JAMANI KWANI LAZIMA?!-14
ILIPOISHIA
Siyo lengo langu shemeji, ila unajua wakati mwingine nakutisha tu ili unisaidie maana hali yangu mbaya, nina uhitaji mkubwa sana shemeji, usinione hivi.
Kwa hiyo hali hii ya wewe kunitisha itakwenda mpaka mwaka gani?
ZUNGURUKA NAYO MWENYEWE
Ah! Sidhani kama nitataka kuendelea tena shemeji, ila sema tu nimeshtuka sana kuona una mimba.
Mimba hii haikuhusu shemeji, nimeshakwambia. Wala usije ukawaza kwamba ni yako, ni ya kaka yako.
Lakini ninavyojua mimi shemeji kaka hana uwezo.
Wa kufanyaje?
Kukupa mimba wewe.
Sasa kama hana uwezo angeniacha niendelee kuishi nyumbani kwake? Acha mambo yako bwana.
Haya, tupo hapa shemeji, maana ujue mimi nafanana sana na mama, kaka anafanana sana na baba.
Kwa hiyo mtoto wangu mimi na kaka yako hawezi kufanana na bibi yake?
Anaweza, sasa cha ajabu ni nini hapo?
Nimesema tu shemeji!
Uangalie mambo ya kusema shemeji, alisema Paulina huku akitoa kitita cha pesa na kumpa Santo, akimwangalia kwa macho yaliyojaa hasira.
Asante shemeji. Nakuahidi kuanzia sasa sitakusumbua tena, nimekuelewa sana.
Nashukuru kwa kunielewa shemeji yangu.
Paulina alisimama, akaondoka zake, Santo aliendelea kumalizia soda yake kisha naye akaondoka zake akiwa na amani na furaha tele.
***
Njiani, Paulina bado alihisi mbele ya safari yake ya mimba ni kubaya kuliko alikotoka. Alikuwa akiwaza namna ambavyo ameanza kupata wakati mgumu. Alikumbuka mazungumzo yake na baba Riziki siku walipokutana
Nilikuwa nakutafuta sana jirani.
Nipo mbona!
Sawa upo, lakini nataka kukwambia kutoka moyoni kwamba hiyo mimba uliyonayo ni yangu.
He! Una uhakika gani?
Nina uhakika, ulinipigia simu ukasema una matatizo ya kutopata mimba, nikakupa namba ya dokta, lakini anasema hukuwahi kwenda hata siku moja na ulikutana kimwili na mimi. Wakati tunakutana uliniambia ndiyo kwanza unazini nje ya ndoa, hujawahi. Kwa hiyo si mimba yangu hiyo kweli?
Si yako.
Ya nani?
Kwani si nina mume?
Hata kama. Huyo mume ndiyo unasema hawezi kukupa mimba, mimi ninavyojua mimba ni yangu.
Sasa baba Riziki kama mimba ni yako, unataka kusemaje?
Nataka utambue hivyo, mtoto akizaliwa iko siku nitamtaka mimi baba mtu.
Paulina alijikuta akishtuka kwa kukumbuka maneno hayo ya baba Riziki
Dah! Baba Riziki anadai mimba yake, Santo naye anataka kushtukia. Itakuwaje? Ukweli mimba ni ya Santo, baba Riziki hahusiki kabisa, alisema moyoni Paulina huku akiwa anakaribia kufika nyumbani kwake.
***
Ilikuwa mwezi wa nane wa ujauzito wake Paulina, siku hiyo akiwa ndani, mumewe yupo kazini ilipigwa hodi!
Karibu, nani? Sauti kutoka nje haikujitambulisha licha ya kuulizwa nani.
Paulina alikwenda kufungua mlango, akakutana na sura ya baba Riziki
Sikai, ila najua bado muda kidogo utajifungua, nitamtaka mtoto wangu, alisema baba Riziki na kuondoka kwa hasira.
He! Umetumwa nini?
Sijatumwa na sitatumwa.
Khaa! Huyu baba vipi? Alisema kwa sauti Paulina baada ya kugundua kuwa, alichokiongea mwanaume huyo kilisikika na msichana wake wa kazi ambaye alimpata kama wiki mbili nyuma.
Kwani dada aliwahi kuwa mumeo kabla ya shemeji? Alihoji msichana huyo
Hamna, nahisi hana akili nzuri kama wanaume wengine.
Sasa itakuaje? Maana shemeji anaweza kusikia maneno yake.
Achana naye.
***
Siku hiyo, mume wa Paulina alipitia kwa wazazi kuwasilimia, alimkuta Santo naye yupo
Kumbe shemeji amebahatika kupata ujauzito, alisema Santo baada ya salamu na mazungumzo marefu.
Ulikutana naye?
Kuna siku nilikutana naye njiani, nikamsalimia.
Eee bwana, amebakiza kama mwezi mmoja ajifungue, Mungu ametenda.
Kweli Mungu ametenda, Santo alisindikizia.
Dawa gani alitumia? Akapeleka swali la msingi kabisa.
Hakuna dawa ni Mungu mwenyewe aliamua kufanya mabadiliko.
Oke oke!
Kuanzia hapo, Santo aliamini mimba ya shemeji yake ni yake na si ya kaka yake. Kama angesikia alitumia dawa angeamini kwamba ni kweli, dawa zimefanya kazi.
Siku ya mwisho, Paulina alijiandaa kwenda kliniki ambapo baada ya siku hiyo, alitakiwa kusubiri saa yenyewe.
Akiwa anashuka kwenye teksi, akutana na bodadoda inatoka, ni yule kijana dereva aliyekwenda kulala naye Magomeni
Yaani nilikuwa nakutafuta kweli, bahati mbaya sikuwa na namba yako, alisema kijana huyo
Kwa ishu gani? Aliuliza Paulina.
Kwanza unanikumbuka?
Ndiyo.
Tulikutana wapi?
We jua tu nakukumbuka, mambo ya tulikutana wapi sidhani kama yana msingi sana.
Oke. Sasa mimi siku ile usiku niliota ndoto eti unaniambia una mimba yangu, nikakwambia mbona sina uwezo wa kumpa mimba mwanamke?! Kesho yake nilikwenda hospitali wakasema nina uwezo wa kumpa mwanamke mimba, sasa leo nakuona una mimba kwa vyovyote vile ni yangu maana ndoto zangu hazisemagi uongo.