Je, Dr. Willibrod Slaa atatufaa? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Je, Dr. Willibrod Slaa atatufaa?

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by PJ, Aug 11, 2010.

 1. PJ

  PJ JF-Expert Member

  #1
  Aug 11, 2010
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 297
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Dk. Slaa atatufaa Ikulu ​


  M. M. Mwanakijiji

  KINYANG'ANYIRO cha uchaguzi mkuu kwenye nafasi ya urais utakuwa ni baina ya Dr. Kikwete na Dr. Slaa. Katika mazingira fulani fulani mwamuzi wa nani atashinda kati ya hawa wawili waweza kujikuta ukiamuliwa na Dk. Lipumba. Lakini kama mazingira yatabaki jinsi yalivyo sasa ni wazi kabisa kuwa Watanzania wanatakiwa kuchagua kati ya kigumu na rahisi, kati ya cha zamani na kipya, kilekile na tofauti. Naamini kinyang'anyiro hiki cha mwaka huu kimekolezwa upya kabisa na ujio wa Dk. Slaa katika ushindani huu wa kiti cha Urais.

  Uchaguzi huu basi tutaona kuwa ni uchaguzi mgumu kwa namna moja na mwepesi vile vile kwa namna nyingine. Kwa mamilioni ya Watanzania yule watakayemchagua kushika nafasi ya urais atakuwa anaendana kabisa na fikra zao kuhusu hali yao ya maisha na nafasi yao ya kufanikiwa katika nyakati hizi.


  Kwa wengine uchaguzi wa Rais Kikwete kumpa na kumpa nafasi nyingine utatokana na kuridhishwa na uongozi wake katika miaka hii mitano inayoisha. Hawa watamchagua tena Kikwete kwa nguvu na kwa hamasa kubwa kwa sababu wanatambua kuwa kweli "amefanya mengi" na kuwa sasa ni wakati wa kumpa nafasi ya kumalizia kile alichoanzisha.

  Kwa upande mwingine wapo watakaotaka kumchagua Dr. Slaa kwa sababu hawajaridhishwa kabisa na mwendo, utaratibu na mwelekeo wa serikali yetu ya sasa chini ya Rais Kikwete. Hawa wanataka kuchagua kiongozi mwingine kabisa ili taifa liweze kupatiwa nafasi ya kuanza upya. Kumbe tukiangalia kwa ukaribu tutaona kuwa uchaguzi huu kwa kweli unahusu mambo makubwa kadhaa ambayo upande mmoja yanawakilishwa na Rais Kikwete na upande mwingine yanawakilishwa na Bw. Slaa. Pande hizi mbili kimsingi ni tofauti sana kama vile Mashariki ilivyo tofauti na Magharibi, maji yalivyo tofauti na moto, na radi ilivyo tofauti na upepo. Ni tofauti ambazo kama tutakavyoona baadaye ni za muhimu sana kiasi kwamba ni lazima lizigawe taifa kabisa.


  Uchaguzi kati ya watu wale wale na watu tofauti


  Uchaguzi huu unaokuja utatupa nafasi ya kuchagua viongozi wale wale au viongozi wapya. Ni wazi kabisa kuwa Rais Kikwete kwa upande wake hana watu wapya ambao anaweza kuwapendekeza kwa Watanzania. Hata kura za maoni zitakapowachuja wengi kutoka ndani ya CCM wiki hii haina maana kuwa wale watakaosimamishwa ndio watakaoshinda. Natabiri kuwa ukiondoa sehemu chache nchini wagombea wengi wa zamani wa CCM watapita kwa urahisi tu huku damu mpya ambayo imejaribu kujitokea itakapopewa somo la kutokumsumbua simba akila.


  Hivyo, Dr. Slaa anataka kutupa nafasi ya kuleta uongozi mpya kabisa ambao wengi wao hatujawahi kuwaon a wakiwa na madaraka makubwa. Wale wa CCM karibu wote ni viongozi ambao tumewajua kwa muda mrefu kabisa. Wale watakaokuja na Dr. Slaa ni wapya katika utendaji wa serikali. Kumbe Watanzania watatakiwa kuchagua "viongozi waliowafikisha hapa" na "viongozi wanaotaka kuwatoa hapa". Kama nilivyosema kwa wale ambao wanaridhika tulipofikia hapa hawatakuwa na uchaguzi mgumu, watamchagua Kikwete kwa furaha kubwa.


  Ni uchaguzi kati ya kipya na cha zamani


  Uchaguzi huu unahusu kuchagua vitu vipya na vya zamani. Rais Kikwete anawakilisha yale ya "zamani" wakati Slaa anawakilisha "Vipya". Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa CCM haiwezi kamwe kudai "upya" kwa sababu mtu yeyote anajua kuwa ni "zamani". Kitu ambacho imeweza kufanya kwa muda mrefu ni kupaka rangi cha zamani, kukiwekea manukato na kukiimbia nyimbo za ‘upya'. Wapo wanaofurahia kuona hivyo wakiamini kuwa ni "kipya" kweli. Ni sawa na mtu ambaye ana gari lake la zamani lililokongoloka lakini amelipaka rangi mpya yenye kunukia huku nyuma kaandika "baba yako analo?". Kwa wengine "upya" huo ndio wanaujali, yaani upya wa mapambo.


  Wengi wetu tumelijua jina la Kikwete kwa muda mrefu sana na kuna wakati ilikuwa tayari imekubalika bila maswali kwamba amepakwa mafuta kuwa Rais wetu na ikawa hivyo. Ameshika nafasi mbalimbali za uongozi na hakuna mtu ambaye amefuatilia siasa za Tanzania ambaye hajui historia na nafasi mbalimbali za Kikwete katika uongozi wa chama.


  Hivyo, hakuna mwana CCM ambaye anaweza kudai (akiwa bado na utimamu) kuwa Kikwete anawakilisha "upya" wa aina yoyote. Kwa hiyo kwa kurudia kumchagua Kikwete watanzania watakuwa wanachagua kile kile cha zamani. Sasa hili laweza lisiwe baya kwa sababu watu wako tayari kuchagua kile walichokizoea wanakijua kuliko kile kigeni wasichokizoea. Kwa miaka mingi hii imekuwa ni kawaida yetu katika kura. Lakini, mwaka huu sitoshangaa Watanzania wakajaribu tofauti.


  Dr. Slaa anawakilisha upya katika safu ya uongozi wa Tanzania. Anawakilisha mawazo mapya ya kiutawala na kimtazamo wa kitaifa. Uelewa wake wa kiini cha matatizo ya Tanzania ni tofauti kubwa kati ya uelewa wa Rais Kikwete na timu yake. Wakati Dk. Slaa anaelewa (na mimi nakubaliana naye) kuwa tatizo kubwa la maendeleo ya Tanzania ni ufisadi Rais Kikwete haoni hili kama ni tatizo kubwa.


  Rais Kikwete yuko tayari kulaumu Ukoloni (ulioondolewa karibu miaka 50 iliyopita) na vitu vingine ambavyo ukiviangalia kwa karibu havioneshi ukweli wa kukubalika. Mawazo ya Kikwete kuhusu umaskini wetu ni yale yale ya zamani. Uelewa mpya na wa ukweli ni lazima ukubali kuwa ufisadi ndiyo sababu kubwa ya umaskini wetu na hivyo hatuwezi kuondokana na umaskini bila kushughulikia ufisadi kwa nguvu zote.


  Majibu yale yale na majibu mapya


  Harakati za kisiasa na uongozi za Tanzania zinahitaji majibu mapya. Chini ya CCM majibu yamekuwa ni yale yale kama vile ni majibu ya hesabu ambapo 2 + 2 ni nne bila kutegemea wakati, mahali, na hali za maisha. Jawamu la nne ni kweli kama swali lingeulizwa mwaka 1970 au 2050 na ni lile lile kama lingeulizwa Uchina au Mbezi Temboni.


  Lakini uongozi wa kisiasa hudumaa unapojaribu kutoa majawabu yale yale kwa matatizo yale yale kana kwamba ni hesabu. Matatizo ya maisha ya watu yana vyanzo vingi na hivyo katika kuyatafutia ufumbuzi unahitajika ubunifu mpya wa majibu mapya yanayoendana na ukweli na uhalisia wa maisha ya watu leo hii. Nitatoa mfano.


  Katika hotuba yake ya kuelezea mafanikio ya serikali yake katika kupambana na vitendo vya rushwa kule Bungeni Rais Kikwete alitamba kwa kudai yafuatavyo:


  "Tumeunda upya chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU). Sasa TAKUKURU ina ofisi katika kila wilaya na tumeiongezea uwezo wa kibajeti na rasilimali watu na vitendea kazi.


  Juhudi hizo, zinadhihirisha utashi mkubwa wa kisiasa tulionao wa kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Kwa sababu hiyo, katika miaka mitano hii, tuhuma nyingi zimechunguzwa, kesi nyingi zimefikishwa Mahakamani ikiwa ni pamoja na zile za rushwa kubwa. Mapambano bado yanaendelea.

  Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumepeleka Mahakamani kesi za rushwa 780. Idadi hii ni kubwa kuliko kesi zote za rushwa zilizopata kupelekwa Mahakamani katika kipindi cha miaka 20 kabla ya hapo, ambazo zilikuwa 543. Kati ya kesi hizo 780 Serikali imeshinda kesi 160. Katika kipindi cha miaka 20 kabl a ya hapo (yaani kuanzia 1985 – 2005) Serikali ilishinda kesi 58 tu."

  Kwa haraka tunaweza kudhania kuwa rekodi hii ni ya kujivunia hadi pale tutakapoiangalia kwa ukaribu. Kabla ya mabadiliko ya sheria ya kudhibiti na kupambana na rushwa ambayo ilikuwa na makosa machache kwa muda wa miaka 20 serikali ilishinda asilimia 10.6 ya kesi zake. Katika uongozi wake Kikwete amedai kuwa sheria hii mpya yenye makosa mengi, vitendea kazi vingi na uwezo mkubwa kuliko miaka 20 iliyopita serikali yake imeweza kushinda asilimia 20 tu ya kesi zakd hivi sasa. Je hii ni rekodi ya kujivunia? Ni lazima tuangalie vile vile kuwa idadi inayotajwa haichukulii maanani rufaa za baadaye na mwisho wa kesi hizo nyingine kwani. Hadi pale rufaa ze kesi hizo 160 zitakapofikia tamati ndipo tutajua kweli ni kwa kiasi gani tumefanikiwa.


  Tunahitaji mawazo mapya kabisa katika mapambano dhidi ya rushwa. Sifa haiji katika idadi ya kesi zinazofunguliwa mahakamani au kesi ambazo serikali imeshinda kwa mara ya kwanza. Mafanikio dhidi ya rushwa yatapimwa hasa kwa kesi ambazo serikali hatimaye inashinda baada ya rufaa zote kukamilika.

  Hicho ndicho kipimo cha kweli cha mafanikio ya vita hii dhidi ya ufisadi. Kumbe tunahitaji uongozi ambao unaweza kuona unaharakisha kesi hizi katika mfumo mzuri na thabiti ambao utahakikisha kuwa hakuna makosa yanafanyika yenye kusababisha watu washinde rufaa kirahisi. Hatuwezi kushangilia watu kufikishwa mahakamani tu kama kwenye sinema, tunatakiwa kufurahishwa tunapowaona wametiwa pingu na kula mvua nyingi gerezani. Nje ya hapo ni geresha.

  Mwendelezo wa kilichopo au mabadiliko


  Tukiangalia kwa ukaribu tutaona kuwa kumbe uchaguzi wenyewe hasa mwaka huu unahusu zaidi mwendelezo wa mfumo wa utawala uliopo, mtazamo ule ule, watu wale wale, itikadi zile zile na mapendekezo yale yale ya kutatua matatizo yetu au kuchagua mabadiliko. Ninaamini kwa kadiri tunavyoelekea uchaguzi mkuu Watanzania wataanza kutamani mabadiliko zaidi kuliko kitu kile kile.

  Hata ule msemo wa "zimwi likujualo" utaanza kupoteza maana kwani watu wataamka na kutambua kuwa kumbe zimwi likubakishalo halikubakishi kwa vile linakuonea huruma kama wengi wanavyodhania. Wengi wakisikia kuwa "zimwi likujualo halikuli likakwisha" wanafikiri ina mana linakuonea "huruma". Kumbe msemo huu umeficha maana ndani yake kuwa Zimwi linalokujua halikuli kikakumaliza kwa sababu bado lina mpango wa kukutafuna tena. Wakati mwingine linakuachia unenepe kidogo ili liweze kujinoma tena.

  Watanzania basi wanaitwa na historia kufanya uamuzi wa nini wanakitaka hasa kati ya watu hawa wawili. Kama wanataka mwendelezo wa yale yale, vile vile, walewale na ule ule basi chaguo lao si gumu, ni lazima wamchague Rais Kikwete tena kwa kufanya hivyo watachagua walichokizoea. Hata hivyo, kama wanaona kuwa wanachotaka ni cha tofauti, chenye mtazamo tofauti, majibu tofauti na bora na mwelekeo mpya basi chaguo lao pia siyo gumu, ni lazima wamchague Dr. Slaa.

  Ni hapa basi tunapoona utamu wa uchaguzi mkuu ujao. Kinyume na wengine wanavyozungumzia naamini uchaguzi huu ni lazima uigawe nchini kiitikadi, kimtazamo na kimwelekeo. Kama vile uchaguzi wa Obama ulivyoigawa Marekani natarajia uchaguzi huu utaigawa Tanzania. Ni lazima vijiweni, kwenye saloon, kwenye mabasi, vyuoni, sokoni na mitaani pande mbili lazima ziibuke. Upande unaotaka "kile kile" na upande unaotaka "cha tofauti". Pande hizi mbili lazima ziamuliwe kwenye sanduku la kura.

  Kutokana na ukweli huo anajidanganya kabisa mtu ambaye anafikiria kuwa Kikwete atashinda kiurahisi. Anajidanganya vile vile ambaye anafikiria kuwa ati kwa vile Kikwete ni Rais basi wananchi watamchagua tu kwa urahisi. Endapo Dr. Slaa atajenga hoja ya kwanini kweli yeye ni tofauti na Kikwete na akawaaminisha Watanzania kuwa atakuwa bora kuliko Kikwete basi kama nilivyowahi kuandika mara kadhaa huko nyuma isije kuwa ajabu kwa Kikwete kujikuta ni Rais wa kwanza wa Tanzania ambaye atanyimwa ngwe ya pili. Na ikitokea hivyo mashabiki wake wasiumie sana au kukwaza yote ni gharama ya demokrasia tu.

  Hata hivyo, wale wanaofikiria vile vile kuwa Dr. Slaa atashinda kiurahisi kwa vile ni "mpya" nao wanaweza kujikuta wanajidanganya. Slaa atashinda si kwa sababu watu wanaichukia CCM au kumchukia Kikwete. Kwa sababu ukiangalia sana utaona kuwa licha ya watu kuchukia CCM kama chama wengi bado wanampenda Kikwete na wanaamini kuwa anaongoza vizuri nchi. Kumbe kazi kubwa aliyonayo Slaa ni kuwashawishi Watanzania kuwa Tanzania chini yake yeye ni bora zaidi kuliko chini ya Kikwete. Hapa ndipo utamu wa uchaguzi huu utakapoonekana. Vyovyote vile ilivyo yeyote atakayeshinda mwaka huu natabiri kuwa itakuwa ni kati ya asilimia 55-60 ya wapiga kura wote. Kuna ujumbe ambao Watanzania wanataka kuutuma mwaka huu, ujumbe kwamba ya zamani hayatakiwi tena wanataka mapya. Ni nani atayaleta hayo?

  Tuangalie mwelekeo wa kampeni. Na katika hili ni lazima Kikwete aweze kuwa tayari kukubali kushindwa itakapotokea hivyo ili asije kulazimika kuapishwa usiku usiku kama ilivyotokea kwa Mwai Kibaki wakati naye alipokuwa anajaribu kutafuta ngwe ya pili.


  Source: Tanzania Daima
   
 2. Sumbalawinyo

  Sumbalawinyo JF-Expert Member

  #2
  Aug 11, 2010
  Joined: Sep 22, 2009
  Messages: 1,286
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 0
  Bila kumpigia kura na kulinda masanduku yenu ya kura Slaa hatofika ikulu ng'oo
   
 3. Ndibalema

  Ndibalema JF-Expert Member

  #3
  Aug 11, 2010
  Joined: Apr 26, 2008
  Messages: 10,916
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Tume ya Uchaguzi wameiweka wao (CCM).
  Mabosi wa Vyombo vya ulinzi ni watu wao.
  Mtawezaje kulinda masanduku ya kura!?
   
 4. Utingo

  Utingo JF-Expert Member

  #4
  Aug 11, 2010
  Joined: Dec 15, 2009
  Messages: 7,121
  Likes Received: 185
  Trophy Points: 160
  hapo ndipo kazi ipo. maana tume ya uchaguzi na walinzi wote ni wao CCM
   
 5. Nyange

  Nyange JF-Expert Member

  #5
  Aug 11, 2010
  Joined: Mar 25, 2010
  Messages: 2,180
  Likes Received: 229
  Trophy Points: 160
  Tutashinda kwa imani. Hata wakati wa Moi au Chiluba, wengi walijiuliza hivyo. Leo hii wanavuna uongozi wenye sura mpya.

  HEBU TUSUGUE MAGOTI na Mungu atatenda make wale wote wenye mipango ya kuiba kura 'WASHINDWE NA WALEGEE'
   
 6. Jethro

  Jethro JF-Expert Member

  #6
  Aug 11, 2010
  Joined: Mar 23, 2009
  Messages: 2,223
  Likes Received: 98
  Trophy Points: 145
  Swala la kutufaaa mi nadhani si hoja kubwa saaana

  Nadhani ni jinsi gani ya alivyojipanga kuingia IKULU na nini akatufanyie IKULU, lakini kama amejipanga kama wanamtandao walivyo tuchezeaaa sakayosa humo ndani 2005 up to date mmmmh
   
 7. RedDevil

  RedDevil JF-Expert Member

  #7
  Aug 11, 2010
  Joined: Apr 30, 2009
  Messages: 2,287
  Likes Received: 903
  Trophy Points: 280
  Cha msingi, kampeni iambatane na uelimishaji wa wananchi jinsi ya kulinda kura. Jinsi watu wanavyoweza kuibiwa kura zao napo waelezwe.
   
 8. M

  MzeePunch JF-Expert Member

  #8
  Aug 11, 2010
  Joined: Jun 8, 2009
  Messages: 1,412
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Hata hao watu wa tume ya uchaguzi na makamanda wa polisi wameshaichoka serikali ya ccm wanataka mabadiliko., hivyo watatusaidia kulinda kura.
   
 9. m

  mapambano JF-Expert Member

  #9
  Aug 11, 2010
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 535
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Dr Slaa ni bora mara 100 zaidi ya JK, lakini sasa......mtu mmoja au niseme watu wachache wenye uwezo CHADEMA. Dr Slaa hawezi kuendesha nchi peke yake. Ninafikiria tu! Waziri Mkuu: Mbowe. Hapo ndipo ninakosa imani. Yatakuwa yale yale ya CCM or even worse. Bado ile article yako ya " Kuingia Ikulu then what? I think it raised good argunments and some challenges ahead. Hate it or not...hizi ni siasa, kila mwanasiasa, ahadi kibao, utekelezaji ndio unakua kazi katika mfumo wetu wa sasa. . Binafsi nafikiri kuleta mabadiliko katika taifa letu sio lazima kuingia katika siasa..sikatai siasa safi na uongozi bora play its role. Ninawasiwasi na hili wimbi la watu kukimbilia siasa kama kweli ni driven by national interests or individual interests.
   
 10. B

  BENSON MSEMWA Member

  #10
  Aug 11, 2010
  Joined: Aug 10, 2010
  Messages: 30
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Sio ikulu tu hata kwenye kero zetu,slaa is visioned and missioned person,lets vote for him
   
 11. Ndachuwa

  Ndachuwa JF-Expert Member

  #11
  Aug 11, 2010
  Joined: Mar 8, 2006
  Messages: 4,530
  Likes Received: 725
  Trophy Points: 280
  Serikali tayari ipo, wizara zimo zina watendaji, kuweka nafasi chache za wasimamia SERA siyo kazi kubwa, Watanzania tuko zaidi ya 40 Million, Wabunge wa CCM ni less than 250 so why so worried?
   
 12. Mpangamji

  Mpangamji JF-Expert Member

  #12
  Aug 11, 2010
  Joined: May 12, 2010
  Messages: 536
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  waamuzi ni watanzania, kama watanzania hawajaamua kubadili uongozi (chama) uliopo madarakani, sisi wachache tunaopiga kura zetu vyama vya upinzani hudhani siku zote kuwa kura zimeibiwa. watanzania wanajukumu la kuamua, maboksi ya kura yatajilinda yenyewe.
   
 13. Kiby

  Kiby JF-Expert Member

  #13
  Aug 11, 2010
  Joined: Nov 16, 2009
  Messages: 5,209
  Likes Received: 1,012
  Trophy Points: 280
  Kufikiri kwamba tanzania ni nchi ya kipee tofauti na nchi zingine duniani ni sawa na kujilisha upepo. Hutuwezi kukiri kwamba upumbavu umeiteka hekima, ni aibu kukiri ukihiyo unaviburuza vyuo vinavyotoa elimu. Namaanisha nini? Habari ya kufikiri kuibiwa kura na kuridhia daima ni ya watu waliokata tamaa kuwepo duniani. Tz hatutaki kuamibi kwamba sisi ni majuha yanayotendewa dhuluma kila wakati. Tunaamini na ni dhahiri kwamba wakati wa mageuzi umewadia, na ukiwadia hakuna nguvu iwezayo kuzuia ama imetoka juu au shimoni. Ccm tutawaondoa kwa kura zetu mwaka huu na kama bado hawataki kusoma sign basi yale ya Zimbabwe na Kenya yatawapata. Naishauri ccm ipumzuke kwa amani kuliko kuchagua kufa kwa kuteseka.
   
 14. B

  Babuyao JF-Expert Member

  #14
  Aug 11, 2010
  Joined: Jun 6, 2009
  Messages: 1,734
  Likes Received: 29
  Trophy Points: 145
  Hakika maandishi yako ukutani. CCM wanapaswa kusoma.
   
 15. m

  mapambano JF-Expert Member

  #15
  Aug 12, 2010
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 535
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM....I wish it was that simple..
   
 16. n

  njori Member

  #16
  Aug 12, 2010
  Joined: Aug 10, 2010
  Messages: 26
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  hawezi kutufaa kama KANISANI tu palimshinda!
  laana za kumdanganya Mungu zinamuandama hawezi kukanyaga IKULU
   
 17. M

  Masonjo JF-Expert Member

  #17
  Aug 12, 2010
  Joined: Aug 8, 2010
  Messages: 2,725
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Majibu marahisi katika maswala magumu yanayobeba mustakabali wa taifa hili
   
 18. n

  njori Member

  #18
  Aug 12, 2010
  Joined: Aug 10, 2010
  Messages: 26
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  fast thinking ndio ulingo wa zama hz Masonjo!
   
 19. mzamifu

  mzamifu JF-Expert Member

  #19
  Aug 12, 2010
  Joined: Mar 10, 2010
  Messages: 3,497
  Likes Received: 854
  Trophy Points: 280
  Asente Mwanakijiji
  Hoja yako ni 'objective' kwa kiasi kikubwa kwani hujaonyesha wazi kabisa msimamo wako ingawa unaonyesha wazi kuwa yanahitajika mabadiliko. Suala ni nani kati ya Kikwete na Slaa anaonyesha wazi kuwa ataleta mabadiliko yaanayotakiwa. Hakuna asiyetaka mabadiliko kwa kweli. Tatizo ni kama wananchi wanawafahamu vizuri wote hawa wawili. Je, wananchi wengi wana mtazamo gani; wa kizamani au wa kisasa? Je, bado walio wengi wana hofu ya mabadiliko au wamegeuka jasiri na kuthubutu, je, bado kuna wanaosema ;Siwezi kuiacha CCM kwa vile imenilea, imenikuza n.k? wengine wanaweza kusema tu wacha yawepo mabadiliko kwa hasira tu. Kwa mfano wafanyakazi wanasema tumekanwa sjui nini sijui kitu gani, hasira inawafanya waamue waonavyo!
  Inaonyesha wazi kuwa kuna haja ya kutoa elimu ya kutosha kwa wapiga kura ili wajue kilicho bora na waweze kufanya uamuzi sahihi. Kama ulivosema, gumzo la uchaguzi huu ni kati ya Kikwete na Slaa, tusubiri tuone mengi yatajiri. Ahsante
   
 20. K

  Kisendi JF-Expert Member

  #20
  Aug 12, 2010
  Joined: Jan 29, 2009
  Messages: 700
  Likes Received: 53
  Trophy Points: 45
  Nafikiri, Tuwe wazalende hao polisi, wenyewe si watoto wa wakulima kama sisi, Mbona nchi zingine wanashinda. We need to believe and say no to ccm
   
Loading...