Rai ya Jenerali
Nkaba nyin'embwa yange
Jenerali Ulimwengu
Agosti 18, 2010
WIKI jana nilijadili suala la watu wazito, wenye nyadhifa kubwa, wenye historia zinazoeleweka, na wenye wingi wa miaka inayowatambulisha kama wazee, lakini hujidharaulisha kwa kutoa matamko ya kipuuzi yasiyofanana na sifa hizo alimradi wajibu hoja za kudumu kwa majibu mepesi ya mpito. Wiki jana ilikuwa ni ya Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM na matamko yake kuhusu uoza ndani ya chama chake. Wiki hii tena, mzee mwingine wa CCM, Katibu wa Uenezi, John Chiligati, naye ameamua kujiingiza katika kundi hilo la kujisemea bora liende.
Chiligati, yeye, ameamua kumzungumzia kijana wa CCM, Hussein Bashe, ambaye hivi majuzi tu, mjini Dodoma, amekatizwa safari yake ya kuwania ubunge kutokana na kile kilichoelezwa kuwa tatizo la uraia.
Chiligati aliwaelezea waandishi wa habari mjini Dodoma alfajiri ya Jumapili kwamba Bashe ameachwa katika mchujo wa wagombea kwa sababu yeye ni raia wa Somalia, na kwa hiyo si raia wa Tanzania. Aliongeza kusema kwamba chama chake kilifanya uchunguzi kikishirikiana na Idara ya Uhamiaji na ndipo ikagundulika kwamba Bashe si raia wa Tanzania, hata kama alizaliwa Tanzania.
Hadi hapo sioni tatizo. Tatizo linakuja pale Chiligati alipotamka kwamba kesi ya Bashe ni sawa na ile ya mwandishi wa makala hii , aliyekuwa kada wa CCM na akavuliwa uraia wake katika miaka ya nyuma.
Nakiri kungali na mapema kwamba haipendezi kwa mwandishi wa makala hii kutumia safu hii kuzungumzia suala linalomhusu binafsi. Nasema haipendezi, lakini ni halali katika hali fulani fulani. Nitajaribu kueleza hapa chini.
Wahaya husema kwamba mtu akibanwa mbavu kuhusu jambo alilotenda na akataka kusema uongo atasema,
nkaba nyinembwa yange. Nilikuwa pamoja na mbwa wangu. Maana yake ni kwamba, kama mnataka ushahidi wa hili ninalosema muulizeni mbwa wangu.
Kwa mitindo mbali mbali na katika mazingira tofauti hii ni silaha inayotumiwa na watu wanaotaka kusema uongo unaofanana na ukweli. Kwa mfano, inawezekana kweli Bwana Bigambo alikuwa na mbwa wake wakati wa tukio husika, lakini haiwezekani kwa mbwa wake kutoa ushahidi, kwa hiyo kuwapo au kutokuwapo kwa mbwa huyo hakuna uhusiano na ushahidi wa Bigambo. Anapoteza lengo tu, na ingawa kwa juu juu anasema ukweli (mbwa wake alikuwapo) lakini anasema uongo (mbwa hawezi kutoa ushahidi).
Ili kuwafariji akina Chiligati, ninaweza kuwaarifu kwamba hawako peke yao, kwani hata wakubwa wa dunia wanatumia vijisilaha kama hivyo wanapokuwa wameshikwa pabaya. Miaka kadhaa iliyopita, wakati Marekani wanangangana kwenda Iraq kumwondoa Saddam Hussein, Marekani walipambana na upinzani mkali mno kutoka kwa maswahiba wao wa Magharibi waliokataa kubariki vita ya Marekani dhidi ya Iraq. Tunamkumbuka Dominique de Vilpein, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa na jinsi walivyoshikana mashati (kwa maneno) ndani ya mkutano wa Baraza la Usalama.
Katika mabishano makali yaliyofanyika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kila aina ya mbinu zilitumika kutetea upande huu na ule, kila mmoja akivutia upande wake. Ilikuwa dhahiri kwamba dunia haikukubaliana na mantiki ya Marekani kuivamia Iraq, na kwamba Marekani walikuwa wamedhamiria kufanya kile walichoazimia na kwamba wangetumia maguvu, hata kama Umoja wa Mataifa ungewakataza.
Lakini, kwangu mimi binafsi, tamko lililoashiria kuchoka kwa uchovu na ubabaishaji wa mantiki ya Marekani ni pale ofisa wake mwandamizi alipoiingiza Tanzania katika ubishi huo, kwa kutamka kwamba hata Tanzania ilipoivamia Uganda haikufanya hivyo kwa kibali cha Umoja wa Mataifa.
Ati nkaba nyinembwa yange.
Huyu msemaji wa Marekani alifanya purukushani (hii ndiyo maana halisi ya neno hili) kuhusu chanzo cha vita baina ya Tanzania na Idd Amin, yaani uvamizi alioufanya Amin dhidi ya Tanzania, na kwamba ilichofanya Tanzania ilikuwa ni kutumia haki yake ya msingi ya kujibu mapigo katika ulinzi wa ardhi yake. Msemaji wa Marekani alisema ukweli (Tanzania haikupata ridhaa ya Umoja wa Mataifa) wakati papo hapo akisema uongo (Iraq haikuivamia Marekani).
Mantiki ya
nkaba ninyembwa yange huweza kupata mashiko miongoni mwa wasemaji na wasikilizaji waliojijengea utamaduni wa fikra nyepesi zinazotafsirika katika matamko mepesi sawia. Katika jamii iliyojizoeza kufanya mambo yake (pamoja na kufikiri)
fasta-fasta, muhimili mmoja wa mtazamo wa maisha ni kwamba hutakiwi kuumiza kichwa chako kufikiri. Unachotakiwa ni
kuwa mjanja ili uweze
kubakia bambucha.
Hebu tuangalie Chiligati anasema nini kuhusu kijana Bashe na mwandishi wa safu hii. Kijana huyu alikuwa, hadi juzi (sijui leo) kada wa chama-tawala, tena kada wa msitari wa mbele ambaye amekifanyia kazi chama hicho hadi juzi. Mwandishi huyu wakati akivuliwa uraia hakuwa tena kada wa chama hicho, akiwa amehitilafiana na uongozi/utawala wa juu wa chama hicho kuhusu masuala ya msingi.
Kijana Hussein Bashe, ambaye sasa anatolewa kafara na wale alioamini ni wazee wake, alikuwa bado anayo hamu ya kukitumikia chama chake katika wadhifa wa juu zaidi. Mwandishi huyu alikuwa amestaafu ubunge na ujumbe wa NEC na alikuwa amejikita katika harakati za asasi za utetezi pamoja na uandishi na uchapishaji wa magazeti makini ambayo hayakusita kuiambia serikali na chama-tawala kwamba mfalme yu uchi, na korodani zinaonekana.
Utamaduni wa uroho na kunyanganyana matonge ndani ya chama-tawala, kama tulivyoushuhudia siku za hivi karibuni huzaa uchafu wa kila aina kiasi kwamba mtu anahitaji pua zenye sugu iliyoingia sugu ili asisikie uvundo unaotoka huko. Katika utamaduni huo, watu hutafunana wenyewe kwa wenyewe, wakubwa wakiwatafuna wakubwa wenzao, wakubwa wakivimeza vitoto vyao, na vitoto navyo vikingatangata visigino vya wazazi wao.
Naamini kwamba wamo watu ndani ya chama-tawala ambao hawakumtaka Hussein (kwa sababu walitaka mbunge wao) na wakaona kwamba mbinu ya kumzuia ni hiyo ya uraia, hasa kwa sababu sura yake inaashiria asili yake. Huyu wamemuweza, kwa sababu, pamoja na maneno ya Chiligati, bado ni dagaa, hajawa hata kambale, achilia mbali papa. Mbona wengine hawawagusi?
Katika majungu wanayopikiana ndani ya chama-tawala, baadhi ya wanachama wasiomtaka Mustafa Mkulo walipeleka pingamizi dhidi yake na wakaenda Dodoma kushadidia pingamizi yao wakati wa kikao cha NEC. Chiligati hakusema kama uamuzi juu ya Mkulo ulitoka ndani ya Idara ya Uhamiaji au ndani ya NEC. Kati ya Bashe na Mkulo bila shaka ipo tofauti.
Shauri analoliingiza Chiligati katika sakata ya Bashe ambalo linamhusu mwandishi huyu lilianza kwa watawala kutafuta njia ya kunyamazisha baadhi ya sauti za kuudhi. Kinara wa kampeni kuhusu uraia wa mwandishi huyu alikuwa ni kachero mwandamizi mstaafu ambaye kwa wakati huo alikuwa amelazimishwa kujiuzulu uwaziri katika serikali ya rafiki yake, Benjamin Mkapa, kwa sababu alikuwa amegundulika na gazeti la mwandishi huyo kuhusiana na wizi wake wa fedha za Serikali kwa kisingizio cha ugonjwa bandia wa mkewe.
Waziri huyo mwizi (labda tumwite mwiziri), badala ya kwenda jela, akawa anahaha mitaani na kuapa kwamba ama zake ama za mwandishi huyu. Waziri huyo akafunga safari hadi mikoa ya magharibi, na hata katika nchi jirani, kutafuta ukweli kuhusu mwandishi huyu, na kufikia hitimisho kwamba mwandishi huyu si raia wa nchi hii, wakati wote akiungwa mkono na mkuu wa nchi wa wakati huo. Wote wanajua kilichofuatia.
Mwandishi huyu, tofauti na Bashe, hakuwa anatafuta cheo wala nafasi ya uongozi; alikwisha kuchoshwa na unafiki uliokuwa umemzunguka kila mahali, na hususan wanasiasa uchwara wanaoingia madarakani kwa ahadi ambazo, ukiwachunguza kwa undani, si kwamba wanashindwa kuzitekeleza, bali hawajawahi kuwa na nia yo yote ya kuzitekeleza.
Tusichanganye mambo, hata kama utamaduni wetu ni wa chakachua. Usomali wa Bashe hauna uhusiano na uamuzi wa NEC (mbona chama-tawala kinao Wasomali wengi tu, tena waandamizi na hawazungumzwi?) na wala hauna uhusiano wo wote na tatizo lililompata mwandishi huyu. Na wala maamuzi mengine yaliyochukuliwa na NEC kwa visingizio (sababu zina sehemu zake) kadhaa hayafanani na maamuzi mengine ambayo hayafanani na visingizio hivyo:
Watoa rushwa na wanunua kura wamo kibao ndani ya orodha iliyopitishwa na chama-tawala, na pia majangili maarufu na maharamia mashuhuri wa kila aina. Wakabila, wadini, wabaguzi wa rangi, washirikina, walaghai, wauaji wa albino, wauza unga.. kama kuna dhambi isiyowakilishwa ndani ya orodha ya wagombea waliopitishwa juzi na NEC, dhambi hiyo haijateremshwa duniani.
Wakubwa, kwa kuamini kwamba wananchi wanaowatawala ni wajinga, wanaendelea na kauli zao nyepesi, ambazo zinaashiria fikra nyepesi.
Raia Mwema Toleo Na 147