Hayati Jiang Zemin kukumbukwa kwa mchango wake wa kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG111412566811.jpg

Tarehe 30 Novemba taifa la China lilikumbwa na msiba mkubwa baada ya kumpoteza rais mstaafu wa China Jiang Zemin aliyefariki mjini Shanghai akiwa na umri wa miaka 96 kutokana na ugonjwa. Akiwa kiongozi mashuhuri wa awamu ya tatu ya China, Jiang aliiongoza China kupata maendeleo makubwa, na pia aliweka msingi imara wa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika.

Baada ya kufariki kwa Jiang, salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi wa nchi za Afrika na wakuu wa mashirika ya Afrika zilimiminika nchini China. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki, amesema Jiang alikuwa mwanasiasa mashuhuri wa China na hata dunia, kifo chake ni pigo kubwa kwa China na marafiki zake kote duniani. Rais wa Kenya William Ruto amesema Jiang alijitolea kuimarisha msingi wa ustawi wa kiuchumi na ulinzi wa amani duniani. Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema Jiang aliiongoza China kuhimiza mageuzi na ufunguaji mlango na kuanza njia pekee ya maendeleo ya kiuchumi, jambo ambalo limethibitisha kwamba nchi inaweza kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kujitegemea.

Hayati Jiang alikuwa anatilia maanani sana uhusiano kati ya China na nchi za Afrika. Wakati alipokuwa rais wa China, alifanya ziara barani Afrika mara nyingi na kufanya maamuzi muhimu kuhusu maendeleo zaidi ya uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika.

Kwa muda mrefu, China na nchi za Afrika zimesaidiana katika mapambano ya kujipatia ukombozi na uhuru. Jiang alipoiongoza China, China iliendelea kuunga mkono nchi za Afrika kuondokana na ukoloni na kupigania ukombozi wa kitaifa. Katika salamu zake za rambirambi, Rais Hage Geingob wa Namibia amesema hayati Jiang alitoa mchango usiofutika katika harakati za kupigania uhuru na maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Namibia, kifo chake sio tu ni pigo kwa watu wa China na Chama cha Kikomunisti cha China, bali pia kwa Namibia.

Wakati karne ya 21 ilipokaribia kuingia, China na Afrika zilikabiliwa na fursa na changamoto mpya. Jiang alifanya uamuzi muhimu wa kuboresha uhusiano kati ya pande hizo mbili. Tarehe 13 Mwezi Mei, mwaka 1996, Jiang alitoa hotuba yenye kichwa “Kujenga Mnara Mpya wa Kihistoria wa Urafiki wa China na Afrika” katika Jengo la Afrika huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, na kutoa mapendekezo matano: China na Afrika zinapaswa kuwa marafiki wa kuaminiana, zinapaswa kuheshimiana na kutoingiliana mambo ya ndani, zinapaswa kutafuta maendeleo ya pamoja, zinapaswa kuimarisha mashauriano na kushirikiana kwa karibu katika masuala ya kimataifa, na zinapaswa kushirikiana ili kuanzisha dunia bora zaidi. Alipendekeza kuwa katika karne mpya, China na Afrika zinapaswa kujenga uhusiano wa kushirikiana wa muda mrefu ulio thabiti na wa kina.

Mwaka 2000, Jiang alipokuwa madarakani, Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lilianzishwa, na likawa moja ya majukwaa muhimu zaidi kati ya pande hizo mbili katika kuimarisha mawasiliano na ushirikiano. Katika Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa FOCAC uliofanyika mjini Beijing, Jiang ambaye wakati huo alikuwa rais wa China alitoa wito kwa China na Afrika kuanzisha ushirikiano mpya wa muda mrefu, wenye utulivu, usawa na kunufaishana, kwa sababu uhusiano wa kirafiki kati ya pande hizo mbili unalingana na maslahi ya watu wao na mwelekeo wa amani na maendeleo duniani. Sasa zaidi ya miongo miwili imepita, kutokana na msukumo wa FOCAC na majukwaa mengine ya ushirikiano, uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika umepata maendeleo makubwa na kuwa mfano mzuri wa uhusiano wa kimataifa.
 
Back
Top Bottom