ILIPOISHIA
"Kwani tunamzungumzia nani we kenge?"
"Ninayo."
"Lete haraka sana aje akuchukue kwenda kwao, si anaishi na baba yake palepale kwa nyuma."
Stela alipeleka mkono kwenye simu na kubofyabofya akazitaja kwa Mozie...
TAMBAA KIVYAKO...
"Enhe...enhe...enhe...oke, mwisho sifuri siyo?" alisema Mozie...
"Ndiyo," akajibu Stela.
Palepale Mozie aliipiga namba hiyo, ikaita kwa muda mrefu ikakatika...
"Mbona hapokei," alisema Mozie...
"Pengine hapokei namba asizozijua," alidakia Paulina...
"Atakuwa na kazi," alisema Stela.
Mozie aliacha kwa muda lakini kabla hajapiga tena, simu ikapigwa...
"Anapiga yeye," alisema akiipokea...
"Haloo... hujambo dogo?"
"Sijambo, shikamoo."
"Marahaba...wewe ni Ali Mapikipiki?"
"Ndiyo mimi, nani mwenzangu?"
"Mimi naitwa Mozie. Ni bosi wa Stela. Anasema ulimpa ujauzito na amejifungua mtoto wako Mwarabu hapa kwangu, tafadhali kabla sijachukua hatua kali kwako njoo umchukue mwanao na mkeo hapa sasa hivi, nguruwe wewe."
Paulina alikuwa akimshika mkono Mozie kuashiria kwamba maneno yake ni makali sana kwa Ali Mapikipiki...
"Sikia bro! Mimi Stela unayemsema simjui wala wewe unayesema ni bosi wako sikujui..."
"Sikia we kima, ongea na Stela huyu hapa," alisema Mozie huku akimpa simu Stela lakini wakati huo, Ali Mapikipiki alikuwa hewani akiongea...
"Kima mwenyewe bwana. Wewe utanipaje jina la kima kama na wewe si kima...mambo mengine unata..."
Kabla Ali Mapikipiki hajamalizia, Stela alikuwa hewani...
"Haloo Ali..."
"We nani?"
"Mimi Stela wa kwa Paulina yule bosi wangu niliyekwambia amepewa mimba na baba Riziki mpaka akagombana na mume wake," alisema Stela bila kuweka nukta achilia mbali kituo.
Paulina alitaka kumvaa Stela, Mozie akamzuia...
"Acha tumalizie hili suala kwanza," alisema Mozie...
"Kwa hiyo unasemaje?" aliuliza Ali Mapikipiki baada ya Stela kujieleza sawasawa...
"Ile mimba niliyokwambia umenipa nimejifungua sasa. Mtoto ni wa kwako."
"Una uhakika gani?"
"Ni Mwarabu kama wewe."
"Wewe ndiyo umewaambia hao mabosi wako mimba ni ya kwangu, kwani tulikubaliana nini?"
"Sasa wamenishtukia Ali. Mtoto ni wewe mtupu."
"Sawa, lakini si nilikwambia mimi naishi kwa wazazi wangu, sasa unadhani nitakutunzaje na mtoto wako?"
"Kwani wewe unajitunzaje?"
"Sikia Stela, mimi sijazaa na wewe na huyo mtoto si wangu, mtafute baba yake, mbuzi wee," alisema Ali Mapikipiki na kukata simu...
"Haa! Amenikatia simu," alisema kwa mshtuko Stela.
Mozie ndiyo alikasirika zaidi...
"Sikia Stela, kusanya kilicho chako twende pale kwa baba yake. Leo atanijua mimi ni nani na nikoje," alifoka Mozie.
Stela kwa sura ya Mozie alivyoiona hakuwa na namna zaidi ya kukusanya kilicho chake kwa ajili ya kupelekwa kwa baba'ke Ali Mapikipiki.
***
Baada ya kukata kuongea na Stela, Ali Mapikipiki akawa kimachale sasa. Aliamini Mozie anaweza kumtokea wakati wowote ule ambapo yeye alifanya siri ya kutowaambia wazazi wake.
"Akija hapa sijui nitamwambia nini mzee Mbaruku," alisema moyoni Ali Mapikipiki akimuwazia baba yake mzazi...
"Mi nitakataa mtoto si wangu, kwani ana ushahidi gani?"
Wakati akiwaza hayo, sauti nyingine kichwani ilimwambia...
"Kama kweli mtoto ni Mwarabu mtupu huwezi kukwepa hata iweje! Hata mzee Mbaruku atajua ni mjukuu wako kama kweli mtoto ni Mwarabu."
Ali Mapikipiki alijaribu kuikataa sauti hiyo lakini ikawa inamwingia tu hata kwa lazima.
Mara, Ali aliitwa ndani na mama yake...
"We umeweka wapi lile boksi la sabuni la jana?"
"Stoo mama."
"Mbona hamna, msichana kaenda kuangalia stoo hakuna boksi."
"Kweli, hebu nikaangalie."
Kijana huyo alikwenda stoo kuangalia boksi hilo. Mama yake alikuwa eneo la jiko wakati baba yake alikuwa chumbani...
"Hodi wenyewe," sauti ilibisha hodi...
"Nani? Ingia," alisema mama Ali huku akimwambia msichana wa kazi akafungue geti.
Ali hakuwa akijua lolote kwa vile alizama stoo kutafuta boski la sabuni...
"Karibuni...karibuni," mama Ali alikaribisha wageni...
"Asante sana...asante sana."
Baada ya wageni kukaa, mama Ali aliwaangalia kama aliyetaka kujua ni akina nani na wametokea wapi maana sura zote zilikuwa ngeni kwake, kasoro ya Stela kwa mbali kama aliijua...
"Samahani sana, mimi naitwa Mozie, huyu ni mke wangu anaitwa Paulina na huyu ni msichana wetu wa kazi, anaitwa Stela," alisema Mozie akimalizia kumwangalia Paulina ambaye alikuwa amempakata mtoto...
"Sawa, niwasaidie nini?" alihiji mama Ali.
Ali ndiyo alikuwa anatokea stoo sasa, kutoka sebuleni anakutana na ugeni huo mkubwa...
"Haa!" alihamaki Ali, wengine wakajua...
"Shida yetu ni huyu bwana Ali," alisema Mozie...
"Kafanyaje?" aliuliza mama Ali...
"Amezaa na huyu msichana wangu wa kazi, akampa mimba, sasa amejifungua mtoto kafanana na yeye kwa asilima mia moja," ‘alifloo' Mozie na kuifanya sebule hiyo kuwa kimya ghafla.