SoC01 Human Trafficking: Biashara ya Binadamu - Hali inatisha sasa! - NAFICHUA, NJOO UFICHUE

Stories of Change - 2021 Competition

Environmental Security

Senior Member
May 21, 2020
181
261
Habarini,

Leo nazungumza juu ya biashara haramu ya binadamu (human trafficking) naielezea, lengo kuu ni wote tuifahamu tujilinde na tulinde ndugu zetu. Ndio maana naomba sana kama una mchango wa mawazo, uzoefu au mifano halisi utushirikishe ili pamoja tulinde wapendwa wetu.

Human trafficking: Biashara haramu ya binadamu

Ni kitendo kinachohusisha kusajili, kuajiri, kuhifadhi, kusafirisha, kukusanya au kupata watu au mtu kwaajili ya kuwatumikisha kazi au vitendo vya biashara ya ngono, kwa kutumia nguvu, hadaa au ulaghai au mabavu.

Biashara hii katili na ya kutisha inahusisha zaidi kusafirisha wahanga toka sehemu moja kwenda nyingine, lakini sasa imebainika pia kuwa inahusisha kufichwa na kutumikishwa ndani ya mji ambao mhanga anaishi.

Aina kuu mbili za biashara hii;
1. Kutumikishwa kwa biashara ya ngono na vitendo vinginevyo vya unyanyasaji wa kingono

2. Kufanyishwa kazi kwa lazima

Matendo yanayohusika ktk biashara hii ni pamoja na;
▪ kufanyishwa kazi za ndani, mashambani, viwandani,
▪ ndoa za lazima, kufanyishwa ukahaba,
▪ kutolewa viungo vya mwili, watoto kufanywa omba omba na kutumikishwa vitani.

Sababu zinazopelekea biashara hii

Zipo sababu nyingi lakini kubwa ni UMASIKINI, japo umasikini pekee hautoshi kuwa sababu kamilifu, unahitaji sababu nyinginezo ili kupelekea hili kutokea. Sababu hizo ni Rushwa, machafuko katika taifa, serikali dhaifu-(iliyoshindwa kudhibiti nchi), watu kukosa elimu, watu kukosa ajira, kugawanyika kwa familia, kukosekana kwa haki za binadamu, hali mbaya ya uchumi wa nchi.

Wahanga wakuu wa biashara hii ni wanawake na watoto, japo biashara hii inahusisha watu wa jinsia zote na marika yote, na inakadiriwa zaidi ya theluthi mbili ya wahanga ni wanawake, pia mmoja kati ya kila wahanga watano ni mtoto.

▪ Wanawake na watoto kwa ukandamizaji wa kingono. Mfano Watoto hutumiwa ktk picha za ngono za watoto na unyanyasaji mwingine.
▪ Wanaume kwa kazi ngumu za shuruba

Pia biashara hii inahusisha kuuzwa kwa watoto wachanga

Kwanini biashara hii katili inaendelea kufanyika?

1. Ina faida kubwa mno


Biashara hii ni moja kati ya biashara haramu yenye fedha nyingi, ikichuana na biashara haramu ya silaha na ya madawa ya kuleta.

▪ Shirika la kazi duniani ILO linakadiria kuwa biashara ya kuwafanyisha watu kazi kinguvu inazalisha hadi dola bilioni mia moja na hamsini za kimarekani ($150 billion USD) Theluthi mbili ya fedha hiyo inatokana na biashara haramu ya ngono

2. Ni ngumu kutambulika

Taarifa zake ni chache na kuna mianya mingi na usiri mkubwa na mbinu hubadilika mara kwa mara

3. Adhabu zake sio kali ukilinganisha na faida

Wahanga hupatikana zaidi maeneo ya vijijini sehemu masikini
wahanga wengine ni wakimbizi kutoka katika kambi za wakimbizi, kutokana na kutoruhusiwa kufanya kazi nchi husika, mazingira mbaya sana ya makambi, huwa rahisi kuhadaika kwa ahadi ya kazi nzuri

MBINU ZINAZOTUMIKA ZAIDI KUWAPATA WAHANGA


1. Ahadi za uongo za kupatiwa kazi zinazolipa vizuri nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kutumia matangazo ya kazi mazuri ya kuhadaa. (Hapa kwetu mbinu hii hutumiwa sana)

▪ ahadi ya kupata ufadhili wa masomo na ahadi za kulipiwa gharama za usafiri ili kwenda ku-enjoy maisha nje ya nchi.

▪ kupitia mbinu hii dada zetu wengi wamehadaiwa kwa kuahidiwa hata kazi za ndani kwa ahadi ya mshahara mkubwa sana, wakati mwingine hata ndugu huhadaiwa kwa ahadi tele, lakini ukifika huko mambo hubadilika, kufanyishwa ukahaba, na wakati mwingine hata kuvunwa viungo vya mwili

2. Kuteka wahanga kinguvu
Mbinu hii haitumiki sana kwakuwa ni vigumu sana kumsafirisha mhanga wa utekaji na wengi hutoroka

3. Kuuzwa na familia
Familia nyingine kwa hali ngumu ya maisha hushawishika kuuza watoto lakini pia baadhi ya familia huuza watoto kutokana na mtoto kuwa yatima au ubaguzi

4. Kuhadaiwa na kusajiliwa na wahanga wa zamani au wahanga wakongwe
▪mbinu hii pia hutumiwa sana kwa kuwatumia wahanga wa zamani au wakongwe kazini ili kushawishi wanawake wengine wakubali kuingia ktk mtego uliopangwa, mara nyingi wahanga wa zamani huwa ni makahaba au machangudoa wazoefu na huwa wanalipwa kamisheni "wanachukua chao" kwa kila dili wanalokamilisha
▪kwa mtego huu wengi hunasa kwakuwa wanawaamini ndugu zao ila wakifika ni mateso

5. Mapenzi (Loverboy tactic)
hapa ndipo utakutana na vijana watanashati wamejaza picha za mapozi mbele ya magari ya kifahari na majumba ya kifahari na kujinadi kwa maisha ya bata mitandaoni, wakiomba urafiki wanawake wengi hudhani ni mahusiano ya kweli lakini wakinasa wakalipiwa hadi ndege, wakifika tu mambo hugeuka.

Wengine hapa wanaweza kuahidi hata ndoa na kwa wazazi wakafika ila ukidanganyika ukasafiri naye kwenda kwao au matanuzi nje ya nchi umekwisha

▪ Mbinu nyingine ni kama kuteka wanawake wadogo hasa naijeria na kuwalazimisha kupata mimba na kisha watoto wakizaliwa wanauzwa

▪ Wengine huja hadi kwenye vituo vya watoto yatima kutoa misaada na kuasili watoto (adopt) ili wakaishi nao kwao kama wana nia njema, kumbe wakifanikiwa kumchukua mtoto wakienda nae kinachofuata ni unyanyasaji wakutisha ili tu kupata fedha.

Mimi nimeanza kwa kusema haya machache kwa ufafanuzi huo, naishia hapa kwa leo, ila nakaribisha maswali na ufafanuzi na zaidi sana naomba wanaoweza kufunua zaidi yanayoendelea ktk biashara hii haramu na katili watiririke ili kila mtu azijue njama hizi na kuepuka yeye na wapendwa wake ili Tanzania na waTanzania tubaki salama.

NB: ukiguswa; VOTE hapo chini 👇 kwa kubonyeza alama hii ^

Asante sana
 
Back
Top Bottom