Jimmy David Ngonya afariki dunia

jim.JPG
Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba na mfanyakazi wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC), Jimmy David Ngonya amefariki asubuhi hii. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi~AMEN na pia awape nguvu na faraja mkewe, watoto na wajukuu wake, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu kwao. Tully, Ikupa na wengineo poleni sana kwa msiba mkubwa uliowafika.
muda wa kuaga ! Any update
 
Ngonya nguzo imara iliyoanguka

Monday, 01 August 2011 11:49


Sweetbert Lukonge
Mwananchi

WAPENZI na mashabiki wa soka wa klabu ya Simba ikiwa ni pamoja na wachezaji hususani wale wa miaka ya 70 na 80 wataendelea kumkumbuka Jimmy David Ngonya ambaye alifariki dunia hivi karibuni na kuzikwa nyumbani kwao Lutengano wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Ngonya alikuwa ni miongoni mwa viongozi waliowahi kuingoza timu ya Simba kwa mafanikio makubwa akiwa katibu mkuu wa klabu hiyo.

Jambo kubwa ambalo litakumbukwa ni uwezo wake mkubwa wa kiutendaji aliokuwa nao ulikokuwa chachu ya mafanikio na mapinduzi makubwa ya maendeleo ya soka katika klabu ya Simba.

Kwa mujibu wa baadhi ya wachezaji wa zamani ambao walikuwa wacheza soka wakati Ngonya akiwa katibu mkuu wanasema kiongozi huyo ndiye aliyeleta mapinduzi makubwa ya soka klabuni hapo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kiutendaji uliokuwa ukizingatia taratibu na maadili yote ya kiutawala bila ya ubaguzi.

Moja kati ya mambo ambayo yataendelea kukumbwa na wapenzi na mashabiki wa Simba ni Ngonya kuanzisha sera ya kutumia wachezaji chipukizi jambo ambalo lilisabisha klabu hiyo kuwa na timu imara ya vijana katika miaka ya 70 na 80 ambayo ilikuwa ni chimbuko la vipaji vingi vya soka hapa nchini.

Ayubu Chamshama, Mwenyekiti wa zamani wa Simba ambaye katibu wake alikuwa ni marehemu Ngonya anasema kifo cha mpiganaji huyo ni pengo kubwa katika maendelo ya soka nchini

"Kwa hakika tutamkumbuka kwa maengi mazuri aliyofanya enzi za uhai wake hususani wakati nikifanya naye kazi akiwa kama katibu wangu katika klabu ya Simba.

"Wakati huo mambo yalikuwa siyo kama hivi sasa, lakini alijitahidi kadri ya uwezo wake katika kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa mafanikio makubwa bila ya kuogopa mtu yoyote.

"Alifafanya mapinduzi makubwa ikiwa ni pamoja na kuwatafutia wachezaji wachezaji wa Simba kazi katika mashirika mbalimbali kwa sababu wakati huo soka ilikuwa siyo mchezo wa kulipwa kama ilivyo hivi sasa hivyo tutamkumbuka kwa mengi mazuri aliyofanya," anasema Chamshama.

Kipa wa zamani wa Simba, Moses Mkandawile ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kucheza soka enzi za Ngonya alipokuwa katibu mkuu wa klabu hiyo yeye anasema Ngonya alikuwa ni mmoja kati ya watendaji waliokuwa na msimamo na aliyekuwa akiheshimu maadili na mipaka ya kiutendaji na kuwaunganisha vema mashabiki na wanachama wa Simba.

Anasema Ngonya alikuwa mchapakazi wa kweli na pia ni miongoni mwa watu ambao walipigana kwa nguvu zao zote katika kuhakikisha Simba inapata mafanikio makubwa bila ya kujali vitisho na chokochoko kutoka kwa mashabiki na wanachama.

"Alijitahidi kwa uwezo wake wote kuhakikisha anasimamia kile alichoamini kuwa kina faida kwa timu jambo ambalo hivi sasa hakuna tena kiongozi katika klabu ya Simba atakayemfikia Ngonya kwa utendaji,"anasema Mkandawile.

Anasema,"Nitamkumbuka kwa jitahada zake za kuinusuru Simba kushuka daraja katika miaka ya 80 ambapo alitujenga kisaikolojia wachezaji wote na mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Yanga tukaweza kushinda,"anasema Mkandawile.

Naye mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Yanga, Imani Madega anasema wapenzi wa soka nchini wamepoteza kiongozi ambaye alikuwa ni mfano wa kuigwa katika maendeleo ya soka nchini.

"Kuna mambo mengi makubwa aliyofanya alipokuwa katibu mkuu wa Simba ambayo kwa hakika tutazidi kumkumbuka, lakini kubwa zaidi ni msimamo thabiti aliokuwa nao marehemu Ngonya ulioisadia klabu ya Simba kwa kipindi chake chote alichoitumikia kama katibu mkuu," anasema Madega.

Ngonya alizaliwa mwaka 1942 katika kijiji cha Lutengano wilayani Rungwe mkoani Mbeya na alifariki dunia Julai 23 mwaka huu wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Ngonya alijiunga na Shirika la Bima la Taifa mwaka 1968 akiwa karani wa Idara ya Establishment, mwaka 1970 alipandishwa chezo na kuwa Assistant Superintendent, mwaka 1972 alichaguliwa kuwa mwalimu wa mafunzo ya Bima kabla ya mwaka 1975 hajapandishwa na cheo na kuwa meneja mipango na maendeleo ya wafanyakazi.

Mwaka 1989 Ngonya alihamishiwa Singida kuwa meneja wa Bima tawi la Singida na mwaka 1991 alirudishwa Dar es Salaam kuwa meneja meneja miradi katika Idara ya Mafunzo, ambapo mwaka 1993 alihamishiwa Chuo cha Bima kama Project meneja hadi alipoacha kazi kwa hiari yake ili aweze kufanya shughuli za Bima kama wakala na baadaye kama Dalali (Insurance Broker).


 
Back
Top Bottom