Je kwanini Yuda alimsaliti Yesu kwa busu?

Underwood

JF-Expert Member
Dec 25, 2020
445
1,000
Natumaini Ijumaa kuu inawaendea vyema wana jamvi wakati huu taifa likiwa kwenye maombolezo ya kitaifa. Bila kupoteza muda, niende moja kwa moja kwenye hoja.

Wengi wetu kama sio wote tunafahamu kuwa waumini wa madhehebu ya kikristo wako katika maadhimisho ya juma kuu kama namna ya kukumbuka na kuenzi mateso na kifo cha Yesu (Kristo) wa Nazareti.

Moja kati ya matukio ya kipekee katika juma hili kuu ni tendo la mmoja wa wafuasi na marafiki wa Yesu anayetambulika kama Yuda Iskarioti kumsaliti mwalimu wake kwa viongozi wa Wayahudi na wakuu wa makuhani ambao walitaka kumkamata Yesu na kumuua kwa muda mrefu bila mafanikio.

-----
Mathayo 26: 14-16 (BHN).

Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu, akawaambia, “Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?” Wakamhesabia vipande thelathini vya fedha; na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti.

-----
Katika vitabu vyote vya injili (injili za Mathayo, Marko, Luka na ile ya mwanafunzi aliyependwa sana, Yohana) tunaelezwa kwamba Yuda Iskarioti aliondoka katika chakula cha jioni kilichokuwa kimeandaliwa na Yesu na kwenda kwa wakuu wa makuhani ambao mwanzo walikuwa tayari wamesha mlipa Yuda fedha na deni lilikuwa kwa Yuda kumkabidhi Yesu kwao.

Basi Yuda alipewa kikundi cha askari na walinzi wa hekalu kwa ajili ya kwenda kumkamata na kazi kubwa ya Yuda ilikuwa ni kuwaongoza mahali Yesu alipo kwani katika kipindi hicho Yesu aliishi kwa tahadhari sana kwa kufahamu kuwa anatafutwa ili ashtakiwe kwa makosa ya uchochezi.

Lakini katika hali isiyo ya kawaida, Yuda hakutakiwa tu kuwapeleka askari mahali alipo tu. Yuda alitakiwa kuwaonyesha Yesu ni nani na yupi hasa!

Yaani kikundi cha askari pamoja na wafanyakazi wa hekalu (ambamo Yesu alihubiri kila siku) walitaka waonyeshwe Yesu ni yupi kati ya wale 12 watakao kuwepo Gethsemane!

Pamoja na Yesu kuwa maarufu katika Yerusalemu na maeneo mengine ya Yudea hadi kuingia Yerusalemu kwa kushangiliwa kwa matawi ya mtende lakini watumishi wa hekalu na askari walitaka kuonyeshwa Yesu ni yupi hasa!

Ndipo Yuda alipo toa wazo kuwa atakaye mbusu shavuni ndiye Yesu Mnazareti wanaye mtafuta.

-----
Mathayo 26: 48-50 (BHN).

Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni.” Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, “Shikamoo, Mwalimu!” Kisha akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.

D063DECE-8C31-4FBC-B794-84FC34A004B9.jpeg

-----

Kama nilivyokwisha kuandika katika aya za mwanzo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, walinzi wa hekalu ambamo Yesu alihubiri mara kadhaa pamoja na watumishi wa makuhani (akiwemo Malko) na askari wa makuhani walishindwa kumtambua mtu maarufu na hatari anayetishia usalama wa taifa la Israeli kwa kitendo chake cha kuingia mjini Yerusalemu kama mfalme. Tena watu wakimwita mwana wa Daudi! Ni ajabu ilimpasa Yuda ambaye alimsaliti mwalimu na rafiki yake kumbusu rafiki yake huyo ili kundi lenye marungu na mapanga liweze kumkamata.Kwanini?

Mwaka 2013 mwandishi na mtafiti wa kidachi Roelof van den Broek alitafsiri kwenda Kingereza kitabu kimoja cha Injili kilichoandikwa kwa lugha ya kiCoptic kutoka huko Misri. Inaaminika kitabu hicho cha kiCoptic kina umri wa takribani miaka 1200.

58FB51A0-FBAA-4948-B902-2D9FB1F7E022.jpeg

Moja kati ya kurasa katika kitabu cha injili cha kiCoptic.

Katika Injili hiyo baada ya Yuda kwenda kwa viongozi wa makuhani walimuuliza kama ifuatavyo :

_________________________________

"Je tutamtambuaje mtu huyu" walisema viongozi wa makuhani na Wayahudi "kwani mtu huyu [Yesu] hana muonekano mmoja na muonekano wake hubadilika badilika,

wakati mwingine ana sura nyekundu,

wakati mwingine ni mweupe,

wakati mwingine ni mwekundu,

wakati wingine anafanana na ngano,

wakati mwingine amepauka kama mtu aliyefunga kwa muda mrefu,

wakati mwingine huonekana kama kijana na wakati mwingine kama mzee?"Ndipo Yuda alipotoa wazo la kumbusu Yesu shavuni kisha wao tamkamata.

_________________________________


Hii ndiyo ilikuwa njia pekee ya wao kumtambua Yesu kwani waliamini kama wangeenda bila kuongozana na Yuda huenda wangekuta watu 12 bustanini na wasijue ni yupi wa kumkamata kwani Yesu (kwa mujibu wa injili ya kiCoptic) alikuwa na uwezo wa kubadili muonekano wake!

Lakini uajabu wa injili hii ni pale inapo tofautiana na injili kuu nne za kikristu kwani injili hii inaeleza kuwa Yesu hakukamatwa siku ya Alhamisi jioni bali ilikuwa siku ya Jumanne!

Pia Injili hii inaeleza kuwa Yesu hakulala korokoroni usiku baada ya kukamatwa bali alipata chakula cha jioni na Ponsio Pilato kiranja wa Kirumi katika Yudea. Katika maongezi yaliyofanywa wakati wa chakula hicho cha jioni, Pilato alivutiwa sana na Yesu hata kumuambia Yesu kuwa yuko tayari hata kumtoa mwanaye wa kiume auliwe baada ya Yesu. Lakini Yesu alikataa Pilato asiingilie mchakato ulio anzishwa na viongozi wa Kiyahudi na amuhukumu kwa sheria za Kirumi yaani kusuluhishwa msalabani.

Hitimisho: Japo hakuna ushahidi kuwa ni kweli mtu maarufu Yesu wa Nazareti alikuwa na uwezo wa kubadili muonekano wake mara kwa mara lakini ni wazi kuwa wa baadhi ya Wakristo wa kwaza waliamini mambo haya. Pamoja injili hii kuwa tofauti na Injili tulizo zizoea na injili nyingine ambazo hazipo katika Biblia, Injili hii inaeleza kama injili kuu tatu (Mathayo, Marko na Luka) kuwa Yuda alimbusu Yesu kama ishara kwa wale watakao mkamata lakini angalau injili hii inatoa sababu.

Muwe na Ijumaa kuu njema.
---

Underwood

2nd of April 2021.

Asanteni.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom