Kwa kuelewa hulka za binadamu bila kujali itikadi zao na mitazamo yao kutegemea wapinzani kuwa wakombozi wa Tanzania kwa vile tu ni Watanzania wanaotoka Chadema, TLP, CUF, NCCR, au vyama vingine ni mategemeo ambayo yatapeperuka kama unyasi upeperushwavyo na upepo, ni kama umande unavyopukutika kwenye majani asubuhi inapofika! Manabii wa upinzani wako wapi watutabirie?
Hoja hujibiwa kwa hoja!
Lunyungu:
Wapinzani wanataka tuwaamini, wanataka tuwape madaraka! Ina maana hadi hivi sasa wamejiamini kiasi cha kutosha na wameamini wameimarika kiasi cha kutosha hadi wamefikia kumsimamisha mgombea Urais. Walishindwa. Kwa wao, kufikia mahali kusimamisha wagombea Urais, Wabunge na wawakilishi kibao ina maana wako tayari kuongoza na kutawala, ama sivyo?
Je kama wapinzani wangeshinda uchaguzi 2005 na kuchukua Ikulu, na Bunge je ni mabadiliko gani yangetokea Tanzania hadi hivi sasa (mwaka mmoja baadaye)? Mimi nawakilisha mawazo ya Watanzania ambao hawajaridhika na CCM na hawajavutiwa na upinzani! Lakini wakipewa uchaguzi wa pande hizo mbili wanaipa kura ya ndio (licha kusita sita) CCM! Ni jukumu lenu wapinzani kuwashawashi Watanzania ni kwa nini wawape madaraka ya kuongoza nchi yetu!!
Msituambie tuwape madaraka ati kwa sababu CCM mbovu na inanuka, tunajua hilo, tuambieni kwanini tuwape nyinyi madaraka na tofauti ya viongozi mtakaowaweka nyinyi na wale waliopo CCM ni nini? Ninawapa somo la bure hapa, mkiweza kujenga hoja inayojibu swali hilo basi mnajitengenezea njia nyeupe kwenda Ikulu!!
Jasusi:
Kwa karibu miaka zaidi ya kumi Democrats walikuwa upinzani na Republicans wakishikilia vyombo vyote vya Ikulu na Bunge. Je, jukumu la kujiimarisha Democrats lilikuwa ni la Republicans kutengeneza mazingira mazuri ili Democrats washinde? Kwanini, unafikiri Democrats walishinda? Unafikiri ni kwa sababu watu wanadhani Democrats ni tofauti sana na Republicans? la hasha! Democrats walijenga hoja kuwa nchi inahitaji kufuata mwelekeo tofauti na wa Republicans na pia viongozi wa Democrats walishajulikana, hakukuwa na suprise!
Ndo maana ninawapa somo la bure wapinzani wa Tanzania:
a. Endapo wanasubiri na kuombea kuwa CCM itaweka mazingira mazuri ili wao wachukue nchi "kwa upole, kama kumsukuma mlevi" wafikiri tena. CCM haina nia wala wazo la kuona upinzani unaimarika Tanzania! It is not in their best interest!
b. Jukumu la kuviimarisha vyama vya upinzani ni kwa wale waliomo ndani ya vyama hivyo! Tarehe 8/10/2005 Freeman Mbowe akizungumza wakati wa kampeni kule Mbeya alisema kuwa kukosekana umoja katika kambi ya upinzani kumedhoofisha upinzani kiasi kwamba wameshindwa kupigia kelele kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi! Alifanya nini kuunganisha nguvu zake na wapinzani wenzake? Je, anafanya nini leo ili kuunganisha kambi ya upinzani kabla ya 2010?
Sheria ya kuruhusu vyama kuungana itajadiliwa baadaye mwaka huu na bila ya shaka itapita. Unafikiri itafanya vyama hivyo vikubwa kuungana na kuunda chama kimoja au yatakuwa yale yale ya NARC Rainbow ya Kenya?
Kuhusu njia za kuimarisha upinzani Tanzania, mbona zipo nyingi na tumezitaja sana. Je wapinzani wa Tanzania wanasikiliza? Haya, ngoja nizirudie hapa.
a. Badala ya kunuia kupewa Urais kwenye uchaguzi wa 2010, wapinzani wadhamirie kuchukua Bunge, kwa kunyakua angala theluthi mbili ya Bunge zima. Kwa jinsi walivyo sasa hiyo itakuwa ni ndoto.
b. Kama wapinzani kweli wanataka kuongoza nchi, njia rahisi ni kujiandalia viongozi watakaochukua nchi. Kwa idadi ya wabunge walionao sasa, hata baraza la mawaziri wasingetosha! Ushauri wangu ni huu. Mara tu sheria ya kuunganisha vyama itakapopitishwa baadaye mwaka huu viongozi wa vyama vya upinzani vikubwa (Lipumba, Mbowe, Mrema, na Mbatia) wakae chini kwa pamoja, waandike Memorandum of Understanding ya kukubali kuviua vyama vyao na kuunda chama kipya kimoja kikubwa cha upinzani, kushirikishana mali za vyama hivyo n.k. Halafu ceremonically, watangaze kuvunjika kwa CHADEMA, TLP, CUF, NA NCCR na kuundwa kwa chama kipya. Wapo viongozi watakaopoteza nafasi zao na kwa maoni yangu, wenyeviti wote wa sasa wa vyama hivyo wasipewe uenyekiti wa chama hicho kipya!!! guess why?
c. Pindi wakishaunda chama hicho kipya, waandike ilani yao ya kuelekea 2010, wainadi kwa wananchi, na wana miaka karibu mitatu ya kuonesha ukomavu wa kisiasa na ya kuwa wanaweza kufanya kazi pamoja licha ya migongano ya huko nyuma na tofauti ya kimitazamo.
d. Jambo la nne, waanze kampeni ya kupata wanachama wapya, na kuwashawishi hata wana CCM mashuhuri kuungana nao ili kuipatia Tanzania mwelekeo mpya, kwani ule wa CCM umeshindwa!!
Quarz:
Sijasema mahali hata pamoja kuwa turudi kwenye Chama kimoja isipokuwa kama kuwepo kwa vyama vingi dhaifu na visivyo na mwelekeo ni sawa na kuwa na chama kimoja! Jukumu la vyama upinzani siyo kukosoa chama kilichoko madarakani (of course, ni sehemu ndogo ya majukumu yake). Jukumu kubwa la chama chochote cha upinzani ni hatimaye kuchukua hatamu za uongozi wa nchi na kutengeneza sera za kuongoza Taifa. Ndiyo sababu nimeuliza wapinzani wa Tanzania kweli wanaweza kuwa ni wakombozi wa Taifa letu? Sijauliza kama wanaweza kuwa wakosoaji wa Taifa letu!
Mimi hapa nawasaidia kimawazo ya jinsi gani vyama vya upinzani vinatakiwa kujijenga na kujiimarisha. Baadhi ya hoja ninazojenga, siyo kusudio langu kuipigia debe CCM bali kuwapa nafasi wapinzani wanaopitia humu wajue jinsi baadhi ya Watanzania wanavyowafikiria na hivyo kuchukua mikakati ya kuwashawishi kuwaamini. Hadi hivi sasa hakuna aliyenijibu angalau kwa kiduchu kuniambia ni kwa nini tuwaamini wapinzani badala ya CCM. Kung'ang'ania kusema CCM imeoza na haifai haitoshi! Tuambieni kwanini nyinyi mnafaa na hamjaoza?!!