato wa kujenga mtandao bora sana (hasa mtandao mahalia) katika kipindi chote cha uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

Hii ni kwa sababu, bahati ya kupata viwanja au majengo yanayolipa sana hutegemea sana mtandao sahihi ulionao. Fokasi ni kuchagua kuwekeza nguvu zako na muda wako kwenye mambo ambayo unayafanya kwa ubora sana na kuacha mambo mengine wafanye wanatimu wako mahalia.

Fokasi ni kuchagua kumiliki nyumba chache ambazo hutengeneza kiasi kikubwa cha kipato endelevu na kuacha nyumba za kipato cha kawaida wamiliki wawekezaji wengine.

Fokasi ni kutafuta na kuchagua mashamba yanayoingiza kiasi kikubwa cha kodi kwa kila mwezi na kuacha wengine wamiliki mashamba ya kodi za viwango vya kawaida.

Fokasi ni kuendelea kukusanya mtaji fedha kwa ajili ya kuanza kununua, kuendeleza na kuuza viwanja bila kuanzisha biashara nyingine katikati ya mchakato wa ukusanyaji wa mtaji fedha.

Darasa la Jumatano hii litakuwa na kanuni muhimu mno kuhusu uwekezaji wa ardhi na majengo.

Unahitaji kipindi cha miaka mitatu (3) ili kujenga ubobevu kwenye wilaya moja unayowekeza kupitia umiliki wa ardhi na majengo.

Maeneo ya Kufokasi

Moja.

Nchi Moja Kwanza.

Kufokasi kwa kuwekeza katika nchi moja ni muhimu sana sana sana. Usiharakie kuanza kuwekeza nchini Kenya wakati hapa Tanzania umewekeza kwa udogo.

Jambo hili linawezekana kwa wale ambao hawachanganyi siasa na uwekezaji. Ukiamua kuwa mwanaharakati wa kisiasa, itakuwa vigumu sana kufokasi na nchi moja.

Kufokasi katika nchi moja ni lazima kwa yeyote anayetaka kujenga himaya imara ya utajiri bila kujali malengo makubwa alinayo.

Baadhi ya wawekezaji wakiona wamewekeza kwa mafanikio makubwa katika mkoa mmoja, huhamia nchi jirani na kuanza kujiita mwekezaji wa kimataifa. Ni kweli utakuwa mwekezaji wa kimataifa.

Lakini ni bora kuendelea kuitwa mwekezaji wa kitaifa, huku uwekezaji wako ukiendelea kukua. Unawekeza Tanzania, bobea kwanza hapa Tanzania. Kwa kufanya, utaweza kupata matokeo chanya kwa haraka na urahisi.

Baada ya uwekezaji wako kukua katika mikoa mingi, sasa unaweza kuanza kuwekeza kimataifa.

Mbili.

Wilaya (jimbo) moja tu.

Unatakiwa kufokasi kwenye wilaya moja au jimbo moja la ubunge. Wilaya moja inatakiwa kuuzaa faida ya kuwekeza katika wilaya nyingine. Kuharakia kuwekeza katika kila wilaya ni kukosa subira ya kiuwekezaji.

Katika kila wilaya kuna sehemu ambapo vyumba vya kupangisha vinalipa sana. Hivyo ni kazi yako kutafuta na kuhakikisha unafokasi maeneo mazuri tu. Baada ya kutengeneza mkondo wa kipato kikubwa, unahamia wilaya nyingine.

Kuhamia wilaya nyingine ni hatua nyingine muhimu sana. Ni hatua muhimu sana kwa sababu ni sehemu ya kutawanya uwekezaji wako wa ardhi na majengo.

Tatu.

Njia za kutengeneza fedha.

Unatakiwa kuendelea kufokasi katika njia moja ya kutengeneza fedha. Njia unayoitumia kutengeneza fedha, inatakiwa kukuzwa, kulelewa na ikomae kwa kukutengenezea kiasi kikubwa cha fedha (faida/kipato).

Faida ndogo unayopata kwa kununua na kuuza viwanja katika wilaya ya kinondoni. Faida hiyo inatakiwa kutunzwa na kuelelewa hapo hapo kinondoni. Baada ya faida yako kuzaa faida kubwa, sasa faida yako imekomaa inaweza kwenda wilaya nyingine na kuzaa faida nyingine.

Sio jambo la busara binti mdogo, kumbebesha mimba. Faida kidogo ni sawa na binti mdogo. Faida kubwa iliyopatikana kwa miezi michache ni sawa na binti mdogo.

Wote wawili hawana uwezo wa kubebeshwa mimba (kwa kuhamishia uwekezaji wako kwenda njia nyingine ya kutengeneza faida/kipato).

Mfano; kununua na kuuza viwanja. Unapata faida kwa kuuza viwanja. Jambo jema, lakini faida inatakiwa upatikane kwa angalau miaka miwili hadi mitatu. Hapa faida yako inakuwa imekomaa kiasi cha kuweza kuzaa njia nyingine ya kutengeneza fedha (mfano; kumiliki majengo ya kupangisha).

Nne.

Vigezo vya Kiuwekezaji.

Vigezo vya kiuwekezaji ni eneo lingine la kufokasi haswa. Kuna fursa nyingi katika wilaya uliyochagua. Lakini unahitaji fokasi ya vigezo vyako vya kiuwekezaji.

Mfano; kigezo chako ni kumiliki nyumba ya kupangisha inayoingiza kodi halisi (net rental income) za zaidi ya 15% kwa mwaka. Ni lazima ufokasi na kigezo hiki. Nyumba huwa zinapatikana hata za kuzidi hiyo asilimia.

Ninaandika mambo ambayo ninayaona kutoka kwenye uzoefu wangu. Mwezi desemba mwaka 2023, hapa Mbeya mjini nimepata nyumba tatu kati ya nyumba 20 ambazo nilizipata.

Hizo nyumba tatu zilikubali vizuri sana ile kanuni ya asilimia mbili ya bei kwa kila mwezi. Simamia vigezo vyako vya kiuwekezaji. Wakati kanuni yangu ni 100:10:3:1. Kanuni hii ina maana kuwa katika nyumba 100, ni nyumba moja tu ambayo itakubali vigezo vyako vya kiuwekezaji.

Usipokuwa na fokasi kwenye vigezo vyako vya kiuwekezaji, kila siku utajiambia NINGESUBIRI, NINGETAFUTA ZAIDI, n.k.

Tano.

Timu ya Uwekezaji Ya Muda Mrefu.

Timu za uwekezaji zipo makundi matatu;-

✓ Kundi la wanatimu wa mahusiano ya ndani (inner circle). Hili hujumuisha menta, mbia, mshauri mbobezi, n.k. Hili ni kundi ambalo unatakiwa kusafiri nalo kwa muda wa miaka mingi sana. Wawekezaji wenye mafanikio makubwa na yanayodumu hufanya hivi.

✓ Kundi la wanatimu wa mahusiano wa kati. Hawa ni wale ambayo unawahitaji mara kwa mara, lakini sio kwa kila kitu.

✓ Kundi la wanatimu wasaidizi (support circle). Hili ni kundi ambalo unalihitaji wakati ukiwa na changamoto ya aina fulani. Usipokuwa na changamoto, hutakiwi kuwa nao karibu.

Sita.

Aina ya Majengo/Viwanja.

Kuna viwanja vya matumizi yafuatayo;-

✓ Viwanja/majengo ya biashara pekee.

✓ Viwanja/majengo ya makazi na biashara.

✓ Viwanja/majengo ya makazi pekee.

✓ Viwanja vya matumizi maalumu kama vile kanisa au msikiti.

Kila majengo yana uzoefu wake na mbinu zake. Haiwezekani kutengeneza fedha nyingi kwa kutuma aina zote za majengo kwa wakati mmoja. Unahitaji kufokasi na aina moja au mbili tu.

Aina fulani ya majengo ikizaa faida/kipato kikubwa, ndipo unatumia faida/kipato hicho kikubwa kuanza kuwekeza katika aina nyingine ya majengo.

Saba.

Kutafuta wateja tarajiwa.

Unatakiwa kufokasi kwa kuendelea kutafuta wateja tarajiwa. Usije kwanza na kuniambia, nina wateja wengi nimeshindwa kuwahudumia. Wateja wengi wanatoa ishara kuwa uongeze idadi ya waajiriwa.

Huu ni msingi muhimu sana sana sana. Haiwezekani kujenga himaya imara ya utajiri huku ukipumzika kutafuta wateja wapya. Uchawi pekee wa kuongeza mauzo ni kuendelea kutafuta wateja wapya.

Ndiye aliyenipa msingi huu. Kutafuta wateja wapya ni jambo la lazima kwa mwekezaji anayeanza, mwekezaji wa kati na mwekezaji mwenye utajiri mkubwa.

Rafiki yako,

Aliko Musa.
 
Jamiiforum ingepata walimu na wachambuzi wa Mambo ya uwekezaji Kama ninyi kumi tu tungekomboa kikazazi chaleo na Lindi la umasikini
 
Jamiiforum ingepata walimu na wachambuzi wa Mambo ya uwekezaji Kama ninyi kumi tu tungekomboa kikazazi chaleo na Lindi la umasikini

Nashukuru sana kwa mrejesho chanya,

Naomba unisaidie kuwasambazia jamaa zako wa karibu wapate maarifa haya mazuri.

Yanaweza kuwa ni chachu ya kubadilisha kiasi cha kipato chao.
 
Back
Top Bottom