Huyu ndie Ally Bin Jahadhamiy,muite Basha Ally

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,136
4,298
ALLY BIN SAID BIN RAASHIDI JAHADHAMIY

Ushairi katika Afrika ya mashariki umekua na historia ndefu,historia ambayo ipo inayo julikana wengi na zipo ambazo zinajulikana na watu wachache mno,na nyingine zikiwa zimepotea na kutoweka bila ya kuandikwa wala kuwekewa kumbumbuku zozote,historia zilizotoweka zinajumuisha wale waliofariki bila ya kumbukumbu zao kuandikwa katika vitabu na historia zao,kumbukumbu hizo zinajumuisha na mashairi na kazi mbalimbali za watunzi hao ambazo zimetoweka na kupotea.

Matukio ya kupotea kwa kazi nyingi za washairi yanasababishwa na mambo mengi,wapo baadhi yao ambao wapo hadi leo lakini kazi zao zilitoweka miaka mingi iliyopita,mshairi kama Audax Kahendaguza,mshairi msomi na mwanasheria aleiwahi kukiri katika kitabu chake kimoja cha CHOPIKWA KIKAPIKIKA kuwa shairi lake la NAZITAKA MBIZI HIZI lilipotea katika ajali ya Mv Bukoba pamoja na mashairi yake mengine.

Abdurahaman Saggaf katika kitabu chake cha kale ya washairi wa Pemba anaeleza kidogo kuhusu upotevu wa mashairi mengi ya wasahiri wa Pemba yalopotea wakati wa mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 kutokana na kuchomwa moto,mashairi mengi ya zamani ya zamani yalipotea kwa sababu njia za utunzaji wa kumbukumbu zilitaku ni kutunzwa katika makaratasi lakini kwa nyakati hizi za miaka hii ya 2000 utunzwaji wa kumbukumbu kidogo umekua imara ingawa bado si wa kuamini kwa asilimia mia moja kuwa kazi zako zinaweza kuhifadhika moja kwa moja na kuwa salama.

Upotevu wa kazi nyingi za washairi wakati mwingine umekuwa ukisababishwa na baadhi ya waandaji wa tuzo za kazi fasihi ambao wamekua wanapokea mashairi ya watu na kubaki nayo bila ya kuyarudisha kwa wenyewe na hili liliwahi kutokea hata kwa mshairi nguli wa Tanzania Shaaban Bin Robert ambae alituma kazi zake kwa waandaji wa tuzo za ushairi na wakatoweka nazo hadi leo hazijulikani zilipofichwa.

Ally Bin Raashid aliwazaliwa katika mwaka wa 1830 katika eneo la Bogowa nakufariki mwaka 1910 akiwa na umri wa miaka themanini.

Ally Bin Raashid alitokana na ukoo maarufu na mkubwa kipindi kile,ukoo wa Jahadhamiy,ukoo ambao ulikuwa mkubwa katika nchi ya Oman na baadae katika pwani ya Afrika ya mashariki.

Alikuwa ni mmoja wa washairi waliovuma sana katika Afrika ya mashariki kwa kipindi hicho kutokana na aina ya mashairi yake alopendelea kutunga huku wakati mwingine akionekana kutungiana mashairi na rafiki yake mkubwa aliejulikana kwa jina la Sarahan Bin Matwar.

Jina lake la kishairi alikuwa akijulikana kama Kamange lakini katika kipindi cha ujana wake alikuwa akijulikana kama Basha ally,jina linalotoka na lugha ya kituruki na alipewa jina hili kutokana na tabia yake ya kuonyesha ukubwa,hakika alikuwa ni mtu imara mwenye uwezo kujibizana yeyote katika serikali ya wakati huo.

Katika tabia yake hiyo ya kuonyesha ukubwa,siku moja alijikuta akikamatwa kwa kosa la kutembea usiku,kwa wakati huo serikali ilokuwepo ilipiga marufuku ya watu kutembea usiku lakini kamange alikaidi amri hiyo na kutembea ndipo alipotiwa nguvuni lakini kwa bahati adhabu haikuweza kumfika kwa sababu aliombewa msamaha na Kapteni mmoja aliekuwa mkubwa wa pemba.

Baada ya kukamatwa na kuachiwa huru ,rafiki yake mkubwa katika sanaa ya ushairi Sarahani alimtungia shairi akisema:

Nimesikia khabari, sana kachukiwa sana
Wala hiyo si fakhari, shekhe Ally si maana
Hapendi mtakabari, inna Llah Subhana
Laa yuhibu man kaana, mukhtaaran fakhura.

Mimi sikubebeuwa, kwani hatujapambana
Wa imam ni kusifiwa, haijuzu kujinena
Wenzio kujitefuwa, faraghani kuwalana
Laa yuhibu man kaana, mukhtaaran fakhura.

Si wajibu si jaiza, mustahila si sunna
Nakukataza aziza, sijione u jununa
Ya takhili hutoweza, wacha basha kushindana
Laa yuhibu man kaana, mukhtaaran fakhura.

Kamange alikuwa akijishughulisha sana na kilimo katika maisha yeke,huku akilima mashamba ya minazi na karafuu ambayo kwa wakati huo ilikuwa ni sehemu ya mazao yenye faida na thamani kubwa.

Baada ya kifo chake mwaka 1910,washairi wengi walimlilia machozi na kumuandikia mashairi ya kumkumbuka,baadhi ya washairi walomlilia ni Hamad Bin Khatoro,alietunga shairi liitwalo KAMANGE KENDA KAPUTI,kwa ufupi alisema:

Inna lillahi muswiba, nawaarifu umati
Basha kenda ughaiba, yamemkumba mauti
Umefika mkataba, kaja Hadimu ladhati
Kamange kenda kaputi, masikini Basha Ali.

Basha Ali alivuma, mshindo kama rakiti
Ali mwingi wa hekima, kwa suudi na bahati
Mwema mno wa kusema, hata katika korti
Kamange kenda kaputi, masikini Basha Ali.

Mshairi mwingine kati ya wengi alie mlilia Kamange ni Muhhamady Bin Juma Kharusi,ambaena yeye aliandika haya:

Hakuna atayedumu, Rabi asiyemuuwa
Hatapatabaki isimu, La ilaha illa huwa
Ndiye hayul Qayyumu, mwingine hata huiwa
Haachi huzunikiwa, mtu kwa mpenzi wake.

Kweli tumeitabiri, Kamange kaghasimiwa
Dunia kuihajiri, nyote mumefurahiwa
Bure kumwita jabari, kipi alichotembuwa
Haachi huzunikiwa, mtu kwa mpenzi wake.

REJEA-KALE YA WASHAIRI WA PEMBA,2011.

MAISHA YANGU BAADA YA MIAKA HAMSINI,SHAABAN ROBERT

CHOPIKWA KIKAPIKIA,AUDAX KAGENDAGUZA

Idd Ninga
Tengeru,Arusha
+255624010160
iddyallyninga@gmail.com
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom