Nimefanya kazi kwenye kampuni mbali mbali za simu hapa nchini kwa muda wa zaidi ya miaka 10, kabla ya kuamua kujiajiri mwenyewe. Katika muda wote huo nimeshuhudia kampuni hizi zikiwaibia wateja kwa namna mbalimbali. Nimekaa na huu ushahidi kwa muda sasa lakini naona roho inanisukuma
niuanike hadharani mbele za watanzania ili wafunguke macho na kufahamu UFISADI huu unaofanywa na kampuni za simu hapa nchini. Nitaanika wizi wote kadri nitakavyoweza kuukumbuka hapa:
Huduma za bure
Kuna hizi huduma ambazo wanaziita huduma za BURE kana kwamba zinapatikana bure wakati si kweli! Kwa mfano, wateja hutumiwa SMS zinazowadanganya kwamba wanaweza kupata huduma za bure na ili wazipate wanaelekezwa kutuma ujumbe kwenda kwenye namba fulani. Na mteja akisharogwa akatuma ujumbe kwenda kwenye namba husika, imekula kwake! Nyingi ya huduma hizi zinzoitwa za bure hugharimu fedha na mara ujiungapo hujikuta unakatwa salio lako kimya kimya. Ni mara nyingi mtakuwa mmewahi kusikia mtu akilalamika kwamba salio lake limepungua
.unaweka airtime ya Tsh 1000 leo bila kuitumia, ikifika kesho unakuta zimebaki sh 350! Tsh 650 zimeenda wapi? Zimekatwa kwenye zile huduma za BURE ulizotangaziwa.
Promosheni feki
Promosheni nyingi zinazoanzishwa na makampuni ya simu zinalenga kuwanyonya na kuwakandamzia wateja. Mfano halisi ni pale wateja wanapotangaziwa kwamba huduma ya FESIBUKU inapatika bure! Thubutuuu! Hakuna kitu cha bure nchi hii, ndugu yangu. Huu ni wizi wa mchana! Kupona kwako ni pale utakapotumia hiyo huduma ukiwa hauna salio kwa kuwa huwezi kupata access ya huduma husika (kama vile fesibuku, twita, nk). Ikiwa utafungua huduma hiyo ukiwa na salio, salio lako lote litakombwa sawia! Kuna mtandao mmoja wa simu unajinadi kwamba unatoa huduma ya fesibuku bure wakati ni uongo mtupu. Ingia kwenye hiyo fesibuku uone utakavyoliwa fedha! Aidha kuna mtandao mmoja uliwahi kuwa na fesibuku ya bure siku za nyuma (kama mtakumbuka). Kwa muda fulani huduma hii ilikuwa ikipatikana bure kabisa. Kumbe ilikuwa ni janja ya nyani
..baadaye ile bure ilifutwa kimya kimya, wateja wakaendelea kukamuliwa kama kawaida na mpaka leo hawajawahi kuwataarifu wateja wao kwamba hiyo bure imesitishwa! Kuna wateja wengi sana, hasa wa kule vijijini, ambao wanaendelea kukamuliwa kwa kujidanganya kwamba huduma ni ya bure hadi leo, kumbe ilishasitishwa kitambo sana!
Ulaghai wa Kimangungo
Kuna wakati ambapo makampuni ya simu hupandisha tariffs kimya kimya bila kuwataarifu wateja wake na kuendelea kuwaibia bila kujua. Mwaka 2006 gharama za kupiga simu, kutuma sms na kutumia data zilipandishwa kinyemela na wateja wakaendelea kukamuliwa fedha kimya kimya hadi pale baadhi yao waliposhtukia dili na kuja juu. Aidha, prosheni fulani zinapoanzishwa, kama vile punguzo la gharama za kupiga simu nyakati za usiku, pindi zinafikia tamati wateja hawapewi taarifa na kujikuta wakitumia fedha zaidi ya matarajio yao. Promosheni inapoisha kampuni hizi huwakataza wafanyakazi wake wasiwaambie wateja ili waendelee kukamuliwa fedha kilaghai. Huu ni wizi, tena wa mchana na hauna tofauti na ufisadi wowote ule.
Kutotoa taarifa kwa wateja kwa makusudi
Wateja wanapojiunga kwenye vifurushi mbalimabli huletewa taarifa immediately via SMS kwamba wamefanikiwa kujiunga lakini kifurushi kikiisha ama wateja huchelewa kutumiwa meseji ya taarifa au hawatumiwi kabisa. Hili tatizo huwakumba zaidi wale wateja wanaopenda kubaki na salio kubwa kwenye simu zao. Kwa mfano, mtu unanunua vocha ya Tsh 2000 kisha unanunua kifurushi cha Tsh 500 na kubakiwa na Tsh 1500 kwenye simu. Pindi kifurushi cha 500 kikiisha hutatumiwa ujumbe wowote hadi utapokuwa umekausha 1500 zilizosalia kwenye simu. Huu pia ni wizi wa mchana na unaofanywa kwa makusudi na kampuni za simu hapa nchini. Ninao ushahidi usiokuwa na mashaka katika huu wizi wa makusudi.
Njia nyingine inayotumika kuiba hapa ni kutotoa call details pindi upigapo simu. Ukimaliza kupiga simu ukiangalia call details unakuta inasoma 00:00:00! Details hizi zinafichwa kwa makusudi ili kujenga mazingira ya wizi. Kwa mfano mtu unaongea kwa dakika 3, wao wanakata dakika 4.30 na kukuibia dakika 1.30! Matokeo yake unakuta muda wa hewani uliopewa wakati wa kujiunga umeibiwa na kampuni kwa maslahi yake binafsi. Lakini pia kuna wizi mwingine huu hapa: unaponunua kifurushi hupewa dakika ambazo ungetegemea zizotozwe kwa sekunde (per second billing) lakini badala yake hutozwa kwa dakika (per minute billing) kinyume cha mkataba kwa lengo la kumkamua mteja kiujanja. Huu ni wizi na haukubaliki hata kidogo.
Kuvuruga mawasiliano kwa makusudi
Kuna wakati wahandisi wa kampuni husika hupewa jukumu la kuvuruga mawasiliano ya wateja ili watumie muda mwingi na pesa nyingi kwenye maongezi. Inakuwaje hapa? Inakuwa hivi: Ukimpigia mtu yeye anakuwa anakusikia lakini wewe humsikii au vice versa. Hii husababisha kutumia muda mwingi kuelewana wakati huo salio likinyonywa kama kawaida hata kama mkichukua muda mwingi kuelewana salio hutafunwa sawia! Njia nyingine inayotumika hapa ni kuvuruga access to customer care ili unapokuwa umepatwa na tatizo usiweze kuwafikia watu wa huduma kwa wateja kupata msaada. Hii ndio sababu 90% ya wateja wenye matatizo genuine hawaipati namba 100. Mtu unaweza kupiga siku nzima na usiunganishwe kuongea na mshauri. Hatimaye wengi wao hukata tamaa na kuamua kukubali kuliwa!
Hii ni sehemu ya ushahidi ambao nimeukusanya while working with different mobile companies in Tanzania. Siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Nawasilisha.