SEHEMU YA 64
Bibi Nyanjige akaingilia kati akimwita Mkuu yule ambaye alielekea kuingia kwenye mtego wa bibi Nyanjige kwa kupandwa na jazba.
“We mwanamke!! Unamfokea mwenzako wakati nimeshakupa ruhusa ya kuniua na ...” Kabla hajaongeza neno zaidi, Msaidizi wa Mkuu wa Majeshi akatupa teke zito, likampata chini ya kidevu.
Bibi Nyanjige akatoa mguno mkubwa wa maumivu. Akajinyonganyoga pale sakafuni huku akihisi ladha yenye chumvi ya damu kutoka kinywani mwake. Akalia kwa uchungu wa maumivu yale.
Mkuu wa majeshi alimgeukia dereva. “Unaona.. Unaona?”
“Sikiliza Mkuu, huyu usimuue, hebu punguza hasira na ukumbuke maagizo tuliyopewa, kwamba tumfikishe huyu akiwa hai mbele ya Wakuu.”
“Amenitia hasira sana, hawezi kunidharau namna hii”.
Dereva aliinama kumwangalia bibi Nyanjige kama yu hai, maana teke alilopigwa na Mkuu wake lilikuwa ni zito kiasi kwamba bibi yule alijinyonga kidogo kisha akalala kimya.
Akagundua kwamba ameumia mno. Kwa kuchanganya na majeraha mengine aliyokuwa ameyapata kutokana na kipigo cha wamasai, Bibi Nyanjige sasa alikuwa hajiwezi. Alikuwa akivuja damu na kuvimba karibu mwili mzima, hii ilimfanya aanze kufikiria upya kuhusu namna ya kumpeleka kwa Wakuu wa Majeshi.
“Mkuu, huyu ameumia sana, tufanyeje?”
“Hawezi kutembea?” Mkuu ambaye alikuwa ameegemea gari na kuangalia upande mwingine, alionekana kupunguza makali ya hasira zake.
“Nadhani, buti ulilompiga ni kubwa sana kwa mtu kama huyu, anaweza kufa kabla ya kufikishwa Makao Makuu”.
“Unafikiria nini sasa?” Sauti ya Mkuu ilishapoa.
“Huyu anahitaji matibabu, Mkuu”
“Na akifia hospitali?”
“Tusifikiri hivyo mapema, maana kama suala ni kifo anaweza kufa hata wakati tuko njiani kumpeleka Makao Makuu.”
Mkuu aliendelea kubaki nyuma ya gari huku akili yake ikifanya kazi haraka haraka juu ya nini cha kufanya.