Uteuzi wake Tume ya Maadili wahojiwa
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
WAKATI Rais Kikwete akiishambulia Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika hotuba yake bungeni wiki iliyopita, yameibuliwa madai ya wafanyakazi wa tume hiyo, yanaoonyesha udhaifu wa utekelezaji wa kazi na ukiukwaji mkubwa wa maadili ndani ya tume.
Wafanyakazi wa tume hiyo wanadai kuwa utendaji wa chombo hicho umekuwa wa mashaka kutokana na uamuzi wenye utata uliofanywa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kumteua Jaji mstaafu Stephen Ihema, ambaye rekodi ya utendaji kazi wake si ya kuridhisha, kuwa Kamishna wa Maadili wa tume hiyo.
Katika barua ya wafanyakazi hao waliyomwandikia Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, Julai 10 mwaka huu, na gazeti hili kupata nakala yake, wafanyakazi hao wanaeleza kuwa uamuzi wa Mkapa kumteua Jaji mstaafu Ihema kushika wadhifa huo, uliwashangaza wanasheria wengi, akiwemo aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta.
Wanadai kuwa Mkapa alimteua Jaji mstaafu Ihema kuwa bosi wa tume hiyo huku akijua kuwa aliyekuwa Jaji Mkuu, Samatta, alitishia kujiuzulu wadhifa wake iwapo Ihema angeongezewa muda wa utumishi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa sababu ya kukiuka maadili ya kazi.
Chombo hiki kimekosa uongozi bora, tunamaanisha viongozi wakuu wa idara hii, kwa maana ya Kamishna wa Maadili na makatibu wawili wanaoshughulika na viongozi wa utumishi wa umma na viongozi wa siasa, Kamishna wa Maadili ndiye mkuu wa idara hii na pia ndiye Ofisa Maduhuli ( Accounting Officer).
Jaji mstaafu Ihema aliteuliwa Oktoba 2005 na Rais mstaafu Benjamin Mkapa kuwa Kamishna wa Maadili, hatujui ni vigezo gani vilitumika kwa kuwa hata majaji wenzake na wanasheria wengine walishangazwa sana na uteuzi wake kwa namna walivyomjua kwa kukosa uadilifu
.. na kiburi dhidi ya Jaji Mkuu Samatta, ambaye alishawahi kumuonya dhidi ya tabia yake ya kutoamua kesi kwa muda unaostahili.
Na alipoomba kuongezewa mkataba Mahakama Kuu baada ya kustaafu ujaji, Jaji Mkuu mstaafu Samatta, alitishia kujiuzulu iwapo angepewa mkataba wa kuendelea na kazi ya ujaji, hii yote inaonyesha ni aina gani ya kiongozi tuliyenaye hapa Sekretarieti ya Maadili, inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Wafanyakazi hao wanamtuhumu Jaji Ihema kwa kukiuka taratibu za fedha kwa kuhodhi madaraka ya kupanga bajeti ya chombo na kutumia fedha anavyotaka, jambo ambalo limeondoa morali ya kazi ya watumishi walio chini yake.
Wanaeleza zaidi katika kile kinachoonyesha kuwa mkakati wake wa kujijengea wigo wa kutoingiliwa na mtu yeyote katika maamuzi yake, alimteua mmoja wa watumishi wa tume hiyo (jina tunalo), kuwa mhasibu mkuu, lakini wafanyakazi hao wanadai kuwa mteule huyo hana sifa za kushika wadhifa huo.
Watumishi tumekuwa tukiambiwa ofisi haina fedha, lakini inapotokea safari inayomhusu Ihema au mhasibu mkuu, fedha zinapatikana mara moja, inaeleza zaidi barua hiyo.
Wafanyakazi hao katika barua yao, pia wanamtuhumu bosi wao huyo kwa kushirikiana na mhasibu mkuu kukandamiza haki za wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kuwanyima posho za safari na kuwapunja stahili zao nyingine na kwa kutumia mwanya walionao wa kutoruhusu mtu yeyote kujua mpangilio wa bajeti ya ofisi hiyo.
Wanadai kuwa wawili hao wamefanikiwa kuandaa taarifa ya matumizi ya tume isiyo ya kweli na kuiwasilisha kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali, aliyetoa hati safi wakati fedha nyingi zinafujwa.
Walipendekeza serikali kuepuka kuteua watu waliostaafu utumishi wa umma kuongoza idara nyeti za umma kwa sababu mara nyingi wateule hao hujali zaidi masilahi yao kuliko kuutumikia umma.
Katika mapendekezo mengine, walimtaka Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kumuamuru Ihema afuate maelekezo ya Wizara ya Fedha ya kugawanya bajeti kwa mujibu wa vitengo vilivyoidhinishwa, na wakuu wa idara husika wasimamie wenyewe mafungu yao bila kushinikizwa naye.
Aidha, walipendekeza kuwa, kiundwe cheo cha Mkurugenzi Mkuu wa Sekretarieti, mwenye taaluma ya uongozi atakayekuwa Ofisa Maduhuli, ili kuinusuru tume na ubadhirifu unaofanyika sasa.
Pia walipendekeza kuwa katika mchakato wa kurekebisha sheria, kuwepo muundo wa utumishi maalumu kwa watumishi wa sekretarieti, kwa vile mbali na kazi ya kutunza daftari la mali na madeni ya viongozi wa umma, wana dhima nzito ya kuchunguza uvunjifu wa maadili kwa viongozi tangu ngazi ya rais hadi wakurugenzi.
Jitihada za Tanzania Daima Jumapili kumpata Jaji Ihema kuzungumzia madai hayo ya wafanyakazi, kwa muda wa wiki mbili hazikuweza kufanikiwa, ambapo kila mara katibu muhtasi wake alidai kuwa bosi wake ana kazi nyingi, licha ya ahadi kadhaa zilizotolewa na katibu wake huyo kuwa apewe muda wa kujiandaa kuzungumzia madai hayo.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi hakupatikana alipofuatwa ofisini kwake katikati ya wiki hii.