Ukitaka Kuwamaliza Wasabato Waambie Wakusomee Wakolosai 2:16 Na Kuendelea!
INAONESHA BIBLIA UNAISOMA KAMA GAZETI
Sabato ya siku ya saba ilitolewa kwa watu wa Mungu wakati wa uumbaji. Hii ina maana kwamba Sabato ilikuwepo kabla dhambi haijaingia ulimwenguni, na hivyo basi kabla ya sheria za kafara na maagizo kuwa zimewekwa. Hivyo, Sabato ya kila juma ya Mungu isingekuwa sehemu ya sheria za maagizo, na isingekuwa imegongomelewa msalabani samabamba na sheria za maagizo .
Kutokana na kwamba wengi wana shida kutofautisha baina ya sheria za maagizo zilizoandikwa na Musa, na Sheria takatifu ya amri 10 iliyonenwa na Mungu, hebu na tuchunguze tofauti za wazi baina ya hizi mbili.
Sheria za maagizo zinahesabiwa kama “sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili” (Waebrania 7:16); na Sheria takatifu ya Mungu, imesemwa, “Twajua ya kuwa torati asili yake ni rohoni.” Warumi 7:14. Moja ni sheria ambayo “hapana budi sheria nayo ibadilike.” Waebrania 7:12. Sheria takatifu ni sheria ambayo Kristo husema, “Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie.” Mathayo 5:18.
Sheria ya maagizo ilikuwa ni “kivuli cha mema yatakayokuwa” (Waebrania 10:1), na iliwekwa tu “hata wakati wa matengenezo mapya.” Waebrania 9:10. Lakini nyingine ilikuwa ni sheria takatifu, ambayo inasemwa na Yohana, “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi [wa sheria].” 1 Yohana 3:4. Moja ni nira isiyoweza kubebwa (angalia Mdo 15:10); nyingine ni ile “sheria ya uhuru” ambayo kwayo tutahukumiwa (angalia Yakobo 2:8-12).
Sheria ya maagizo ni ile ambayo Kristo “aliiondoa katika mwili wake” (angalia Waefeso 2:15); sheria takatifu ni ile ambayo hakuja kuiondoa (angalia Mathayo 5:17) . Moja inahesabiwa kama “hati ya kutushitaki kwa hukumu” “iliyokuwa na uadui kwetu,” ambayo iligongomelewa msalabani na kuondolewa kwa kifo cha Kristo (angalia Wakolosai 2:14); nyingine ni ile Sheria ambayo alikuja kutimiliza na kuitukuza (angalia Isaya 42:21) na ambayo Yakobo hueleza kama “sheria ya kifalme” ambayo ni dhambi kuiasi (angalia Yakobo 2:8-12). Moja ilikuwa ni sheria ya muda ambayo ilibatilishwa “kwa sababu ya udhaifu wake, na kutokufaa kwake” (Waebrania 7:18); nyingine ni Sheria isiyobadilika ya milele ambayo haiwezi kutanguliwa: “Basi, je twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.” Warumi 3:31.
Sheria ya maagizo ni sheria ambayo ilikuwa ni ukuta wa katikati wa kiambaza baina ya Wayahudi na Mataifa (angalia Waefeso 2:14); nyingine ni Sheria ile, kazi ya hiyo hata mataifa wanasemwa kuwa imeandikwa katika mioyo yao (angalia Warumi 2:14-15). Moja ni sheria ya amri iliyo katika maagizo (angalia Waefeso 2:15); Sheria takatifu ni amri za Mungu, ambazo ni wajibu wa jamii ya wanadamu kuzitunza (angalia Mhubiri 12:13).
Hii Sheria kuu takatifu ya amri 10 inaletwa mbele na ujumbe wa malaika wa tatu (angalia Ufunuo 14:9-12 ). Hii ni Sheria ambayo masalio wa mbegu ya mwanamke walikuwa wanatunza wakati joka alipofanya vita juu yao (angalia Ufunuo 12:17). Sheria hii takatifu itawahakikishia, wale wote wanaoitunza, haki kuingia mbinguni na kula mti wa uzima (angalia Ufunuo 22:14).
Hakika, sheria hizi mbili hazitakiwi kuchanganywa. Sheria takatifu ilitimilizwa, kutukuzwa, kuadhimishwa, na ni takatifu, ya haki, ya kiroho, njema, na ya kifalme; wakati nyingine ni ya mwilini, kivuli, mzigo, na iliondolewa, kuvunjwa, kufutwa, kugongomelewa msalabani, kubadilishwa, na kubatilishwa kwa sababu ya udhaifu wake na kutofaa kwake.
Ni kweli kwamba shuhuda za Sheria takatifu zimewekwa hapa na pale kote katika vitabu vya Musa na kuchanganywa na mausia ya sheria ya maagizo. Lakini hii haiwezi kwa njia yoyote kuzisababisha ziunganishwe kama sehemu ya sheria hii ya maagizo na ambayo iliondolewa pia. Sheria takatifu ni ya milele kama alivyo Mungu, wakati sheria ya maagizo ilikuwa na nguvu tu mpaka Kristo alipokufa msalabani. Wale ambao bila uzito wanaligawanya neno la ukweli hawataweza kupambanua kwa ufasaha sheria hizi mbili tofauti, wala hawatatumia kwa Sheria ya Mungu ya kifalme lugha iliyotumika kuheshimu hati ya maagizo.
Amri Kumi ni sheria kamilifu zenyewe, huonekana kutoka katika ukweli kadhaa: Mungu alizitangaza kwa sauti yake mwenyewe; na inasemekana, “wala hakuongeza neno” (angalia Kumb 5:22), hivyo basi akiwaonyesha kwamba alikuwa ametoa Sheria iliyokamilika. Aliziandika peke yake kwenye mbao mbili za mawe kwa kidole chake mwenyewe, uthibitisho mwingine kwamba hii ilikuwa sheria takatifu iliyokamilika (angalia Kumb 9:9-11). Aliweka mazingira kuwa hizi tu ziwekwe chini ya kiti cha rehema katika chumba cha pili cha Patakatifu (angalia Kutoka 30:6; Waebrania 9:4-5), ushahidi ulio wazi kwamba hii ilikuwa Sheria ambayo ilifanya upatanisho uwe muhimu kwa sababu ilikuwa imevunjwa. Na Mungu kwa kueleza huita kile alichokiandika kwenye mbao mbili za mawe, Sheria na amri (angalia Kutoka 24:12).
Sheria zote mbili zilikuwa na Sabato,
lakini bado kulikuwa na tofauti wazi baina yake. Sabato ya siku ya saba ilianzia Eden kabla dhambi kama sehemu ya Sheria isiyobadilika ya Mungu, na mara zote ilitokea siku ya saba ambayo leo tunaiita Jumamosi. Wakati sabato za sikukuu zilianza baada ya dhambi kama sehemu ya sheria ya maagizo, na zingetokea siku yoyote ya juma. Sabato ya siku ya saba iliandikwa katika jiwe na kidole cha Mungu mwenyewe. Wakati sabato za sikukuu ziliandikwa kwenye nguo, au karatasi, au ngozi, kwa kidole cha Musa. Sabato ya siku ya saba, sambamba na amri zingine 9, iliwekwa kwenye sanduku [la agano] moja kwa moja chini ya kiti cha rehema pamoja na utukufu wa Mungu na uwepo juu angalia Kutoka 30:6, 40:20, 34), zikimaanisha kwamba zilitakiwa kutumika daima na zilikuwa zisizobadilika. Wakati ambapo sabato za sikukuu ziliwekwa pembeni mwa sanduku (angalia Kumb 31:26), zikimaanisha kwamba zilitakiwa kutumika kwa muda tu mpaka kusudi lake lilipokuwa limekamilika. Katika Sabato ya siku ya saba hakuna kupika ambako kungefanyika, lakini chakula chote kilitakiwa kuandaliwa na kupikwa siku ya sita au siku ya maandalizi (angalia Kutoka 16:23). Wakati ambapo katika sabato za sikukuu ungeandaa na kupika chakula chako (angalia Kutoka 12:14-16). Na Sabato ya siku ya saba, hakuna kazi ambayo ingefanyika – hata kuni zisingeweza kukusanywa kwa ajili ya kuandaa chakula (angalia Hesabu 15:32-36). Wakati ambapo sabato za sikukuu kazi ingeweza kufanyika ya kukusanya matawi mbalimbali ya mti (wakati wa sikukuu za vibanda) ili kujenga vibanda kwa ajili ya hifadhi (angalia Law 23:34-40).
Kwa hiyo kuna tofauti ya wazi baina ya amri ya Mungu ya nne isiyobadilika ya Sheria takatifu kuitunza kitakatifu Sabato ya siku ya saba, na sabato na sheria za maagizo za mifano na vivuli vya muda . Sabato ya siku ya saba “ilifanywa kwa ajili ya mwanadamu” kabla hajaanguka katika dhambi; hivyo basi isingekuwa mfano au kivuli kuelekeza kwenye mauti ya Kristo na, pia, isingekuwa imegongomelewa msalabani, lakini inaendelea kutuelekeza nyuma kwenye mwanzo wa historia ya dunia hii na kwa Mwumbaji wetu sote. Lakini sabato za siku za sikukuu, na hali kadhalika mifano mingine ya uchumi wa Kiyahudi, ilikuwepo baada ya mwanadamu kuanguka na kuhitaji Mwokozi; hivyo basi zilikuwa ni kivuli cha kuelekeza kwenye ukombozi na kusema kweli ziligongomelewa msalabani (angalia Wakolosai 2:14).
Paulo hata anaeleza kwamba watu wa Mungu wanatakiwa kuendelea kutunza Sabato ya Sheria takatifu baada ya kifo cha Kristo, lakini hakuna sehemu yoyote anaposema kwamba tunatakiwa kutunza sabato za sheria za maagizo! (angalia Waebrania 4:4-11).
Inatakiwa kuwa wazi kwa wote wanaotaka kuona kwamba kuondolewa kwa mkono wa kuelekeza kwa sheria ya maagizo kunaacha kwa nguvu kila ushuhuda wa Sheria ya kifalme, na pia kwamba sheria za vivuli vilivyokuwa vinaelekeza kwenye kifo cha Kristo kupitwa na wakati tukio hilo lilipotokea. Kuvunjwa kwa Sheria takatifu ndiko kulikosababisha Mwokozi kuutoa uhai wake kukuokoa wewe na mimi kutoka dhambini. Hivyo basi mwendelezo na kutobadilika kwa utakatifu wa amri 10, ikiwa ni pamoja na amri ya nne ya Sabato ya siku ya saba, vyaweza kuhitimishwa kwa ukweli kwamba Mungu alimtoa Mwanawe wa pekee kuondoa laana yake juu yake mwenyewe na kufa kwa kuvunja kwetu [sheria] hiyo.