" Saluti ya Kova kwa Kanumba yazua balaa"MSIBA wa msanii maarufu wa filamu nchini Steven Kanumba umezidi kuibua mambo, safari hii Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Suleiman Kova, amejikuta kwenye mjadala mzito, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Sambamba na hilo, kamati ya mazishi ya msanii huyo imesema kuwa imetumia sh milioni 70 kwa ajili ya gharama za kuuaga hadi kuuzika mwili wa Kanumba, huku mama mzazi wa msanii huyo, akiambulia sh milioni 4 za rambirambi.
Tukirejea kwenye sakata la Kova, kamanda huyo ameingia kwenye mjadala wa kifo cha Kanumba kutokana na hatua yake ya kuamua kutoa salamu za mwisho kwa kupiga saluti mbele ya jeneza la Kanumba.
Tukio hilo limeibua hisia mbalimbali miongoni mwa askari na wananchi kwa ujumla, huku kila mmoja akisema lake.
Baadhi ya askari na wananchi waliohudhuria hafla ya kuagwa kwa msanii huyo, walionyesha kushangazwa na kuhoji hatua ya Kova, kupiga saluti wakati wa kumuaga marehemu Kanumba.
Mmoja wa maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi, ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alibainisha kuwa Kova alichanganyikiwa kuipigia saluti maiti ya Kanumba kwani ni kinyume cha kanuni na taratibu za kijeshi.
Askari ukiwa umevaa sare katika misiba ya kijeshi ni sawa kuaga maiti kwa kutoa salamu ya kijeshi (saluti), lakini napo inazingatia na cheo husika kwa kweli kama siku hiyo Kova alikuwa amekusudia kumpigia saluti aliyekuwa mgeni rasmi, (Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Ghalib Bilal), ila katika kuaga mwili wa Kanumba, alikuwa amekosea, alibainisha ofisa huyo.
Baadhi ya wanaomjadili Kova wanahoji uhalali wa afisa huyo wa juu ya Jeshi la Polisi kutumia saluti katika kutoa heshima wakati salamu za aina hiyo hutolewa kwa polisi waliozidi vyeo.
Kwa upande wake, Kamanda Kova ametoa ufafanuzi wa saluti aliyoitoa wakati akitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa Kanumba.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Kova alisema anawashangaa askari wanaomshangaa kwani salamu hiyo ni ya kawaida tu katika nidhamu ya kijeshi.
Alisema kwa majeshi yote nchini, saluti ni salamu au heshima na alifanya hivyo kwa Kanumba kuonyesha heshima na jinsi alivyothamini kazi na mchango wake kwa taifa.
Alisema askari yeyote aliyevalia sale ya polisi kama anataka kusalimia au kutoa salamu kwenye shughuli kama ile ya Kumuaga Kanumba, lazima apige saluti.
Katika hali ya kawaida askari mdogo anapaswa kupiga saluti kwa askari mkubwa, lakini askari anaweza kupiga saluti kwenye tukio la kutoa heshima za mwisho kama nilivyofanya kwa mtu yeyote na sio lazima kwa askari kwa hiyo nilikuwa sahihi, alifafanua Kova.
Kwa mujibu wa Kova ni kosa kwa askari kutompigia saluti mkubwa wake, lakini sio kosa kwa askari yeyote kutoa heshima kwa marehemu hata kama aliyefariki ni mtu wa kawaida kama Kanumba.
Alisema siku ya kuuaga mwili wa Kanumba kulikuwa na watu mbalimbali na kila mtu alitoa heshima kuendana na utamaduni au imani yake, lakini kwake ilikuwa lazima apige saluti.