Hivi ni nani mshauri wa Rais Kikwete?

Invisible

Robot
Feb 11, 2006
9,075
7,878
Mwandishi Maalum
Septemba 23, 2009


kikwete_2.jpg

Rais Jakaya Kikwete

KABLA sijazungumzia mada hii, niseme kidogo juu ya mada yangu ya juma lililopita, iliyochambua hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuwazuia viongozi wa dini na makundi mengine kusema na kuandika kwa uhuru juu ya mustakabali wa Taifa.

Nilichambua inayoitwa hofu yake ya kuligawa Taifa ambalo tayari limegawanyika katika matabaka mbalimbali ya kijamii na kiuchumi. Nimepokea maoni mengi sana yenye pongezi na shukrani kupitia simu na hata barua pepe.

Lakini zipo pia "sms" sita kati ya nyingi zilizofanya mashambulizi ya aibu dhidi yangu. Uandishi si kazi yangu, hivyo basi nachelea nisije kuvamia kazi na fani ya watu wengine, kwa hiyo sitaweza kujibu maoni hayo kutokana na wingi wake na upana wa mawazo yaliyoibuliwa na makala ile.

Kwa uchache, mpaka ninapoandika makala hii, nina "sms" 312 na barua pepe 13. Nimetiwa moyo sana na tabia ya usomaji makala inayoonekana kukua pande zote za nchi, kwa sababu ikiwa waliotuma maoni ni wakweli, basi kuna fukuto la mabadiliko linakuja. Maoni hayo yalitoka kila kona ya nchi na kuwakilisha kada mbalimbali, jinsi na umri tofauti.

Wapo waliopendekeza makala ile ichapishwe na magazeti mengi zaidi, na wengine wakapendekeza itafsiriwe katika Kiingereza ili hata wageni waisome. Wapo wachache sana walionitukana, na wengine wachache sana kunitisha kwa visingizio mbalimbali. Bado natafakari kuandika makala maalumu ya kujibu hoja za maoni ya watu kuhusu makala ile – panapo majaliwa!

Mwisho niwajulishe wale waliohoji juu ya jina langu halisi, kazi yangu, mahali ninapoishi, na wengine kutaka kuniona ili tuongee zaidi na kwa upana! Mimi ni Mtanzania halisi, ninayeipenda nchi yangu baada ya Mungu. Niliamua kutokutaja jina langu wazi kwa sababu moja tu: kuwapa wasomaji fursa ya kushughulikia hoja badala ya mtu.

Wapo Watanzania wenye tabia ya kusoma au kusikiliza maoni ya mtu kwa sababu tu mtu huyo wanamfahamu. Ndugu zangu Watanzania naomba muamini kuwa wapo watu wasio na majina makubwa, lakini wana mawazo mazuri na yenye uzalendo. Uzuri na ukubwa wa jina si kibali cha kusikilizwa. Vumilieni labda panapo majaliwa, tutafahamiana siku moja. Tuendelee na mada ya leo.

Kwa hatua ya Rais Kikwete kuchukizwa na tabia ya madhehebu na makundi aliyoyazuia kuendelea na kuwahamasisha wananchi juu ya elimu ya uraia, ni wazi amefanya hivyo kutokana na ushawishi binafsi au ushauri maalumu.

Maamuzi ya kidola hutokana na sehemu hizo muhimu mbili; yaani dhamira binafsi ya kiongozi itokanayo na ushawishi binafsi au ushauri utolewao na washauri wake. Kwa hali hiyo, ni sahihi kuhoji sasa, Rais anamsikiliza nani? Nani ni mshauri wa Rais katika masuala ya msingi ya kuongoza taifa letu? Unapotokea mgongano kati ya utashi wa Rais na ushauri kwa Rais, nani asikilizwe?

Ni nani anaweza kumwambia mambo ambayo yeye binafsi hayapendi, lakini akavumilia na kumsikiliza? Jino linapouma sana, mara nyingi dawa yake ni kuling'oa na hatua ya kufanya hivyo inauma sana. Madaktari humpa mgonjwa ganzi ili waweze kuondoa jino hilo, lakini kama hakuna ganzi, jino hutolewa hivyo hivyo bila ganzi.

Kuongoza nchi yenye watu wenye tabia na mahitaji tofauti ni kazi ngumu. Kiongozi inabidi awe na uvumilivu wa kuambiwa hata yale asiyopenda kuambiwa, na mara nyingi watu wa kumwambia haya si wale aliowateua kufanya kazi ya kumshauri.

Watu wa kumwambia haya mara nyingi hujiteua au hupata fursa ya kumshauri rais kwa sababu ya nafasi zao katika jamii. Na hawa pia si vema rais kuwaita ili wamshauri, maana akifanya hivyo watamwambia yale anayopenda kusikia ili apate usingizi.

Washauri hawa humshauri rais kwa kujialika wenyewe, na ajenda huipanga wao wenyewe, si rais. Kwa hiyo, ninapochambua mada hii juu ya ni nani mshauri wa Rais, kimsingi ninalenga kuonyesha hatari zaidi ya hatua ya Rais kuwanyamazisha washauri wake wasiolipwa kwa kazi waifanyayo kumshauri Rais na hapo hapo akawaalika wakutane naye ili kushauriana naye. Nasisitiza tena, mkutano huo hauna tija.

Sasa kuna malalamiko ya watu wengi kuwa washauri wa Rais wanampotosha. Wengine wanasema Rais hana washauri kabisa. Ukiwauliza washauri wenyewe, katika mazungumzo yasiyo rasmi wanasema, "wao wanasema" lakini hawawezi kumlazimisha Rais kukubali ushauri wao.

Baadhi yao nadhani wanajisikia vibaya wanaposikia lawama za watu wengi juu ya wajibu wao wa kushauri, na wamefikia siku za karibuni kuanza kusema, "Rais hashauriki", "haambiliki", "ni mbishi" n.k.

Haya si maneno mazuri kusemwa na washauri wa Rais, na ikiwa wanayoyasemani kweli, itakuwa heshima kubwa kwao kujiuzulu warudi katika vibarua vyao vya zamani. Kuendelea kumshauri rais asiyeshaurika, asiyeambilika na mbishi ni kosa kwa mshauri, si kwa mshauriwa.

Ukiendelea kushauri bila kusikilizwa, basi ujue umekubali kuwa sehemu ya tatizo. Wakati ni kosa la kimaadili kwa rais kutowasikiliza washauri wake, lakini ni kosa zaidi kwa washauri kuendelea kutoa ushauri usiosikilizwa.

Kama wanabaki ili baadaye waje kuunda asasi za kutuambia yaliyotokea Ikulu wakati wa utumishi wao, wajue hatutawasikiliza. Twaweza kuwasikiliza sasa na kuwaheshimu ikiwa watajiheshimu na kuacha kushauri bila kusikilizwa.

Kundi la kwanza la washauri

Rais wetu ana makundi sita ya kumshauri na ambayo kwa hali ilivyo yameshindwa kumshauri kama nitakavyobainisha kwa kila kundi. Kundi la kwanza ni la wazee wastaafu, wengi wao ni wanasiasa. Kundi hili linajumuisha majeruhi wa mheshimiwa Rais katika mbio zake za kuingia Ikulu.

Tangu mwaka 1995, Jakaya Kikwete alijichimbia katika mikakati ya kuingia Ikulu, na si siri kuwa baadhi ya mikakati ilijaa fitna na vikumbo vilivyowajeruhi baadhi ya wazee hawa.

Ili kuwashinda, ilibidi timu yake itumie mbinu za medani ambazo hata sasa, miaka minne baadaye, zinamfanya ashindwe kufungua moyo wake na kuzungumza na wazee hawa au kuteta nao bila kujisikia kusutwa.

Kutokana na hali hii, wazee hawa hawawezi kumshauri, akapokea ushauri wao bila kuutilia shaka hata kama wakifanya kwa moyo mweupe. Hali kadhalika, wazee hawa, kibinadamu, hawawezi pasipo shaka kusema wanasikitika pale wanapoona mambo hayaendi sawa.

Kwao, yasipokwenda sawa ni rahisi kusema, "tulijua haya yatatokea". Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Rais katika siku za karibuni, ameshindwa kuwadhibiti mashabiki wake na wana habari wake pale walipoanza tena kuwashambulia wazee hawa kwa kejeli na vijembe katika magazeti kadhaa yenye kulenga kumsifia lakini yakiendelea kuwachafua wazee hawa.

Laiti kama yangemsifia bila kulazimika kuwachafua wazee hawa, Rais angejipatia fursa murua ya kushauriana na wazee hawa. Hili limeongeza ufa kati ya Rais na wazee wastaafu na kwa hiyo niseme, hawawezi kumshauri kwa lolote.

Kinachotawala ni unafiki na usanii wa kupiga picha katika matukio maalumu.

Kwa upande wao, wazee baada ya kushambuliwa magazetini, wamekaa kimya kwa sababu pia sehemu ya fadhila zao za kikatiba zimo mikononi mwa Ikulu, kama vile pensheni, matibabu, ulinzi, na matunzo mengine.

Unahitajika ujasiri wa ajabu kumsema mtu anayekutunza kwa mambo haya hata kama ni haki yako kikatiba.

Kundi la pili la washauri

Kundi la pili la washauri ni la wanaoitwa "Wana Mtandao". Hiki ni kikosi-kazi kilichomwingiza Rais Ikulu. Kilijaa wababe na kuongozwa zaidi na maslahi binafsi badala ya uzalendo. Kutokana na mbinu chafu zilizotumika kufikia lengo, kikosi hiki kilijeruhi na kujeruhiwa, na hapajakuwapo na nafasi ya kutibu majeraha haya kwa pande zote.

Falsafa ya Rais wetu juu ya majeraha haya ni kutegemea muda uyaponye, lakini baadhi ya vidonda vinanuka na uvundo wake unasikika kitaifa. Kwa juu juu Mtandao umesambaratika, lakini kivuli na mwangwi wake vinamtisha Rais na kumnyima raha kila wakati. Anahitaji ushauri nasaha kuishi na hali hii asiyoweza kuibadili.

Kinachotisha kuhusu Mtandao ni ukweli kuwa kwa macho yake alishuhudia wana Mtandao wakiwararua washindani wake bila huruma, na kwa hiyo anawajua jinsi wanavyorarua. Ujuzi huu ukigeuziwa kwake hapatatosha, kwa sababu wana mtandao walitanda kila mahali – majeshi yote, serikalini, chamani, kwenye madhehebu ya dini, asasi za kiraia, vyuo vikuu na hata katika balozi zetu.

Kundi hili lingeweza kumshauri Rais lakini sasa haliwezi kwa sababu kwanza linaogopana lenyewe; pili, Rais analiogopa pia na tatu, haliwezi kukutana kwa uhuru kama ilivyokuwa zamani.

Hivi sasa linakutana kwa kujificha kana kwamba linapanga ujasusi au ugaidi. Mara nyingi ushauri unahitaji kuaminiana kila upande na wakati wote ushauri unaojenga haufichwi.

Kundi la tatu la washauri

Kundi la tatu ambalo humshauri Rais kwa masuala mazito ni Idara ya Usalama wa Taifa. Tangu Rais Kikwete aingie Ikulu idara hii imekumbwa na matatizo makubwa mawili. Kwanza, historia yake na Rais huyu ni ya shaka, kwa sababu inadaiwa kuwa idara hii "haikumtaka" kuwa kati ya wagombea.

Kuna madai kwamba taarifa maalumu iliyoandaliwa na Idara kuhusu mgombea ambaye ni Rais wa sasa, haikuwa "nzuri" japo haikufuatwa na vikao vya chama.

Wengine wamedai kuwa hayo madai si chochote bali ni uzushi tu, lakini wengine wanahoji kuwa kama ni uzushi, basi hiyo ni hatari zaidi kama Idara hii haikuandika taarifa hiyo kwa jinsi ambavyo wana Mtandao walikuwa wanafanya rafu za awali katika mchakato.

Kama hoja ya kwanza ni kweli, basi hilo linatosha kuwanyima wana Idara hiyo fursa ya kumshauri Rais waliyemkataa katika "taarifa yao maalumu" kwa Mwenyekiti aliyepita. Kumtumikia Rais, au mtu mwingine yeyote, uliyemkataa au kumwandika vibaya, kunahitaji ujasiri wa pekee.

Pili, Idara hiyo imekumbwa na mgongano wa maslahi pale inapolazimika kutumikia Taifa au kutumikia fedha. Matokeo ya mgongano huo ni watumishi wa Idara kujikuta wakitumikia wana Mtandao wenye fedha au kumtumikia Rais na Taifa bila kujali kama wanalipwa vizuri au la.

Hali hii haiwezi kuwapa fursa ya kumshauri vyema Rais katika masuala makubwa ya kitaifa kwa sababu Rais anashawishika, wakati mwingine, kuwaangalia usoni kujiridhisha kama hawakutumwa na watu fulani.

Katika hali ya sasa, ambamo chama tawala kimegawanyika katika makundi ya kimaslahi, kwa maumbile ya binadamu, Idara itavutika zaidi kuelekea kundi lenye dau kubwa. Dalili ya mgongano huu ni uvujaji wa taarifa nyeti za vikao vya chama na Serikali, ufisadi wa kidola unaowezeshwa na idara hii na ukuwadi wa idara kwa chama tawala.

Enzi ya Mwalimu Nyerere Idara hii ilikuwa kioo. Tuliopitwa na wakati, tunaangalia hali hii na kutoa machozi. Kimsingi, Idara hii imebaki kujikomba kwa watawala na si kushauri tena.

Kundi la nne la washauri

Kundi la nne ambalo lingemshauri Rais ni chama chake. Tumekwisha kuona jinsi CCM ilivyosambaratika katika makundi ya kimaslahi katikati ya ombwe la kiuongozi na kiitikadi.

Rais hutoka katika chama na wakati wote chama huwa ndicho kimbilio lake mambo yanapokwenda mrama. Hata kama rais ni wa watu wote, lakini mchango wa ushauri kutoka chama chake husaidia kuboresha afya ya rais katika kuliongoza taifa.

Hali si hivyo kwetu. Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa chama chake, lakini ndani ya chama kuna wenyeviti wengi wa makundi yaliyomo. Ni kama yeye ni Mwenyekiti kwa nje ya chama lakini ndani ya chama wamo wengine, tena wenye nguvu na ushawishi kuliko yeye.

Watendaji wa kazi za chama wanawasikiliza wenyeviti wa ndani kuliko wanavyomsikiliza Mwenyekiti yeye ambaye ni Rais wa nchi. Lazima katika hali hii, pale chama kinapojaribu kumshauri Rais, atashuku ushauri huo na anaweza kuupuuza akiuita kuwa ni fitna au majungu.

Kwa ujumla, fursa hii imepotezwa na haiwezi kupatikana kwa sababu makundi ya ndani yamekidhoofisha chama na hakuna jitihada za wazi kurejesha mshikamano. Kwa upande mwingine hii ni fursa kwa Taifa kufikiria maisha bila CCM!

Kundi la tano la washauri

Kundi la tano ni la watendaji wateule serikalini; yaani mawaziri, makatibu wakuu, makamishna, wakurugenzi na wateule wengine wa Rais. Chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, timu hii ndiyo hujenga hoja kwa njia ya madokezo, taarifa na hata mikakati ya kushughulikia masuala muhimu ya kila siku katika Taifa.

Enzi za Mwalimu Nyerere, kundi hili lilimsaidia sana Baba wa Taifa na lilikuwa na uhuru wa kumwona, kumshauri na hata kumwandaa kwa ajili ya kukabiliana na matukio makubwa.

Mwalimu alilipa uhuru wa kubishana naye nje ya jukwaa ilimradi ajenda ilikuwa na maslahi ya Taifa, na si maslahi ya kundi au mtu. Kwa hali ilivyo sasa, kundi hili la wataalamu ni kama halipo au liko katika vipande vipande vya kimaslahi pia.

Kashfa nzito kama EPA, Deep Green, Richmond, TRL, IPTL n.k zimeliacha kundi hili likiwa hoi bin taabani. Haliwezi kumshauri Rais kwa sababu ama linanuka rushwa nzito au lenyewe linahofia lisije kuwajibishwa baadaye endapo ufisadi utakuja kujitokeza katika ushauri lililoutoa kwa Rais.

Hata pale Rais anapolitaka kama kundi au mtu binafsi, kumpa ushauri katika masuala nyeti, kigugumizi kinatawala na hakuna uwazi wa kweli uliojengwa katika utii utokao moyoni. Balaa zaidi katika kundi hili ni pale uteuzi wake ulivyogubikwa na maslahi ya kundi fulani.

Inapotokea kuwa uteuzi wa Rais kwa mtu unatanguliwa na michakato isiyo rasmi nje ya mamlaka ya Rais, mteuliwa hujikuta ana mgongano wa utii kati ya anayeteua na aliyefanya ukuwadi kwa manufaa ya mteuliwa.

Si siri sasa kuwa wateuliwa wa Rais wanasogezwa mezani kwa Rais na watu wenye historia zinazotia shaka juu ya uadilifu wao na uzalendo kwa Taifa.

Mgongano huu hauwezi kumpa ujasiri mtoa ushauri na wala hauwezi kumpa ujasiri Rais kupokea ushauri huo kwa moyo mweupe. Mifano iko mingi ya maamuzi yaliyofanywa na Serikali au na Rais mwenyewe na baadaye yakaja kubatilishwa kwa kushindwa kutekelezeka kutokana na ukweli kuwa hapakuwa na uwazi na ukweli katika kuyaandaa.

Tukubali ukweli – kundi hili liko taabani na ndiyo maana maamuzi mengi yanachukua muda mrefu sana kwa sababu watendaji wanakwepa kufanya maamuzi.

Kundi la sita la washauri

Kundi la sita ni la viongozi wa dini. Rais wetu ni Mwislamu lakini pia amekuwa karibu na viongozi wa madhehebu kadhaa ya Kikristo. Nimemshuhudia mwenyewe kwa mazungumzo ya ana kwa ana akihangaika na kulalamika juu ya mnyukano wa dini mbili kubwa nchini (Uislamu na Ukiristo), na kweli haumpi raha hata kidogo.

Anajua jinsi dini hizi mbili zinavyotuhumiana juu ya maamuzi ya Rais na Serikali yanayozigusa.

Wakristo wanadai kwa wazi na sirini kuwa Rais anawapendelea Waislamu, wakati Waislamu nao wakidai Wakristo wanapendelewa sana na Serikali ya Rais wetu.

Matokeo yake ni Rais kukosa msimamo na kubaki kulalamika na kutilia shaka kila ushauri anaopewa na watu watokao pande hizo mbili za dini. Katika harakati za kuwasikiliza, Rais amejikuta njia panda katika maamuzi mbalimbali.

Panapo majaliwa, mada hii itafikia mwisho wiki ijayo tutakapochambua ugumu wa kumshauri Rais katika mazingira ya sasa.


Chanzo:http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=1711

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa ni msomaji mzuri wa Raia Mwema na mmoja kati ya viongozi wa Ukiristo nchini. Barua Pepe: msomajiraia@yahoo.co.uk, Simu: 0712881704
 
Mshauri wa raisi yule kijana mahiri na MWENYE AKILI SANA KUSHINDA WATANZANIA WOTE, JANUARY MAKAMBA!!
 
nchi yetu hatuwezi kusema rais ana washauri kwa jinsi inavyoendeshwa, yaani ipo kama maamuzi yote yanatoka kwa rais moja kwa moja bila kpitia kwa washauri
 
Nimefurahia uchambuzi huu mzuri unaoangalia suala la ushauri wa Rais kwa upana na kina...Nasuburia tamati ya mada hii kuijadili. Kazi nzuri mwandishi.
 
Huyu mwandishi amefanya kazi nzuri. Nionavyo Anayemshauri rais anamdanganya kama hamwambii mambo yamebadilika. Watu wamechoka hadithi wanataka vitendo
 
Sana tu...nasikia kamesoma Harvard, Yale, na Oxford na kana IQ kama ya Einstein.

Kusoma hadi Havard maana yake nini?? Hivi Mzee wa Vijisenti si naye alipitia huko na alikuwa mshauri wa Raisi na serikali kwa ujumla kwa masuala ya sheria. Sasa as Taifa tulifaidika nini kutoka huko Havard zaidi ya kulaghaiwa na kuibiwa????????? What the f`~^&%*k is Havard???
Hakuna cha Havard, Makelele, UDSM and whatever, SISIEMU na serikali yake have to go coz wamesahau mwajiri wao ni nani.
 
Huyu mwandishi amefanya kazi nzuri. Nionavyo Anayemshauri rais anamdanganya kama hamwambii mambo yamebadilika. Watu wamechoka hadithi wanataka vitendo
Ni uchambuzi makini.Lakini nani mwenye uamuzi wa mwisho.Na hapo ndipo linakuja suala la tasisi kuwa imara pidi kama Raisi kashauriwa hivi na yeye kwasababu zake hakubali ushauri. Wangombea wote wa uraisi walikuwa na nia na sababu.Daima utendaji wake utaonyesha nia yake hiyo kwa njia mbalimbali.Na daima atawasikiliza wale washauri wenye nia yake iwe nzuri au mbaya.Washauri ni watu ambao wanamfahamu vizuri raisi na hivyo wanamshauri kufuatana na raisi jinsi alivyo.Kama hapendi ukweli maana yake anapenda kudanganywa.Mfumo wetu wenyewe ndio mbaya.Una mianya kibao ya kulinda uovu.Na mianya hiyo hubuniwa na kutungiwa sheria mara kwa mara.Afisa anashauriwa na anaambiwa kuwa mkataba huo haufai lakini Afisa huyohuyo anasaini.Anafanya hivyo kwa kuwa anajua kuwa yu salama.
 
Mshauri wa raisi yule kijana mahiri na MWENYE AKILI SANA KUSHINDA WATANZANIA WOTE, JANUARY MAKAMBA!!
Nakubaliana sana na wewe ndio maana niliweka ile Mada kule kuhusu Dada yake maana unaona jinsi gani famili hii inaweza kuwa na ushawishi mkubwa sana na ndio mwandishi wa Speech nyingi zake
 
nchi yetu hatuwezi kusema rais ana washauri kwa jinsi inavyoendeshwa, yaani ipo kama maamuzi yote yanatoka kwa rais moja kwa moja bila kpitia kwa washauri

Nadhani ni tabia mbaya iliyorithiwa toka enzi za Nyerere inaonyesha naye hakuwa na washauri/ au hawasikilizi/ au amaweka barrier ina such a way washaur hawako so free kumweleza.

ndiyo huwa nasisitiza masomo ya uongozi yanatakiwa yaanzie kufundishwa tangu primary, maana hata katika nagzi ya familia kama baba hapokei ushauri wa mama au watoto wake, then this guy will not do different when he becomes a leader.

kwa hiyo wakati tunaangalia rais, is high time to addres the problem to the public as a whole.Hatuna tabia ya kuona uongozi ni kuwa chini ya watu, tumekuwa na tabia ya kuwa kiongozi ni miungu watu, the same way in family ambapo baba kuchukua ushauri wa mtoto, mpaka mitume labda warudi. Jamani this seems cultural problem, ambapo elimu na utandawazi vinatufungua, ni tatizo la jamii yetu.

Kama hauamini uliza walimu wakuu wa sekondari kama wanachukua ushauri wa viranja!!!

mawaziri au viongozi wanagpi huwa wanachukua ushauri kutoka kwenye media?, mikutano, makanisani , NGO n.k, hakuna, then kama makatibu tarafa leo hawana tabia hiyo, then the same katibu tarafa akiwa rais atabadilika? JK hajatoka mwezini, is a prodcut of this ver same society.

Ni ushauri gani kutoka kwa wananchi ambao JK alishawahi kuufuata na akauchuka tangu akiwa waziri kwenye wizara mbalimbali? kama hakuna LEO AKIWA RAIS NDIYO ATAPOKEA????
 
Mshauri wa raisi yule kijana mahiri na MWENYE AKILI SANA KUSHINDA WATANZANIA WOTE, JANUARY MAKAMBA!!

jamani ni kwa nini mnasema kana akili kuliko watanzania wote la hasha napinga tena napinga sana ,

Kuna baadhi hawajapata nafasi tu ya kuonyesha ukomavu wao wa mawazo
 
baada ya hapo mie narudi nyuma na kusema kama kuna mtu anamshauri MR Prezident basi anachemka ,sijui kama nitakuwa mtovu wa shukurani lakini from Bottom of my heart sijaona Rais amefanya nini mpaka sasa:(
 
Kusoma hadi Havard maana yake nini?? Hivi Mzee wa Vijisenti si naye alipitia huko na alikuwa mshauri wa Raisi na serikali kwa ujumla kwa masuala ya sheria. Sasa as Taifa tulifaidika nini kutoka huko Havard zaidi ya kulaghaiwa na kuibiwa????????? What the f`~^&%*k is Havard???
Hakuna cha Havard, Makelele, UDSM and whatever, SISIEMU na serikali yake have to go coz wamesahau mwajiri wao ni nani.

Julius was just mocking around I think
 
Ushauri wa rais ni busara, siyo kusoma wala nini. Wasomi walio wengi ni vihiyo tu kama peresida wao. Mtu gani kucheka tu hata pasipochekeka. Hivi jamani kuna mtu anafatilia hotuba za Nyerere? Alisema yule hajakua, urais hauwezi. watanzania kwa ufinyu wa akili tukajua eti ni umri. Kumbe hajakua fikra na siyo rahisi kuwa alivyo sasa hivi. We are suffering the consequence.

Shughuli kwenu.
 
Naam,

Mwandishi nadhani kuna kipengele aidha kakiruka kwa makusudi ama hajui au hata ameandika na wachapishaji wakaona wakiweke kapuni.

Katika kundi la Sita basi kasahau kitu. Basi mimi nitaliita kundi la saba.

Kundi la saba na la ajabu ni la waganga wa kienyeji na wapiga ramli. Rais wetu ni mwafrika halisi kwa hiyo hajakumbatia kikweli kweli dini yoyote ya kigeni. Kwa hali hiyo, si vibaya nikisema, kwa uafrika wake ni mfuasi wa siri wa dini za jadi. Hili si tusi, dhambi wala dharau. Nimemshuhudia mwenyewe kwa mazungumzo ya ana kwa ana akihangaika na kulalamika juu ya mnyukano wa dini mbili kubwa hapa nchini (Uislamu na Ukiristo) na kweli haumpi raha hata kidogo.

Anajua jinsi dini hizi mbili zinavyotuhumiana juu ya maamuzi ya rais na serikali yanayozigusa dini hizi mbili. Wakiristo wanadai kwa wazi na sirini kuwa rais anawapendelea waislam wakati waislam nao wakidai wakiristo wanapendekelewa sana na serikali ya rais wetu. Matokeo yake ni rais kukosa msimamo na kubaki kulalamika na kutilia shaka kila ushauri anaopewa na watu watokao pande hizi mbili.

Kuna “uvumi” wa muda mrefu sasa kuwa rais wetu anapata faraja pale anaposhauriwa na waganga wa kienyeji kwa sababu anaamini hawana mgongano wa maslahi katika dini hizi mbili kuu! Kimantiki na kimsingi hii ni njia nzuri ya kutatua mnyukano wa dini kubwa pale unaposhauriwa na mtu wa tatu au wa katikati.

"Uvumi" huu umeendelea kueleza kuwa katika harakati za kuwasikiliza hawa waganga, rais amejikuta njia panda katika maamuzi mbalimbali. Ushauri wa waganga humfikia rais ama moja kwa moja au kupitia wapambe maalum, lakini utekelezaji wa ushauri huo huonekana kwa njia mbalimbali kama vile tabia sugu ya rais kuchelewa katika matukio mbalimbali na tabia ya rais kutoroka na kwenda sehemu huria kama michezoni. Mara kadhaa ndani na nje ya nchi, rais amekutwa katika maeneo yasiyo rasmi bila maandalizi wala kuwamo katika ratiba. Najua rais ana maisha binafsi lakini ni ruksa kuyahoji hasa yanapoonekana kuwa rasmi kwa kuwa yanatokea mara kwa mara.

Inasemekana kuwa kwa ushauri wa waganga rais pia amejikuta katika misiba, mazishi, kutembelea wagonjwa nyumbani na hospitali, sherehe za harusi, na hafla za asasi za kiraia zenye utata. Imesikika pia waganga hawa ndiyo wanaosikilizwa hata katika masuala ya afya yake kuliko hata madaktari wa ndani na nje ya nchi.

Eneo hili limejaa “uvumi”, umbeya na maneno ya mitaani yanayochangamsha mabaraza na vijiwe, lakini cha msingi na kinachogomba ni pale yanayosemwa yanapofanana na yanayosemwa. Ikiwa uvumi huu au sehemu yake ina ukweli, basi kundi hili ndilo pekee linalomshauri mheshimiwa rais katika mambo mengi na kwa hiyo ndilo limeshikiliwa mustakabali wa taifa letu kwa sasa.

Katika mazingira ambamo makundi mengine yamenyamazishwa, salama yetu iko wapi tunapokuwa mikononi mwa hawa washauri ambao ushauri wao haujapimwa na chombo chochote kinachojulikana?


Pimbi
 
Mwandishi ameyaacha makundi mawili muhimu ambayo yako naye kila sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi na mwaka. Kundi la kwanza ni Mkewe, wanaye, ndugu, jamaa na marafiki wa familia. Kwa Maraisi wetu wa sasa kundi hili lina ushawishi mkali mno kuanzia kwenye teuzi za Rais hadi hotuba zake.

Kundi la pili ni YEYE mwenyewe akiongozwa na TABIA, HULKA aliozaliwa nayo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom