SoC03 Ipo siku wazazi wangu watanyanyua vichwa vyao na kutizama mbingu kwa furaha watasema "ahsante sana Mungu kwa kutupatia mtoto huyu"

Stories of Change - 2023 Competition
May 9, 2023
18
13
UTANGULIZI

Andiko hili ni maalum kwa vijana wote wapambanaji wenye ndoto ya kurejesha, amani, furaha ya familia iliyopotea, dhiaka, dharau na kulipa madeni wazazi wetu waliyokopa pindi wanatuhangaikia. Ungana nami kwa kusoma nilichokiandika ukivutiwa nacho naomba usapoti andiko hili kwa kunipigia kura.


Watoto wa kimaskini furaha yetu siyo magari ya kifahari, mapenzi na pesa za kuchezea, furaha yetu ni kurejesha amani ya familia iliyopotea, dhiaka, dharau na kulipa madeni waliyokopa wazazi wetu pindi wanatuhangaikia. Asilimia kubwa ya vijana wengi tunatoka kwenye familia maskini zenye makazi yaliyochakaa, huku vifuani mwetu tumebeba majonzi na huzuni, tunapambana sio kwa lengo la kujionyesha kwa watu wala hatupo kwa kushindana na watu bali nia yetu ni kutaka kubadili ile hali iliyopo katika familia zetu. Hadithi za maisha yetu zimejaa majonzi, huzuni, taabu na shida lakini tofauti na hayo bado mioyo yetu imejaa shauku ya kuzitimiza ndoto zetu ili tuje tuwafariji wanaotutegemea. Sisi wengine watoto wa kimaskini tu tumezaliwa kwenye shida, tumekulia kwenye shida, na shida ndio zimetukomaza hivyo msituombee tufeli walio nyuma yetu wanatutegemea sisi.

Mara nyingi ndoto ya kila mzazi ni kumuona mwanae akifanikiwa na kuishi maisha ya furaha hivyo hufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba watoto wanakuwa katika malezi na maadili yanastahili. Hivyo wazazi huwapa nasaha au mafundisho ya kukabiliana na changamoto pindi wanapokuwa wanapambana kurejesha thamani ya familia zao ili isije tokea wanavunja miiko na maadili na mwisho wa siku kutumbukia katika maadili yasiyostahili na kuishia jela.

Yafuatayo ni baadhi ya mafundisho/ nasaha ambazo sisi kama vijana yatupasa kuziweka akilini tukiwa katika harakati za kujiinua kimaisha Ambazo wazazi wetu hutuhusia mara kwa mara.

Tupambane sana na maisha ili tukifika ukubwani tusije kuleta ushauri kwenye kikao kinachohitaji hela; Ni kweli ya kwamba tunda lililoiva hudondoka lenyewe lakini haliwezi kukudondokea mdomoni inatubidi kuamka, riziki haiji miguuni kwetu yatupasa kujishughulisha kwa kufanya kazi ambazo zitatuingiza kipato kupitia kufanya shughuli Mbali mbali za ujasiriamali, tuamke tusitegemee tu kazi za kuajiriwa maana zina changamoto nyingi kwa hali ilivyo sasa.

Siku zote moyo imara huwa na makovu mengi; vijana wengi tunapoanza safari ya kujitafutia riziki kuna mengi huwa tunayaona na kuyasikia ila tunafundishwa kuyaacha yavume kama upepo kwakuwa harakati za mpambanaji inabidi kukomaa kwakuwa tulizaliwa ili tushinde. Hatutakiwi kuhofu ni kipi watu wanachokisema nyuma ya migongo yetu maana Mungu anaenda kutubariki mbele ya a nyuso zao . Hivyo yatupasa kuishi kama bahari ambayo hupokea kila aina ya uchafu lakini hukaa ikiwa safi. Hatua ndogo ndogo tunazopiga kila siku ndizo zitakazozaa na kutuletea matokeo makubwa kwenye maisha yako tuendelee kuamini kwa kile tunachokifanya.

Kama familia yako inakutegemea basi acha kushindana na wanaotegemea familia zao.; Furaha ya kweli katika maisha hupatikana pale tu unapoacha kujilinganisha na wengine na kuthamini baraka ulizopewa. Sisi kama vijana tusikubali kuishi maisha ambayo siyo yetu ili tu kuendana na wanaotuzunguka tutaumia maana mafanikio siyo mashindano twende na mwendo wetu Mungu humpa kila mtu kwa wakati wake. Hatuna budi kukumbuka kwamba marafiki wapo na watapita ila hali ya nyumbani kwetu itaendelea kudumu endapo tukijifanya tumesahau tulipotoka sababu ya hao marafiki. Mfano mzuri ni wanachuo ambao asilimia kubwa huishi maisha ya kuigiza ili kuendana na marafiki zao huko chuoni wakati wametokea katika familia maskini. Tuepukane na tatizo hili.

Tusiwasahau wale wote ambao walitusaidia hata kabla hatujawa omba msaada; hata tufanikiwe kiasi gani kamwe tusiwasahau wale watu waliotupa thamani kabla ya kufanikiwa kwetu. Mfano mara nyingi wale tuwaombao msaada wanaweza kukusaidia halafu wanakuchokoza makusudi ili ukinena vibaya waseme huna fadhila . Vijana wenzangu katika harakati zetu za upambanaji wa kimaisha tujitahidi sana hatuwasahau wote waliotupa msaada kwenye shida kipindi ambacho kila tuliyemuomba msaada aliishia kukupa visingizio.
Sura nzuri huzeeka, mwili shupavu utachoka pia lakini roho nzuri itabaki milele tusichoke kutenda wema; Kuna siku miaka yetu tuliyowahi kuishi na kila kitu tulichowahi kukifanya kitaandikwa kwenye kipande kidogo cha karatasi na kitasomwa kama historia mbele ya umati wa watu kwa dakika zisizopungua tano hivyo tujiepushe na majivuno, kiburi, dharau na tuishi kwa upendo na tumche Mungu sana. Mikono inayosaidia wafu ni mitakatifu kuliko midomo inayosali kama wazungu wasemavyo " the strongest people make time to help others even if they are struggling with their own problems"

HITIMISHO
Tulipokuwa watoto tulifanya kazi kwa juhudi huku wazazi wetu wakiwa wanatupa ahadi kubwa kama tutaimaliza kazi basi siku hiyo tutakula WALI, lengo lao halikuwa sisi tule wali lengo lao lilikuwa ni kutujenga kiakili na kimwili kuwa bila juhudi na kujituma maisha mazuri kwetu itabaki kuwa ndoto. Pia sio wazazi pekee yao hujitoa sadaka kwa ajili ya kutimiza ndoto za watoto wao, kuna watoto pia hujitoa sadaka ili watimize ndoto zao kwa ajili ya maisha ya wazazi wao. Heshima ziende kwako, kwa wewe unayepambana kwa ajili ya wazazi wako Mungu akubariki.


Ahsanteni 🙏
 
Back
Top Bottom