SEHEMU YA 49...
“Hakuna sehemu yoyote anayoweza kuwa amekimbilia zaidi ya humohumo porini! Hivyo hakikisheni pori lote linazingirwa ili asipate mahali pa kutokea! Na mkimpata naomba maiti yake iletwe hapa makao makuu, tunahitaji kuikausha ili iwekwe makumbusho kwa ajili ya historia ya nchi yetu kwani mpaka sasa siamini kama kuna bibi kizee anayeweza kufanya maajabu kiasi hiki……!” Mkuu wa majeshi alimwambia msaidizi wake na kabla hajamaliza simu yake ililia.
“Hallow, nani anaongea?” Aliuliza.
“Ni mimi Brigedia Bukuku!” Alijibu Brigedia aliyekuwa akiongoza msako msituni.
“Ndiyo Brigedia mnaendeleaje?”
“Tunaendelea vizuri nilitaka tu kukutaarifu kuwa tayari ule mtambo wa kutungulia ndege tumeupata ulikuwa umefichwa kichakani kabisa!”
“Vizuri, endeleeni na kazi mpaka mmkamate huyo bibi kizee, yupo hapohapo porini!”
“Sawa afande!”
*
*
Habari za msako wa bibi Nyanjige zilishaenea kila mahali mjini na vijijini, hapakuwa na mtu asiyefahamu juu ya bibi huyo! Hata katika kijiji cha wamasai cha Kiambali ambako bibi Nyanjige aliendelea kusambuliwa kwa mawe akidhaniwa mchawi, kijana mmoja aliikumbuka sura yake na kupiga kelele akiwaomba wenzake wasitishe zoezi la kumpiga.
“Nimemkumbuka huyu bibi!” Alisema kijana huyo kwa kimasai.
“Ni nani?”
“Ni bibi Nyanjige!”
“Mama yangu nimekwisha!”Bibi Nyanjige alijisemea moyoni akiwa amelala chini damu nyingi zikimtoka katika majeraha aliyoyapata sababu ya kipigo kibaya alichopewa na wananchi wenye hasira, alijua kutambuliwa kulimaanisha kifo!
Alijua tayari alishaingia mkononi mwa wanajeshi na kwa zawadi iliyokuwa imetolewa na serikali hapakuwa na njia ya kuwshawishi wamasai wamwachie.
“Bibi Nyanjige ndiye nani?”
“Si anayetafutwa kwa mauaji!”
“Una hakika ndiye huyu?”
“Ni yeye!” Kijana huyo aliendelea kusisitiza.
“Sasa tufanye kitu gani?”
“Mimi naomba tuchague morani watatu ili twende kupeleka taarifa hizi makao makuu ya jeshi waje wamchukue!” Alisema kijana huyo na maneno hayo yalimfikia bibi Nyanjige moja kwa moja, aliomba wazee wa Kimasai wamkatalie kijana huyo lakini haikuwa hivyo, wazee wote walikubaliana na jambo hilo.