Ikulu, Dar: Rais Samia aongea na viongozi wa Machinga Dar es Salaam. Machinga Watambuliwa kama kundi Maalum

Replica

JF-Expert Member
Aug 28, 2017
1,447
7,825
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu leo aanaongea na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wa wamachinga Ikulu ya Dar es Saam.

Kumekuwa na badiliko la sera ya wamachinga karibuni kutoka utawala uliopita kwa 'kupangwa upya' ama kwa wengine kuondolewa na vibanda vyao kuvunjwa. Pia majanga ya moto hayako nyuma

Nini kitajiri! Kuwa nami.


========




AMOS MAKALLA, RC DAR-ES-SALAAM
Mafanikio tulioyapata tutayalinda. Na katika kuyalinda tumekuja na kampeni ya usafi. Usafi ni sehemu ya kulinda mafanikio ya kutokufanya biashara holela. Dar es Salaam itaendelea kupendeza na yenye mazingira mazuri ya watu kufanya biashara katika mpango mzuri kama ambavyo tumepangana sasa.

STEVEN LUSINDE, MAKAMU MWENYEKITI MACHINGA TAIFA
Kwenye hotuba yako Mh. Rais uliagiza Wamachinga tupangwe vizuri. Jambo lile lilitupeleka mchakamchaka kidogo. Sasa tumepangana vizuri na mambo yamekwenda kama tulivyotarajia.

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN
Nimeamua kukutana nanyi wa Dar es Salaam lakini haimaanishi sitakutana na wengine. Dar es Salaam inaleta mkusanyiko wa watu wote na meseji ikitoka Dar itawafikia na wengine.

Dar es Salaam mmeonesha mfano wakati wa kupangana. Kuna watu walikuwa wanasubiri vurugu zitokee nchi iharibike lakini mmekuwa waungwana, mmekuwa wazalendo. Mmeshirikiana na viongozi wa serikali na hayo hayakutokea.

Niwape pole kwa mioto inayotokea ndani ya mkoa wetu wa Dar. Tulishuhudia moto pale Kariakoo na hivi majuzi pale Karume. Na mioto hii ina sababu mbalimbali.

Ni matumaini yangu mbele tuendako tutakaa kitako. Timu za serikali na zinafanya uchunguzi wa sababu za mioto. Lakini uongozi wa achinga na masoko utakaa kitako kuona sababu ni zipi na tuweze kuzichukulia hatua.

Niwape pole kwa yale yote yanayotokea. Serikali ipo pamoja nanyi katika hili.

Machinga kama kundi maalum
Nataka niwaambie kuwa hili kundi lenu serikali inawatambua vyema. Katika mipango yetu yote ya Serikali, mpango wetu wa miaka 5 uliomalizika, mpango wa pili na huu tunaokwenda nao na wanne tutakaotunga, mtazamo wetu mkubwa ni kwa vijana. Watanzania asilimia 65 kama siyo 70 ni vijana. Na vijana hawa lazima wawe na ajira, wawe na kazi.

Kwa Serikali peke yetu si kweli kwamba tutaweza kutoa ajira kwa vijana wote. Mlilolifanya kujiajiri wenyewe katika biashara, mkaunda umoja wen una mkajipanga vyema, hii itatusaidia sana Serikali kulihudumia kundi hili na kuhakikisha ajira zao zinaendelea kuwepo.

Sasa ni rasmi Serikali inalitambua kundi hili kwamba ni moja ya makundi katika yale makundi maalum yali katika wizara wizara maalum tuliyounda. Ni moja kati ya makundi maalum yatakayofanya kazi na serikali.

'Tulipangana' ili kupunguza uhalifu Kariakoo
Tuliamua kupangana kwakuwa hata nyie hali mliiona. Ilikuwa Kariakoo huna pa kupita. Wale vijana waovu walitumia fursa ile ya kuchanganyika kule ili kufanya uovu. Mitaani wakasema, wamachinga wezi, wamachinga majambazi, wamachinga wanatukupua kumbe siyo wamachinga ni vijana waovu waliotumia fursa ile.

Lengo letu ni kuendeleza sekta binafsi na kundi lenu ni sekta binafsi. Na katika maeneo kadhaa nilikuwa naongea, kwamba lengo letu ni kuwafanya wamachinga wakae mahali pazuri wafanye biashara vizuri ili wahitimu waingie kwenye kundi la wafanyabiashara ili tutanue wigo wa kulipa kodi.

Ndiyo tumepangana lakini wengine wamekosa maeneo. Hilo tunalitambua. Ndiyo maana juzi niliongea na mkuu wa mkoa nikamwambia akaweke mambo sawa Karume lakini acha wamachinga warudi haraka Karume.

Kariakoo itabeba watu 4000
Kwa sasa nimetoa fedha nyingi kidogo kwa ajili ya Kariakoo. Kariakoo imeanza na tutaijenga nadhani kwa miezi 18. Baada ya hapo wale walioondoshwa Kariakoo tutawarudisha na wengine wataingia. Kariakoo ilikuwa inabeba watu kama 2500 lakini tukimaliza itabeba watu kama 4000.

Masoko mengine kujengwa
Hatua ya pili nimemwambia mkuu wa mkoa twende tukajenge Jangwani. Na fedha za kujenga Jangwani zipo. Nimemwambia mkuu wa mkoa aanze kutafuta mkandarasi kwa ramani ambayo mtakubaliana.

Baada ya Jangwani, sasa tutahamia Karume. Lazima katikati ya mji kuwe na masoko yale yanayotakiwa na yenye miundominu yote yatakayofanya kazi usiku na mchana.

Tunajitahidi kutafuta maeneo mengine ya wazi ili tuweke masoko. Tutaweka masoko ili watu wa pembezoni waweze kutumia na yote yatakuwa masoko ya hadhi ya juu.

Ukosefu wa mitaji
Makamu mwenyekiti alikuwa na uhakika kabisa kuwa katika pesa za Uviko-19 Kuna bilioni 5 zetu. Nitakaa na TAMISEMI nijue wamepanga zitumikaje. Katika bilioni 5 zitatoka pesa kwaajili ya SACCOS yenu.

Kwakuwa kuna kanzidata kutakuwa na mafunzo kwanza ili kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuiendesha na fedha zinazoingia zitumike vipi.

Ili kutatua changamoto ya mitaji kwa Machinga, Pia Rais Samia Suluhu ameelekeza halmashauri kutenga 10% ya mapato kusaidia kundi hilo. Pia ameagiza kwenye bajeti za halmashauri zitenge fungu litakaloboresha maeneo ya biashara za Machinga ikiwemo kuweka vyoo, barabara, maji na umeme.

Mabenki na programu maalum za kusaidia wanawake/ vijana
Nimeyaelekeza mabenki yaje na programu maalum zitakazosaidia aidha wanawake au vijana, baadhi yameanza kunipa mrejesho wa programu. Kupitia programu hizo makundi ya Machinga katika madaraja yao tutaangalia mtakavyokopa kwenye mabenki kwa njia nafuu sana.
 
Mama tafadhali usije kuingia ubaridi ukaruhusu hawa watu wajae mabarabarani tena kwa kipigiwa makofi. Tafadhali sana mama soma hii msg. Hawa jamaa wameshajipanga vizuri wanaendelea
 
Asipowaambia "..tumewavumilia sana, and now enough is enough, mnatakiwa kuhama pale Mchikichini kwa sababu tunataka kuweka mwekezaji anayelipa kodi" basi atakuwa anawadanganya, na kwahiyo kikao kizima kitakuwa ni matumizi mabaya ya muda na pesa za serikali.
 
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu leo aanaongea na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wa wamachinga Ikulu ya Dar es Saam...
Asante,Rais wetu,kipenzi cha wananchi,raia wanakupenda.Rais msikivu,na wakututatulia shida zetu.Mungu atakulipa mema.
 
Sioni kama ni kosa kwa Rais kukaa chini na machinga kama jamii yenye watu wengi....Lengo ni kujadili na kusikia kero zao kutoka kwenye ground then waone namna bora ya kutatua..
 
Back
Top Bottom