Jini wa daraja la Salendar

Jini wa daraja la Salendar

JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.18.


“Kwa hiyo kuna umuhimu wa kwenda kwa mganga?”
“Ikiwezekana, lakini kwanza nenda kwa mwenzako ili umuulize kama kweli jana mlilala pamoja.”
“Mmh! Itabidi nifanye hivyo.”
“Asubuhi hii?”

“Sharifa siwezi kufanya kazi vizuri, akili yangu bado ipo njia panda ukweli wa kitu hiki nitaupata kwa Brighton.”
“Kazi?”
“Lazima niombe ruhusa, nimechanganyikiwa, sijui itakuwaje kama huyo jini atakuwa kanivaa na mimi?”

“Kama kukuvaa kakuvaa muda mrefu, sasa inawezekana ndiyo anajionesha kwamba na wewe upo kwenye mtandao wake.”
“Mungu wangu! Kama ni hivyo nitakuwa nimekwisha,” Suzana aliingiwa na hofu.
“Suzana acha kujikatia tamaa, hebu tafuta ukweli ili tujue tufanye nini, ikiwezekana twende leo leo, nitaomba ruhusa nikusindikize.”

“Basi wacha nikaombe ruhusa niende kwa Brighton nikapate ukweli, bila hivyo nitachanganyikiwa.”
“Haya shoga utanijulisha,” Suzana aliagana na Sharifa na kwenda kuomba ruhusa kisha alielekea nyumbani kwa Brighton.
***
Balkis akiwa amejilaza kitandani na Brighton, alimuona Suzana akielekea pale, kama kawaida yake alimueleza mpenzi wake:
“Suzana anakuja.”
“Umejuaje?”

“Nijue vipi, la muhimu jiandae kumpokea mpenzi wako.”
“Sasa nimpeleke chumba gani?”
“Mlete humu humu.”
“Wewe unatoka?”
“Niende wapi?”

“Si chumba wa wageni.”
“Mi sitoki, Suzana anakuja kukuuliza kama jana alikuja kulala hapa.”
“Umejuaje?”
“Nisikilize kwanza ndipo uliniulize maswali.”
“Mh!”

“Naomba unisikilize, ukijichanganya shauri yako.”
“Mbona unaniambia hivyo?”
“Ndiyo maana nakueleza, nisikilize kwa makini.”
“Sawa.”
“Suzana anakuja kuulizia kama kweli jana alikuja hapa, mjibu kuwa hakuja. Tumeelewana?”
“Lakini mbona mimi nafahamu jana alikuja?”

“Kama alikuja mbona asubuhi hukumuona?”
“Hata mimi nashangaa.”
“Wewe na Suzana mliota ndoto ya aina moja kuwa jana mlikuwa pamoja lakini kila mmoja alipoamka hakumuona mwenzake.”

“Balkis! Mbona unanitisha, wewe ni nani?”
“Kwani wewe unanionaje?”
“Nakuona mtu wa kawaida, lakini unayozungumza yananishangaza sana.”
“Mbona ya kawaida, ni kipawa ambacho mwanadamu hupewa na Mungu kujua yajayo.”
“Mmh! Nilikufikiria vibaya.”

“Ulinifikiria vipi?”
“Labda jini!”
“Brighton tokea lini jini akazungumza na mwanadamu?”
“Huwa nasikia majini huweza kujigeuza na kuwa wanadamu na kuishi nao.”
“Kama ningekuwa jini ungefanyaje?”
“Ningekufa kwa mshtuko.”

Mara kilipita kimya cha ghafla, kitu kilichomshangaza Brighton. Haukupita muda mlango wa chumbani uligongwa.
“Mkaribishe Suzana,” Balkis alimwambia Brighton aliyepatwa na mshtuko.
“Wapi?” Ilikuwa ajabu Balkis alizungumza kwa sauti ya juu, lakini Brighton aliuliza kwa sauti ya kunong’ona.

“Kuwa muelewa, nimekueleza mkaribishe humu ndani.”
“Ili atufumanie?”
“Ndiyo.”
“Ili iweje?”
“Utajua akiishaingia ndani.”

Sauti ya kugonga mlango iliendelea nje huku ikionekana kabisa kitendo cha kuchelewa kufunguliwa mlango kilimuudhi sana Suzana.
“Brighton kama hutaki nije kwako si uniambie kuliko kunifanyia visa?”
“Mkaribishe,” Balkis alimueleza Brighton kwa kumkaripia.
“Ingia,” alimkaribisha akiwa na wasiwasi mkubwa.

Suzana aliingia na kwenda kukaa kitandani, pembeni kabisa ya Balkis. Brighton alikuwa kama mtu aliyeshikwa na ganzi na kushindwa kuelewa kama mpenzi wake ameingia ndani. Suzana baada ya kuingia alimshangaa kwa mara nyingine.
“Brighton upo sawa?”

“Eeh.... aah.. Unasema?” Brighton alijikuta akibabaika kujibu.
“Makubwa ina maana hujaniona naingia?”
“Nimekuona.”
“Hata kunikaribisha? Kweli mapenzi yamekwisha,” Suzana alizungumza kwa sauti ya kilio.
“Suzana...,” Brighton alipotaka kusema alimtupia jicho Balkis aliyekuwa amejilaza pembeni ya Suzana huku akitabasamu.

“Brighton, una nini mpenzi wangu?”
“Si..si..sina,” majibu ya Brighton yalizidi kumshangaza Suzana.
“Kuna nini humu ndani, mbona sikuelewi? Jana nilikuja ukawa katika hali hii hii na leo tena, kuna kitu gani mpenzi wangu! Kwa nini hutaki kuniambia?”
“Brighton mkatalie kwamba jana hakuja hapa,” Balkis alimwambia kwa sauti aliyosikia Brighton peke yake.

“Brighton mbona kama haupo na mimi! Una nini mpenzi wangu?” Suzana aliporomokwa na machozi na kumfuata Brighton alipokuwa amesimama kama kapigwa na shoti ya umeme. Alianza kumpapasa huku akiendelea kumuuliza jinsi alivyoonekana mtu aliyehama kimawazo.

Je, nini kitaendelea? Brighton atamsikiliza nani kati ya Suzana na jini Balkis?








JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.19.


Brighton alikuwa kama yupo ndotoni akijiuliza yanayotokea mbele ya macho yake ni kweli au ni kiini macho. Chumbani kulikuwa na watu watatu, Balkis hakujificha zaidi ya kulala kitandani, tena peupe. Hata Suzana alipoingia, pamoja na kukaa pembeni yake hakuonesha kuona kitu cha tofauti mle ndani.

Alizidi kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda Balkis si kiumbe cha kawaida, hata sauti yake aliyompa maelezo bado ilionesha kuisikia peke yake. Kuhama kimawazo kulizidi kumnyima raha mpenzi wake ambaye naye alikuwa na yake yaliyotakiwa kupata majibu kutoka kwa Brighton.

“Brighton jana nimekuja hapa na kulala na wewe, lakini ajabu nilipoamka asubuhi nimejikuta nipo kitandani kwangu. Ni kweli jana nilikuja au nilikuwa naota?”
“Brighton, kataa! Sema hakuja?” Balkis alipaza sauti ya juu.
Lakini Brighton alijikuta mdomo ukiwa mzito kumjibu mpenzi wake huku jasho la hofu likimtoka.

“Brighton una nini mpenzi wangu, nijibu basi, si ni wewe ndiyo ulinipigia simu jana na kuniambia nije?”
“Brighton kataaa,” Balkis alizidisha sauti iliyoumiza ngoma za sikio.
“Brighton kuna nini hapo kitandani mbona unapaangalia sana, au kuna mwanamke?”
“Ha..ha..kuna..ki..”

“Brighton unafanya nini?” Balkis alipiga kelele iliyokuwa na mlio mkubwa kama radi iliyofanya ngoma za sikio za Brighton zisikie maumivu makali.
“Brighton mpenzi wangu una nini au umeshavamiwa na jini Balkis?”
“Nani?” Jina la Balkis lilimshtua.

Kauli ile ilimuudhi jini Balkis, akapuliza upepo uliompata usoni Suzana ambaye aliishiwa nguvu na kupitiwa na usingizi mzito. Brighton alimuwahi kabla hajaanguka chini na kumlaza kitandani pembeni ya Balkis.
“Suzana... Suzana,” alimwita kwa kumtikisa.

Suzana hakujibu kitu, alionekana mwenye usingizi mzito. Brighton alimuona Balkis jinsi alivyompuliza hadi kupitiwa na usingizi mzito.
“Balkis umemfanya nini Suzana?”
“Acha upumbavu,” Balkis alimjibu kwa hasira.

“Balkis mbona sikuelewi?”
“Hunielewi kivipi?”
“Itakuwaje umpulize mtu apoteze fahamu?”
“Nilikwambia nini?”
“Nilikwambia utoke, kwa nini hukutoka?”

“Mimi ni nani yako?”
“Kwa tabia yako ya miujiza siwezi kukuoa, unaonekana si mtu wa kawaida.”
“Unasemaje?” Kauli ile ilimchefua Balkis.
“Siwezi kukuoa.”
“Kweli?”

“Kweli,” Brighton alijibu kwa kujiamini.
“Asante.”
Baada ya kusema vile Brighton alishangaa kuona sura ya Balkis ikijikunja na kuwa kama mzee, uzuri wote ulipotea. Wasiwasi ilizidi kumjaa kwa kuamini huenda kweli Balkis si mwanadamu wa kawaida bali ni jini.

Baada ya kugundua kuwa Balkis si kiumbe wa kawaida, aligeuka ili awahi kuchukua Biblia ili amkemee, hakupiga hata hatua moja, mkono wa Balkis alinyooka na kuwa mrefu, ukamrudisha alipokuwa, kisha alimshika sehemu za siri na kuzivuta kwa nguvu kama anatoa kitu.

Brighton alihisi kama amepigwa shoti ya umeme sehemu za siri kisha alizisikia zikiwa za baridi kama zimetoka kwenye jokofu. Kwa sauti kali ya hasira Balkis alisema:
“Hutasimamisha milele, na mkeo hatazaa milele.”

Baada ya kusema vile aliingiza mkono sehemu za siri za Suzana ili amtoe kizazi, kabla hajamtoa Brighton alipiga kelele:
“Hapana, Balkis usifanye hivyo.”
“Lazima niwatie adabu, binadamu gani asiye na shukrani.”
“Nisamehe Balkis nipo tayari kukuoa.”

“Mpaka kwa shinikizo?”
“Siyo hivyo, mambo yako yananichanganya nashindwa kukuelewa wewe ni mtu wa aina gani?”
“Mimi ni jini?”
“Eeh!” Brighton alishtuka.
“Unashtuka nini, mimi ni jini la chini ya bahari.”

“Mungu wangu nimekwisha miye.”
”Uishe kivipi, katika muda tuliokuwa wote uligundua tofauti gani kwangu?”
“Sijagundua.”
“Penzi langu na wanadamu wenzio lipi lilikuwa tamu?”
“La kwako.”

“Mimi na mchumba wako nani mzuri?”
“Wewe.”
“Nani aliyesema kwamba Suzana hafai kuolewa?”
“Mimi.”

“Nilijitoa kwako ili kurudisha furaha iliyopotea, pamoja na kukubali kunioa bado nilimheshimu mpenzi wako, kosa langu nini?”
“Nisamehe.”
“Nitakusamehe, lakini nakurudishia ugonjwa wako ambao hautapona milele.”
“Nisamehe Balkis nilikuwa sijajua.”

“Hujajua nini?”
“Hata sijui nilimaanisha nini nimechanganyikiwa Balkis, nisamehe sana.”
“Mimi nakusamehe, lakini nakuacha na matatizo yako na mpenzi wako.”
“Hapana usinifanye hivyo.”
Balkis atamsamehe Brighton?
Tukutane baadae...........................
 
Mmmh na wewe jini nini?mwaya usijechukua alama zetu za vidole
 
JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.20 +21



"Nimekubali kuendelea kuwa na wewe Balkis usinifanye hivyo," Brighton alijitetea kwa kupiga magoti mbele ya Balkis.
"Kwa nini hutaki kunisikiliza?"
"Nilichanganyikiwa baada ya kukuona ndani, nilijua lazima Suzana atakuona."
"Nilikueleza mimi ni nani?"

"Jini."
"Jini huonekana kwa kupenda, Suzana asingeniona hata mara moja."
"Ningejuaje bila kuniambia?"
"Kweli kosa ni langu la kutokukueleza mapema, nitakurudishia nguvu zako na leo hii nitaondoka na wewe kwenda kwetu kuishi maisha mazuri."
"Wapi?"

"Ujinini," Balkis alizungumza kwa sauti ya upole huku akijirudisha katika hali yake ya uzuri wa shani.
"Na Suzana?"
"Mwache tu, sitamdhuru, nitamrudisha kwake akiamka atajikuta kitandani amelala."
Baada ya kusema vile alimkumbatia Brighton na wote walitoweka mle ndani na kutokea pembeni ya bahari maeneo ya Daraja la Salenda.

"Unanipeleka wapi?"
"Brighton mpenzi acha woga, tunakwenda kwetu chini ya bahari."
"Si nitakufa na maji?"
"Huwezi, ni sehemu nzuri sana ukifika hutakumbuka kurudi duniani."
"Nitaishi vipi na majini na mimi ni mwanadamu?"

"Kama nilivyokueleza majini tupo kama wanadamu wa kawaida na kufanya mambo kama ninyi."
"Mmh! Sawa."
Walitembea taratibu kuelekea ndani ya maji, Brighton alikuwa na wasiwasi wa kuzama, wasiwasi wake labda Balkis anataka kumzamisha na kumuua baada ya kuonesha kiburi.
"Balkis usiniue," alijitetea.

Balkis badala ya kumjibu alicheka sana, jambo lililozidi kumtisha Brighton, hakusimama aliendelea kusogea mbele katikati ya bahari akiwa bado amemshika mkono. Maji yalimfika magotini, tumboni yakaanza kuelekea kifuani mwishowe yakavuka mabega.
"Balkis naomba unisamehe usiniue kwenye maji."
"Brighton hakuna mtu anaweza kuitupa shuka yake wakati wa baridi."
"Una maana gani?"

"Wewe ndiye shuka langu, siwezi kukupoteza, bora nipotee mimi."
Wakati huo maji yalikuwa yamewafika chini ya kidevu, Balkis alimshika Brighton kichwani na kumzamisha ndani ya maji kwa nguvu, alitaka kupiga mayowe lakini alikuwa amechelewa. Aliposhtuka alijikuta wametokea kwenye mji mzuri ajabu.

"Brighton, karibu sana huu ni mji wetu, nawe utaishi kama mfalme, mimi ni mtoto wa Mfalme wa Majini. Baba yangu anaitwa Bashami Hudirud."
"Asante."
Walikuja vibaraka weusi kama wanadamu wa kawaida lakini miili yao ilikuwa na nguvu sana. Juu walikuwa vifua wazi na chini walikuwa wamejifunga shuka kama nepi wakiwa wameongozana na vijakazi waliojifunga shuka nyeupe na kuiacha migongo yao nje wakiwa wamebeba maua na farasi weupe wawili waliokuwa wametandikwa matandiko ya dhahabu.

Vibaraka wenye nguvu walimbeba Brighton na kumketisha juu ya farasi, baada ya kukaa walimbeba Balkis na kumketisha kwenye farasi mwingine aliyekuwa mzuri kuliko aliyembeba Brighton. Baada ya wote kukaa kwenye farasi, safari ilianza kuelekea kwenye jumba la kifahari.
Brighton alipatwa na wasiwasi kukuta mji unaosemwa ni wa majini ni mzuri ajabu na viumbe wake ni watu wa kawaida kama wa duniani. Ila njia nzima hakuna gari wala chombo chochote kinachotumia moto.

Alikaribishwa ndani huku akipigiwa muziki wa vyombo vitupu lakini ulikuwa mtamu masikioni. Kabla ya kuingia ndani lilitandikwa zulia jekundu ambalo hakuwahi kuwaza kulikanyaga katika maisha yake. Baada ya kuingia ndani alikaribishwa na wasichana wazuri waliovalia magauni meupe yaliyowapendeza, walimwaga maua ya kunukia.
"Brighton karibu kwetu," Balkis alimkaribisha Brighton kwenye sofa lililotengenezwa kwa manyoya ya kondoo.

"Asante," alijibu huku akikaa kwenye sofa lililomfanya ahisi usingizi.
"Jisikie upo nyumbani."
"Asante, mbona ni tofauti na nilivyofikiria?"
"Kuhusu nini?"
"Nilijua ninyi ni viumbe wa ajabu wenye mikia na meno ya kutisha, mbona ni binadamu kama sisi, kwa nini mnaitwa majini?"

"Majini ni viumbe wenye uwezo mkubwa wa kufanya jambo lolote tofauti na wanadamu. Lakini nasi tunamuabudu Mungu kama ninyi."
"Mbona mnaua watu?"
"Unatushangaa kwani hakuna wanadamu wanaoua wenzao?"
"Wapo."

" Mbona mnatushangaa sisi?"
"Lakini nasikia majini hutumika kuwaua watu?"
"Bado hakuna kitu tofauti na wanadamu, kuna wanadamu wachawi mbona hao hamuwazungumzii."
"Lakini mbona nasikia kuna majini kazi yao ni kuua tu sijui Jini Makata."

"Brighton hakuna wanadamu wanaotumwa kuua, hakuna majambazi wanaoua na kuchukua mali zao? Duniani sasa hivi kuna vita, wanadamu wanauana mamia kwa mamia bila sababu, hapo napo kuna majini?"
Swali lile lilimfanya Brighton akose jibu, Balkis aliendelea kuzungumza.

Je, nini kitaendelea?........TUKUTANE KESHO KWA MUENDELEZO WA STORY HII.........TUPIA MAONI YAKO HAPA?UMEJIFUNZA NINI?STORY UNAIONAJE? JE HAYA HAYAWEZI KUTOKEA KTK MAISHA HALISI?.....


JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.22






sorry ep.21 imefutika....

IIPOISHIA;
"Ewe mwanadamu, acha kumkosea heshima mtukufu mfalme, kila utakalojibu tanguliza neno mtukufu mfalme." Mkuu wa watwana alimkumbusha tena Brighton.
"Ndiyo mtukufu mfalme."
"Vizuri, Balkis."
"Mtukufu Mfalme."

"Unajua sababu ya kukutuma duniani?"
"Ndiyo mtukufu mfalme."
"Mbona imekuwa kinyume?"
"Mtukufu mfalme nimekwisha kujibu kila kitu."
"Bado hujanibu."

"Unataka jibu gani mtukufu mfalme?"
"Sababu kuu ya kukutuma huko, hujanijibu."
"Ni kweli mtukufu mfalme shida kubwa ni kuongeza familia yetu."
"Sasa kwa nini umekaidi amri yangu, nakuomba urudi duniani akaifanye kazi niliyokutuma." SASA ENDELEA...

"Mtukufu mfalme, kupitia huyu mwanadamu nitapata mtoto unayemtaka. Nina imani tatizo lilikuwa damu zetu kukosa virutubisho. Lakini damu ya mwanadamu huwa ina virutubisho vingi."
"Hatutaki mtoto mchanganyiko."
"Lakini mtukufu mfalme si atakuwa mwanangu?"
"Sipo tayari kuchanganya damu."

"Mtukufu mfalme, nami sipo tayari kumpoteza mpenzi wangu."
"Tunabishana?" mfalme Barami alikuja juu.
"Baba hatubishani, ila ukweli ni huo."
"Mwana wa mfalme mwite mtukufu mfalme si baba," mtwana mkuu, Kulani alimwambia Balkis aliyekuwa amemvunjia heshima baba yake na kusimama wima.

"Wewe nani unayeingilia mazungumzo na baba yangu? Nani kakupa ruhusa ya kunikemea. Huna heshima, kibaraka mkubwa wee," Balkis alimfokea mkuu wa watwana.
"Balkis umekosa heshima?" mfalme Barami alimfokea mwanaye.
"Sijakosa baba, natetea haki yangu."

"Kulaniiii, wachukueni mkawaweke kwenye chumba cha giza haraka."
Mfalme Barami alisema kwa sauti ya juu baada ya kumuona mwanaye amemvunjia heshima. Kulani na wenzake waliwabeba juu juu na kwenda kuwafungia katika chumba cha giza.

****
Suzana alishtuka siku ya pili na kujikuta akiwa amelala kwa mara nyingine kitandani kwake. Alijiuliza kuwa pale kitandani ni kweli au anaota, kumbukumbu zake zilimkumbusha kuwa jana yake alitoka nyumbani na kwenda ofisini na kisha alitoka.

Breki yake ya kwanza ilikuwa ofisini kwa shoga yake Sharifa na kumuelezea yaliyomsibu baada ya kulala kwa mpenzi wake Brighton, lakini ajabu siku ya pili alijikuta kitandani kwake. Alikumbuka baada ya kumuelezea shoga yake alimpa ushauri kabla ya kufanya lolote aende kwa Brighton kupata ukweli kama ni ndoto au kweli.

Suzana akiwa bado amekaa kitandani aliendelea kuvuta kumbukumbu ya mambo aliyoyafanya jana yake. Alikumbuka baada ya kushauriana na Sharifa aliaga kazini na kwenda moja kwa moja kwa mpenzi wake. Alipofika Brighton alionesha kubabaika hata majibu yake yalikuwa kama mtu aliyemfumaniwa.

Baada ya hapo hakumbuki kilichoendelea mpaka alipoamka na kujikuta tena kitandani kwake. Tukio la kujikuta kwake tena wakati anaamini jana asubuhi alikwenda kwa Brighton lilizidi kumchanganya akili.
Kabla hajafanya lolote simu yake iliita alipoangalia ilikuwa ya Sharifa, aliipokea na kuzungumza.

"Haloo Sharifa."
"Eeh, Suzy vipi, ndiyo ukaondoka kimoja na simu ukazima. Lakini hiyo ni tabia gani ukiwa na tatizo tuko pamoja likikuishia ananisahau?" Sharifa alilalamika upande wa pili.
"Najua utanilaumu bila kujua."
"Suzy hata kama ulichokifuata kimekwenda vizuri, kwa vile uliniacha na mimi na maswali ulitakiwa kunijulisha."

"Sharifa nashindwa sijui nikuambie nini?"
"Uniambie nini Suzy? Kitendo cha kukosa uungwana kwa kweli siyo kizuri hasa tukiwa watu wa karibu."
"Kabla sijakuambia kitu naomba nikuulize swali?"
"Uliza tu. "

"Ni kweli jana nilikuja ofisini kwako asubuhi?"
"Mbona unaniuliza hivyo?"
"Shoga yangu nina maana kubwa sana ya kukuliza hivyo naomba unijibu usinidanganye."
"Ni kweli ulikuja."

"Si nilikuja kukueleza maajabu yaliyonitokea nilipolala kwa mpenzi wangu na kujikuta kitandani kwangu?"
"Ndiyo."
"Ni kweli asubuhi sikufanya kazi nilikuaga nakwenda kwa Brighton."
"Ndiyo.""Basi dada yangu yaliyonitokea juzi kuamkia jana ndiyo aliyonitokea jana kuamkia leo."

"Una maana gani kusema hivyo?"
Suzana alimweleza yote aliyokutana nayo na siku ya pili alipoamka na kujikuta kitandani kwake.
"Suzana usiwe unachanganya mambo, pengine ulipotoka hapa badala ya kwenda kwa Brighton ulikwenda kwako ukalala na kupitiwa na usingizi mzito?"

"Sijafikia huko kiasi cha kupoteza kumbukumbuku hivyo, nilipotoka ofisini nilikwenda moja kwa moja kwa Brighton. Jamani hata kama nilirudi nyumbani asubuhi ile ndiyo nilale nishtuke asubuhi ya siku ya pili?"
"Mmh! Suzana kuna tatizo."

"Yaani huwezi kuamini sasa ndiyo inajidhilisha kuwa kuna kitu kinanichezea akili."
"Kwani Brighton yeye anasemaje?"
"Lazima na yeye atakuwa na tatizo, siku mbili hizi simwelewi kabisa, amekuwa kama mtu aliyechanganyikiwa."

"Suzana umezidi ubishi kila kitu nilikueleza, lakini hutaki kuamini wacha yakukute."

Suzana yupo njia panda anataka kujua yaliyomzunguka ni kweli au ni ndoto.









JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.23






"Tuache masihara, hebu nipelekwe kwa huyo mtaalamu, kilea kidonda mwisho kukatwa mguu."
"Leo ndiyo unagundua, nilikueleza toka mwanzo kuwa majini wana hadaa inayokuchanganya na mwisho wa siku wanakuingiza sehemu mbaya."
"Sharifa huu si wakati wa kunilaumu, nahitaji msaada wako la sivyo nitachanganyikiwa."
"Kama upo tayari, twende pamoja Bagamoyo."

"Lini?"
"Leo hii."
"Saa ngapi?"
"Safari yetu itakuwa saa tatu?"
"Basi shoga tutakuwa wote hali inatisha."

Walikubaliana kwenda wote Bagamoyo, baada ya kukata simu Suzana alinyanyuka kitandani ili kujiandaa na safari ya Bagamoyo.
Baada ya maandalizi waliingia kwenye gari kwenda nyumbani kwa Sharifa kumpitia kwenda kwa mganga Bagamoyo. Njiani alijitahidi kumpigia simu Brighton simu yake haikuwa hewani, aliachana naye na kuendelea na safari yake mpaka kwa Sharifa.

Aliwakuta wameisha jiandaa wakimsubiri, walipomuona tu hawakutaka kupoteza muda.
"Jamani tutatumia magari yote?" Suzana aliuliza.
"Hakuna haja ya kutumia magari yote, moja tu linatosha"
"Hakuna tatizo."

Walikubaliana kwenda kwenye usafiri mmoja walipanda kwenye gari la Sharifa na kuelekea Bagamoyo. Walitumia dakika arobaini na tano kufika Bagamoyo, walipofika waliuliza wenyeji sehemu aliyopo mganga Njiwa Manga.
"Samahani kaka," Sharifa alimuuliza kijana mmoja aliyepita karibu na mlango wa gari lake.
"Bila samahani dada yangu," kijana yule alijibu huku akisogea karibu.
"Habari za saizi?"

"Nzuri tu dada."
"Eti, Njiwa Manga anaishi wapi?"
"Njiwa Manga! Yupi, yule mganga?"
"Eeh, huyo huyo."
"Unaona hii barabara kubwa?"
"Ndiyo."

"Ifuateni, acha barabara ndogo mbili zinazokatisha kulia, ya tatu ufuate nenda moja kwa moja mpaka mbele utaona kuna nyumba ina bendera nyekundu hapo hapo kwa mzee Njiwa Manga."
"Asante," Sharifa alishukuru huku akimpa elfu mbili.
"Nashukuru dada yangu."

Waliachana na yule kijana na kufuata maelekezo yake, walipofika barabara ya tatu inayoingia kulia waliifuata na kwenda mwendo kidogo mpaka kufika kwa mganga Njiwa Manga. Walipaki gari sehemu iliyo salama na kutelemka, ilikuwa sehemu yenye eneo kubwa lililokuwa na nyuma kubwa moja na pembeni kulikuwa na mabanda madogo.
"Karibuni," binti mmoja aliyekuwa amevalia gauni refu na kitambaa kichwani aliwakaribisha.
"Asante," waliitikia kwa pamoja.

"Karibuni kwenye benchi hapo chini ya mti."
"Asante," walikwenda wote kukaa chini ya mti kusubiri maelekezo.
Ilipita zaidi ya saa nzima bila kupata maelezo yoyote zaidi ya kukaribishwa kana wageni wengine na kuonesha sehemu ya kukaa.

"Samahani dada," Sharifa alimwita yule msichana aliyewakaribisha na kuendelea kuwakaribisha wageni wengine kama watatu, mmoja alikuja na gari na wengine wawili walikuja kwa miguu kuonesha walikuja na usafiri wa daladala.
"Bila samahani," alisema huku akisogea kuwasikiliza.
"Eti mganga tumemkuta?"

"Yupo, kama asingekuwepo nisingewaacha mkae mpaka muda wote huu."
"Kwa hiyo tutaonana naye saa ngapi?"
"Mmh! Sijajua ila si muda mrefu, leo hakuna wagonjwa wengi."
"Wengine wapo wapi?"
"Wapo ndani, wakipungua nanyi mtaingia."

"Haya," waliachana na yule msichana aliyerudi sehemu yake kusubiri wateja wengine.
Baada ya nusu saa waliitwa ndani, wakati huo ilikuwa imefika saa tatu na nusu asubuhi. Waliongozana wote watatu mpaka kwenye sebule kubwa iliyokuwa imetandikwa zuria bila kiti. Baada ya kuketi msichana aliyewafuata aliingia chumbani na kuwaacha wasubiri.

Ilipita kama robo saa tena waliitwa ndani, waliingia wote watatu. Chumbani kulikuwa na mzee wa makamo aliyeonekana kula chumvi nyingi kutokana na kuenea mvi sehemu kubwa ya nywele zake. Alionekana ni mtu wadini kutokana na mavazi yake ya kanzu iliyokuwa nyeupe sana na juu alivalia kilemba cheupe. Pembeni yake kulikuwa na msahafu.
"Asalamu aleykum," mama Sharifa alimsalimia mganga.

"Waleyku msalamu, karibuni."
"Asante," waliitikia kwa pamoja.
"Shikamoo," Sharifa na Suzana walimwamkia mganga.
"Marahaba mabinti zangu, karibuni."
"Asante."
"Haya, mna shida gani?"

"Kuna vitu vimewatokea mabinti zangu, mpaka sasa vinawachanganya, japo kuna sehemu tulikwenda na kuelezwa tatizo lao, mmoja hakuwepo na mwisho wa yote ilionesha tatizo lile kwa upande wake ni zito hivyo alituelekezwa kuja kwako," mama Sharifa alitoa maelezo mafupi.
"Mmh, nimekupateni, nipe majina yao."

Nini kitaendelea, watapata msaada kwa mganga Njiwa Manga?


Jini la daraja la salenda -24


ILIPOISHIA:




"Haya, mna shida gani?"
"Kuna vitu vimewatokea mabinti zangu, mpaka sasa vinawachanganya, japo kuna sehemu tulikwenda na kuelezwa tatizo lao, mmoja hakuwepo na mwisho wa yote ilionesha tatizo lile kwa upande wake ni zito hivyo yule tuliyemwendea alituelekeza tuje kwako," mama Sharifa alitoa maelezo mafupi.
"Mmh, nimekupateni, nipe majina yao." SASA ENDELEA...

"Naitwa Sharifa."
"Jina la mama yako?"
"Habiba."
"Mmh! Na wewe mama?"

"Naitwa Suzana."
"Jina la mama?"
"Monika."
"Vizuri."

Baada ya kuyaandika majina yale kwenye karatasi nyeupe kwa kutumia wino mwekundu, mganga alifungua kitabu kimoja na kutafuta sehemu ya kusoma,alipoipata aliisoma kimya kimya huku akiandika baadhi ya vitu alivyoviona kwenye kitabu kile katika karatasi kwa lugha ya kiarabu.

Baada ya robo saa ya kutulia na kusoma huku akiandika, alikohoa kidogo na kusema:
"Nimeona vizuri, nina imani yaliyosemwa na mganga aliyetangulia yapo vile vile."
"Haa! Ina maana kweli sina kizazi?" Sharifa alishtuka kusikia vile.

"Ni kweli huna kizazi, kilichoelezwa na mganga wa awali hakuna kilichopungua kwako wala kuzidi. Ila kwa Suzana yeye yake yameongezeka."
"Eeh?" Suzana alishtuka.
""Ila msiwe na wasiwasi"
"Ninaweza kupona?" Sharifa aliuliza.

"Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu."
"Na mimi matatizo yangu?" Suzana aliuliza.
"Ni kweli kuna mambo yanaonesha hapa yamekuchanganya na kushindwa kuelewa ni kweli au ni ndoto?"

"Ni kweli mzee wangu," alijibu Suzana.
"Kilichotokea kwako ni kweli wala siyo ndoto, ni kweli ulilala na mpenzi wako na asubuhi ulipoamka ulijikuta ukiwa kwako. Pia, jana ulipokwenda kuulizia yaliyokutokea juzi kama ni kweli, ulishangaa alfajiri ya leo kujikuta upo tena kwako kitu ambacho kimekuwa kikikuchanganya sana.

"Ukweli ni huu, anayewasumbua ni jini la kike linaitwa Balkis, jini huyu yupo chini ya bahari akiwa mtoto wa kwanza wa mfalme wa majini yaliyoko huko. Baba yake anaitwa Barami Hudirud. Wakati alipotakiwa kuolewa alionekana hana kizazi hivyo alipewa kazi ya kuja dunia kutafuta vizazi vya wanawake mia moja kama dawa ya kumuwezesha kushika ujauzito.

"Kazi ile aliianza muda mrefu kwa kuja kwa nadra duniani, sehemu yake kubwa ilikuwa Daraja la Salenda ambako aliwaingia wanawake na kwenda nao makwao, usiku alivichukua vizazi vyao na kurudi chini ya bahari. Kazi ilionekana ikienda taratibu mno, hivyo wazazi wake walimuomba aje rasmi duniani ili aweze kupeleka kwa urahisi vizazi vya wanawake wengi na kumfanya awahi kufunga ndoa.

"Siku ambayo uliona sherehe ya ajabu ndiyo ilikuwa siku rasmi ya jini Balkis akiagwa kutoka chini ya bahari kuja duniani.

"Katika watu mwenye bahati ya kuiona sherehe ile ni wewe na ndiye uliyemvutia jini huyo hadi akaamua kukufuatilia kila ulichokuwa ukikifanya, alipomuona mchumba wako alivutiwa naye, ili ajue siri yako alianzisha uhusiano na mchumba wako bila ya yeye kujua kwa kufanya naye mapenzi kwenye ndoto.

"Alifanikiwa kuwapotezeni kwenye ukumbi wa starehe, shida yake kubwa ilikuwa kukuchukua na kwenda kukuficha chini ya bahari ili aweze kuishi na mchumba wako kwa sura yako. Lakini alipokupeleka alikataliwa na wazazi wake kwa vile sicho kitu alichotumwa.

"Ile ndiyo iliyokusaidia kurudi duniani bila hivyo ungejulikana kuwa umekufa.
"Baada ya kukurudisha aliingia nawe katika vita nyingine ya kuchangia mapenzi, baada ya kuona mapenzi ya mchumba wako yote yapo kwako.

"Aliamua kumuondoa nguvu za kiume ili msiweze kufanya tendo lile na yeye alikuja usiku na kufanya naye huku akiwa amemrudishia nguvu zake kamili.

"Lakini la kuja usiku ndotoni hakulipenda, alitaka aje kama mwanadamu wa kawaida na kufanya mapenzi ya kawaida ya kutambuana na siyo ya ndotoni.

"Aliweza kujitokeza hospitali, mpenzi wako hakujua kama yule ni jini, alimuona kama mwanamke mzuri na kumpa tiba ya ajabu iliyomponya kwa kuzirudisha nguvu zake za kiume.

"Bila kujijua mchumba wako akaingia kwenye mtego wa kukubali kuanzisha uhusiano naye, kwa makusudi alipotoka hospitali alikwenda kumsuburi njia aliyojua atapita.
"Baada ya kutoka hospitali, alimtafuta bila kumuona na kujikuta akitamani kuonana na mrembo yule tena.

"Wakati anatoka hospitali alikupigia simu mkutane nyumbani ili kukuondoa majonzi yote kutokana na kushindwa kukufikisha katika tendo la ndoa. Hata alipokueleza hukuamini, lakini alikuhakikishia kitu kilichokufanya uahilishe safari ya kwenda kwa mganga kumuangalizia matatizo yake.

"Nina imani mmebahatika kumuona Balkis jinsi alivyo mwanamke mzuri sana, ambaye hakuna mwanaume atakayemtaka akamkataa. Mchumba wako akaingia kichwa kichwa kumtaka kimapenzi, naye kujifanya kana kwamba hana shida na mumeo.

"Lakini alimuuliza maswali, kama mumeo angekuwa na akili angetambua kuwa yule si mtu wa kawaida."

Mambo yanazidi kufunguka, endelea kujua wasifu wa jini Balkis, nini kitaendelea? Kuyajua yote tukutane baadae
 
JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.25+26

LIPOISHIA:
“Nina imani mmebahatika kumuona Balkis jinsi alivyo mwanamke mzuri sana, ambaye hakuna mwanaume atakayemtaka akamkataa. Mchumba’ako akaingia kichwa kichwa kumtaka kimapenzi, kana kwamba hana shida na mumeo, alipoonesha dalili za kumtaka alimuuliza maswali ya mitego, kama angekuwa na akili angetambua kuwa yule si mtu wa kawaida. SASA ENDELEA...

Lakini kutokana na kuchanganyikiwa na mapenzi, hakupata muda wa kujiuliza, Balkis alimuuliza maswali kuhusiana na uhusiano wenu, hakushangaa mtu kuonana naye mara ya kwanza kumuulizia vitu ambavyo hata watu wenu wa karibu hawajui.

Alipomuulizia kuhusu kumtaka yeye wakati wewe ni mchumba wake, mwenzio alikukana na kusema kuwa wewe ni mpenzi wake si mke wake. Alipoulizwa kama yupo tayari kuoa mwanamke mwingine na kuachana na wewe, kutokana na kiwewe cha mapenzi alikubali kuwa yupo tayari na kuusema udhaifu wako.

“Alipoulizwa tena yupo tayari kumuoa yeye Balkis alikubali. Aliutumia udhaifu wa mchumba wako kujenga uhusiano wa haraka na kutaka kuwa naye siku ile, pia alikubali. Walikubaliana kwenda nyumbani kwa mchumba wako, ili kutowagonganisha, mchumba wako alitaka kukupigia simu ili usiende, lakini Balkis alimzuia asikupigie simu na kukueleza uende na ulipokwenda ulimuona jinsi alivyobabaika baada ya kuingia na kwenda moja kwa moja chumba cha wageni alichokuwa ameingia Balkis muda ule ule. Ulishtuka baada ya kumuona ameingia ghafla chumbani, ni kweli?”

“Ni kweli,” Suzana alijibu kwa sauti ya chini huku akiwa anaona muujiza mkubwa kutokana na maneno ya mganga ambayo mwanzo aliyaona kama simulizi ya kusisimua isiyo na ukweli. Lakini swali lile lilikuwa kama kitu kilichomtoa kwenye bumbuwazi.

“Basi kitendo cha kuingia na kwenda moja kwa moja kilimtia wasiwasi mkubwa mchumba wako kwa kujua lazima utamkuta Balkis na kumfumania. Hata lugha zenu ziligongana kitu kilichokushangaza. Kingine kilichokushangaza kilikuwa kwa mpenzi wako kuwa tofauti na siku zote kukujibu kwa ukali jambo la kawaida.

Baada ya kumuona humuelewi, ulikwenda chumba cha kulala, yeye alirudi hadi chumba cha wageni na kushangaa kumkuta Balkis akiwa amejaa tele kitandani. Alipotaka kujua alikuwa wapi alimwambia akuwahi chumbani ili akurudishe kwenye hali ya kawaida.

Baada ya kuingia chumbani, penzi alilokupa ndilo lilikuchanganya na kusahau yaliyotokea muda mfupi. Usiku jini Balkis alikuja kukuchukua ukiwa usingizini na kukurudisha kwako na yeye kulala na mchumba wako mpaka asubuhi. Wote mlipoamka mlishtuka lakini hakuna aliyejua ukweli wa tukio la usiku ni kama ndoto au kweli.

Ulipokwenda kwake asubuhi ya jana kupata uhakika kwa kilichotokea, ndani walikuwa mchumba wako na Balkis, ndiye aliyemweleza ujio wako. Ulipofika alikuwa mule mule chumbani amelala kitandani. Wewe hukumwona ila mwenzako alimwona kama kawaida, kitu kile ndicho kilichompa kigugumizi.

Hali ile ilikuchanganya na kumuona kama mtu mwenye matatizo, wakati huo Balkis alimwambia mchumba wako kwa sauti ya juu ya kumkemea kuwa akikuuliza useme hukuja jana ili ujue kilichotokea si kweli bali ni ndoto.

Lakini kwa yeye kuwepo pembeni ya kitanda karibu na Balkis aliyekuwa amelala pembeni yako bila wewe kumuona, ilizidi kumchanganya.

Mchumba wako alipatwa na kigugumizi kwa kujua utanamuona Balkis, kubabaika kwake kulikufanya umtilie wasiwasi na kumuuliza swali ambalo lilimchanganya pale ulipotaja jina la Balkis kama jini, jina ambalo lilikuwa la mpenzi wake, kumtaja kama jini ilimuudhi sana Balkis na kukupuliza upepo uliokufanya upoteze fahamu.

Kitendo kile mchumba wako alikiona na kumpandishia na kutaka kujua amekufanyia nini, Kauli ile ilimfanya Balkis kukasirika na kuondoa nguvu za kiume za mchumba wako na kutaka nawe kukutoa kizazi.”

“Mama yangu!” Suzana alishtuka na kushika mdomo kusikia vile.
“Usiogope, hakukutoa kizazi baada ya mchumba wako kumuomba msamaha na kuwa tayari kumuoa baada ya kumkataa kutokana na vitendo vyake visivyo vya kawaida. Baada ya Balkis kumsamehe aliamua kuondoka naye kwenda kuishi chini ya bahari.”

“Mamaaa!” Suzana alipiga mayowe ya mshtuko.
“Mungu wangu unataka kutuambia Brighton yupo ujinini?” Mama Sharifa aliuliza.
“Ndiyo, lakini kwa sasa yupo katika matatizo.”
“Matatizo! Matatizo gani tena jamani?” Suzana aliuliza kwa huzuni.

“Baada ya kufika katika mji wa majini, baba mzazi wa Balkis alishtuka kuona mwanaye amekwenda na mwanadamu akimsema ndiye mume wake badala kupeleka alichotumwa.
Hapo palitokea kutoelewana kati ya Balkis na baba yake, baba akitaka mwanaye arudi duniani kuendelea kutafuta vizazi zaidi vya wanawake ili apate dawa ya kuweza kupata ujauzito ili aolewe na jini mwenzake.

Lakini Balkis hakuwa tayari kuolewa na jini mwenzake baada ya kuonja penzi la mwanadamu. Yeye aliamini kuolewa na mwanadamu kusingekuwa na haja ya kuendelea kuwatoa uzazi wanawake. Kwani angekutana kimwili na mwanadamu angeweza kupata bila kutumia dawa hiyo.

Hapo ndipo palipozuka mvutano wa mtoto na baba, Balkis aliamini kwa vile anapendwa sana na baba yake atakubaliwa, lakini baba yake hakuwa tayari kuchanganya damu ya jini na mwanadamu. Baada ya kuona mtoto wake amemkosea adabu, alimuamuru mkuu wa Watwana anaitwa Kulani, Jini mweusi lakini mwenye nguvu. Kumchukua Balkis na mchumba wako kuwapeleka katika chumba cha giza.”

“Kwa hiyo ndiyo harudi tena?” Suzana aliuliza.
“Anaweza kurudi lakini mpaka atoke sehemu aliyofungwa.”
“Bila ya hivyo hawezi kutoka?” Sharifa aliuliza.

“Inategemea na uamuzi wa mfalme wa bahari kumtoa.”
Mambo yanazidi kuwa mazito. Je, Brighton atapona au atauawa katika mji wa majini? Mganga njiwa Manga atawasaidia?




JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.27

LIPOISHIA;
“Sasa kama unasema wazazi wake hawakukubali wataweza kumtoa salama Brighton?” Suzana aliuliza.

“Hapa inaonesha maisha yake yapo zaidi ya hapo, kwa hiyo inamaanisha hawezi kuuawa.”
“Kama umeona anaweza kuendelea kuishi, itakuwa wapi duniani au kuendelea kufungwa kwenye chumba cha giza?” Suzana alikuwa na shauku kujua hatima ya mchumba wake.

“Kwa kweli haioneshi ataishi wapi ila kuna maisha marefu ya mchumba wako.”
“Na kuhusu kazi yangu ya kurudisha kizazi kuna vitu vinatakiwa kwenda kununua?” Sharifa aliuliza.
SASA ENDELEA...

“Anatakiwa njiwa mwekundu tu, kwenye mabanda yangu atapatikana.”
“Na mimi kumpata mchumba wangu utanisaidiaje?”
“Kama akitoka kwenye chumba cha giza tutampata, lakini kumtoa kule ni kazi ngumu, haonekani kila nikimtafuta.”

“Kwa hiyo utanisaidia vipi?”
“Kwa vile kazi ya mwenzako ni nyepesi ngoja tuifanye usiku wa leo, ya kwako itabidi nichimbe sana kuona kama kuna uwezekano wa kumtoa hata akiwa chumba cha giza.”
Walikubaliana kuifanya kazi ile usiku wa siku ile, mganga aliwaruhusu wakapate chakula na kupumzika ili kuvuta muda.
***
Majira ya saa sita usiku Sharifa alisimamisha gari lake pembeni kabisa na bahari maeneo ya pwani ya Bagamoyo, sehemu aliyoelekezwa na Mganga Njiwa Manga. Hali ya hewa ilikuwa giza la wastani, kwa mbali ilionekana miale ya moto ya wavuvi wa usiku.
Baada ya kusimamisha gari hakuteremka walisubiri maelekezo ya mganga. Mganga Njiwa Manga alianza kuteremka kisha aliwaita, wote walitoka nje ya gari.

Baridi la ufukweni lilikuwa kali, kila aliyekuwepo pale lilimchonyota hadi kwenye mifupa. Mganga alitoa vifaa vya kufanyia kazi, njiwa wa kazi alikuwa ameshikiliwa na Sharifa.

Wote walikuwa kimya wakimsikiliza mganga ambaye alikuwa akitembea kuelekea baharini, mawimbi muda ule hayakuwa makali sana yalipiga taratibu. Mganga aliingia majini usawa wa maji ya mafuti na kumwaga vitu huku akizungumza maneno kwa sauti ya juu.
“Ewe jini la bahari nakuletea zawadi hii ili bahari iwe tulivu, pia nimekuletea zawadi ya njiwa ili kuniruhusu niifanye kazi yangu bila kikwazo.”

Baada ya kusema vile aligeuka bila kutoka ndani ya maji na kumwita Sharifa.
“Kavue nguo zote kisha ujifunge upande wa kanga halafu uingie ndani ya maji na njiwa wako.”

Sharifa alifanya kama alivyoelekezwa na mganga, aliingia ndani ya maji na kuwaacha mama yake na Suzana wakiwa wamesimama huku wakiendelea kupigwa na baridi kali ya upepo utokao baharini. Aliingia ndani ya maji ya baridi huku akiwa na hofu ya kutojua mganga anataka kumfanya nini hasa akiwa amejifunga upande wa kanga bila kitu chochote mwilini.

Alipomfikia mganga alisogea naye mbele hadi maji ya shingo njiwa wake akiwa amemnyanyua juu. Baada ya kufika kimo kile cha maji, mganga alimwambia Sharifa amuweke kichwani, naye alifanya vile. Mganga alimshika sikio la kushoto na kuanza kuomba kwa lugha ya kiganga.

Aliomba kwa kuzungumza maneno haraka haraka bila kumeza mate kwa zaidi ya nusu saa. Baada ya robo saa Sharifa alianza kusikia vitu vikikoroga tumboni, Sharifa alishindwa kufanya kitu kutokana na mikono kuwa kichwani amemshikilia njiwa.

Mganga aliendelea kuzungumza maneno ya kiganga akiwa bado amemshikilia sikio, tumbo nalo liliendelea kumkoroga huku mwili ukizidi kupungua nguvu. Mara alianza kuona kiza mbele na kuangukia ndani ya maji na njiwa wake mkononi.

Mganga aliwahi kumdaka na kujitahidi kumsimamisha lakini miguu haikuwa na nguvu, alipiga kelele kuomba msaada kwa mama Sharifa na Suzana waliokuwa nje ya maji. Nao walijikuta wakiingia kwenye maji na nguo zao bila kujijua kuwahi kutoa msaada kwa mganga.

Walipofika ndani ya maji ya shingo walimsaidia mganga kumsogeza ufukweni, walipofika ilionesha kama Sharifa amepoteza fahamu.
“Mganga mbona hivi?” Mama Sharifa aliuliza.
“Ni kawaida kuna kitu kilikuwa mwilini mwake kimetoka lakini baada ya muda atakuwa katika hali ya kawaida.”

Pamoja na Sharifa kupoteza fahamu mganga aliwaomba wambebe hadi ndani ya maji ili aendelee na tiba yake.
“Sasa baba si unamuona alivyo kwa nini tusisubiri arudiwe na fahamu kisha uendelee na tiba?” Mama Sharifa aliuliza akiwa amejawa na wasiwasi juu ya hali ya mwanaye.
“Mama unanifundisha kazi?” Mganga alimuuliza kwa sauti ya ukali.
“Samahani baba.”

“Sipendi kufundishwa kazi kama ulikuwa unajua kwa nini mlimleta kwangu?”
“Nisamehe baba yangu.”
“Basi naomba kila utakachokiona hapa ukae kimya.”
“Nimekuelewa baba yangu nisamehe sana.”
“Haya mbebeni muda unakwenda.”

Mama Sharifa na Suzana walimbeba Sharifa mpaka maji ya chini ya mafuti mganga alimuomba Suzana akae chini ili ampakate mgonjwa. Suzana alifanya kama alivyoelezwa na mganga kisha Sharifa alilazwa chali juu ya Suzana. Mama yake alimshika sehemu ya kichwani ili kisiingie kwenye maji. Baada ya kulazwa mganga aliendelea na tiba yake kwa kuendelea kusema maneno ya kiganga kwa zaidi ya nusu saa. Huku njiwa aliyekuwa amelowana akimshikilia kwenye tumbo la Sharifa.

Baada ya muda mganga alinyamaza ghafla na kupita kimya kizito kikifuatiwa na upepo mkali. Baada ya muda upepo ulikoma. Suzana na mama Sharifa kila mmoja aliingiwa na wasiwasi kutokana na hali iliyojitokeza mle baharini. Kila moja alimuomba Mungu kimoyomoyo.

Baada ya upepo kutulia ilisikika sauti ya Sharifa ikiita.
“Mama...mama...mama.”
Mama Sharifa hakuitikia alimuangalia mganga aliyekuwa bado akitazama upepo ulipotokea na kunyanyua mkono.




JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.28.




Ilipoishia:
“Bila ya hivyo hawezi kutoka?” Sharifa aliuliza.
“Inategemea na uamuzi wa mfalme wa bahari kumtoa.”Sasa endelea:


“Hawezi kumuua?” Suzana aliuliza kwa sauti ya kukata tamaa.
“Hawezi, nina imani atatoka tu, kinachotakiwa ni kuvuta subira.”
“Mmh! Na mimi tatizo langu?” Sharifa aliuliza.

“Wewe tatizo lako limepata bahati moja kubwa ambayo sawa na bahati ya mtende.”
“Bahati gani?” Sharifa aliuliza huku akijiweka sawa.
“Kitendo cha kufungiwa Balkis katika chumba cha giza, kimewawezesha kuja huku bila ya matatizo.
“Una maana gani?” Sharifa aliuliza.

“ Majini ni viumbe wasiokubali kuona wanavurugiwa mipango yao, Balkis kama angekuwa hajafungiwa lazima angeizuia safari yenu.”
“Angeizuia kivipi?”
“Mngekutana na vitu vya ajabu njiani hata kupinduka na gari lenu.”
“Si tungekufa?”

“Msingekufa, mngeumia tu ili msiweze kumfuatilia.”
“Na bahati nyingine?”
“Bahati nyingine wakati wa kufanya dawa ya kurudisha kizazi chako hakutakuwa na upinzani wowote. Wala kazi yako haitahitaji vitu vingi vya kufanya na itaanza leo saa sita za usiku baharini.”
“Kama angekuwepo?”

“Mmh! Pangechimbika, waganga wengi wamepoteza maisha kwa ajili ya kutaka kuvuruga mipango ya majini. Pia tungehitaji vitu vya gharama ili kumdhibiti hapo kazi ingetakiwa kufanyika saa nane za usiku baharini katika maji ya shingo.”
“Mmh! Sasa akitoka si ataweza kutuua?”

“Balkis ni jini lenye huruma sana, katika maisha yake hapendi kufanya vitu vibaya, hata kuolewa ilikuwa ni shinikizo la wazazi wake tu ambao walimlazimisha kutafuta vizazi vya wanawake ili aweze kupata tiba ya matatizo yake ya kushindwa kupata ujauzito.

“Mwanzoni alikataa katakata lakini aliahidiwa kupewa zawadi kubwa kama atapata mtoto hasa wa kiume. Alikubali kuifanya kazi ile kwa shingo upande, lakini moyoni mwake hakupenda hata siku moja kutenda kitendo chochote kibaya kwa wanadamu, siku zote aliwaza kuishi duniani na kuolewa na binadamu.

“Hata kazi ya kutoa vizazi ilimchukua muda mrefu sana, kitu kilichowafanya wazazi wake kumleta duniani moja kwa moja ili aweze kupata vizazi hivyo kwa muda mfupi, bila kujua Balkis hakupenda kuifanya kazi ile.

“Siku Suzana alipoona sherehe ya ajabu juu ya bahari, hiyo ndiyo ilikuwa siku rasmi ya kuja duniani kwa Balkis kusaka vizazi vya wanawake na kuvipeleka baharini. Aliandaliwa jini mwingine ambaye kazi yake ilikuwa ni kuvipokea vizazi hivyo juu ya bahari katika eneo lile la Daraja la Salenda na kuvipeleka kwenye stoo chini ya bahari.

“Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake, tangu Balkis alipofika rasmi duniani kwa kazi hiyo, kwa siku moja alipeleka vizazi vinne tu na chako kikiwa kimojawapo.
Kazi aliyotumwa alisahau baada ya kuvutiwa na uzuri wa mchumba wa Suzana na kujikuta akianzisha uhusiano wa siri bila mwenzako kujua.

“Katika harakati za kuhakikisha anamdhibiti mchumba wako, muda mwingi aliutumia kuhakikisha anamchukua jumla badala ya kuifanya kazi aliyotumwa.
“Aliweza kuwagonganisha kwa kuziua nguvu za kiume za mchumba wako na usiku ulipoingia alizirudisha ili afaidi yeye.

“Hali ile ndiyo iliyowasukuma kutafuta suruhu ya tatizo lenu, alipoona mmeanza kupata mwanga aliwachanganyeni kwa kuzirudisha kitu kilichokufanya uone kama hakuna tatizo.Balkis alipofanikiwa kumnasa mchumba wako kwenye mtego wake, hakupanga kuondoka naye mapema.
“Mngeendelea kushea mapenzi bila wewe kujua mpaka angeshika ujauzito.
“Kosa alilolifanya mchumba wako ni kwenda kinyume na yale aliyokuwa akielekezwa na Balkis.

“Kubabaika kwake kulipelekea wewe kuingia wasiwasi na kutamka neno lililomchukiza Balkis na kukupulizia hewa iliyokupoteza fahamu.
Hali ile ilimfanya Balkis aone mpango wake umeharibika mapema, ili asiweze kumpoteza mpenzi wako aliamua kuondoka naye kwenda chini ya bahari.

“Kutokana na huruma yake aliamini kama ataolewa na binadamu atakuwa ameokoa tatizo la wanawake kutolewa vizazi. Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake ambao wao walimtuma kuishi duniani ili kufanikisha kupatikana kwa vizazi vingi vya mwanamke vitakavyomuwezesha kupata dawa ya kushika ujauzito ili aolewe na jini mwenzake.

“Walishangaa kumuona akiwa na mwanaume wa kibinadamu na kumtambulisha kwao kama ni mume wake. Kitendo kile kiliwaudhi sana, naye hakutaka kukubali.Baada ya mvutano Balkis na mchumba wako waliwekwa kwenye chumba cha giza.”
“Sasa kama unasema wazazi wake hawakukubali wataweza kumtoa salama Brighton?” Suzana aliuliza.

“Hapa inaonesha maisha yake yapo zaidi ya hapo, Kwa hiyo hawezi kuuawa.”
“Kama umeona anaweza kuendelea kuishi, itakuwa wapi duniani au kuendelea kufungwa kwenye chumba cha kiza?” Suzana alikuwa na shauku kutaka kujua hatma ya mchumba wake.
“Kwa kweli haioneshi ataishi wapi ila kuna maisha marefu ya mchumba wako.”
“Vipi kuhusu kazi yangu ya kurudisha kizazi kuna vitu vinatakiwa kwenda kununua?” Sharifa aliuliza.

“Anatakiwa njiwa mwekundu tu, kwenye mabanda yangu anapatikana.”
“Na mimi kumpata mchumba wangu utanisaidiaje?”



JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.29.


ILIPOISHIA:
“Nipo mimi” Suzana alijibu.
“Haya fanyeni haraka mkimaliza mniite.”
Walimbeba Sharifa ambaye hakuwa na nguvu hadi ndani ya gari na kumbadili nguo zake kisha walimwita mganga ili waondoke kurudi nyumbani.
SASA ENDELEA...

Mganga aliingia kwenye gari, Suzana aliliendesha mpaka nyumbani kwa mganga, walipofika walimteremsha Sharifa ambaye alitembea kwa tabu. Walipomfikisha sebuleni walimlaza kwenye mkeka na kumsuburi mganga aliyekuwa amemshika njiwa aliyekuwa tayari ameshamchinja tangu baharini.

Mganga alimwomba mkewe awape nguo za kujifunga wateja wale kutokana na nguo zao kulowana na maji ya bahari walipokuwa wakimtoa Sharifa kwenye maji. Baada ya kubadili nguo alimpa mkewe yule njiwa na kumweleza amnyonyoe na kumchemsha. Mkewe alimchukua na kuondoka naye na kuwaacha kina Suzana sebuleni.

Majira ya saa kumi za usiku mganga alimwamsha Sharifa na kumpa dawa ya njiwa aliyechemshwa kwa ajili ya kumla akiwa katika sufuria ile ile aliyochemshiwa.
“Mle njiwa wote na unywe na supu yake,” mganga alimwambia Sharifa ambaye bado mwili wake ulikuwa hauna nguvu.

Sharifa alianza kumla njiwa na kunywa supu yake kwa shida kwa vile alichemshwa bila kuwekwa chumvi, alipomuona kama anamshindwa kutokana na kutokuwa na kiungo hicho aliuliza.

“Mbona hana chumvi?”
“Huyo hawekwi chumvi, jitahidi umle vivyo hivyo, tena una bahati njiwa ni mdogo, watu wanakula kuku mzima bila chumvi.”

Sharifa hakuongeza neno alimuinamia njiwa wake na kuendelea kumla taratibu mpaka alipommaliza, wakati huo Suzana na mama yake walikuwa wakikoroma. Baada ya kumaliza kumla njiwa aliruhusiwa kuendelea kulala na wenzake ambao walikuwa hawajitambui kwa usingizi.

Wote waliamshwa alfajiri kwa ajili ya tiba ya mwisho ya kuoga maji ya bomba yaliyochanganywa na yale ya baharini. Baada ya kuoga waliingia kwenye chumba cha mganga kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Wote walikaa kwenye mkeka baada ya mganga kutulia kwa muda huku akipitia maelezo kwenye karatasi nyeupe iliyoandikwa kwa wino mwekundu kisha alisema kwa sauti ya chini:
“Nina imani kazi yetu imekwenda vizuri sana tofauti na nilivyofikiria, shughuli kama hii niliifanya siku za nyuma kwa muda wa wiki nzima, tena nikiwa na majeraha mengi kutokana na kushindana na jini.”

“Unataka kuniambia nimepona?” Sharifa aliuliza.
“Umepona.”
“Kwa hiyo nina uwezo wa kushika mimba?”
“Bila shaka.”

“Nashukuru sana mzee wangu,” Sharifa alinyanyuka kwa lengo la kumpigia magoti.
“Hapana mama kaa tu, wakushukuriwa ni Mungu yeye ndiye mwenye kukubali au kukataa maombi yetu.”

“Ina maana kama Balkis angekuwa hakufungwa kazi isingeisha leo?” Suzana aliuliza.
“Kazi ya kushindana na majini ni ngumu msione imekwenda kirahisi kiasi kile, kama Balkis angekuwa hajafungwa vita ingekuwa kubwa asingekubali tuchukue kizazi katika stoo yake. Lazima ingetakiwa niwe na vijana wangu wa kazi na katika kumdhibiti wangetakiwa mbuzi wekundu wawili, shuka nyekundu mbili na vitu vingine vingi.”

“Kutokana na kauli za mganga wa awali kuwa matatizo mengi ya tumbo yanatokana na jini Balkis kuchukua vizazi vya wanawake, lakini mbona ni wanawake wengi wana matatizo tofauti na idadi ya vizazi vilivyoko kwenye stoo ya Balkis?” Sharifa aliuliza.

“Kama nilivyowaeleza majini wanaishi kama wanadam, jinsi matatizo yetu yanavyofanana basi na ya majini huwa ni vivyo hivyo. Majini wengi wenye matatizo ya kukosa uzazi hutumwa duniani kuifanya kazi kama ya Balkis, hivyo vita si vyake peke yake ni kwa majini wengi.”

“Mungu wangu sasa tutapona vipi?” Suzana aliuliza.
“Kupona inategemea na wewe kuonana na watu wenye uwezo kama sisi au kusimama katika imani yako.”
“Kusimama kwenye imani una maana gani?” Sharifa aliuliza.

“Kila anayesimama katika imani humtanguliza Mwenyezi Mungu mbele kwa kila jambo, kabla ya kulala huomba ulinzi wake na baada ya kuamka humshukuru kwa kumvusha usiku salama, kisha humuomba tena amlinde na mchana wote.”
“Mbona tunafanya hivyo?” Alisema Suzana.

“Unaweza kuwa unafanya kutimiza wajibu wa maombi lakini imani yako si kamili, siku zote imani husimama kwa matendo siyo kwa maneno.”
“Unataka kuniambia aliyesimama kwa imani ya matendo mema hawezi kupatwa na tatizo hili?’

“Litaingilia vipi wakati Mungu ndiye mlinzi wake, hata hao majini wanamuogopa na kumuabudu yeye.”
“Kutokana na maelezo yako sasa hivi nimepona kabisa?” Sharifa aliuliza.
“Umepona na wala haitakutokea tena.”
“Kwa mfano Balkis akitoka gerezani, akijua nimerudishiwa kizazi changu si litakuwa tatizo?”

“Tatizo litabakia kwake, wewe utakuwa salama kuanzia asubuhi hii.”
“Ile hali ya tumbo kuvurugika nilipokuwa pale baharini ilitokana na nini?”
“Kizazi chako kilikuwa kikirudi sehemu yake.”

“Baba tunashukuru kwa msaada wako,” mama Sharifa alisema kwa niaba ya mwanaye.
Nini kiliendelea?




JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.30.




ILIPOISHIA;
Uso wake ulionesha huzuni kitu kilichomtisha mumewe ambaye alitaka kujua kulikoni.
“Vipi mahabuba wangu?”
“Mambo yameharibika.”
“Kivipi?”

“Mpango wetu umeingia kwenye mtihani wa kwanza.”
“Mtihani upi?”
“Kizazi kimoja kimechukuliwa.”
“Tufanye haraka kabla hakijarudishwa kwa mwenyewe tumtume Kulani akaifanye kazi hii kabla hakujapambazuka.”

“Tumechelewa tayari kimeisharudishwa kwa mwenyewe.”
“Umejuaje?”
“Damu ya sehemu kilipotoka nilipoigusa imeganda kidoleni.”

“Ooh! Nani anataka kuchezea himaya yangu lazima nimkomeshe,” Mfalme Barami Hudirud alisema kwa hasira.
“Hebu kaniletee damu ya sehemu iliyotoka kizazi ili nimjue ni nani?”
SASA ENDELEA...

Malkia Huleiya alikwenda hadi kwenye chumba cha siri na kurudi na damu ya sehemu iliyochukuliwa kizazi cha Sharifa na kumpelekea mumewe.
“Naomba niilambe.”
Malkia Huleiya alimlambisha mumewe, mfalme alitulia kwa muda kisha alisema:
“Nimeishamjua, nitamtuma Kulani akishindwa nitakwenda mwenyewe.

Lazima nitamuonesha mimi ni nani.”
“Umemgundua ni nani?”
“Kuna mshenzi mmoja anataka kushindana na nguvu zangu, nataka mpaka kutakapopambazuka awe amebakia jina.”

“Kulaniiiiii,” aliitaka kwa sauti ya juu ambayo kama mwanadamu angeisikia basi angepasuka ngoma za masikio.
Kulani aliyekuwa mbali alikuja mbio na kupiga magoti mbele ya mfalme.
“Rabeka mtukufu mfalme.”
“Nataka uende duniani, damu hii itakuongoza mpaka kwa mtu huyu, nataka umfutilie mbali, sawa?”

“Sawa mtukufu mfalme.”
“Haya ondoka mbele yangu, usirudi mpaka umemfutilia mbali kiumbe huyo dhaifu anayetaka kucheza na nguvu zangu.”
Kulani alizama chini ya ardhi na kutoweka, baada ya muda alikuwa pembeni ya bahari eneo la Bagamoyo, aliilamba damu aliyopakwa kidoleni ambayo ilimuelekeza aende upande upi. Alitoka eneo baharini na kuelekea kwa Mganga Njiwa Manga.

Alitembea taratibu toka eneo la bahari akiwa katika umbile la kibinadamu, hakuchelewa kufika kwenye makazi ya watu. Aliilamba tena ile damu iliyokuwepo kidoleni mwake, kwa vile kulikuwa na giza, sehemu ya Mganga Njiwa Manga ikawaka mwanga wa taa.

Mwanga ule ulimuongoza hadi karibu kabisa na nyumba ya Mganga Njiwa Manga. Nia yake kubwa ilikuwa kwenda mpaka mlangoni na kugonga ili akifungua tu wakutane uso kwa uso na ammalize pale pale kisha aondoke kabla hakujapambazuka.

Alitembea kuelekea eneo la nyumba ya mganga, ajabu alipokaribia nyumba yake alishangaa kuona moto ukiwaka kuizunguka nyumba ile. Hali ile ilimshtua sana, aligeuka na kutimua mbio hadi baharini ambako alikunywa maji mengi na kurudi hadi kwenye eneo la nyumba ya mganga.

Alipoikaribia moto uliwaka tena, alilisogelea eneo la nyumba huku akimwaga maji aliyoyachukua baharini kwa lengo la kuuzima moto ule. Alifanikiwa lakini alipotaka kuingia kwenye himaya ile moto uliwaka tena. Alijikuta akifanya kazi ya kwenda baharini na kurudi, kila alipouzima moto na alipotaka kuingia uliwaka tena.

Kulani alijikuta akitumia muda mwingi kwenda baharini kuchukua maji na kurudi huku moto ukizimika na kuwaka. Mpaka kulipokuwa kunakaribia kupambazuka hakuweza kuingia katika himaya ya Mganga Njiwa Manga. Kwa upande wake aliiona kazi imekuwa ngumu au maji yalikuwa marefu na kuamua kurudi chini ya bahari, aliogopa kutokana na kauli aliyopewa na Mfalme Barami Hudirud kuwa asirudi chini ya maji mpaka ahakikishe amemmaliza Mganga Njiwa Manga.

Kulani alijikuta kwenye wakati mgumu katika kazi ile, tofauti na zilizotangulia ambazo alizifanya kwa muda mchache. Lakini ile ilikuwa ngumu kwake, baada ya kukutana na kikwazo cha moto.
Aliamua kurudi hadi baharini akiwa katika umbile lile la kibinaadamu, alisubiri jua litochomoze ili aweze kwenda jirani kwa mganga na kumsuburi akitoka ammalize.

Jua lilipotoka na watu kuwa wengi kujaa ufukweni kwa ajili ya kununua samaki na wengine wakipanda ngarawa kwenda kuvua.
Kulani alijichanganya na watu bila ya kujulikana kama ni jini. Baada ya pwani kuchanganya na watu kuongezeka, alijitoa eneo la bahari na kwenda kwa mganga kwa kutembea kama mtu wa kawaida.

Kila aliyemuona hakumdhania vibaya, aliacha eneo la bahari na kuingia makazi ya watu, alipokaribia maeneo ya nyumba ya mganga aliuona moto ukiwaka tena. Alikwenda kwenye nyumba ya jirani na kuomba kupumzika, kutokana na kuonekana kama mstaarabu, alikaribishwa na kupewa kiti. Mwenyeji wake hakujishughulisha naye aliendelea na shughuli zake na kumuacha Kulani akitupia jicho njia ya kutokea kwa Mganga Njiwa Manga.
Jini Kulani ataweza kutimiza azma yake ya kumuua Mganga Njiwa Manga?
Etaendelea Baadae nisawachoshe tu wasomaji wangu..........



 
Mkuu MziziMkavu, we nimekukubali aisee! Hadithi tamu kweli!

Sent from my BlackBerry 8520 using JamiiForums
 
Last edited by a moderator:
JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.31



ILIPOISHIA:
Kila aliyemuona hakumdhania vibaya, aliacha eneo la bahari na kuingia makazi ya watu, alipokaribia maeneo ya nyumba ya mganga aliuona moto ukiwaka tena. Alikwenda kwenye nyumba ya jirani na kuomba kupumzika, kutokana na kuonekana mstaarabu alikaribishwa na kupewa kiti. Mwenyeji wake hakujishughulisha naye aliendelea na shughuli zake na kumuacha Kulani akitupia jicho njia ya kutokea kwa Mganga Njiwa Manga.
SASA ENDELEA...

Muda ulikwenda bila mganga kuonekana, kila alipopata wazo la kwenda kwenye nyumba ile alishangaa kuuona moto ukiwaka, lakini ulipotulia nyumba ilikuwa katika hali ya kawaida. Alijikuta yupo kwenye wakati mgumu akiamini kabisa ngoma ile ni nzito kwake kuchezeka.

Kilichomchanganya zaidi ilikuwa ni kauli ya mfalme Barami Hudirud ya kuhakikisha anammaliza mganga ndipo arudi, japo muda aliopewa ulipita.
Kulani alipata pigo baada ya mwenyeji wake kutaka kuondoka, akiwa bado kichwa kinamuuma alimwambia:

“Samahani kaka.”
“Bila samahani.”
“Nataka kuondoka kwenda pwani.”
“Hakuna tatizo funga mlango wako mimi niache hapa nimekaa baada ya muda nitaondoka.”
“Hapana kaka sikujui nimekukaribisha kibinadamu, lakini siwezi kukuamini kukuachia nyumba yangu, dunia haiaminiki siku hizi.”

“Sawa.”
Kulani alikubali kuondoka pale, lakini sehemu iliyokuwa nzuri kupaona kwa mganga ilikuwa kwenye nyumba ile iliyokuwa ikitazamana na ya mganga. Aliondoka kwa kuzunguka nyumba ile na kujigeuza haraka kuwa mjusi. Aliupanda ukuta haraka na kwenda kujificha chini ya bati bila kuonekana.

Mwenye nyumba ile alishtuka na kuzunguka nyuma ili kupata uhakika kama kweli yule mgeni atakuwa ameondoka. Lakini ajabu alipozunguka nyuma ya nyumba iliyokuwa na uwazi mkubwa wa kumuona mtu kama anatembea kutoka pale, hakumuona mgeni wake. Alijiuliza kwa sauti:

“Sasa atakuwa amekwenda wapi, mtu azunguke sasa hivi asionekane, mmh! Lisiwe jini lile, Mungu aniepushie mbali.”
Kulani alimtazama na kutulia akiwa amejilaza kwenye ukuta chini ya bati. Baada ya kusema yale mwenye nyumba ile aliondoka na kumwacha Kulani palepale nyumbani bila kujua.

Baada ya kuondoka, Kulani aliendelea kumsubiri mganga palepale ukutani chini ya bati katika umbile lile lile la mjusi kama atatokea Mganga Njiwa Manga amvae na kumuulia mbali. Alisubiri kwa saa kumi mpaka jioni ilipoingia ndipo alipomuona akiwa anamsindikiza mmoja wa wateja wake.

Jini Kulani aliteremka na kurudi katika umbile la mwanadamu na kumfuatilia kwa nyuma bila ya mganga kujua. Nia yake ilikuwa kukutana naye wakati anarudi ili amvae. Taratibu alitembea kumfuata kwa nyuma mganga aliyekuwa mbele akitembea huku akizungumza na wateja wake.

Njiani Mganga Njiwa Manga alianza kuhisi kama ardhi inatetemeka na mwili kuwa mzito, kitu kile kilichomfanya ageuke na kutazama nyuma. Alishtuka kukiona kiumbe cha ajabu kwa mbali kikija taratibu. Kwa haraka alichutama chini na kushika michanga huku akilikemea jitu lile ambalo liligundua limejulikana.

Wakati Kulani akijitayarisha kumvaa Mganga Njiwa Manga baada ya kugundua amejulikana, kabla hajamfikia alirusha vumbi la mchanga lililomuingia machoni na kumpofua macho. Alipiga kelele za maumivu na kujipiga chini kwa hasira na kusababisha kishindo kizito kilichotikisa eneo kubwa la Bagamoyo.

Kishindo kile kilisababisha watu waliokuwa karibu na sehemu kilipotokea waanguke na kupoteza fahamu. Nyumba nyingine zilipata nyufa kutokana na kushindo cha Kulani kupasua ardhi na kupotea. Baada ya robo saa hali ya eneo la Bagamoyo ilirudi kuwa ya kawaida.
Baada ya kurudi hali ya utulivu Mganga Njiwa Manga alinyanyua alipokuwa ameangukia baada ya kurushwa na udongo uliotoka kwenye shimo alilozama jini Kulani baada ya kupofuka macho. Alimtuma mtu kwenda nyumbani kumletea dawa ambayo alikunywa na kujimwagia kichwani.

Baada ya kuyafanya yale alikwenda hadi kwenye shimo lililokuwa limechimbika kama kumelipuka bomu. Sehemu ile aliweka dawa kisha aliondoka na kurudi nyumbani kwake. Alipofika nyumbani mwili ulikuwa umechoka sana, hakuweza kuendelea na kazi ya matibabu, aliwaomba wagonjwa wake apumzike baada ya kunusurika kifo toka kwa jini ambaye hakujua ametoka wapi.

Siku ile hakufanya kazi yoyote, alilala mpaka siku ya pili huku akiviona viungo vyake vikipoteza nguvu. Hata alipolala hakuweza kujigeuza mpaka siku ya pili, kwake ulikuwa upinzani mkubwa katika kazi yake. Mara nyingi upinzani uliishia nje ya ngome yake, lakini hakikuwahi kiumbe chochote cha ardhini majini au angani kilichoweza kumdhuru.

Pia katika kazi yake haikuwahi kutokea kiumbe kilichowahi kumvizia njiani kwa ajili ya kumdhuru. Wengi walivamia sehemu aliyokuwa akifanya kazi na kukutana na vikwazo. Lakini uwezo wa kinga yake ya mwili ndiyo uliomsaidia, bila hivyo angemalizwa na jini yule.
***

Jini Kulani baada ya kuzama chini ya ardhi kwa kujipigiza kwa hasira, aliibukia pembeni ya bahari. Alitembea taratibu huku akipapasa ili kuingia majini. Baada ya kutembea kwa muda alibahatika kuyakanyaga maji. Pale pale alizama chini.
Mfalme wa bahari alishangaa kumuona Mkuu wa Watwana Kulani amesimama mbele yake akiwa haoni.

“Kuna nini tena kimekusibu mtwana wangu mtiifu?”
“Mtukufu mfalme, safari yangu imekuwa mbaya.”
“Kulani umefanya makosa, kwa nini jana hukurudi?”
“Niliogopa mtukufu mfalme kurudi bila kutimiza ulichonituma.”
“Umekitimiza?”

“Hali yangu kama unavyoniona.”
“Tatizo nini?”
“Nimepofuka mtukufu mfalme.”
“Lakini hujanijibu, umemmaliza?”
“Sikuweza, yule mtu hata wewe sikushauri uende.”
“Kwa nini?”

“Amejidhatiti, ana nguvu za ajabu sijawahi kuona, ameizindika ngome yake haiingiliki, na yeye mwenyewe alichonifanya sitasahau mpaka nakufa.”

Jini Barami Hudirud, mfalme wa bahari atakubali ushauri wa Kulani kuachana na Mganga Njiwa Manga?








JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.32


“Hapana lazima niende, hawezi kushindana na nguvu zangu.”
“Mtukufu mfalme, bado himaya ya chini ya bahari inakuhitaji lazima atataka kutumia nguvu za ziada kukumaliza. Nashukuru sikugusana naye ningeweza kupoteza maisha.”
“Kwa hiyo tuwaache wanadamu watuchezee?”

“Hapana, ila nguvu zinazidiana, yule mwanadamu ana nguvu za ajabu sana, nilijitahidi kuuzima moto alioutega kwenye himaya yake, nilishindwa kila nilipouzima na nilipotaka kuingia uliwaka tena nikajikuta kukipambazuka bila ya kuweza kuingia kwenye himaya yake. Ndiyo sababu ya kuchelewa kurudi na kuamua kubaki ili nihakikishe nammaliza akitoka kwake. Lakini haikuwa hivyo matokeo yake nimekuwa kipofu.”

“Mmh! Nimekuelewa, basi mpelekeni akapate tiba.”
Watwana wengine walimchukua Kulani na kwenda kumpatia tiba ya macho, baada ya kuondoka, mfalme alimgeukia mkewe aliyekuwa kimya akimuangalia Kulani kwa huruma.
“Mke wangu umeona hali ilivyo, unanishauri nini kutokana na hali aliyorudi nayo Kulani?”

“Mmh! Mume wangu hali inatisha, inaonesha wazi vita ni nzito, tukifanya mchezo tutakwisha, mpaka Kulani kusema hivyo ujue kuna kazi. Kwa nini tusiachane na mpango wa kumfuatilia huyo mwanadamu?”
“Lakini mke wangu si unajua uwezo wangu? sijawahi kushindwa na kitu,” Mfalme alijitapa.

“Naujua vizuri, hata Kulani anaujua lakini mpaka kakukueleza vile naomba umsikilize huenda kuna kitu amekiona kinaweza kukupotezea maisha kama utashindana na yule mwanadamu.”
“Lakini kumbuka jini ana nguvu kuliko mwanadamu?’
“Lakini mwanadamu ndiye kiumbe mwerevu kuliko viumbe wote wa Mungu?”
“Hilo nalijua lakini bado hawawezi kushindana na sisi.”
“Mume wangu majini sisi hatuna ushirikiano, kuna majini wengine huwakinga mwanadamu na kuwafanya kuchanganya nguvu za kijini na akili ya kibinadamu lazima tu atakushinda.”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“La muhimu tuachane na mpango huo.”

“Na suala la Balkis kuolewa na jini mwenzake?”
“Hilo nalo ni gumu, tuendelee kumshawishi aweze kubadili mawazo na kuendelea na kazi ya kukusanya vizazi vya wanadamu na kutengenezewa dawa.”
“Mimi nina hasira, jaribu kuongea naye wewe.”

“Nitafanya hivyo jioni nitazungumza naye.”
Walikubaliana mke wa mfalme azungumze na Balkis ili aweze kubadili uamuzi wake wa kung’ang’ania kuolewa na mwanadamu.
****
Baada ya kuamka siku ya pili, Mganga Njiwa Manga bado mwili wake haukuwa na nguvu, wagonjwa wengi waliofika siku ile hawakupata huduma kutokana na hali yake. Ilibidi siku ile na yeye kutumia dawa za kujifusha na kunywa ili kujirudisha katika hali ya kawaida, baada ya kukumbwa na upepo wa jini Kulani.

Kilichomshangaza kilikuwa rangi ya jini yule, alikuwa mweusi kama rami tofauti na majini wote aliowahi kukutana nao. Siku ya pili tangu akutane na dhahama nzito ya jini Kulani, aliendelea na kazi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotoka mbali.

Baada ya kuingia katika chumba chake kutoa huduma, alitulia kwenye mkeka kisha aliweka ubani kwenye kitezo na kutulia kwa muda ili ajiandae kwa matibabu ya wagonjwa waliokuwa wameongezeka kutokana na kusimama kwa huduma yake.

Ilikuwa ajabu baada ya moshi wa ubani kupanda juu, ulimfuata mbele ya uso wake na akaanza kuona picha asiyoielewa. Alikiona kiumbe cha ajabu kikitoka kwenye maji na ghafla kiligeuka na kuwa mwanadamu, kisha kilitembea taratibu toka kwenye ufukwe na kuingia maeneo ya watu.

Baada ya kiumbe kile kilichojigeuza kuwa binaadamu kukaribia ngome yake, kilijigeuza umbile na kurudia lile alilotoka nalo chini ya maji. Ajabu kilipotaka kuingia kwenye himaya yake aliona moto ukiwaka kuzunguka eneo lake, ghafla kiumbe kile kilitoka mbio kurudi baharini na kuchota maji kisha kuja kuzima moto.

Kiliendelea kuzima moto mpaka kulipopambazuka, kila kilichoendelea alikiona mpaka kupambana na jini lile. Hapo ndipo alipogundua jini lile lilitoka wapi, alicheka na kuona kinga aliyokuwa nayo ndiyo iliyomsaidia bila hivyo angekufa vibaya.
Taratibu moshi ulipungua na hali ya ndani ikarudi kuwa ya kawaida, Mganga Njiwa Manga aliendelea kuweka tena ubani uliotoa moshi wa kawaida bila kuwepo na kitu kisichokuwa cha kawaida. Alimtuma msaidizi wake kuwaita wagonjwa.

Nini kiendelea baada ya mganga kuonekana kudhibiti nguvu za kijini? Je, nini hatma ya Brighton katika chumba cha giza?











JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.33




CHINI YA BAHARI
Malkia Huleiya, mama mzazi wa Balkis alikwenda hadi chumba cha giza na kuomba Balkis atolewe, baada ya kutolewa alimpeleka kuoga na kukaa naye kwenye pwani ambayo huitumia kupumzika familia ya kifalme. Muda wote Balkis alikuwa akibubujikwa na machozi.
Baada ya kukaa kimya kwa muda malkia Huleiya alimwita mwanaye.
“Balkis”

“Abee mama.”
“Najua utatuona sisi wazazi wako makatili lakini unajua kabisa ubaya wa wanadamu na pia ni aibu jini kutoka katika ukoo wa kifalme kuzaa na mwanadamu.”
“Mama kabla ya kuzungumza lolote naomba mumtoe mpenzi wangu na kama hamtaki awe huku naomba mumrudishe duniani.”

“Hakuna tatizo.’ Alitumwa mtu kwenda kumtoa Brighton kwenye chumba cha giza na kumpa maji ya kuoga kisha kuwekwa kwenye chumba kizuri. Baada ya hatua zile mazungumzo yaliendelea.
“Nina imani imefurahi?” Mama yake alimuuliza.
“Siwezi kufurahi kwa vile sijatimiza dhamira yangu.”
“Ipi?”

“Ya kuolewa na mwanadamu.”
“Hilo ndilo baba yako hataki kusikia.”
“Lakini kumbuka tunachokifanya hakimpendezi Mwenyezi Mungu.”
“Kipi hicho.”

“Cha kuwafanya wanawake matasa.”
“Ni kweli, lakini tunafanya hivyo kwa ajili yako.”
“Kama unaona kufanya vile ni dhambi kwa nini msiniache na mpenzi wangu aliyekuwa tayari kukaa huku hata watoto wangezaliwa wangekuwa wetu.”
“Mwanangu hujui vita ya wanadamu ni kubwa, huwezi kuamini kizazi kimoja kimechukuliwa. Kama kizazi kimechukuliwa je, mwanadamu watakubali aishi huku?”
“Mwanadamu kanipenda mwenyewe wala sikumlazimisha.”

“Lakini si ana mchumba wake?”
“ Alimkana mbele yangu na kuwa tayari kunioa.”
“Kwa sababu hakujua kuwa wewe ni jini.”
“Hata alipojua alikubali ndiyo maana nimekuja kuishi nae huku.”
“Lakini kumbuka baba yako alikuwa akikutegemea sana, ulichokifanya kimemchanganya sana.”

“Lakini mama tatizo nini, kutafuta vizazi vya wanawake na kuzaa bila vita na wanadamu kipi bora, ona kama ulivyoniambia mkuu wa watwana Kulani kawa kipofu, kwa nini tusiachane na vita na wanadamu ili hamu ya mtoto apatikane bila kupata madhara zaidi.”
“Uamuzi wako umemuweka baba yako katika wakati mgumu, kumbuka anakupenda kuliko kitu chochote, hakuota hata siku moja utamkosea heshima.”

“Ni kweli najua baba ananipenda lakini alitakiwa kunisikiliza kuliko kuchukua maamuzi mazito, ona katumia nguvu nyingi matokeo yake Kulani kawa kipofu.”
“Balkis mwanangu hakuna jini anayekubali kushindwa na mwanadamu.”
“Ni kweli lakini kuna wanadamu nao huamini kabisa majini hawawawezi, kama wameweza kuchukua kizazi kimoja wanashindwa nini kuvichukua vyote?”

“Balkis mwanangu kama ungekwenda kwa kitu tulichokutuma, nina imani kazi yako ingekuwa nyepesi sana kuliko ulichokifanya cha kuanzisha uhusiano na mwanadamu.
“Kitendo kile kilituchanganya sana hasa baba yako, hata kuzungumza na wewe alishindwa na kunituma mimi. Anaamini hata matatizo ya Kulani chanzo ni wewe.”
“Chanzo ni mimi kwa vipi? Wakati niliwakataza tuachane na vita na wanadamu lakini mkawa wabishi.”

“Balkis mwanangu naomba uifanye kazi tuliyokutuma, tunaamini wewe ni mtoto mwenye heshima na usikivu. Nakuomba chonde chonde mwanangu msikilize baba yako.”
“Mamaa kwa nini msinikubalie, kwani kuna ubaya gani?”
“Kumbuka baba yako ni mfalme wa majini, ni aibu kwa mwanaye kuolewa na mwanadamu, ndiyo maana alikutuma kutafuta kizazi cha mwanamke ili kuhakikisha unapata tiba na kuolewa na jini mwenzako.”

“Kwa hiyo nimrudishe Brighton duniani?”
“Ikiwezekana.”
“Mbona unasema ikiwezekana.”
“Lazima tumuulize baba yako ataamua nini juu ya mwanadamu aliyejua siri yetu.”
“Sasa naona unataka kuharibu mazungumzo, mmenikataza kuolewa na mwanadamu basi nimrudishe kwao.”

“Lakini si atakuwa amejua siri yetu?”
“Sasa mnataka kumfanya nini?”
“Sijajua mpaka tupate maelekezo ya baba yako.”
“Sikiliza kama nimekubaliana na uamuzi wenu wa kuachana na mwanadamu ili niendelee na kazi yangu ya kutafuta vizazi vya wanawake, naomba kwenye suala la kurudi kwao mpenzi wangu msiniingilie.”

“Lakini kumbuka mwanangu chini ya bahari hii mwenye sauti ya mwisho ni baba yako.”
“Hata awe na sauti gani uamuzi wowote tofauti na kumrudisha duniani hatutaelewana.”

Nini hatima ya Brighton? Je, ataruhusiwa na mfalme kurudi duniani baada ya kuijua siri ya majini?






JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.34



“Mbona umefika mbali, ngoja nimpelekee taarifa hizi, atafurahi sana kusikia kuwa umekubali kurudi dunia kutafuta vizazi vya wanawake. Pia nitamueleza suala la mpenzi wako la kurudishwa duniani. Siamini kama atakuwa na maamuzi mazito ya kukuumiza.”
“Mmh! Haya basi naomba nafasi ya kuzungumza na Brighton.”
“Mmh! Basi ataletwa huku ili baba yako asijue chochote.”

Baada ya kusema vile, Huleiya aliondoka na kumuacha Balkis akiwa amejilaza kwenye kiti cha uvivu. Japo moyo ulimuuma kumuacha Brighton mwanaume aliyeamini ndiye mume wa maisha yake. Bado hakuamini kama anaweza kutoa siri za majini. Lakini aliamini hakuwa akijua lolote katika siri za chini ya bahari kutokana na kufikia kwenye chumba cha giza.

Baada ya muda Brighton alifikishwa bustanini na kukutana na Balkis, baada ya kukutana Balkis alimueleza hali halisi na yeye kuwa tayari kumrudisha duniani. Kwa upande wake Brighton alijikuta akizama kwenye dimbwi la mahaba ya Balkis na kumuomba atafute njia yoyote ili asirudishwe duniani.

“Mpenzi kwa nini usimbembeleze baba yako ili tuishi pamoja?”
“Hilo ndilo lilikuwa lengo langu lakini limeleta mtafaruku mkubwa ndani ya familia. Kwa hiyo nakuomba ukubali kurudi duniani ila sitakuwa mbali nawe.”

“Mmh! Sawa lakini nitalikosa penzi lako.”
“Ni kweli, lakini lazima nikubaliane na matakwa ya wazazi wangu.”
“Sawa, sina jinsi,” Brighton alikubali kwa shingo upande.

Malkia Huleiya baada ya kuzungumza na mwanaye alipeleka taarifa ya kikao kwa mumewe mfalme Barami. Alipofika alimkuta akimsubiri kwa hamu.
“Karibu malkia wangu.”

“Asante mfalme wangu.”
“Mh, nijuze yaliyojiri huko?”
“Mmh! Namshukuru Mungu yamekwenda vizuri.”
“Kakubali?”

“Ndiyo.”
“Ooh! Afadhali.”
“Lakini..”
“Lakini nini tena malkia wangu?” Mfalme alishtuka.

“Kuhusu yule mpenzi wake.”
“Ana nini?”
“Anataka arudishwe duniani.”

“Ina maana hajui sheria yetu mwanadamu anayejua siri zetu huwa harudi tena duniani?”
“Hapo ndipo penye tatizo.”
“Tatizo gani?”
“Mwanao anataka amrudishe duniani.”
“Haiwezekani.”
“Amesema iwe isiwe lazima tumrudishe duniani.”

“Yeye ni nani anayetaka kutulazimisha tufanye anavyotaka, siwezi kuwa na sauti mbili katika himaya yangu ya chini ya bahari.”
“Lakini mume wangu..”
“Hakuna cha lakini, aendelee na kazi ya kutafuta vizazi tena tutampangia kwa siku moja alete vingapi ili awahishe kutimiza lengo la kuolewa tuondokane na adha hizi.”
“Mume wangu si vyema kila wakati kutumia nguvu, ifike wakati mwingine uwe unawasikiliza walio chini yako.”

“Siwezi, nasema kauli yangu ni ya mwisho na maamuzi yangu yaheshimiwe,” mfalme alikuwa mkali.
“Mume wangu hii itakuwa vita nyingine, kwa jinsi nilivyomsikiliza mwanao hawezi kukubali hili.”
“Nitakachomsikiliza ni kumuacha hai, lakini si kumrudisha duniani.”
“Mwanao amesema kwa hili hamtaelewana.”
“Hebu kamlete hapa,” mfalme alisema kwa hasira.

Alitumwa kijakazi kumfuata bustanini, Balkis alifika mbele ya baba yake kusikiliza kile alichoitiwa.
“Abee mtukufu mfalme,” Balkis aliitikia akiwa amesimama mbele ya baba yake.
“Kwanza nimefurahi kusikia umeweza kubadili uamuzi wako ila umeniudhi kwa kunilazimisha nifanye utakavyo.”
“Baba kukulazimisha kitu gani?”
“Kuhusu kumrudisha mwanadamu duniani.”

“Sasa tatizo liko wapi? Mmemkataa asinioe sasa si nimrudishe nilipomtoa.”
“Ina maana hujui sheria za majini, kama mwanadamu atajua siri zetu?”
“Nazijua lakini huyu nimemleta miye hakujileta mwenyewe, wala hakuletwa kwa lipizo.”
“Sheria za huku mwanadamu yeyote atakayeingia huwa hatoki salama, lakini kwa heshima yako hatutamuua bali ataishi huku milele.”

“Kwa hilo baba sitakubali hata kwa kukatwa kichwa, ni mimi ndiye niliyemlazimisha kuja huku iweje mumshikilie?”
“Hiyo ndiyo sheria ya huku kamwe haibadiliki.”
“Nasema kwa hili itabadilika.”
“Tunabisha?”

“Hatubishani ukweli ndiyo huo, ikifanywa kinyume nikiondoka hapa sitarudi tena.”
“Sooba,” alimwita mtwana msaidizi wa Kulani kwa sauti ya juu.
“Rabeka mtukufu mfalme,” Sooba aliitika na kusimama imara mbele ya mfalme.

“Mpeleke huyu kwenye chumba cha giza.”
Balkis alichukuliwa tena na kurudishwa kwenye chumba cha giza.
Nini kiliendelea?




JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.35





Baada ya mwezi mmoja na nusu kupita, Suzana akiwa ofisini kwake, muda mfupi baada ya kuingia alijikuta akiwa na mawazo mengi. Hiyo ilikuwa ni kutokana na maneno ya Mganga Njiwa Manga alipokwenda kwake jana yake kufuatilia suala la kurudi mchumba wake Brighton, aliyekuwa chini ya bahari katika chumba cha giza.

Majibu ya mganga yalimkatisha tamaa tofauti na alivyofikiria kupatiwa matibabu kama ya Sharifa ya kuingizwa ndani ya maji ya bahari usiku wa manane. Alishangaa kuambiwa baada ya kukutana naye na kuchukua vitabu vyake vya uganga na kuvisoma kwa muda. Alipomgeukia alimueleza:

“Kazi yako inanichanganya sana, mpenzi wako bado yupo chumba cha giza, inaonesha alitolewa na kurudishwa tena, kuna utata mkubwa juu ya hatima ya mumeo kutolewa chini ya bahari kurudishwa duniani.”
“Mungu wangu! Si atauawa?” Suzana aliuliza.
“Hawezi kuuawa, inaonesha uhai wake bado mrefu.”
“Sasa itakuwaje ikiwa kila siku mambo yanazidi kuwa mabaya kwake, huoni kama maisha yake yapo hatarini?”

“Ni kweli yapo hatarini lakini..”
“Lakini nini mganga? Naomba msaada wako wa kumtoa huko.”
“Nilikueleza toka siku ya kwanza kuwa ni vigumu kumtoa kwenye chumba cha giza kwani kila nikimtafuta haonekani. Kuna siku mchana nikiwa katika shughuli zangu nilikiona kivuli cha mchumba’ako, ilionesha ametolewa chumba cha giza lakini usiku nilipotaka kuifanya kazi ile sikumuona.

“Kitendo kile kilinichanganya sana, hasa baada ya kuwa nimefika baharini na mbuzi wangu wawili, mweupe na mwekundu. Nilijikuta nikimtafuta tena lakini sikuweza kumuona. Niliamua kurudi nyumbani ili kuangalia upya, wasiwasi wangu nilidhani labda amekwisharudi duniani.

“Nilimtafuta kila kona ya dunia mpaka chini ya udongo sikumuona, kila nilipomtafuta ilionesha bado yu hai, lakini alikuwa haonekani zaidi ya kiza kinene. Baada ya kuhangaika sana niliweza kukiona kivuli chake kwa taabu sana kikionesha yupo kwenye chumba cha giza.

“Lakini kila nilivyojaribu kumvuta hakuonekana, huwezi kuamini kazi yako nimeifanya kwa muda mrefu bila mafanikio kuliko kazi nyingi nilizowahi kufanya. Wakati nikiendelea kuhangaika kutafuta nilishangaa kuona taarifa ikinionesha kuwa mumeo atatoka chini ya bahari bila kutumia dawa yoyote.”

“Sasa atatokaje ikiwa bado ameshikiliwa na majini?”
“Mara zote huongozwa na maandiko ya vitabu vya uganga ili niweze kumtibu mgonjwa, siwezi kukurupuka ndiyo maana dawa zangu huwa sibahatishi.”
“Hakuna njia nyingine ya kunisaidia?”

“Siwezi kukudanganya ila nakuhakikishia mpenzi wako atarudi bila dawa yoyote.”
Suzana alikubali kwa shingo upande kwa kuamini sifa za mganga yule kuwa hashindwi na kitu ni za uongo. Aliona ni ajabu Brighton kurudi bila dawa yoyote. Baada ya kuondoka na kurudi nyumbani aliondoa tumaini la kurudi kwa mpenzi wake.

Akiwa bado ofisini, katikati ya mawazo ya kukumbuka maelezo ya mganga yaliyomkatisha tamaa, baada ya kuonekana ameshindwa kumrudisha mpenzi wake na kuweka visingizio lukuki. Alishtushwa na sauti ya Sharifa aliyeingia ofisini kwake bila kumuona kutokana na kuzama kwenye dimbwi la mawazo.

“Suzana vipi shoga mbona unaonekana upo mbali, una tatizo gani?”
“Ooh! Shoga karibu.”
“Mbona hivyo, una tatizo gani maana nimeingia bila wewe kuniona?”
“Sharifa ina maana huyajui matatizo yangu?”
“Nayajua lakini leo umekuwa tofauti na siku zote.”

“Ni kweli.”
“Tatizo nini?”
Suzana alimtonya Sharifa aliyoelezwa jana yake na Mganga Njiwa Manga alipofuatilia kumrudisha duniani mpenzi wake. Kutokana na majibu yake juu ya mganga, ilionesha kabisa hakukuwa na uwezekano wa kurudishwa kwa mchumba wake.

“Nina imani mzee yule si mganga, wala hana lolote! Anafanya kazi kwa kubahatisha, iweje aweze kumuona ashindwe kumrudisha? Kisa, oooh, nilimuona mchana usiku akapotea, mwongo mkubwa hana lolote yule,” Suzana alilalamika.
“Lakini si alikueleza atarudi, tena kizuri hakukudanganya, au ulitaka akudanganye ili achukue fedha zako?”

“Kuna mtu gani anaweza kutoka kwa majini bila dawa au maombi?”
“Muamini yule babu, analokueleza ndilo linalokuwa.”
“Kipi cha kunifanya nimuamini zaidi ya sifa za kusikia?”
“Basi shoga mguu huu ni wako.”
“Una maana gani?”

“Mambo yamejibu.”
“Mambo gani?”
“Kazi ya mzee Njiwa Manga.”
“Kazi gani?”
“Kweli Suzana umechanganyikiwa.”

“Unafikiri kidogo, mtu siku zinakatika hakuna dalili zozote za kurudi kwa mpenzi wangu.”
“Suzana kwa mganga Njiwa Manga si nilikwenda kwa ajili ya kurudishiwa kizazi?”

“Ndiyo.”
“Basi majibu yametoka.”
“Ina maana wewe ni mjamzito?”







JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.36



“Ndiyo maana yake.”
“Utani huo.”
“Kweli shoga nimeamini yule babu ni mganga kweli.”
“Kama ni hivyo basi hataki kunisaidia.”
“Amekataa vipi wakati kakueleza ukweli juu ya ramli yake ilivyomuongoza. Ingekuwa hawezi kitu angekwambia japokuwa hajawahi kushindwa matatizo ya majini.”

“Mmh! Kwa hiyo una uhakika kuwa Brighton atarudi bila kufanya dawa yoyote?”
“Kama amekueleza atarudi ujue atarudi, si alikwenda baharini na mbuzi wawili. Kama angekuwa hataki kukusaidia asingeona umuhimu wa kwenda kujisumbua baharini saa nane za usiku.”
“Mmh! Mimi nilijua labda ni njia ya kujitetea tu.”

“Suzana, kwa taarifa nilizozipata kutoka kwa mama, Njiwa Manga kazi ya uganga huu ni mwaka wa thelathini na siyo watu wa hapa tu nchini, kuna watu wanatoka mbali kwa ajili ya kufuata tiba zake. Si hivyo tu, ameshachukuliwa sana na watu wa mbali kwa ajili ya kwenda kufanya matibabu, kuna kipindi alikuwa akiondoka zaidi ya mwaka, kitu ambacho baadaye alikiona kuwa si kizuri kwa watu wengi hukosa huduma zake na kuamua kutosafiri.

“Si wewe hata mimi siku tulipokwenda baharini na hali iliyonitokea kisha kusema eti tayari kizazi changu kimerudi niliona ni uongo. Lakini hali iliyonitokea hivi karibuni na kufanya vipimo vyote na kujiona nina ujauzito nimekubaliana na mama kuwa, kweli mzee Njiwa Manga ni mganga wa kweli.

“Kwa hiyo shoga yangu nakuomba uvumilie kama amekuhakikishia uhai wa mpenzi wako ni mrefu ni kiasi cha kuvuta subira, nina uhakika alichosema kitakuwa kweli.”
“Mmh! Itabidi nikubali lakini moyo haunipi kabisa.”
“Sikuzuii kufikiria hivyo, lakini amini usiamini mzee Njiwa Manga ni mganga wa kweli.”
“Mmh! Haya,” Suzana alikubali kwa shingo upande.

“Basi shoga mguu ulikuwa wako kukujulisha mzee Njiwa Manga amefanya mambo, punguza mawazo kila alilosema mganga litatimia mimi naamini Brighton atarudi bila ya dawa kama alivyosema.”
“Kama alichokisema ni kweli nitampa zawadi kubwa.”
“Hata mimi najiandaa kumpelekea zawadi kubwa, sijui hata nimpelekee nini?”
“Utakachojaaliwa.”

“Shoga baadaye.”
“Sawa, wacha na mimi nianze kazi kidogo umeichangamsha akili yangu bila hivyo siku ya leo ingekuwa ngumu kwangu.”
“Najua hata mimi baada ya kuona mabadiliko ya mwili moyo wangu ndipo ulipofunguka.”
“Wacha na mimi nisubiri.”
Sharifa alirudi ofisini kwake na kumuacha Suzana akijiandaa kuanza kazi za siku ile.
****

Baada ya Balkis kupelekwa katika chumba cha giza, mfalme alionekana kuzidi kukasirika kwa kuona mtoto wake amemkosea adabu. Mkewe muda wote alikuwa ameinama bila kusema kitu, baada ya mwanaye kurudishwa chumba cha giza alimgeukia mumewe na kumuuliza kwa sauti ya ukali ambayo hakutakiwa kuitoa mbele ya mfalme.
“Sasa ulinituma kufanya nini na umefanya nini?”

“Kwanza punguza sauti yako ujue unaongea na nani?”
“Nazungumza na mume wangu na aliyepelekwa katika chumba cha giza ni mwanangu,” bado malkia Huleiya hakushusha sauti yake.
“Unabishana na mimi?” Mfalme aliuliza kwa sauti ya juu.
“Sibishani na wewe kwa vile anayeteseka ni mwanangu.”
“Lakini huoni kama amevunja sheria ya majini pia na wewe unanivunjia adabu kama mumeo na mfalme wako?”

“Nimekuvunjia adabu kivipi wakati nakueleza kitu cha kweli?”
“Kwa hiyo nivunje sheria kwa ajili ya mwanao?”
“Kwani unataka aolewe na jini mwenzake au atoroke?”
“Siwezi kuvunja sheria, majini wengine watanielewa vipi?”

“Kwani si ni wewe ndiye uliyeiweka sheria hii kwa roho mbaya yako baada ya majini wengi kuwa na uhusiano na wanadamu. Umemkataza mwanao asiolewe na mwanadamu, anakuomba umrudishe duniani mpenzi wake hutaki. Kuna faida gani kuwa mfalme wakati huna mapenzi hata na familia yako.”

“Kwa hiyo nawe unaungana na mwanao?”
“Ndiyo na pia nasema hivi, Soobaaa,” malkia Huleiya alimwita mkuu wa watwana msaidizi kwa sauti kubwa.

“Wa nini?” Mfalme Balami aliuliza.
“Naam Malkia mtukufu,” Soba aliitikia akiwa amesimama mbele ya malkia.
“Soba kamtoe haraka Balkis.”
Soba alibakia amesimama na kusita kutekeleza amri hiyo kwa kuhofia kupingana na mfalme.

Ni kweli kauli ya mganga Njiwa Manga itatimia? Mfalme wa majini atasalimu amri kwa mkewe?



ETAENDELEA BAADAE KIDOGO..................
 
JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.37

Soba alibakia amesimama kama sanamu, malkia Huleiya alipaza sauti yake tena:
”Soooba hujanielewa, kamtoe haraka Balkis chumba cha giza.”

Bado Soba alibaki amesimama huku akisubiri mfalme ataamua nini baada ya mkewe kutoa amri ya kupingana na mumewe kwa mara ya kwanza. Siku zote alijua mwenye sauti ya mwisho ni mfalme, malkia sauti yake siku zote aliitoa kwa taratibu tena ya chini. Toka awe ndani ya jumba lile la kifalme hakuwahi kusikia amri kali ya malkia.

“Sooooba, unanidharau?” Alimuuliza huku akiteremka sehemu ya juu alipokuwa amesimama pembeni ya mumewe.

Soba bado alisimama kikakamavu kusubiri kauli ya mfalme aende au la, aliamini siku zote mke wa mfalme hakuwa na maamuzi tofauti na mumewe. Kitendo cha Soba kukataa kwenda kumtoa Balkis kilimuudhi sana malkia na kuona umevunjiwa heshima.

Pembeni yake kabla hajafika kwa Soba alichomoa upanga uliokuwa kiunoni kwa mmoja wa walinzi wa nyumba ya mfalme na kulipunga hewani usawa wa shingo ya Soba. Wengi walijua anamtisha ili akubali kumfuata Balkis chumba cha giza alipofungiwa na mumewe.

Soba naye aliendelea kusimama kikakamavu akisubiri kauli ya mfalme aliyekuwa amepata kigugumizi kwa kitendo cha mkewe kumvunjia heshima mbele ya wasaidizi wake na watwana.
Panga alilopunga hewani bila hiyana lilitua kwenye shingo ya Soba na kutenganisha kichwa ni mwili. Kitendo kile kilimtisha kila mmoja aliyekuwepo pale, hata mfalme hakuwahi kuona hasira nzito ya mkewe kama siku ile. Kila mtwana aliyekuwa pembeni yake aliingiwa na mchecheto wa kuhofia maisha yake.

Malkia Huleiya baada ya kuona mwili wa Soba ukianguka chini kama gunia na kichwa kikigaagaa chini, alishtuka kwa kuona ameua, alilitupa upanga chini kisha aliangua kilio na kukimbilia chumbani. Kila tukio lililotokea muda ule lilimshangaza kila mmoja.

Mfalme alijikuta amebaki amesimama kama sanamu asielewe kilichotokea ni kweli au alikuwa akiota. Ulikuwa mwaka wa sabini na tano toka amuoe mkewe aliyekuwa msikivu na mtulivu pia mnyenyekevu kwa mumewe muda wote. Malkia Huleiya siku zote alikuwa kiumbe mwenye huruma na kumkanya mumewe pale anapotumia nguvu bila kutumia muda wa kufikiri katika maamuzi yake ya kutoa adhabu kwa majini yanapofanya kosa.

Lakini siku ile kwa mara ya kwanza alifanya kitendo kilichomshtua kila mmoja aliyemfahamu. Hata adhabu anapotoa mfalme, yeye ndiye aliyesimama kutetea.
Lakini kitendo cha kutenganisha kichwa na kiwiliwili cha jini hakuwahi kukifanya zaidi ya mumewe ambaye kila alipokosewa adhabu yake kubwa ilikuwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

Kitendo cha mkewe kumuua mtwana mkuu msaidizi aliyekuwa akitegemewa na mfalme baada ya Kulani kuwa kipofu kilimfadhaisha sana.

Alitoka sebuleni na kumfuata mkewe aliyekuwa amejitupa kitandani akilia kwa uchungu huku akijutia kitendo cha kumuua Soba.
Japo Soba alionesha jeuri lakini moyoni alijuta kwa uamuzi mzito alioutoa kwa kumtenganisha kichwa na mwili.

“Malkia wangu,” mfalme Balami alimwita mkewe kwa sauti ya upole.
“Nisamehe mume wangu, nimeshindwa kuzuia hasira zangu, yote ni kwa ajili ya mapenzi mazito kwa mwanetu wa pekee Balkis.”

“Najua mke wangu, lakini kitendo chako kimenifanya nijione nina mke mwenye maamuzi mazito.”

“Hapana sikutarajia kutoa uamuzi mzito kama ule, lakini yote umeyasababisha wewe.”
“Hapana mke wangu, ningejuaje uwezo wa maamuzi yako bila kufanya vile?”
“Si kwa kutoa roho ya kiumbe kisicho na hatia.”

“Ile imeonesha kumbe hata nikiondoka au nikifa hakuna mtu wa kukuchezea, kwa kitendo kile Balkis namtoa kwenye chumba cha giza pia kumrudisha duniani mchumba wake bila masharti.”
“Unasema kweli?” Malkia Huleiya alishtuka kusikia kauli ya mumewe.

“Kweli kabisa, hii itakuwa kama zawadi kwa ujasiri uliouonesha mbele yangu.”
“Asante mume wangu kwa uamuzi wako uliorudisha furaha yangu.”
“Si kurudisha furaha yangu tu bali kuendelea na msimamo huo huo ili kuongeza heshima ndani ya himaya yangu.”

Baada ya makubaliano alitumwa kibaraka kwenda kumtoa Balkis kwenye chumba cha giza lakini aligoma kutoka kama hawatamuachia Brighton. Waliamuliwa kwenda kuwatoa wote, walifanya hivyo na Balkis alikubali kutoka ndani ya chumba cha giza.

Pia alitoa masharti kuwa, kabla ya kuzungumza lolote wahakikishe Brighton anatolewa chini ya maji na kurudishwa duniani. Kwa vile uamuzi ulikuwa amepitishwa ombi lake halikupingwa na baba yake. Lakini kabla ya kurudishwa duniani Brighton alipewa masharti na mfalme kuwa siku atakayoitoa siri ya majini ndiyo siku ya mwisho ya uhai wake.

Baada ya kukubaliana na masharti, Brighton alisindikizwa na watwana kumi baada ya kumfikisha pembeni mwa bahari walimlaza pembeni. Ubaridi wa alfajiri na maji vilimfanya Brighton ashtuke na kujikuta amelala ufukweni, miguu ikiwa majini na mwili nchi kavu. Baada ya kunyanyuka alipokuwa amesimama kwa mshtuko. Aliifahamu sehemu ile ilikuwa ni eneo la daraja ya Salenda.

Baada ya kujinyanyua alipokuwa amekaa, alitembea kuelekea barabarani ili apate lifti ya kumrudisha kwake.

Je, kurudi kwa Brighton ndiyo mwisho wa Balkis kuchukua wanaume wa kibinadamu?







JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.38



Brighton alitembea kusogea barabarani kwa mwendo wa taratibu kutokana na mwili wake kukosa nguvu. Alikuwa akitembea kwa mwendo wa kuyumba yumba hadi alipofika chini ya mti uliokuwa pembezoni mwa barabara na kuuegemea kutokana na kuishiwa nguvu.

Suzana akiwa kwenye gari lake akielekea kazini, alishtuka kuona kitu ambacho hakukitegemea kwa muda ule. Roho ilimwambia aamini kitu anachokiona lakini akili ya kawaida ilikataa kwa kuamini kitu kile. Baada ya kuvuka eneo lile bado roho ilimwambia kuwa kitu alichokiona ndicho chenyewe.

Alisimamisha gari na kuliegesha pembeni, kisha aliteremka kwenye gari na kurudi sehemu alipomuona mtu aliyemfananisha. Alitembea taratibu hadi sehemu ile alipokiona kitu alichokifananisha. Brighton alikuwa kama mtu aliyelewa pombe kutokana na kuzidi kuishiwa nguvu.

Suzana alipomkaribia, alipunguza kasi ya mwendo wake zaidi huku akimkazia macho mtu yule, alipomsogelea karibu aligundua aliyekuwa mbele yake ni kipenzi chake Brighton.
“Brighton,” alimwita kwa sauti ya juu japo hakuwa mbali naye.
Brighton alinyanyua kichwa na kumtazama aliyekuwa akimwita, macho yake yaliona maluweluwe japo alimfahamu aliyekuwa mbele yake.

“Brighton,” Suzana alimwita tena huku akiogopa kumgusa.
“Suzana,” Brighton alimwita baada ya kuitambua sura ya mpenzi wake.
“Ni wewe Brigton?”
“Ni mimi Suzana umejuaje kama nipo hapa?”
“Ha! Siamini,” Suzana alimvamia Brigton na kumkumbatia kwa furaha.

“Ni mimi mpenzi wangu,” Brighton alisema huku akitokwa na machozi.
“Hapana Brighton, twende nyumbani,” alimshika mkono na kwenda naye kwenye gari.
Suzana aliligeuza gari na kurudi nyumbani kwake kwa kuwa alijua nyumbani kwa Brighton kusingekuwa katika hali ya usafi baada ya nyumba kukaa kipindi kirefu bila ya matunzo. Alipofika nyumbani alimtengea maji ya kuoga, kisha akamtayarishia chakula.

Baada ya kula Brighton alionekana kuwa na uchovu, aliamua kujilaza na usingizi mzito ukamchukua. Suzana alijikuta akiahirisha kwenda kazini ili aweze kuwa karibu na mpenzi wake aliyemtafuta kama maji kwenye ardhi kame.

Alijikuta akiyakumbuka maelezo ya mganga Njiwa kuwa, Brighton angerudi bila tiba yoyote, hamu yake kubwa alitaka kujua mpenzi wake alikuwa wapi na aliishi maisha gani. Alijikuta akisahau hata kutuma ujumbe kazini kuwaarifu mabosi wake kama amepata dharura, muda mwingi alimuangalia mpenzi wake aliyekuwa amelala.

Alimpapasa akiwa haamini kama kweli mtu aliyekuwa amechukuliwa na majini angeweza kurudi salama. Akiwa katika dimbwi la mawazo simu yake iliita. Alipoangalia juu ya kioo aliliona jina la Sharifa.
“Haloo Sharifa.”
“Suzana, upo sawa?”
“Nipo sawa.”

“Mbona hujaonekana kazini?”
“Huwezi kuamini yaliyosemwa yametimia?’
“Yepi hayo?”
“Brighton amerudi.”
“Acha utani!”

“Kweli kabisa na sasa hivi nipo pembeni yake.”
“Suzana hebu acha kunirusha roho.”
“Sharifa, naamini kabisa mzee Njiwa Manga ni mganga wa kweli.”
“Si ulikuwa unamuona tapeli.”
“Wee dada wee, kuchanganyikiwa kubaya.”

“Kwa hiyo kazini itakuwaje?”
“Naomba uniombee ruhusa kuwa naumwa nitakuja kuchukua ‘sick sheet’ baadaye.”
“Mmh! Huwezi kuamini furaha niliyoipata leo haina kifani ili kujiridhisha na maneno yako nitaomba ruhusa kuja kumuona shemeji.”

“Njoo dada umuone, huwezi kuamini amerudi amenenepa na kupendeza.”
“Basi nakuja na sick sheet yako kabisa.”
“Utakuwa umefanya jambo la mbolea.”
“Basi nakuja,” Sharifa alionekana kuwa na mshawasha wa kumuona Brighton.

****
Baada ya kutolewa kwa mpenzi wake chini ya bahari, Balkis alifurahi sana na kukubaliana na wazazi wake kurudi duniani kutafuta tena vizazi. Kitendo cha kukubali kulimfanya mfalme afanye sherehe kubwa ya kumuaga kwa mara ya pili. Sherehe ilifanyika juu ya bahari.

Majira ya saa saba za usiku Balkis aliagwa eneo la bahari na kuingia duniani kwa mara nyingine tena. Aliondoka eneo lile kwa kutembea taratibu pembeni mwa barabara eneo la Daraja la Salenda kuelekea maeneo wanayoishi binadamu. Alipokaribia njia panda ya Masaki aliona gari dogo likisimama ghafla na kuteremka mwanamke na baadaye akafuatia mwanaume.

Balkis amerudi tena duniani, nini kitatokea?







JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.39

Hakutaka kujionesha kwao, alisimama pembeni yao aone kuna nini. Cha kwanza kilichomvutia kilikuwa tumbo lililoonesha ujauzito la mwanamke aliyetoka kwenye gari. Kingine kilikuwa sura na mvuto wa mwanaume aliyefuatia. Mwanamke alionekana mwenye hasira sana kutokana na maneno yake.

“Umenifuata ili iweje? Nimekwambia niache na maisha yangu na ujauzito huu nautoa.”
“Lakini mbona umefikia huko mke wangu?”
“Wewe si unaniona mimi si mwaminifu, basi kwa taarifa yako kuanzia leo achana na mimi.”

“Mke wangu mimi mumeo nina haki ya kukuuliza jambo lolote linalokwenda kinyume na maadili ya ndoa.”
“Kama umeniona nimetoka nje ya maadili ya ndoa si uniache.”
“Siwezi kukuacha kwa vile bado ni mke wangu.”

“Kwani ndoa lazima, ukiona hivyo ujue sina shida na wewe.”
Mwanamke alionesha jeuri kwa mumewe, Balkis alitulia ajue mwisho wake.
“Mke wangu bado tuna nafasi ya kulizungumza hili,” mwanaume alimbembeleza mkewe.
“Ngoja nikueleze kitu, ujauzito huu sio wako na mwenye ujauzito huo utamuona muda si mrefu.”

“Mke wangu umefikia hivyo?”
“Ulikuwa hujui?”
“Usifanye hivyo mke wangu bado nakupenda sana.”
“Mimi sikupendi,” mwanamke alisema huku akifunua simu na kupiga namba, alimsikia akizungumza.

“Eeh... nipo njia panda ya Masaki... njoo utanikuta.”
“Mke wangu unampigia simu nani?”
“Mume mwenzio anayejua kulea asiye na gubu kama wewe.”
“Mke wangu ni maneno gani hayo?”
“Najua litakuuma na mwaka huu wako, kama ulimwacha mkeo kwa ajili yangu sasa imekula kwako.”

Maneno yale yalimchoma sana Balkis aliyekuwa amesimama pembeni yao akifuatilia mazungumzo yale. Alimuonea huruma mwanaume aliyekuwa akimbembeza mwanamke mpaka kumpigia magoti na machozi yakimtoka. Alitamani kuingilia ugomvi ule lakini hakuna ambaye angemuelewa kwa muda ule kutokea mbele yao.

Alitulia kufuatilia mazungumzo yale bila kuzungumza chochote, mwanaume akiwa bado anaendelea kumbembeleza mkewe, gari aina Toyota VX lilisimama pembeni ya gari la wanandoa wale.
Baada ya kusimama aliteremka mwanaume mwenye mwili uliojengeka kimazoezi aliyekuwa amevaa bukta na fulana ya mikanda. Yule mwanamke alimsukuma mwanaume aliyekuwa amepiga magoti na kumfuata aliyekuja na VX.

“Vipi Sweet?” aliuliza yule mwanaume.
“Si huyu ----- ndiyo anayeniwekea usiku.”
Walizungumza wakiwa wamekumbatiana pembeni ya mwenye mke aliyekuwa bado amekaa chini baada ya kusukumwa na mkewe. Kitendo kile kilimtoa machozi Balkis na kuapa kuwashikisha adabu.
“Pole sweet, twende zetu.”

Walishikana mikono na kwenda ndani ya gari na kumuacha mwanaume akilia kwa uchungu huku akizungumza maneno yaliyokwenda na upepo lakini Balkis aliyasikia.
“Kweli mwanamke shetani yaani yote niliyokufanyia umeniona sifai, nimekosana na familia yangu kwa ajili yako. Mwisho unanivua nguo mbele za watu, sioni faida ya kuishi bora nife.”

Kauli ile ilimtoa machozi Balkis na kuona jinsi gani wanawake wanavyoweza kuwaingiza wanaume kwenye matatizo. Alimuona yule mwanaume kama mtu aliyechanganyikiwa akienda ndani ya gari na kutoka na kipande cha kamba ili ajinyonge.

Alisogea kwenye mti wa pembeni na kuifunga ile kamba, akatafuta tawi zuri ambalo alifunga kamba ili ajinyonge. Kabla hajajitundika Balkis alijitokeza mbele yake, jamaa alishtuka kumuona mwanamke mzuri kasimama mbele yake usiku ule wa manane. Alipomuona alisogea pembeni ya kamba ili Balkis asijue kama alikuwa anataka kujinyonga.
“Mudy kwa nini unataka kujiua?” Balkis alimuuliza.

Balkis atamuacha Mudy ajiue nini adhabu ya mke wa Mudy? Kuyajua yote tukutane Risasi Jumatano.
Mudy kama alivyoitwa na Balkis alishangaa kuona mwanamke mzuri mbele yake usiku ule tena akimfahamu kiufasaha.
“Umenijuaje?” alimuuliza.

“Kukujua si muhimu kuliko kujibu swali langu kwa nini unataka kujinyonga?”
“Nani kakwambia?”
“Mudy niambiwe na nani wakati naiona kamba ikining’inia?”
“Basi tu nimeamua.”

”Uamue nini wakati umekataliwa na mkeo.”
“Wewe umejuaje?”
“Kwani uongo?”
“Hata kama si uongo wewe umejuaje na usiku kama huu unatoka wapi huogopi?”
“Mudy si muda wa kutaka kujua nimejuaje au natoka wapi? Unataka kuniambia wanawake wamekwisha mpaka umng’ang’anie mwanamke asiyekupenda?”

“Sio kumng’ang’ania, bali kanitia umaskini wa kutumia fedha nyingi kwa ajili yake.”
“Sikiliza Mudy, ulitakiwa kumshukuru Mungu kwa kukuonesha hili mapema, au ulitaka ufilisike kabisa ndiyo akuache.”
“Kama hivi nimekosana na ndugu na jamaa zangu kwa ajili yake wakisikia ameniacha nitakuwa mgeni wa nani?”

“Sikiliza Mudy, hakuna mtu anayechukiwa milele, kama utaomba msamaha watakusamehe.”
“Mmh! Kwangu ni ngumu, kuwa na mwanamke yule niligeuka adui wa familia, wote waliniombea mabaya. Leo wasikie si utakuwa sherehe, kwa vile hunijui sikujui kwa nini usiniache nitimize dhamira yangu?” Mudy alimuomba Balkis amuache ajiue.

Balkis atamuacha Mudy ajiue nini adhabu ya mke wa Mudy?






JINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.40



“Sina budi kufanya hivyo.”
“Sikiliza Muddy, ulitakiwa kumshukuru Mungu kwa kukuonesha jambo hili mapema, au ulitaka hadi ufilisike ndipo mkeo akuache?”

“Nimekosana na ndugu na jamaa zangu kwa ajili yake, wakisikia ameniacha nitakuwa mgeni wa nani?”
“Sikiliza Muddy, hakuna mtu anayechukiwa milele, kama utawaomba msamaha ndugu na jamaa zako watakusamehe.”

“Mmh! Kwangu ni vigumu, kwa kuwa mwanamke yule alinifanya niwe adui wa familia, wote waliniombea mabaya. Leo wakisikia si itakuwa sherehe, kwa vile hunijui sikujui kwa nini usiniache nitimize dhamira yangu?” Muddy alimuomba Balkis.

“Inawezekana wewe ndiye hunijui lakini mimi nakujua vizuri, toka ulipoanza maisha ya shida, hadi pale mpenzi wako wa kwanza alipoiba fedha kwao zilizokufanya upate utajiri na kukuvimbisha kichwa kwa dharau na kukufanya uwatelekeze mkeo na mtoto wako.

“Mkeo kwa aibu kutokana na kuidharau ya familia yake, baada ya kumtelekeza aliamua kunywa sumu pamoja na mtoto wake. Kwa vile ulikosa shukrani wala fadhila, kifo cha mkeo na mtoto wala hakikuugusa moyoni mwako, ukaamua kuendelea na maisha yako na mpenzio mpya ambaye mlifunga ndoa ndani ya wiki tatu baada ya vifo hivyo.

“Fedha zilikupa jeuri na kudharau wazazi na nduguzo waliokueleza tabia chafu za mkeo, kwako uliona kama wanaleta fitina ili muachane. Lakini ukweli uliuona baada mambo kuanza kukuendelea kombo, mke uliyemuoa tabia yake ni kuharibu ndoa za watu baada ya kukufilisi mwisho wake ndiyo kama ulivyokuwa ukitaka kufanya.

“Lakini kwa tabia hiyo nitawakomesha, siwezi kuona familia zinahangaika kwa ajili ya upumbavu wa watu wachahe,” Balkis alisema kwa sauti ya hasira.
“Kwani dada wewe ni nani na utawakomesha vipi?”
“Utajua muda si mrefu.”

“Samahani dada yangu wewe ni nani maana unanijua vizuri kuliko hata watu wangu wa karibu.”
“Naitwa Balkis.”
“Hii siri yangu nani kakwambia?”
“Narudia tena usitake kumjua aliyeniambia,zaidi ya kujua ubaya wa mtu uliyekuwa naye. Kwa mchezo wake ndoa yako ni ya tano kuvunjwa na yeye na kila alipopita aliacha msiba, ningechelewa kidogo jina lako lingebaki historia midomoni mwa watu.”

“Mmh! Wewe huku unatoka wapi usiku huu?”
“Kwetu siyo mbali naomba ikiwezekana ukalale kwa vile najua huwezi kuendesha gari kutokana na kuchanganyikiwa. Ningekuwa nimeaga nyumbani ningekupeleka kwako.”
“Unataka nikalale kwako na mumeo?” Muddy aliuliza.

“Sijaolewa.”
“Unakaa na nani?”
“Nipo na wazazi wangu.”
“Ulijuaje kuna tukio hili?”

“Nilipokuwa nimelala nilisikia mkibishana, nikatoka ndani na kusogea hadi pembeni yenu kwa vile kila mmoja alikuwa na hasira hamkuweza kuniona. Nilipowaona niliwatambua kutokana na maelezo ya watu juu ya matatizo yenu ya ndoa kutokana na kuijua tabia ya mkeo toka zamani.

“Mambo mengi nilikuwa nayajua, nilipotoka nje na kuwakuta sikushangaa kusikia tambo za mkeo. Baada ya kuondoka nilijua nini kinafuata, nilijua utataka kujinyonga tu kama walivyofanya wanaume wengi walioachwa kama wewe. Kwa vile ulikuwa hujui upande wa pili wa mkeo.

“Hata mkeo alipoondoka anaamini kabisa uamuzi utakaochukua ni huo, hushangai alikueleza uchukue kamba bila kukupa maelekezo. Kesho anasubiri kusikia kifo chako na kuchukua vitu vyako vyote bila familia yako kuambulia chochote.

“Na hata akisikia hujafa lazima atafungua kesi ya kudai mgawane mali kuhakikisha anakufilisi kabisa. Utavumilia lakini mwisho wake ni kujiua kwa sumu au kamba.

“Niliona kuna umuhimu wa kukueleza kilichokuzunguka katika ndoa yako, yule si mwanamke ila ni mwizi tena muuaji. Hebu niangalie mimi nilivyo mrembo, yule mkeo tapeli ananifikia?” Balkis alimuuliza Muddy huku akijigeuza na kupigwa na mwanga wa taa za barabarani.

“Hawezi kukufikia.”
“Sasa mwanamke kama mimi nikikupa penzi la kweli bila kuhitaji fedha zako unasemaje?”
“Unataka kuniambia mwanamke mzuri kama wewe hujaolewa?”
“Sijaolewa bado nipo kwa wazazi wangu kama nilivyokueleza awali.”

”Maeneo haya unakaa nyumba gani?”
“Ingia kwenye gari nikakuoneshe.”
Muddy aliingia kwenye gari na Balkis naye aliingia upande wa dereva na kuanza kuendesha gari. Baada ya mwendo mdogo gari lilikata kushoto na kuingia kwenye jumba la kifahari.

Muddy pamoja na kuwa mwenyeji wa eneo lile lililopo karibu na Daraja la Salenda hakuwahi kuliona jumba zuri la kifahari. Baada ya gari kuingia katika jumba lile ambalo toka azaliwe hakuwahi kuingia, Balkis alimkaribisha hadi chumbani.

“Karibu mpenzi nikupoze machungu yote.”
“Asante.”
Balkis alimshika mkono Muddy na kumuongoza, hakuamini mahaba aliyooneshwa na Balkis mwanamke mwenye uzuri wa ajabu.

Nini hatima ya Muddy mikononi mwa Balkis? Kuyajua yote tukutane kesho hapa hapa UNLIMITED SWAGGAZZ!!!!!
*story unaionaje?
*mpk sasa umejifunza nini?
*je tufanyeje ili kuepukana na balaa km hili???

ETAENDELEA BAADAE KIDOGO NINAKUACHA KWA MUDA...........
 
JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.41.


ILIPOISHIA:
“Karibu mpenzi nikupoze machungu yote.”
“Asante.”
Balkis alimshika mkono Mudy na kuingia naye ndani, Mudy hakuamini mahaba aliyooneshwa na Balkis, mwanamke mwenye uzuri wa ajabu.
SASA ENDELEA...

Muddy aliingizwa kwenye jumba la kifahari lililokuwa na mapambo ghali ambayo aliwahi kuyaona katika picha za majumba ya Falme za Kiarabu.
“Karibu sana.”
“Asante.”

“Muddy naomba ukaoge kwanza ndipo tupumzike.”
Muddy alinyanyuka na kupelekwa kwenye bwawa la kuogelea lililokuwa mbele ya nyumba. Baada ya kuoga alipewa taulo laini la sufu na kupewa makubazi ya kuvaa kisha alirudi ndani. Kwa vile usiku ulikuwa umeingia sana alipelekwa moja kwa moja kitandani.

Kila mmoja alilala chumba chake, Muddy alilala usingizi mzuri ajabu ambao hakuwahi kulala katika maisha yake. Alijikuta akitamani siku moja aishi maisha kama yale. Balkis aliingia katika mawazo ya Muddy na kuamini kama atatumia udhaifu ule basi atampata kirahisi.

Majira ya saa kumi na nusu za usiku Balkis alimuamsha Muddy kisha alimpa chai yenye viungo na kumueleza:
“Muddy muda wa kurudi baba yangu umekaribia, naomba nikurudishe kwako.”

“Mmh! Sawa lakini bila ya baba yako nisingeamka mapema sijawahi kulala usingizi mtamu kama leo.”
“Muddy, jitahidi kumuondoa akilini mkeo tapeli ambaye hatarudi kwako tena baada ya kukamilisha kilichomleta. Ukimuona anarudi ujue anaifuata roho yako. Kama utaachana naye nakuhakikishia kuishi maisha mazuri. Kama utakuwa mkweli na mwaminifu, nitayabadilisha maisha yako,” Balkis alimueleza Muddy ambaye hakuamini nguo zake kufuliwa usiku ule na kupigwa pasi kisha kupuliziwa manukato.

“Kama unayosema ni kweli mke wangu hatarudi basi, nitakuwa na wewe.”
“Muddy usitake kuniudhi, wewe ni mwanaume gani mkeo anachukuliwa mbele yako unaishia kulia, kwa kinywa chake kakueleza hakutaki, unataka upate ukweli gani?”

“Ni kweli usemayo, lakini kumbuka yule bado ni mke wangu, hivyo tunaweza kuzungumza na kuyamaliza.”
“Muddy nikueleze mara ngapi? Siku utakayorudiana na mkeo ujue ndiyo siku ya mauti yako. Wewe si mtu wa kwanza kufanyiwa hivyo, kama huamini kesho utaletewa karatasi itakayokutaka ufike mahakamani kwa ajili ya madai ya kugawana kidogo ulichobakia nacho.

“ Kibaya ni kwamba una deni la mkeo ambalo litasababisha usipate hata fedha nusu ya kuuza vitu vyenu. Kwa vile hukujua deni alilokukopesha riba yake inazidi thamani ya vitu ulivyobakia navyo.
“Kwa vile ni mzoefu wa mchezo ule, lazima atashinda kesi na wewe utachanganyikiwa, kitakachofuatia itakuwa ni kuokota makopo. Inawezekana una masikio ya kenge mpaka utoke damu ndipo usikie, usinitafute wala ukiniona usinifuate.”
“Sasa dada utanisaidiaje?”

“Niite Balkis.”
“Sasa Balkis utanisaidiaje?”
“Nakuomba chochote atakachokifanya asikushtue, wewe kubaliana nacho, mimi nitakuwepo mahakamani siku ya mwisho.”

“Nitashukuru.”
“Basi acha nikuwahishe kabla baba hajarudi.”
Walitoka na kuingia kwenye gari, kisha Muddy aliendesha kurudi nyumbani kwake baada ya akili yake kuwa imetulia kidogo. Alipofika waliingia wote ndani, Balkis hakukaa sana aliondoka na kumuacha Muddy amalizie usingizi.

***
Muddy alishtuka saa nne asubuhi na kujikuta akiwa na mawazo juu ya matukio yaliyomtokea jana ya kuachwa na mkewe pia kukutana na mwanamke mrembo mwenye mapenzi na huruma, Balkis. Pamoja na kuoneshwa ukarimu wa hali ya juu bado kitendo cha mkewe kumkataa kilimuumiza na kukumbuka vitu vingi alivyopoteza kwa ajili yake.

Alikumbuka jinsi alivyotelekeza familia yake kwa ajili yule mwanamke na kusababisha kupoteza mke na watoto. Bado hiyo haikutosha, aliweza kutumia fedha nyingi alizowekeza mke wake wa kwanza vibaya kiasi cha kumtia katika umaskini.

Pia alisababisha kutengwa na familia yake na kuwa adui yao mkubwa baada ya kugoma kutoa fedha za matibabu zilizosababisha dada yake mkubwa kupoteza maisha baada kukatazwa na mkewe asitoe kitu.
Kila alipokuwa akifikiria yote yale moyo ulikosa amani, aliamini njia nyepesi ya kukimbia aibu ile ni kunywa sumu au kujinyonga. Akiwa katikati ya uamuzi mzito, hodi mlangoni iliyahamisha mawazo yake yaliyokuwa yamefanya atokwe na machozi na macho kuwa mekundu kutokana na maumivu ya moyo.
Alifuta machozi na kwenda hadi mlangoni na kufungua, alikutana na kijana mtanashati.

“Karibu,”
“Asante, siingii ndani natoka mahakama ya mwanzo kuna barua ya madai toka kwa aliyekuwa mkeo.”






JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.42.



LAKINI likatokea jambo la ajabu, Muddy kila alipokuwa akikitafuta kisu hakukiona. Alihangaika nyumba nzima, hakukiona. Wazo lingine lilikuwa ni kutafuta kamba ili ajinyonge, vile vile alishangaa kuikosa kamba hata ile aliyotaka kujinyongea usiku na kuiacha kwenye gari, alipoifuata pia hakuikuta.

Hakurudi ndani, alikwenda dukani na kuchukua sumu ya panya, aliichanganya katika chupa ya maji ya kunywa kisha akanywa yote na kwenda kulala akisubiri malaika wa kifo amchukue.
***
Ashura mke wa Muddy alikuwa mwenye furaha, yeye pamoja na mwanaume wake walikuwa wakipongezana kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kumfilisi Muddy.
“Nina imani kazi imekwenda vizuri,” mwanaume huyo alisema.

“Ni kweli, lakini pamoja na kuyafanya yote bado namuonea huruma Muddy. Kwa nini tusimuachie gari na nyumba?” Ashura alisema katika hali ya kumuonea huruma Muddy.
“Tukiwa na huruma hatuwezi kuifanya kazi hii, ona leo tulivyo na utajiri wa kutisha.”
“Mmh! Kweli.”

Wakati Ashura na mwanaume wake wakiwa katikati ya mazungumzo, mlango uligongwa. Wote walikaa kimya kusikiliza, mlango ulipogongwa tena mwanaume alinyanyuka na kwenda mlangoni. Alipoufungua alikutana uso kwa uso na Balkis, akamkaribisha.
“Karibu mrembo.”

“Ahsante sijui Ashura anakaa hapa?”
“Wewe nani?”
“Sasa kaka yangu badala ya kunijibu, unaniuliza mimi nani?”

“Eeh, si vibaya kukujua wewe ni nani kwa vile unayemuuliza ni mke wangu na wewe ni mgeni kwangu.”
“Mimi naitwa Balkis, ina maana Ashura ameshaachana na Muddy?” Balkis aliuliza swali la uongo.
“Hiyo haikuhusu, sema kilichokuleta.”
“Kilichonileta ni kuonana na Ashura.”
“Karibu ndani.”

Alimkaribisha sebuleni ambapo alimkuta Ashura amejilaza kwenye kochi. Ashura alimshangaa yule mgeni kutokana na uzuri wake wa ajabu, pia vito vya thamani alivyovaa mwilini mwake. Hata manukato yake yalikuwa mageni puani ambayo yaliifanya nyumba nzima kunukia.
“Habari Ashura?”

“Nzuri, umenijuaje?”
“Ina maana jina lako ni siri? Wanapaswa kulijua watu wachache?”
“Siyo kwamba ni siri ila sikujui.”
“Huwezi kuwajua wote mdogo wangu.”
“Mh! Nikusaidie nini?”
“Nimetumwa na Muddy.”
“Muddy! Muddy ndiye nani?”
“Mumeo.”

“Mimi nina mwanaume anayeitwa Muddy?”
“Sasa unashangaa au unakataa? Ndoa yako na Muddy imevunjika lini wakati mpaka jana usiku majira ya saa sita mmenipita Daraja la Salenda mkiwa pamoja, leo hii unamkana?”
“Basi muda mfupi baada ya kutuona wewe ndipo tulipoachana.”
“Sasa nani kamuacha mwenzake?”
“Maswali gani hayo?”

“Ndiyo maana nipo hapa,” Balkis alisema kwa kujiamini.
“Wewe ni nani kwa Muddy?” Ashura alihamaki.
“Kabla sijakujibu nataka useme ukweli mbele ya mwanaume wako, upo tayari kurudiana na Muddy?”
“Sipo tayari.”

“Na ukirudiana naye tena?”
“Nitembee uchi.”
“Rudia.”
“Nitembee uchi.”
“Kaka umesikia?” Balkis alimgeukia mwanaume wa Ashura na kumuuliza.
“Umesikia?”

“Kuwa?”hi akirudiana na Muddy.”
“Basi ni hayo niliyofuata hapa.”
“Mbona umeniuliza hivyo?” Swali la Balkis lilimtisha Ashura.
“Si umeachana na Muddy?”

“Ndiyo, nirudiane naye kwa kitu gani alichonacho, tena muda si mrefu ataokota makopo.”
“Usiokote makopo wewe, tena kabla sijaondoka nawapeni onyo mchezo wenu wa kudhulumu mali za watu utawatokea puani,”
Balkis alimweleza Ashura ambaye bado alikuwa akimshangaa kwa maswali yake.

Nini kiliendelea? Fuatilia katika Gazeti la Risasi Jumamosi.
Vituko
ndani ya daladala
Abiria wawili ambao majina yao hayakujulikana, juzikati walitwangana makonde mazito baada ya mmoja wao kutoa nauli ya shilingi 200 badala ya 300.

Abiria wa kwanza alipanda daladala hiyo Buguruni akielekea Gongo la Mboto na wa pili Vigunguti.
Kondakta alipoanza kutoza nauli, abiria wa kwanza alitoa shilingi 200. Kitendo hicho kilionekana kumkera abiria wa pili kwa kumwambia kwa nini katoa nauli nusu.

Abiria hao walianza kuzozana na kondakta akaungana na kauli ya abiria wa pili ya kumtaka wa kwanza kutoa shilingi 300 na si 200.
Hali hiyo ilionekana kumkera abiria wa kwanza na kuamua kumrushia ngumi abiria wa pili. Kitendo cha abiria huyo kurusha konde kilisababisha timbwili kali kwa washkaji hao kuanza kutwangana kavukavu.

Mbaya zaidi abiria wa kwanza alikuwa amekaa kiti cha mbele na walipoanza kurushiana makonde mazito gari lilianza kuyumba na kusababisha abiri wengine kuanza kupiga kelele ya kumuomba dereva asimamishe gari.

“Dereva simamisha gari utatuua, tunakuomba sana tumeshinda salama tunataka tufike nyumbani tukiwa wazima, tafadhali,” alisikika abiria mmoja huku wengine wakimuomba Mungu awaepushe na balaa hilo.

Wakati abiria wakipiga kelele, daladala hilo ilikuwa mwendo mkali. “Jamani mnataka kutuua kwa sababu ya shilingi 100? Acheni kugombana nitampa konda,” jamaa mmoja alisikika akisema.
Gari liliposimama jamaa hao walishuka na kuanza kukunjana vema na abiria wengine wakaingia ndani ya gari na kumwambia dereva aendeshe.
Mabondi hao wasiotambuliwa na shirikisho la ngumi Bongo waliachwa kituoni hapo wakitifuana.






JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.43.


Muddy alishtuliwa katika usingizi mzito na sauti ya Balkis, aliposhtuka alijishangaa kujiona bado yupo hai hakufa kama alivyodhamilia.
“Muddy vipi?”
Muddy hakumjibu alimshangaa Balkis aliyekuwa ameshikilia barua mkononi.

“Muddy mbona unanuka sumu ya panya?”
Bado Muddy hakuwa najibu aliendelea kupepesa macho na kuitazama glasi aliyokunywa sumu ilikuwa juu ya sturi.
“Muddy kwa nini unataka kujiua?” Balkis alimuuliza akiwa ameshika glasi iliyokuwa na sumu.
“Umejuaje?”

“Muddy nikufundishe mara ngapi swali mwenzake jibu na si swali kwa swali.”
“Umeisoma hiyo barua?”
“Niisome ili iwe nini, haya nilikueleza tokea awali kwa nini hutaki kunielewa?”
“Samahani Balkis nimechanganyikiwa.”

“Nilikueleza toka awali hutakufa bali unaelekea kwenye wendawazimu na usiponisikiliza sasa hivi utaokota makopo.”
Muddy alishangaa jinsi Balkis mwanamke mrembo mara kumi Ashura ameonesha mapenzi ya kweli kwake. Kingine kilikuwa uelewa wa ajabu wa Balkis kuonekana kumfahamu vizuri yeye na Ashura bila kuhadithiwa na mtu.

Hatua ya kupelekwa mahakamani ili wakagawane vitu pia deni la mkewe lililokuwa likizaa liba kila kukicha lilizidi kumchanganya. Alijikuta akinyanyuka na kuketi kwenye kitanda na kumuuliza Balkis.
“Balkis unaonekana unajua mambo mengi juu yangu ya Ashura?”
“Ndiyo maana nipo hapa kuokoa maisha yako, kwa vile lengo la mkeo wa uongo limetimia.”
“Yote haya umeyajulia wapi?”

“Utajua ukinipa moyo wako uliojeruhiwa niuponye.”
“Kwa ukweli niliouona nipo tayari kukukabidhi moyo wangu.”
“Je, Ashura akirudi kukubembeleza?”
“Kwa uliyonieleza siwezi kurudiana na mwanamke yule ambaye kwangu ni muuaji.”

“Nakuhakikishia kama utakuwa mkweli nitayabadili maisha yako, lakini chonde unigeuke baada ya kuwa na maisha mazuri utanisamehe.”
“Nikuhakikishia nitakupenda kwa moyo wangu wote, najiona kiumbe mwenye bahati kupendwa na mwanamke mrembo tena mwenye maisha mazuri. Nakuapia kukupenda mapenzi ya dhati.”
“Asante Muddy.”
***
Balkis baada ya kujua Muddy ataletewa barua ya kuitwa mahakamani aliingia ndani kwa Muddy bila kuonekana na kwenda kukaa sebuleni kusubiri kitakacho tokea. Baada ya barua kuletwa na kukabidhiwa Muddy, alijua nini kitafuata. Baada ya kuisoma na kuonekana amechananyikiwa alitumia muda ule kuficha kila kitu ambacho angetumia kwa ajili ya kujitoa uhai. Hata alipokwenda dukani aliyemuuzia sumu ya panya, Balkis alijigeuza na kumuuzia kitu kingine kisicho na madhara yoyote.

Kwa vile alikuwa amechanganyikiwa hakuichumza aliiweka kwenye glasi na kuichanganya na kuinywa kisha aliinywa. Lakini Balkis alikuwa amemuwekea dawa za usingizi ambazo zilimlevya baada ya kunywa na kulala usingizi mzito. Baada ya kumuona amelala, ndipo alimpomwacha na kwenda kwa Ashura mke wa Muddy.
******
Siku ya pili Muddy alifika mahakama kama ilivyopangwa, baada ya kesi kusikilizwa iliahilishwa wiki moja. Muddy alishangaa kutomuona Balkis mahakamani, baada ya kutoka mahakamani aliamua kwenda nyumbani kwao Balkis ili akajue nini kimemsibu baada ya kukosekana asubuhi ile kama alivyomuahidi kufika. Aliendesha gari lake ambalo kutokana na maelezo ya Balkis kuwa litapigwa mnada pamoja na nyumba na kugawana fedha zake, ambazo nazo zitachukuliwa na mtalaka wake na kumuacha bila kitu.

Njia nzima alikuwa na mawazo juu ya hatima ya maisha yake kama atanyang’nywa kila kitu. Alipofika maeneo ya Daraja la Salenda alitembea taratibu kuitafuta nyumba ya kina Balkis ambayo aliamini ilikuwa maeneo yale.
Lakini alijikuta akichanganyikiwa kutoliona jumba la kifahari alilopelekwa na Balkis. Mawazo yake yaliamini huenda amekosea eneo.

Kutaka kupata uhakika wa sehemu aliyopelekwa usiku na Balkis, aliendesha gari mpaka sehemu waliyotelemka na mkewe usiku. Alipofika pale alirudi taratibu huku akipepesa macho kuangalia labda ataliona jumba la kifahari. Lakini hakuona chochote zaidi ya miti na bahari kwa nyuma.

Alijikuta akijiuliza lile jumba alilolala mbona halionekani, alipanda ndani ya gari na kuanza kulitafuta kwa kuendesha gari taratibu kuelekea Masaki labda ataliona jumba lile. Aliendesha gari taratibu huku akipepesa macho labda ataliona jumba la kifahari kama lile ambao katika maisha yake hakuwahi kuona.

Lakini gari lilizidi kwenda bila kuliona, majumba mengi alioyaona yalikuwa mazuri lakini hayakuweza kufikia hata robo ya uzuri wa jumba la kina Balkis Ambalo lilikuwa na eneo kubwa tofauti na majumba yaliyokuwa yamepangana pia maeneo yake yalikuwa madogo.

Mpaka anafika Sea cliff Hotel hakuona jumba lile alilopelekwa na Balkis, aliamini kabisa atakuwa amekosea tu. Aligeuza gari na kurudi tena hadi sehemu aliyoachwa na mkewe usiku na kuonana na Balkis. Aliamua kutelemka kwenye gari na kutembea kwa miguu kufuata njia aliyopelekwa na Balkis, alikumbuka hakwenda njia ya Masaki bali alirudi kama anakwenda Daraja la Salenda.

Muddy alitembea taratibu huku akipepesa macho huenda akaliona jumba lile la kifahari, lakini mpaka anavuka Daraja la Salenda bado hakuona jumba lile.





JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.44.


Hakukata tamaa alitembea hadi Agha Khan, pia nyumba zilikuwa zile zile za siku zote alizozizoea. Baada ya kutembea kwa muda mrefu alijikuta akichoka sana na kuamua kurudi taratibu kulifuata gari lake ili arudi nyumbani. Alitembea kwa mwendo wa kivivu huku kiu na njaa ikiwa kali.

Alimwita muuza maji ambaye alimletea maji, alikunywa kidogo na mengine alijimwagia kichwani kupunguza uchovu. Lakini ilikuwa tofauti na alivyofikiria, alihisi usingizi wa ajabu na mwili kuchoka maradufu. Alitafuta mti wa kivuli uliokuwa pembeni ya bahari na kujilaza chini yake.

Usingizi mzito ulimpitia uliomfanya alale kwa muda mrefu, alishtuka saa moja usiku, giza lilianza kuimeza nuru ya mchana. Alijikuta amelala pembeni ya maji yaliyokuwa yakirudi baada kupwa kuanzia asubuhi. Alishangazwa na sehemu aliyojikuta kuwa eneo la ndani ya bahari wakati yeye alilala nje ya bahari kwenye miti ya pembezoni. Alinyanyuka na kujikung’uta kisha taratibu alielekea sehemu lilipokuwa gari lake. Wasiwasi wake mkubwa gari linaweza kuibwa au kuchukuliwa baadhi ya vitu.

Alijiuliza kama gari litaibwa ataieleza nini mahakama, lakini ilikuwa ajabu gari lilikuwa lipo katika usalama pia hakuna kitu chochote kilichopotea. Alimshukuru Mungu na kuingia kwenye gari ili arudi nyumbani, lakini kabla hajawasha gari ili aondoke alishtuka kumuona Balkis.
Balkis alitokea mbele yake na kulisogelea gari huku akichanua tabasamu pana, alipomfikia alimsemesha:
“Muddy vipi?”

“Safi.”
“Za toka jana?”
“Nzuri.”
“Mbona upo huku?”
“Mbona hukuonekana mahakamani kama ulivyoniahidi?”

“Kwa hilo naomba samahani mpenzi wangu, nilitumwa na baba asubuhi nilijua nitawahi lakini amini usiamini ndiyo narudi. Na hivi nilikuwa nimetumwa tena nashangaa kukuona hapa.”
“Balkis huwezi kuamini toka nizaliwe leo nimesulubika vibaya.”
“Kwa nini tena mpenzi wangu?”

“Baada ya kutoka mahakamani...”
“Kabla ya kuendelea hebu nielezee imekuwaje huko?”
“Kesi imehahirishwa mpaka wiki ijayo.”
“Hakuna kitakachobadilika, kila kitu wamekwishakamilisha hata hakimu wa kesi yako ameshachukua chake mapema, kinachosubiriwa ni kukumaliza tu. Lakini nakuhakikishia fedha watakazochukua zitawatokea puani.”
“Utawapeleka polisi?”

“Wakafanye nini, ila utasikia tu nini kitawatokea.”
“Alafu...”
“Nimekuelewa Muddy, kwanza samahani kwa kutotokea mahakamani, umesema umesulubika kivipi?”
“Hivi kwenu wapi?”
“Muddy, si hapo mbele.”
“Wapi?”

“Unataka kupajua au kufika, twende maana sasa hivi nipo peke yangu.”
“Sehemu gani?”
“Si hapo mbele? Unaona nyumba ile kwa nyuma.”
“Mbona jana tulikwenda huku?”
“Si ndipo tunapopitia, kwani tatizo nini?”

“Hakuna tatizo twende nikapumzike nimechoka hapa nilipo pia nina kiu na njaa kali.”
Kama kawaida Balkis aliingia kwenye gari na kuliendesha, pamoja na Muddy kukaza macho ili ajue nyumba ile ipo wapi. Gari lilienda kidogo na kukata kidogo, Muddy hakuamini kuona jumba la kifahari lile lile alilolala jana yake. Baada ya kupaki gari sehemu yake aliteremka na kumfungulia mlango Muddy kisha alimshika mkono na kumuongoza mpaka ndani.

“Karibu mpenzi wangu,” alimwambia kwa sauti ya mahaba huku akimlegezea macho na kumfanya Muddy asahau tabu zote alizokutana nazo.
Kama kawaida alipelekwa kuoga kisha alifungwa vazi refu na kupelekwa kwenye meza iliyokuwa na vyakula tayari. Wakati akiendelea kula chakula kitamu ambacho kwake ilikuwa siku ya kwanza kukila, Balkis alimuaga kwenda kuoga. Aliondoka kwa mwendo wa madaha na kumfanya Muddy aache kula na kumsindikiza kwa macho huku akiusifia utundu wa Rabuka kumuumba binti mrembo kama yule.

Kwake aliona kama ndoto kumpata msichana mzuri kama Balkis pamoja na uzuri wake lakini umemuonesha mapenzi ya kweli kiasi cha kumsahau mkewe Ashura. Akiwa katikati ya chakula, alimuona Balkis akisogea mezani akiwa amejifunga upande wa khanga.

Kila dakika Balkis alizidi kujijaza moyoni kwa Muddy ambaye kwake aliona ngekewa kuokota dhahabu katikati ya soko la Kariakoo. Baada ya chakula kama kawaida alipelekwa kwenye chumba alicholala jana yake. Kwa raha za muda mfupi hakutamani kufa na kujilaumu kwa uamuzi wa kijinga aliotaka kuchukua.

Kama kawaida alfajiri alirudishwa kwake huku akijiuliza kwa nini baba yake arudi alfajiri tu anatoka wapi. Kitu kingine kilichomchanganya kilikuwa jumba zuri analoishi Balkis lipo sehemu gani mbona hajawahi kuliona. Wazo lake lilikuwa mchana arudi tena kulitafuta.

Lakini aliporudi alipitiwa na usingizi na kuamka jioni ya siku ile na wakati huo Balkis alikuwa amekwishafika na kumfanya siku ile aimalize nyumbani, lakini bado alitaka kutoka usiku ule kama Balkis akiondoka ambaye alikuwa halali pale na kwenda kufanya uchunguzi wake.






JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.45.


Baada ya Balkis kuondoka majira ya saa nne usiku, Muddy aliamua kurudi tena maeneo ya Daraja la Salenda kufanya uchunguzi wa jumba lile la ajabu. Aliingia kwenye gari lake na kwenda hadi sehemu aliyokutwa na Balkis. Alisimamisha gari lake na kufunga kila sehemu kwa usalama wa gari lake kisha aliteremka na kutembea taratibu kuifuata njia aliyopita na Balkis.

Kila alivyolitafuta lile jumba la kina Balkis hakuliona, alijikuta akitoka sehemu moja kwenda nyingine bila mafanikio. Saa zilimkatikia kwa kuzurula kulitafuta lile jumba ambalo aliamini kwa muono wake akiwa ndani yake kama akiwa kwa mbali angeliona kutokana na kuwa na taa kila kona ya jumba lile zilizokuwa na mwanga mkali.

Lakini kila alipotupa macho labda ataziona taa angani, kulikuwa na kiza tu kilichotawala angani. Bado hakuamini alirudi sehemu aliyoanzia zaidi ya mara kumi ili aanze upya kulitafuta jumba la kifahari la kina Balkis. Muda ulizidi kukatika, kutokana na kutembea sana kulitafuta jumba hilo alijikuta akichoka sana na kukaa chini ya mti mmoja apumzike kidogo ili arudi kwenye gari lake na kurudi nyumbani kulala kwani usiku ulikuwa mkubwa.

Alipokaa chini ya mti usingizi haukuchelewa ulimchukua, ulikuwa usingizi mtamu ajabu uliomfanya alale kama yupo kitandani. Kibaridi cha alfajiri kilimshtua kwenye usingizi mzito na kujikuta amelala pembeni ya ufukwe chini ya mnazi, sehemu ambayo ilimchanganya kidogo.

Alitembeza macho yake na kuwaona watu waliokuwa wakiteremsha samaki kwenye boti. Sehemu ile ilimchanganya sana na kujiuliza pale ni wapi? Pamoja na kuwa amejilaza chini ya mnazi bado hakuna mtu aliyekuwa na habari naye kwani kila mmoja alikuwa na hamsini zake.

Wengi walipita pembeni yake wakiwahi kununua samaki walioletwa na majahazi asubuhi ile. Akiwa bado amekaa chini akitafakari yupo wapi, kijua nacho kilianza kuchomoza kwa mbali lakini bado baridi iliendelea kumchonyota mwilini.

Alijinyanyua taratibu alipokuwa amekaa na kuanza kutembea taratibu pembeni ya bahari huku akijitahidi kuyakumbuka maeneo yale ambayo yalikuwa mageni kichwani mwake. Aliona akikaa kimya atazidi kupotea, ilibidi amuulize kijana mmoja aliyekuwa na kapu lililoonekana limejaa samaki wabichi, alionekana ni mchuuzi aliyelangua na kwenda kuwauza mitaani.

“Samahani ndugu,” Muddy alimuuliza baada ya kumkaribia.
“Bila samahani kaka yangu.”
“Kwanza ni vizuri kutanguliza salamu kuonesha uungwana, habari za asubuhi?”
“Nzuri tu.”
“Eti hapa ni wapi?”
“Kigamboni.”

“Mungu wangu, kuja huku si lazima utumie pantoni?”
“Kutoka wapi?”
“Mjini.”
“Ndiyo.”
“Sasa mimi nimefikaje bila kutumia Pantoni?”
“Kutoka wapi?”
“Mjini.”
“Kwani wewe umefikaje huku?”
“Hata najua, hii kali ya mwaka.”

“Samahani kaka, mbona kama unajishangaa kwani wewe mara ya mwisho ulikuwa wapi?”
“Njia panda ya barabara ya Ali Hasani Mwinyi na Masaki.”
“Ulikuwa ukifanya nini?”
“Mmh! Tuachane na hayo, hebu nioneshe njia ya kuelekea kivuko cha Pantoni?”
“Twende pamoja na mimi naelekea huko huko.”

Muddy aliongozana na yule kijana kuelekea kwenye kivuko cha Pantoni, njiani alijawa na mawazo jinsi alivyojikuta Kigamboni wakati yeye alikuwa maeneo ya Daraja la Salenda. Alijiuliza kuhusu gari lake atalikuta kwenye hali gani, alipofika kivukoni bahati nzuri alikuta kivuko ndiyo kinapakia abiria na magari.

Alipanda na kutulia kwenye siti huku kichwa chake kikiwa hakikubaliana na kilichotokea.
Bado alijawa na mawazo juu ya kujikuta Kigamboni bila kujielewa, kivuko kilivyofika mwisho aliteremka na kuelekea kwenye daladala za kuelekea Mwenge iliyomrudisha mpaka njia panda ya kuelekea Masaki. Alipofika alilikuta gari lake lipo katika hali ya usalama.

Aliingia ndani ya gari lake na kurudi hadi kwake, alishangaa alipofika kwake kumkuta Balkis amekaa mlangoni akilia. Alijikuta akishtuka, akateremka kwenye gari bila kufunga mlango na kumfuata alipokuwa amekaa.
“Mpenzi unalia nini?”
“Muddy hunipendi.”
“Mimi?” Muddy alishtuka kusikia vile.

“Muddy nazungumza na nani?”
“Na mimi.”
“Ulikuwa wapi?”
“Nilitoka kidogo alfajiri kuna sehemu nilikwenda mara moja.”
“Muddy unanipenda?”
“Tena sana.”
“Niambie ukweli ulikuwa wapi?”
“Kama nilivyo kueleza mpenzi,” Muddy alijua Balkis alikuja asubuhi ile.
“Nikuambie nini mpenzi zaidi ya hayo.”

“Mbona kichwani una majani na mwili na nguo zimechafuka?”
Kauli ile ilimshtua Muddy na kujikuta akijikagua upya na kujikuta kweli alikuwa amechafuka kwa mchanga wa bahari pia kichwani alikuwa na majani. Alijikuta akipatwa na kigugumizi, alijifikiria amjibu nini Balkis aliyekuwa akimtazama usoni huku machozi yakimtoka.


Etaendelea baadae Kidogo..............




 
JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.46.



"Muddy nipo hapa toka saa tano usiku baridi lote limeniishia nikijua haupo mbali, kumbe umekwenda kwa wanawake zako," Balkis alijiliza kiuongo.
"Nisamehe Ba..Ba..lkis," Muddy alijitetea baada ya kujua kuwa ameumbuka.
"Niambie ukweli ulikuwa wapi?"

"Nilikufuata kwenu."
"Kufanya nini, wakati niliondoa kwako hukuniambia kitu?"
"Nililipenda jumba lenu nilitaka kuliona kwa macho yangu nikiwa kwa nje."
"Si ungenieleza unataka kupajua kwetu ili nikupeleke kuliko kunichunguza au huniamini?"

"Nakuamini lakini basi tu, yaani nimechanganyikiwa, jumba kama lile sikuwahi kuliona hata mchana huwa silioni maeneo yale."
"Narudia tena, kwa nini usiniulize jumba letu lilipo? unaweza kulitafuta mwaka mzima na usilione."

"Naomba unisamehe kwa yote yaliyojitokeza."
"Muddy nilishakusamehe tangu siku ya kwanza nilipokuona ukipasuliwa moyo wako kwa kisu butu bila ya ganzi na mkeo wa bandia, niliamini mtupo uliotupwa haukujua ungeangukia wapi na muanguko wako ungekuwa mkubwa sana na usingesimama tena."

"Nashukuru Balkis kwa kuyaokoa maisha yangu, nisamehe kwa yote, siyo kwamba sikuamini la hasha, bali nilipenda kuuona utukufu wa utajiri wa familia yako. Bado nipo njia panda kujiuliza jumba zuri kama lile limejengwa lini maeneo yale."
"Maeneo gani?"

"Si pale pembeni ya njia panda ya kuelekea Masaki."
"Nataka nikutaadharishe kitu kimoja, yaani usije tena maeneo yale kwani baba yangu akikuona anaweza hata kukutoa uhai."
"Atanijuaje?"

"Mbona anakujua, aliponiuliza nilimdanganya, sasa kama atakuona tena maeneo yale lazima atajua namdanganya na atakufanyia kitu kibaya."
"Je, akinikuta kwenu?"
"Kwa sasa baba yupo, hivyo hutuwezi kwenda tena mpaka tutakapooana."
"Kwa hiyo utakuwa unakuja kulala hapa?"

"Ndiyo maana yake."
"Si umesema nyumba hii itapigwa bei itakuwaje?"
"Usiwe na wasiwasi kila kitu niachie mimi, ukitoka mahakamani nitakupeleka kwenye nyumba yako mpya."

"Nitashukuru mpenzi wangu."
Balkis baada ya kuingia ndani aliisikia nyumba ukinuka sana, aliogopa kusema kwa kuhofia kumuudhi mpenzi wake. Alitafuta mbinu ya kumuondoa Muddy ili afanye usafi ndani mle.

Alimtuma kitu ambacho alijua hawezi kukipata karibu, alijua nafasi ile ingempa fursa ya kuwaita wajakazi wake kufanya usafi kwa muda mfupi. Alimuomba samahani kabla ya kumtuma:
"Samahani mpenzi wangu."
"Bila samahani."

"Najua umechoka lakini naomba nikutume kitu."
"Nitume tu mpenzi wangu."
"Kwa vile nataka kufanya usafi, naomba kaninunulie udi sehal"
"Upo sehemu gani?" "Kwenye maduka wanayouza manukato utaupata."
"Hakuna tatizo wacha niwahi."

"Nioneshe ufagio."
Baada ya kumpa ufagio Muddy alitaka kuondoka na gari lakini Balkis alimkataza alijua akitembea kwa miguu atachukua muda mrefu kurudi kuliko akitumia gari.
"Unaweza kuupata karibu wala usitumie gari."
"Hakuna tatizo."

Muddy aliondoka na kumwacha Balkis akijifanya anafagia, baada ya kuondoka tu, aliacha kufagia na kujishika kwenye paji lake la uso. Haikuchukua sekunde wajakazi kumi walikuwa mbele yake wakiwa wamepiga magoti.
"Rabeka mwana wa mfalme una shida gani?" Waliuliza kwa pamoja.

"Nataka mfanye usafi wa nyumba yote, sitaki kusikia harufu mbaya kama hii."
Mara moja wajakazi walianza kusafisha nyumba nzima, ilikuwa ajabu waliondoka vitu vyote vya ndani na kuviweka vipya na vyenye thamani kwa muda mfupi, ndani pakabadilika, pakapendeza na kuvutia kila kona ya nyumba ilinukia kwa harufu nzuri.

Muddy alijikuta akitembea umbali mrefu kutafuta udi sehal, kila alipouliza watu hawakuujua. Alijikuta akikata tamaa na kuamua kurudi kumweleza Balkis kuwa udi wenye jina hilo kila alipouliza watu hawakuujua. Kutokana na kwenda umbali mrefu ilibidi wakati wa kurudi apande gari, jasho likimvuja kwa kutembea.

Alipofika nyumbani aliingia ndani lakini alishtuka kukuta nyumba yake ikiwa imebadilika na kupendeza sana, aliviona vitu tofauti kiasi cha kuamini kuwa alikuwa amekosea, hakukuwa kwake. Alitoka nje ili akaitafute nyumba yake lakini mlangoni alikutana na Balkis akiwa amebeba siagi na jam.

"Vipi mpenzi mbona nimekuona umeingia na unatoka?"
"Ha! Hapa ni kwangu?" Alishtuka.
"Eeh! Kwako, kwani vipi?"
"Umefanya usafi mkubwa hivi kwa muda gani?""Usinione nipo hivi mimi ni mwanamke wa shoka."

"Na mbona kuna vitu vipya?"
"Sasa kipi cha ajabu, yote haya nimeyapanga kwa muda mrefu, nilipokuwa nakuja kulala hapa. Nilimtuma mtu avilete vitu hivi, wakati unaondoka vilikuwa vinaingia."
"Sasa nyumba ikiuzwa?"

"Achana na wazo hilo hebu nenda kaoge ufungue kinywa."
Muddy hakujibu kitu alichukua taulo na kwenda kuoga, nyumba ilikuwa ikinukia kama ujinini kwa akina Balkis. Muddy alipotoka kuoga alikuta chai imeshatayarishwa juu ya meza, ilikuwa tamu ambayo Muddy aliwahi kuinywa nyumbani kwa akina Balkis tu.

Pamoja na kuisifia chai lakini Muddy kila alipomuangalia Balkis moyo wake haukuamini kama alikuwa na mwanamke mzuri kama yule tena tajiri mwenye mapenzi ya dhati kwake.







JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.47.


"Muddy nihakikishie kuwa huwezi kurudiana na Ashura?"
"Nakuhakikishia kukupenda siku zote na kamwe sitarudiana na yule mwanamke muuaji." "Muddy unayosema yanatoka moyoni au mdomoni?"
"Yanatoka moyoni mwangu?"
"Ukinigeuka?"
"Nifanye lolote."

"Muddy kama unayosema ni kweli basi kitu nilichotaka kukifanya naachana nacho."
"Kipi hicho?"
"Nilitaka kusimamia kesi yako kuhakikisha hawachukui kitu chochote."
"Kwa nini usifanye hivyo?"
"Naacha ili maisha yako yakiwa mazuri mtu yeyote asikuguse."
"Kwa hiyo nitakuwa na maisha mazuri zaidi ya haya?" Muddy aliuliza.
"Mara kumi ya haya."

"Usiniambie!"
"Kwangu fedha si tatizo, ninachokitaka kutoka kwako ni mapenzi ya kweli, sihitaji kitu kingine."
"Nakuahidi utayapata hapa."
"Basi tegemea kuishi maisha ya raha mpaka kufa kwako."
"Asante mpenzi wangu," Muddy alisema huku akimkumbatia Balkis.
***
Muda ulipofika Muddy aliitwa mahakamani na hukumu ilikuwa ile ile ya kugawana mali. Kwa vile alishaelezwa na Balkis maisha yake baada ya hukumu, hakuchanganyikiwa baada ya kuelezwa yale. Baada ya hukumu ile, Muddy pia alitakiwa kumlipa fidia ya fedha ambayo ilimfanya asipate kitu katika mali zitakazouzwa, vikiwemo gari na nyumba.

Ashura alishangaa kumuona Muddy pamoja na pigo zito yupo katika hali ya kawaida. Baada ya hukumu Muddy alitoka nje ya mahakama na kwenda moja kwa moja kwa Balkis aliyekuwa akimsubiri. Muddy alishtuka kumuona Balkis akiwa pembeni ya gari la kifahari.
"Karibu mpenzi."
"Asante."
"Pole na masaibu yote."
"Asante," walikumbatiana, kitendo kile hakuna aliyekiona zaidi ya Muddy peke yake.
"Nina imani mambo yamekwenda kama nilivyokueleza?"
"Yaani umekuwa kama wewe ndiye uliyeyapanga yote, hakuna hata kimoja kilichokwenda kinyume."

"Basi huyo ndiye Ashura ambaye pia hilo si jina lake halisi."
"Una maana gani kusema hivyo?"
"Nitakueleza, kila mwanaume aliyemchezea mchezo huu anamjua kwa jina hili lakini jina halisi anaitwa Shuuna."
"Ina maana hata hayo majina aliyotumia kwa hao mabwana wa awali unayajua?"
"Nayajua."
"Alikuwa anaitwa nani?"
"Twende kwanza nyumbani ukapumzike, mengine tutazungumza tukifika."
Muddy aliingia kwenye gari na kuondoka, kabla ya kuingia kwenye gari Ashura alishtuka kumuona Muddy na mwanamke mrembo aliyejitambulisha kuwa ndiye mkewe siku aliyokwenda kwake kumuonya.

Alijikuta akikosa raha na kujiona wamefanya kazi bure sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Waliona kama hawakufanya kitu na kujikuta akimuuliza mwanaume wake.
"Yule mwanamke mwenye fedha Muddy kamtoa wapi?" Ashura aliuliza.

"Hata mimi nashangaa, ni wazi wameanza uhusiano kipindi mkiwa wote."
"Ndiyo maana hata ilipotolewa hukumu hakushtuka."
"Hata mimi nilishangaa kuona anakubali kila kitu."
"Kwa hiyo tutakuwa tumefeli?"
"Hapana, hatujafeli kwani tulivyovitaka tumevipata, ila kuna biashara nyingine nzuri," mwanaume wa Ashura alisema.

"Biashara gani?"
"Tukafungue mashitaka ya kudai kuhujumiwa penzi lako lililosababisha muachane na mumeo wakati bado unampenda."
"Aisee, wazo zuri sana! Kweli wewe bwana mipango, sasa mpango huo tuufanye lini?"

"Kwanza tupajue wanapoishi ili tufanye mpango wa kufungua mashitaka."
"Hilo wazo, mbona mwaka huu tutatengeneza fedha mpaka zitukimbie."
"Hiyo ndiyo kazi yetu."
"Lakini Mussa kuna jambo nimekumbuka."
"Jambo gani hilo?"

"Unakumbuka yule mwanamke alivyotuonya kuhusu tabia yetu kuwa itatutokea puani?"
"Sasa wewe unamuogopa, atatufanya nini mwanamke yule?"
"Mmh! Nashangaa moyo unanienda mbio nilipomkumbuka."
"Si kwa vile amekuchukulia mumeo."

"Yule si mume wangu nilikuwa naye kibiashara zaidi."
"Basi mpango wa haraka ni kudili na Muddy kuhakikisha anaokota makopo."






JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.48.



Wakati wakipanga kuchukua fedha za Balkis, muda huo Muddy alikuwa akikaribishwa kwenye jumba la kifahari.
"Karibu mpenzi wangu hapa ndipo kwako ishi kwa furaha na mapenzi ya kweli," Balkis alimkaribisha kwa sauti tamu.
"Ha! Siamini."

"Hata lile gari ni lako."
"Usiniambie!" Muddy alizidi kupigwa na butwaa.
"Ukweli ni huo, leo usiku kutakuwa na sherehe fupi ya kufunga ndoa yetu ili uweze kunitumia kihalali kama mkeo."

"Hakuna tatizo, asante sana mpenzi."
Muddy alishukuru kwa kupiga magoti huku machozi yakimtoka na kujiuliza bila ya Balkis maisha yake yangekuwaje baada ya kufanyiwa utapeli na Ashura.

****
Ashura na mwanaume wake baada ya kutoka mahakamani waliongozana na madalali kwenda kuuza mali za Muddy zikiwemo gari na nyumba siku ile ile, kutokana na mipango iliyopangwa mapema. Baada ya kufanikiwa kuuza gari na nyumba waliendelea kufurahia mafanikio yao kufuatia kazi yao ya utapeli na kujipanga kwa ajili ya kupambana na Balkis kuhakikisha wanapata fedha kupitia kwa Muddy.

Pamoja na kupata vitu walivyovitaka kutoka kwa Muddy, bado Ashura moyo wake ulikosa raha, alijiuliza atamtazamaje Muddy siku wakikutana kutokana kuonekana ameingia kwenye maisha mazuri tofauti na awali walipokuwa pamoja.

Baada ya kumuacha Muddy na kuonesha kuchanganyikiwa, alitegemea kusikia amejinyonga. Kufuatia kupona kifo hicho, Ashura alitegemea siku ya hukumu angemuona Muddy akitoka mahakamani na kuanza kuokota makopo, lakini ilikuwa ni kinyume na mategemeo yake.

Wasiwasi wake Muddy lazima angelipa kisasi, wazo lake lilikuwa kumuwahi kabla hajawahiwa yeye. Akiwa amekaa na mwanaume wake, Ashura alimueleza jambo:
"Mussa nina jambo linaniumiza akilini mwangu."
"Lipi tena mpenzi?"

"Nina wasiwasi na Muddy kutulipizia kisasi."
"Ni kweli hata mimi nilikuwa na wazo hilo."
"Sasa tufanye nini kabla hajafanya lolote, maana akitulia atajipanga na yule dada anaonekana ana fedha hivyo anaweza kutufanyia kitu kibaya."
"Ondoa hofu hawawezi kutufanya lolote zaidi ya sisi kuwamaliza wao."
"Hayo ndiyo maneno." Ashura alipata faraja.
***
Wakati Ashura na Musa wakipanga mipango yao, usiku wa siku ile ufukweni mwa Bahari ya Hindi maeneo ya Daraja la Salenda kulikuwa na sherehe kubwa ya harusi kati ya Balkis na Muddy. Katika kundi la watu wote waliokuwepo kwenye sherehe ile Muddy peke yake ndiye aliyekuwa mwanadamu, lakini waliobakia walikuwa majini.

Lakini hakuwajua kwa vile walikuwa katika maumbile ya kibinadamu, Muddy alimuoa rasmi Balkis na kuwa mkewe wa halali. Ilikuwa sherehe kubwa kuwahi kutokea katika maisha ya Muddy. Baada ya harusi walilala kwenye kitanda cha bembea kilichowabembeleza mpaka kunakucha.

*****
Taarifa ya ndoa ya Balkis ilifika chini ya bahari kwa Mfalme Barami Hudirud, kitendo kile kwake alikiona kama ni dharau kutoka kwa mwanaye kufunga ndoa na mwanadamu. Alimfuata mkewe aliyekuwa amekaa kwenye bustani akibembea kwenye kiti.

"Mama Balkis," alimwita kwa sauti ya juu iliyomshtua.
"Mtukufu Mfalme wa chini ya bahari, mbona sauti kali, kuna usalama?"
"Mwanao ananitafuta nini?"

"Kwani kafanya nini tena mtukufu mfalme?"?"Tunamkataza nini na anafanya nini?"
"Amefanya nini?"
"Anaweza kuvunja amri yangu?" Mfalme Barami alisema huku akipiga ngumi kifuani kwa hasira.

"Mume wangu, lakini si bado anaendelea kuleta vizazi vya wanawake?"
"Kwa nini ameolewa na mwanadamu?"
"Ha! Ndiyo kafanya hivyo!" Malkia Huleiya alishtuka.
"Eeh! Tena nasikia watwana na vijakazi walikuwepo kwenye harusi hiyo."
"Usiniambie!"

"Kwa jinsi alivyovunja amri yangu, wote waliohudhuria harusi ile watakutana na adhabu kali," alisema kwa hasira mpaka povu likamtoka mdomoni.
"Mume wangu usimguse mtu yeyote ni wewe uliyempa amri mwanao kwa watwana na vijakazi juu ya kuheshimu amri zake."

"Basi kama sivyo hivyo nitamtuma mtwana mkuu Muhuru akammalize huyo mwanaume."
"Bado hujatumia busara, kumbuka kosa lako lolote litatugharimu, kitendo cha kukataa kumuondoa mwanaume wa kwanza huku kilizua patashika na ulipotaka kumuua ulisikia alichosema mwanao. Hivi umuue huyu aliyefunga naye ndoa itakuwaje?"

"Sasa kuna haja gani kuendelea kuleta vizazi vya wanawake wakati ameishajiamulia kuolewa na mwanadamu?"







JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.48...B

ILIPOISHIA:
"Bado hujatumia busara, kumbuka kosa lako lolote litatugharimu. Kitendo cha kutaka kumuondoa mwanaume wa kwanza huku kukiwa na patashika ulipotaka kumuua ulisikia alichosema mwanao. Hivi umuue huyu aliyefunga naye ndoa itakuwaje?"
"Sasa kuna haja gani kuendelea kuleta vizazi vya wanawake wakati ameshajiamulia kuolewa na binadamu?"
SASA ENDELEA...

"Labda ana sababu zake, ngoja akija tumuulize."
"Hakuna cha kumsubiri, tumtume Muhuru aende akamwite mara moja."
"Siamini, kama jana kafunga ndoa leo aje huku, hebu kuwa na subira mume wangu."
Walikubaliana kumsubiri ili aje awaeleze kwa nini amevunja amri ya mfalme wa bahari, tena akiwa binti wa mfalme.

BAADA YA MIEZI MIWILI
Maisha ya Muddy yalibadilika ghafla, kila aliyemuona alimshangaa. Mmoja kati ya watu waliomshangaa alikuwa ni Ashura aliyemuona akitoka super market akiwa ameongozana na Balkis katika mwonekano wa mahaba mazito. Roho ilimuuma na kujikuta akipata wivu wa kutaka kuwa na Muddy.
Aliamini kuwa kilio cha Muddy alichokitoa siku alipomuacha, kama angemuomba warudiane angeweza kukubali. Alipanga kumtafuta na kumuomba msamaha.

Ashura aliamua kumtafuta Muddy kwa udi na uvumba kila kona ya mji. Lakini alishangaa kila alipomuona Muddy na kumfuata alipomkaribia Balkis alitokea bila kujua ametokea wapi, kitu ambacho kilimkosesha amani ya moyo wake. Hata alipojaribu kumfuatilia kwa nyuma alimpotea kimiujiza. Aliamini njia rahisi ya kumrudisha mikononi mwake ni kwenda kwa mtaalam wake aliyekuwa anakaa Mbagala Kimbangulile, Mzee Chujio.

Aliwasha gari na kuelekea Mbagala kwa mtaalam ili akamvute tena Muddy kama alivyofanya mwanzo na kupelekea kuisahau familia yake. Alipofika Mtoni kwa Azizi Ali dada mmoja aliomba msaada kwenye gari lake. Hakutaka kumnyima lifti, alimsaidia.

"Unafika wapi dada yangu?" alimuuliza baada ya kuingia kwenye gari na kufunga mlango.
"Mbagala Zakheem," alijibu yule dada kwa sauti ya chini.
"Ooh! Mimi nafika mbele, nitakushusha kituoni."
"Nitashukuru."

Wakati safari ikiendelea mwanamke aliyeomba msaada alianzisha mazungumzo.
"Dada yangu huku ni mwenyeji?"
"Hapana nakwenda kumuona mtu mmoja Mbagala mwisho."
"Nani mganga Chujio?"
"Mmh!" Ashura alishtuka.

"Mbona umeshtuka?"
"Walaa, siendi huko."

"Lakini dada shida ya nini kumuendea Muddy kwa mganga wakati mmekwisha achana?" Kauli ile ilimshtua sana Ashura.
"Nani amekwambia mimi nakwenda kwa mganga, pia habari za Muddy nani kakueleza?"
Ashura alishtuka kujiona yupo uchi japo amevaa nguo, alijuta kumpa lifti yule mwanamke ambaye aliharibu safari yake yote.

"Ashura," mwanamke aliyepewa lifti kwenye gari alimwita jina lake.
"Ha! Umejuaje jina langu?" Ashura alizidi kumshangaa mtu aliyempa lifti kwa kumjua kwa mapana.

"Nijue unataka kufanya nini nitashindwa kujua jina lako? kwanza jina lako si Ashura."
"Kama siitwi Ashura naitwa nani?"
"Shuuna."

"Mungu wangu! Umenijuaje?"
Ashura nusura aliingize gari kwenye mtaro kwa mshtuko, ilibidi alisimamishe pembeni maeneo ya Mbagala Misheni.

"Kwani kuna siri, la muhimu achana na Muddy endelea na maisha yako, pia mpango wenu wa kumfuatilia Muddy na mkewe mtaokota makopo ninyi kabla ya huyo Muddy."
"Wewe ni nani?" Ashura alimuuliza huku jasho likimtoka.
"Mke wa Muddy," sauti ilijibu pembeni.

"Muongo...Ha!" Ashura alijibu huku akigeuka kumtazama aliyejiita mke wa Muddy, wakati huo manukato makali yalinukia ndani ya gari. Hakuamini kumuona mtu aliyempa lifti amebadilika na kuwa mke wa Muddy, Balkis.

"Punguza hofu, sipo hapa kwa shari bali kukuonya kwa kitu unachotaka kukifanya, kumbuka nilikuuliza mapema kuhusu kurudiana naye nawe ulinihakikishia hutarudiana naye tena.

"Sasa sikiliza Ashura, huenda utashangaa kuniona hapa. Sitaki kujieleza sana, ila ukitaka vita na mimi ambavyo najua hutaweza kushinda endelea na mambo yako. Nitakufanya kitu kibaya ambacho kitabakia katika kumbukumbu zako mpaka unafukiwa chini.

"Mwambie na mpumbavu mwenzako mpango unaopanga wa kutaka kuichukua mali yangu mtakufa kifo kibaya. Leo sikuja kwa shari nimekuja kistaarabu. Mara ya pili utashangaa na hutaamini kuwa ni mimi," Balkis alisema kwa sauti kali kidogo iliyomtisha Ashura.






JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.49


ILIPOISHIA:
"Sasa sikiliza Ashura huenda utashangaa kuniona hapa, sitaki kujieleza sana ila ukitaka vita na mimi najua huwezi, nitakufanyia kitu kibaya ambacho kitabakia katika kumbukumbu yako mpaka unafukiwa chini.

"Mwambie na mpumbavu mwenzako kwamba mpango mnaoupanga wa kutaka kuzichukua mali zangu mtakufa kifo kibaya. Leo sikuja kwa shari bali kwa ustaarabu, mara ya pili utanishangaa, hutaamini kuwa ni mimi," Balkis alisema kwa sauti kali kidogo iliyomtisha Ashura. SASA ENDELEA...

Baada ya kusema maneno yale, Balkis aliufungua mlango wa gari na kutoka nje huku akifyonya kwa sauti kali, alipolizunguka gari akatoweka.
Baada ya kuondoka eneo lile, Ashura alishtuka kama mtu aliyetoka usingizini na kujiuliza alichokiona na kukisikia kama kilikuwa ni cha kweli au alikuwa akiota.

Wazo lililomjia haraka aliamini kabisa kuwa ile ilikuwa ni ndoto, aliamua kwenda kwa mganga kupata tiba ya kumrudisha Muddy mikononi mwake.
Alijishangaa mwanaume aliyemgeuza mradi amekuwa kero moyoni mwake kila dakika alijikuta akimpenda na kumtamani kuwa naye tena.

Aliendesha gari huku akiapa kutompa msaada kiumbe yeyote kwa kuhofia kukutana na matatizo ambayo bado aliamini kuwa ni ndoto.
Hakuamini kama mtu angeweza kugeuka mara mbili katika hali ya kawaida, kwake alijua ile ilikuwa ni ndoto mbaya tu.

Alipofika Mbagala Rangi Tatu alikata kushoto na kuelekea Kimbangulile, alipofika kwa mganga alishangaa kukuta watu wakiwa wamejaa kuonesha kulikuwa na jambo.

Alisimamisha gari mbali kidogo na nyumba ya mganga na kuteremka kisha akajisogeza kwenye kundi la watu ambapo kila mmoja alikuwa akisema lake. Alimsikia mmoja akisema;
"Lazima yule atakuwa ni jambazi aliyefanyiwa kitu kibaya na mganga."
"Hapana mbona hakutoka mle ndani yule lazima atakuwa ni jini tu."

Yalikuwa naneno yaliyomchanganya Ashura na kujiuliza mganga amefanya nini, ilibidi amwite pembeni dada mmoja ili apate kumhoji vizuri.
"Samahani dada yangu kuna nini?"
"Mmh! Kuna jambo limetokea linawachanganya watu wengi."
"Jambo gani?"

"Mzee Chujio ameuawa."
"Mzee Chujio gani?"
"Yule mganga."
"Mganga?" Ashura aliuliza kwa mshtuko.
"Eeh, unamfahamu?"

"Sasa dada yangu nani asiyemjua mzee Chujio sehemu hii?"
"Basi ndiyo hivyo, ameuawa katika mazingira ya kutatanisha."
"Una maana gani?"

"Nasikia kuna dada mmoja mrembo alikuja na kuingia ndani kwa mganga na kuwaacha wateja wachache wakiwa kwenye foleni. Lakini inasemekana hakutoka, baada ya wateja kusubiri kwa muda bila kusikia wakiitwa ndani waliamua kuingia lakini cha ajabu wakamkuta mganga amelala chini akiwa amekufa na kutoka funza mdomoni kama aliyefariki wiki moja iliyopita."

"Funza mdomoni?"
"Ndiyo."
"Sasa jamani mtu wa kutoka funza si mtu aliyekufa zaidi ya wiki?" Ashura alisema kwa mshtuko.
"Hapo ndipo watu walipochanganyikiwa na kuamini kuwa yule mwanamke mzuri alikuwa ni jini."

"Jini! mna maana gani?"
"Wanasema alikuwa mzuri sana, tena alikuwa akinukia na alipoingia ndani hakutoka."
"Alivaa nguo gani?"
"Mmh! Hebu muulize yule dada aliyesimama katikati ya watu," alimuonesha dada mmoja aliyekuwa akizungumza na watu huku akilia na kuweka mikono kichwani.
"Naomba uniitie."

Yule binti alimfuata yule dada aliyekuwa akizungumza huku akitokwa na machozi, baada ya kusogea karibu ya Ashura, ilibidi ajitambulishe kuwa ni mmoja wa wateja wa mzee Chujio mtu aliyemtegemea kwenye mambo yake.
"Samahani mdogo wangu hata mimi nilikuwa nimekuja kwa mzee Chujio lakini kuna habari zimenichanganya sana. Nini kimemsibu mganga wetu?"

"Dada yangu hata kuzungumza nashindwa, siku tano zilizopita mzee Chujio alinisaidia matatizo yaliyonitesa kwa miaka kumi. Dawa alizonipa zilinionesha yote aliyonieleza, dada yangu walimwengu ni wabaya, niliteswa na mke mwenza na kufikia hatua ya kunuka mwili mzima hata kukaa mbele za watu nilikuwa siwezi.

"Nilitengwa na watu, wanaume walinipenda kwa kuniona, lakini waliponisogelea walikuwa wakikimbia kutokana na harufu kali kama ya mzoga uliooza. Leo dada yangu nilikuwa nafuata dawa na kupatiwa kinga baada ya awali kuondolewa tatizo langu.

"Ajabu wakati nasubiri kuingia kwa mganga alipita dada mmoja mrembo na kuingia ndani bila kufuata foleni. Kwa vile ilikuwa ni zamu yangu nilitaka kumfuata ndani kumtoa kwani hakuonesha ustaarabu, lakini wenzangu walinisihi nikamuacha amalize shida yake ndipo nami niingie.
"Baada ya muda kidogo tulisikia watu wakibishana, kauli ya mganga ilikuwa ya juu akionesha kuna kitu hakukubaliana na yule mwanamke mrembo mwenye kunukia manukato.

"Mganga alisema hawezi kufundishwa kazi na mtu, mara tulisikia sauti ya yule mwanamke mrembo akisema kuwa hana jinsi ile ndiyo zawadi yake.
"Baada ya hapo kilipita kimya kirefu huku muda ukizidi kuyoyoma.

"Baada ya nusu saa bila kusikia mazungumzo wala yule mwanamke mrembo kutoka, niliamua kuingia ndani kujua kilichokuwa kikiendelea.
"Nilipoingia nikamkuta mganga akiwa amelala chini, kilichonishtua zaidi ni funza waliokuwa wakimtoka mdomoni kama mtu aliyekufa muda mrefu."





JIINI LA DARAJA LA SALENDA........EP.50



"Funza?" Ashura aliuliza tena japo taarifa ya kutoka funza alielezwa mapema.
"Funza dada, kama mtu aliyekufa muda mrefu."

"Unataka kuniambia kabla ya kutokea tukio lile ulionana naye?"
"Tena alitoka nje na mgonjwa aliyekwenda kumfanyia tiba nyuma ya nyumba yake, aliponiona alitaka kujua hali yangu, nilimweleza ninavyoendelea na kuniambia vitu vyote alivyovitafuta kwa ajili ya kazi yangu vimepatikana...Yaani..," Kufikia pale yule dada aliangua kilio mikono kichwani, Ashura aliingia kwenye kazi ya kumbembeleza.

"Mdogo wangu hebu nyamaza kwanza."
"Dada inauma, haiwezekani niwe miye, nimeteseka muda mrefu, napata tiba mganga anauawa katika mazingira ya utata," aliendelea kulia kilio cha kukata tamaa. Ashura, japo alijitahidi kujikaza na kumbembeleza kwa kumlalia kifuani, lakini moyoni alikuwa na maumivu makali kama angepata sehemu iliyojificha, basi naye angeangua kilio ambacho hakuna mtu ambaye angeweza kumbembeleza.

Kifo cha mzee Chujio kilikuwa pigo kubwa maishani mwake, ndiye aliyekuwa tegemeo lake katika mambo yote aliyoyafanya ya kuwatapeli wanaume kwa kuwapumbaza kwa dawa. Alijiuliza nani atakayemsaidia katika maisha yake baada ya kifo cha mzee Chujio ambaye alimgeuza kama Mungu wa pili.

"Unasema ulimuona?" Ashura kwa kuchanganyikiwa alijikuta akiuliza swali alilojibiwa awali.
"Ndiyo."
"Unasema alipoingia ndani hakutoka?"
"Ndiyo."
"Au wakati anatoka huyo mwanamke ulikuwa umesinzia?"
"Dada yangu kusinzia tusinzie wote tulio
kuwa tunasuburi huduma?"
"Alivaa nguo gani?"
"Gauni refu jekundu lenye maua shingoni na kifuani, sielewi maua yale ya rangi gani kutokana na kumeremeta."
"Mmh! Shingoni alikuwa na mkufu wenye herufi M?"
"Eeeh."
"Mtandio wake wa bluu yenye maua ya kumetameta?"
"Huo huo!"
"Ana kipini cha mkufu?"

"Eeeh dada, umemjuaje?"
"Mmh! Kazi ipo," Ashura aliguna na kusema kwa sauti ya chini.
"Kwani unamfahamu?"
"Kuna mtu nilikutana naye njiani uliponielezea alivyovaa nilikisia basi lazima atakuwa yeye."
"Kwa hiyo si jini kama watu wanavyomdhania?"

"Mmh! Sijajua, kwani hakuna mlango wa kutokea nyuma?"
"Dada kama wewe ni mteja wa mzee Chujio, chumba chake unakijua, mlango utoke wapi?"
"Mna uhakika hakutoka?"
"Angetoka tungemuona kama si mimi basi wenzangu wangemuona."
"Mmh! Nina wasiwasi alitoka hamkumuona."


"Sawa alitoka, kile kifo nacho cha muda mfupi mtu aoze na kutoka funza kwa sekunde chache kinatokana na nini?"
"Inawezekana alimnywesha sumu kali iliyomuozesha tumboni na kuzalisha funza."
"Mmh! Labda."

"Basi dada, acha nirudi zangu hata mimi nimechanganyikiwa sana."
"Sawa dada, lakini mimi ndiye nimechanganyikiwa hata kuliko familia yake."
Wakati huo polisi walifika kuchukua mwili wa marehemu, alishuhudia mwili wa mzee Chujio ukitolewa huku familia yake na wateja wakiangua vilio.

Ashura alishindwa kujizuia, alikimbilia kwenye gari lake na kujifungia, alilia hadi macho yakamvimba. Alijiuliza yule mwanamke atakuwa nani, japo ilikuwa vigumu kukubali kuwa Balkis ni jini, lakini mambo yaliyomtokea kwenye gari alipombadilikia kama kinyonga yalimfanya aanze kuamini kabisa mke wa Muddy ni jini.

"Mungu wangu Muddy atakuwa ameoa jini?" Alijikuta akipayuka kwa sauti.
"Haiwezikani lazima nifanye chini juu nimtoe kwenye balaa lile."
Ashura alijiingiza kwenye vita nyingine ya kujua hatima ya Muddy kwa Balkis kwa kuamini kuna njia ya kuyafukuza majini. Aliwasha gari lake na kurudi nyumbani.
*duh!!tamuje??







Etaendelea leo jioni.................
 
jamaaani !!!! yangu tangu mroning nasomaga tuu hii hadithi! MziziMkavu ..............lohivi Risasi ni la shigongo?
 
Last edited by a moderator:
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom