Ipi faida yangu, mbona siioni?

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,891
IPI FAIDA YANGU, MBONA SIIONI?

Na, Robert Heriel

Nipo nipo, sina hili wa lile, sina lila wala fila. Sina mbele wala nyuma. Nimekuwa mtu wa hivi hivi, Loooh!

Niite Taikon wa Fasihi, nisiye na faida.

Hata nyanya linatumika kwenye kachumbari, tena ni kiungo kizuri cha mboga. Tena lafaa kwa kula kama tunda. Je, mimi, nini faida yangu?

Hata panya anafaida, waulize wauza sumu za panya watakuambia faida ya uwepo wa panya, kama hukuwaona hao wauzaji basi mfuate Paka, yeye atakuambia faida za panya. Je mimi, nina faida gani?

Labda ningesema mimi ni kijana mwenye nguvu, hiyo ingefaa nini ikiwa sina pakuzitumia nguvu zangu, Kutwa kucha nakaa vijiweni, ati vijibweni, huko vilingeni nikipiga soga mchana kutwa, stori za town za udaku ati najadili kwa ubishi unaoishi pasipo kuisha leo mpaka mtondogoo. Je hiyo ndio faida yangu, kujadili watu huko vijiweni?

Huenda ningetumia nguvu zangu kulima ningepata mazao na kuuza, thubutuu! Nilime? Labda sio mimi Shalobaro wa kitaa, kutwa kutembea na gitaa, ati mwanasanaa ninayeng'aa kama taa. Sababu za kutokulima siwezi kukosa; sina dhana za kilimo, Pili, sina shamba wala kiamba, tena hata ujitolee kunipa dhana na shamba bado nitakuambia soko linasumbua. Ati nilime mimi alafu upange bei wewe. Pengine nilijionea faida ya kutokulima pale nilipoona wakulima wakilima alafu wakakosa soko la kuuzia mazao yao. Bado nilime? Kumbe faida yangu ni ipi sasa, huenda ndio hiyo.

Ningekuwa na akili zenye manufaa ningeiona faida yangu, au pengine watu wengine wangesema ipi faida yangu. Lakini akili yenyewe sina, Elimu nilizosoma ni kama nimezipatia faida zoo, wala sio kunipa faida mimi. Kumbe shahada niliyonayo ingetumika kuisaidia jamii yangu masikini, ningeielimisha na kuifunza, ningeihamasisha na kuihamisha kutoka gizani kwenda nuruni. Lakini sipo hivyo. Mimi ndio naitegemea jamii yangu badala yoo ndio initegemee. Jamii ndio inanifunza wakati mimi ndiye nilipaswa niifunze kwani mimi ndiye mwenye elimu kubwa, tena nilisomeshwa kwa gharama kubwa sana. Je, nini faida yangu?

Nisingesahau mchango wangu niwapo kijiweni, huenda hiyo ndio faida yangu niwapo duniani. Nategemewa kwa stori kali za ngono, stori za matusi, yaani kujadili wanawake wazuri wenye makalio, mahipsi na mapaja makubwa, kazi hiyo ninaimudu, usiniulize ninapata faida gani. Stori hizo ninavyojadili ungesema nimesomea mambo hayo. Rafiki zangu wao hujichapuza na kunipa stori za udaku, wasanii na wachezaji wa mpira. Sijui nani kafanya nini, nani analelewa, nani...;..;nani.....nani isiyoisha. Stori kama Isidingo, jua lichweapo ndipo episode inaishia hapo muendelezo wake ni pale jua lichomozapo asubuhi, hapo tutakutana tena kijiweni. Looh! Ipi faida yangu?

Ati huenda mimi ni kijana mwenye mvuto kwa wanawake, hilo ningejivunia mno, tena ni jambo linalotamanika kwa wanaume wengi hasa vijana. Kupendwa na wanawake ni jambo kubwa mno duniani, huenda ni tunu kutoka kwa Mungu. Lakini licha ya kupendwa na Dada zangu hao, je faida yake ni ipi? Maana sitaki kuwahadithia yaliyonikuta zamani na hivi majuzi. Hesabu ya wanawake niliowatia mimba ni kubwa mno. Hiyo inaweza kuwa sifa endapo ningezikubali mimba hizo, lakini sio mimi Taikon, Hakuna mimba niliyoikubali hata moja, Hivi majuzi alimanusura nihamishiwe mimba ya mgongo na Mzee Ngonyani. Ni bahati tuu, niishie kusema ni bahati hata kama unatamani kujua kilichotokea.

Juzi tu nimekoswa koswa kutupwa korokoroni baada ya kumpa mwanafunzi mimba, ati mimba ya mwanafunzi Looh! Taikon nina hatari kubwa. Kumpa mwanafunzi mimba ati ni kama kuipa mimba serikali, hivi utaweza matunzo ya kuilea mimba ya serikali ambayo mpaka serikali ijifungue ni miaka thelasini. Looh! Kazi yangu kuharibu watoto wa watu mtaani. Kila atakayesimamisha maziwa ninanaye, atakayeyashusha naachana naye, ili mradi tuu. Lakini watu wamejigeuza manabii ati wananitabiria kuwa ipo siku nitafungwa miaka thelasini kwa kutembea na wanafunzi. Nami nawaambia kuwa hizi ni siku za mwisho hivyo manabii wauongo watatokea, na ndio wao wanaotabiri unabii wa uongo. Loooh!

Ipi faida yangu? labda wewe msomaji utaweza kuijua.

Ninavyopendeza lazima unihofie kama hukupata kunijua, wengi huniita Afisa mwandamizi, wengine huniita Usalama wa Taifa, labda ni hivi ninavyochomekea kama mwalimu wa kwaya, suruali yangu ya kadeti, nikiitinga na shati kali mbona lazima unisalimie. Mwendo wangu wa Kidiplomasia wengi unawatetemesha. Basi minong'ono hutokea pale nipitapo, utasikia kijana wa Magufuli huyo, Hahaha! sipendi nikueleze ninavyojisikia pale nikisikia maneno yao. Kwanza nafurahi mno, lakini ambalo ungelipenda ni vile nitakavyoongeza madoido ya kutembea. Ingawaje ungesikitika kusikia kazi yangu ni kubet, nabet mipira ya wazungu huko, kisha nabet pia kwenye mabasi ya mikoani kuwa lipi litakuwa la kwanza kufika stand, tunaiita Gamelanda. Je, ipi faida yangu ikiwa nabetia mpaka uhai wa abiria?

Siasa siasani, michezo michafu isiyokifani. Nisingependa kuongea habari za propaganda za Kifo cha mkulu, ati moshi wa Ruangwa uliotiwa chumvi na wajameni wa fix. Ati uchawi ulimpiga Mkulu, ati wazee wa Ruangwa wamoto Looh! Michezo ya Siasa bhana. Uongo uongo tuu! Pengine faida yangu ni ile ya kuikosoa serikali, au labda kuisifia. Lakini ni faida ipi hasa?

Mimi ni Kibenten, kiswaswadu, almaarufu kama Smart kitochi, nalelewa na majimama kama mtoto. Ati huo ndio ujanja. Wamama wananikimbilia mithili ya mafuta ya upako. Nami nachekelea mithili ya mchungaji niliyeona sadaka za waumini. Nadekezwa na kupumbazwa, nakula bila kusaza. Maisha ni bure kwani sina ninacholipia. Huenda ningelipia chochote ningeona faida yangu, lakini ikiwa sitoi iweje nipokee?

Kama sio mbio zangu ningefanywa kitu mbaya, wake za watu wataniua jamani, nitalogwa mimi, nitafanywa kitu mbaya Taikon miye. Ile siku chamoto nilikipa, nilitolewa baru kama subaru wangu wangu nikikimbia kushikwa ugoni. Nikaapa sitorudia tena lakini ilikuwa geresha tuu, kwani nitaishije bila kitonga. Ipi faida yangu?

Hivi sasa natimiza miaka thelasini na tano, huenda nilipaswa niwahudumie wazazi wangu, niwape matumizi, lakini sijawahi kupeleka kwa mama hata kitenge achilia mbali elfu tano kama sehemu ya kijana anayejitambua. Walahi naapa, sijawahi kuepeleka. Bado unione nina faida, faida ipi hiyo?

Pengine kama kijana mwenye nguvu ningepaswa kutumia nguvu zangu kuhakikisha naijenga nchi yangu, lakini hata kuishauri siwezi, kuikosoa siwezi, kupinga maovu siwezi, hakuna ninaloweza mimi jamani. Yaani ni aibu mpaka aibu yenyewe haitoshi. Ipi faida yangu?

Labda wewe msomaji uniambie ni ipi faida yangu?

Taikon nimemaliza, leo sitaki maswali.

Robert Heriel

Taikon wa Fasihi

0693322300
 
Kweli huna faida yeyote

Bora ungezaliwa ng'ombe, ndugu zako wangekunywa maziwa na ungezaa ndama wengi na kipato cha familia kingeongezeka.

Ni hatari kwa taifa kama utaendeleza kizazi chako.
😃
Jamani
 
Ndugu mwandishi sijui kama umekosea au umeandika mskusudikale....ni ZANA sio DHANA
 
Back
Top Bottom