JPM, Chuma, Jiwe Kwelikweli. Hivyo ndivyo alivyopenda kujiita. Kuna wakati alilala juu ya mawe kuthibitisha kuwa ni kweli yeye ni JIWE KWELIKWELI. Hatupo naye tena.
Katika Uchaguzi wa mwaka jana alitumia mbinu zote kuhakikisha anarudi madarakani kwa kura za kutosha ambazo ni zaidi ya asilimia 80+. Aliiba kura akisadiana na wasaidizi wake husani Tume ya Uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama na baadhi ya makada wa CCM. Kuna watu walikufa, walipigwa risasi, kuna watu ni vilema hadi leo ili tu mwamba aingie madarakani.
Wabunge zaidi ya asilimia 90 ni wana CCM. Baada tu ya kuapishwa wabunge hawa, Wabunge wengi wa CCM walianza kumpigia chepuo kuwa wabadilishe katiba ili aendelee kutawala kwa kile walicho kieleza kuwa amefanya mambo mengi na makubwa. Wengine wakasema ulikuwa ni mwanzo tu wa kubadilisha katiba ili atawale milele.
Lahaula, Mungu wetu hapangiwi. Damu zilizo mwagika hulia, na Mungu hujibu kwa wakati.
Katika utawala wake wateule wake walitishia watu risasi mchana kweupe, wengine walivamia vituo vya runinga na bunduki huku rais akiwaambia majangili hao wachape kazi na WASITISHWE.
Watu hatukuruhusiwa kuzungumza na kumkosoa mkuu, waliojaribu kuwa wakaidi watekwa na kupotezwa, miili kadhaa iliokotwa kwenye sandarusi jirani na Coco Beach, Simon Kanguye, Ben Sanane hawajulikani waliopo. Rais hakujali hata kidogo. Vyombo vya habari viliambiwa na mwamba visidhani vina fridomu ya namna hiyo, VIKAUFYATA MKIA.
Mitandao ya kijamii nayo ikapigwa pingu kwa kutungiwa sheria za makosa ya mitandaoni. Hata tulipojua mkuu anaumwa na kujaribu kusema kupitia mitandaoni ya kijamii, tuliambulia kuambiwa kuwa ni uzushi na tunahatarisha amani. Wengi wapo Korokoroni hadi sasa kwa kosa la kumuulizia rais Magufuli na kuandika kuwa huenda alikuwa anaumwa.
Tuseme nini basi?? Tumshukuru Mungu wa Mbinguni na tusherekee maisha yake hapa duniani huku tukiyasema mema aliyo lifanyia taifa hili na tukisema kwa nguvu zote mabaya yote aliyotutendea ili waliopo madarakani wasije kurudia tena mabaya aliyo yafanya.
Ameandika Kumbusho Dawson