Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe, amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kimevamiwa na watu ambao wameanza kutumika kwa maslahi binafsi ya watu wachache.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kamati ndogo anayoiongoza ya kukusanya maoni na kuandaa mapendekezo ya mageuzi ndani ya umoja huo.
Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusu shutuma zilizoelekezwa kwake na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa umoja huo Mkoa wa Dar es Salaam, Augustino Matefu, kuwa yeye (Bashe) ni fisadi.
Alisema tuhuma hizo hazina msingi na ni za jumla jumla kwani Matefu hakusema ufisadi huo ni wa aina gani na umefanyika wapi.
Alisema hakuna sababu kwa viongozi wa UVCCM akiwemo Katibu Mkuu, Martin Shigela, Makamu Mwenyekiti, Beno Malisa kujiuzulu kwenye nafasi zao kama ilivyoshauriwa na Matefu.
Alisema kuna vijana ndani ya umoja huo ambao wamenunuliwa na watu fulani ambao huwatumia kwa ajili ya kampeni zao za urais wa mwaka 2015.
Bashe alisema vijana hao wamekuwa wakiandaliwa maneno ya kuzungumza na hata sehemu za kuzungumzia na waandishi wa habari, gharama ambazo kwa uwezo wao binafsi wasingemudu.
Kuhusu kuenguliwa kwake kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kutokana na tuhuma za utata wa uraia wake, Bashe alisema uraia wake hauna utata na hapendi kuzungumzia suala hilo kwa undani.