Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,762
- 40,985

Hatimaye mchawi wa Richmond ni yule ambaye watu walimhisi kwa muda mrefu. Na sasa tumegundua hakuwa peke yake. Taarifa ya leo ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa mwishoni mwa mwaka jana kuchunguza mkataba wa Richmond imeonesha kuwa siyo tu taratibu zilikiukwa bali pia kuna ushahidi mkubwa wa rushwa.
Ripoti hiyo ambayo unaweza kuipata kwenye tovuti ya http://www.klhnews.com inaonesha wazi kuwa mhusika mkubwa wa sakata hili zima ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa vile bwana Lowassa aliapa kuilinda na kuitetea Katiba yetu na kwa vitendo vyake ameshindwa kufanya hivyo hana budi kuwa wa kwanza kuwajibika yeye mwenyewe bila ya kungojea kuwajibishwa. Mhe. Lowassa kwa hili umekosea na liwe somo kwa viongozi wengine wote kuwa Tanzania inabadilika na viongozi wasioongoza hawana budi kuwekwa pembeni. Mhe. Lowassa tunataka ujiuzulu wadhifa wako mara moja.
Pamoja na wewe wahusika wengine wote ambao wanatajwa katika ripoti hiyo akiwemo Waziri Msabaha, Karamagi, Rostam Aziz na Mwanyika nao pia wajiuzulu mara moja kwa kutumia madaraka yao vibaya, kulidanganya Taifa, kufanya kazi kinyume na maadili, na kwa kuliletea Taifa letu hasara.
Watanzania wana mambo mengine ya msingi ya kufuatilia (kama BoT na mengine) na wakati umefika suala la Richmond lifikie kikomo kwa viongozi na wahusika wote kujiuzulu. Tulishasema toka awali kuwa Baraza hili la mawaziri ni la kishikaji na ambalo limemwangusha sana Rais na kwa hakika ni kujiangusha alikojitakia kwani alishaonywa, halina budi kuvunjwa ili Baraza jipya litakalokidhi hamu na matamanio ya Watanzania na ambalo wajumbe wake watatoka hata nje ya CCM liundwe ili tuendelee na jitihada za kulijenga Taifa letu
Watanzania naomba kutoa hoja!