Hotuba za Viongozi kadhaa wa mataifa ya Afrika katika mkutano wa kila mwaka wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,502
9,281
Miongoni mwa waliosimama jukwaani kuhutubia alikuwa ni rais Paul Kagame wa Rwanda. Alijikita kuzungumzia mzozo wa madeni unavyoyatia kitanzi mataifa yanayoendelea na kuyapunguzia kasi ya kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ikiwa ni pamoja na kutokomeza umasikini.

Amesema sababu ya hali hiyo ni kupandishwa viwango vya riba kwenye mataifa yaliyoendelea ambayo ndiyo wakopeshaji wakubwa wa nchi masikini.

Ametumia hotuba yake kutoa rai ya mageuzi kwenye mifumo ya fedha ya kimataifa kuziwezesha nchi masikini kuifikia mitaji huku ikiwepa uhuru wa kupanga vipaumbele vyake vya maendeleo na matumizi ya rasilimali ilizonazo.

Wito wa aina hiyo ulitolewa pia na rais wa visiwa vya Ushelisheli, Wavel Ramkalawan. aAmesema ili mfumo wa ushirikiano na mshikamano ulimwenguni ufanye kazi kwa ufanisi, ni lazima kuwe na juhudi za pamoja na kubadilishana maarifa na uzoefu katika kuzishughulikia changamoto kubwa kama umasikini, ukosefu wa chakula na athari za uharibifu mazingira.

Aliyataka vilevile mataifa yanayoendelea chini mwavuli unaofahamika kama "muungano wa nchini za kusini mwa dunia" kushirikiana kwa kupeana ujuzi na kuwa mfano wa mabadiliko akisema Ushelisheli iko tayari kubadilishana uzoefu wake na nchi nyingine.

Marais wa Ghana na Angola wahoji kukawia kwa mageuzi ya Umoja wa Mataifa

Rais Joao Manuel Lourenco wa Angola yeye alikumbusha kuwa hata baada ya miaka 78 tangu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa bado imesadifu kuwa vigumu kuzuia mifarakano duniani.

Kwa mtazamo wake, sababu za hayo yote ni kuendelea kukosekana usawa ulimwengu baina ya nchi tajiri na zinazoendelea.

Amesema hali hiyo inayanyima fursa mataifa masikini kushiriki kwenye kutafuta ufumbuzi wa matatizo na mizozo inayotokea na kwa upande mwengine sauti ya nchi hizo hasikilizwi.

Ametanabahisha kuwa mwenendo huo unazifanya nchi hizo kutotimiza matarajio ya umma ambao baadaye inakuwa rahisi kushawishika kutumia njia zisizo za kiungwana kufanya mabadiliko kwa matumaini ya kutatua changamoto zilizomo kwenye mataifa yao.

Kwa upande wake rais Nana Akufo Addo wa Ghana naye aligusia eneo hilo hilo la ukosefu wa usawa kwenye jukwaa la kimataifa.

Alikwenda mbele zaidi na kuhoji juu ya sababu za Umoja wa Mataifa kutofanyiwa mageuzi hata baada ya karibu miongo minane tangu kuundwa kwake.

Eneo mojawapo ni muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Rais Akufo-Addo amesema muundo uliopo hauakisi ujumuishaji wa kila kanda ya dunia ikiwemo Afrika.

Ameweka wazi kuwa mfumo uliopo hauwezi kujenga imani ya chombo hicho kilicho na jukumu muhimu la kusimamia amani na utulivu duniani.

Ukosefu usawa kati ya nchi tajiri na masikini ndiyo ajenda ya viongozi wa Afrika?

Yumkini ukosefu wa usawa kati ya mataifa tajiri na yale masikini ndiyo iliyokuwa ajenda ya mwaka huu kwa viongozi wa Afrika kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kwa sababu waliotangulia kuzungumza hapo jana ikiwemo rais Bola Tinubu wa Nigeria na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini waliligusia.

Hata rais Hage Geingob wa Namibia naye alilijumuisha hilo kwenye hotuba yake aliyoitoa usiku wa kuamkia leo. Yeye alikumbusha kuwa tangu kuzuka kwa Janga la Virusi vya Corona, hali ya umasikini imezidi kuwa mbaya.

Amesema magonjwa ya mlipuko yanafahamika kihistoria kwa kuwa taathira za kutisha na za muda mrefu kwenye ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi.

Akagusia pia ukosefu wa usawa uliojotokeza kwenye harakati za kusambaza chanjo dhidi ya UVIKO-19. Akakumbusha kuwa hilo halipaswi kujirudia tena akitoa mwito wa kukomeshwa katika siku za usoni kile amekiita "ubaguzi kwenye utoaji chanjo".

Suriname yalilia Umoja wa Mataifa wenye nguvu, Jamhuri ya Dominica ´yaichongea´ Haiti kimataifa

Mbali ya viongozi wa Afrika kulikuwa na wengine kutoka kanda nyingine duniani waliohutubia. Rais wa taifa dogo la Amerika ya Kusini la Suriname, Chandrikapersad Santokhi, alitumia hotuba yake kukumbusha umuhimu wa kutafuta majibu juu ya changamoto za dunia badala ya kulalamika au kuendelea kutoa ahadi bila utekelezaji.

Aliweka bayana kuwa mzozo wa madeni, athari za mabadiliko ya tabianchi na hata kudodora kwa uchumi baada ya Janga la Virusi vya Corona vyote vimeleta kizaazaa karibu kila kona ya dunia lakini ni wajibu kwa mataifa kushirikiana kutatua changamoto hizo.

Kwa upande wake amesema licha ya dosari na udhaifu iliyonao Umoja wa Mataifa, bado anaamini chombo hicho cha ulimwengu kinaweza kusaidia kumaliza changamoto ndani ya nchi moja moja na ulimwengu mzima.

Iwe ni kuushughulikia mzigo wa madeni unaoyakumba mataifa masikini au kuunganisha nguvu kuutatua mzozo wa Ukraine, yote hayo kwa rais wa Suriname yanaweza kutimizwa chini ya Umoja wa Mataifa wenye dhamira na uliojizatiti.

Ama kuhusu mizozo, ilikuwa ni rais Luis Abinader wa Jamhuri ya Dominica aliyepeleka malalamiko ya nchi yake mbele ya walimwengu kuhusu uamuzi wa taifa jirani la Haiti kujenga mfereji utakaochepusha maji ya mto unaokatisha kwenye nchi hizo mbili.

Kiongozi huyo alitumia jukwaa la Umoja wa Mataifa kueleza kwa utuo, chanzo cha msuguano, sababu za nchi yake kuupinga mradi huo na hatua serikali yake ilizochukua kuonesha hasira ya matendo ya Haiti.

Msuguano huo umeshuhudia Jamhuri ya Dominica ikiifunga mipaka yote na Haiti kwa sababu serikali ya nchi hiyo inasema ujenzi wa mfereji wa kuchepusha maji ya mto Massacre unatishia ustawi wa wakulima wa nchi hiyo


DW Swahili
 
Hili ni kosa viongozi wa afrika wanafanya, sijui kwa makusudi au kutokujua au kujikomba tu,
Kukubali unyonge ni upuuzi kabisa, ningekua mimi ndio rais wa inchi ningeongea kimamlaka zaidi
 
Hili ni kosa viongozi wa afrika wanafanya, sijui kwa makusudi au kutokujua au kujikomba tu,
Kukubali unyonge ni upuuzi kabisa, ningekua mimi ndio rais wa inchi ningeongea kimamlaka zaidi
Unaongeaje kimamlaka wakat unataka upige mizinga
 
Back
Top Bottom