Kavazi la Dr. Salim, Jenerali Ulimwengu, Gazeti la Rai na Ugombea wa Dr. Salim Uchaguzi Mkuu 1995

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,261
KAVAZI LA DR. SALIM: JENERALI ULIMWENGU, GAZETI LA RAI NA UGOMBEA WA SALIM UCHAGUZI WA 1995

Katika Kavazi la Dr. Salim anaeleza simu aliyopigiwa na Jenerali Ulimwengu tarehe 29 March 1995 na walizungumza kuhusu Burundi, siasa za Tanzania na Uchaguzi Mkuu.

Mimi nilivutiwa na hili la Uchaguzi Mkuu wa 1995 kwa kuwa kwa njia moja au nyingine nilihusika na nilikuwa kama alivyokuwa akifanya Dr. Salim kuweka shajara (diary) nami pia nikifanya hivyo kwa yale niliyoshiriki.

Dr. Salim anasema mazungumzo yao ghafla yaliingia katika Uchaguzi Mkuu.

Siwezi kueleza aliyoandika Dr. Salim lakini kitu ambacho kiliniburudisha kwanza ni ujuzi wake wa lugha ya Kiingereza na pili Dr. Salim anachagua maneno yake kwa utaalamu wa hali ya juu mno.

Ili kumweleza nini khasa anasema inabidi msomaji ufanye kazi ya ziada kwa kutembea katikati ya mistari.
Hii si kazi ndogo na inaendana na kitu kinachoitwa kuelewa ''difficult passages,'' na hili ni somo maalum.

Dr. Salim nathubutu kusema kabobea katika fani hii.

Dr. Salim anahitimisha kwa kusema siku ya pili baada ya mazungunzo yake na Jenerali Ulimwengu taarifa zikamfikia Addis Ababa kuwa habari kuu ukurasa wa mbele wa gazeti la Rai Mhariri wake akiwa Jenerali Ulimwengu limeandika, ‘’Salim Si Mgombea Lakini...’’

Haraka nikashuka kwenye notes zake.

Hapa kwa mara ya kwanza nakutana na maajabu ambayo mtu usihadithiwe unataka uone kwa macho yako mwenyewe.

Katika uzinduzi wa Kavazi la Dr. Salim, Prof. Saida Yahya alieleza kuwa Dr. Salim anaweka notes zake akianza na tarehe, saa na dakika ya tukio nk.

Naam nimekutana na ukweli huu na kushuhudia kwa macho yangu.
Lakini hili si lililonishtua sana.

Lilonifanya moyo wangu ubadili mapigo ni pale niliposoma Dr. Salim anaeleza kuhusu ujumbe aliopelekewa kutoka Geneva na Balozi Khamis Suedi, kutoka kwa Hamza Aziz, Idi Simba, Abbas Sykes na Ambassador Abdalla Suedi.

Hawa wote waliotajwa hapo nilipata kufanyanao mazungumzo nyumbani kwa Abbas Sykes, Sea View ambako alinialika chakula cha mchana na hawa wazee wangu walikuwapo pamoja na Ahmed Rashaad Ali.

Mazungumzo yetu yalikuwa kuhusu Uchaguzi Mkuu na wazee wangu walitaka kujua Waislam wana msimamo gani?

Miaka mingi imepita.

Haraka sana nikaingia Maktaba na kutoa shajara yangu ya mwaka wa 1995 nikafungua mwezi March kuangalia nimeandika nini.

Kipindi hicho joto la Uchaguzi Mkuu lilikuwa juu sana.

Gazeti la Serikali Daily News ukurasa wa mbele katika wino mweusi uliokoza kulikuwa na kichwa hiki cha habari: ‘’Sendoro Speaks on Election.’’

Elinaza Sendoro alikuwa Bishop wa Evangelical Lutheran Church in Tanzania (ELCT) Eastern Diocese.

Bishop Sendoro alikuwa anaonya kuhusu siasa kali na kuwa kura zitapigwa kwa kuangalia dini na sio uwezo wa wagombea.

Bishop Sendoro akatoa wito wa kuepuka uwezekano wa Tanzania kugawanyika katika kambi mbili zinazokinzana.

Shajara yangu inanieleza kuwa nilikuwa na mazungumzo na Prof. Haroub Othman na akanieleza kuwa Dr. John Sivalon alikuwa anataka kufanya semina kuhusu ‘’Dini na Siasa’’ kwa kuwa Uchaguzi Mkuu utatawaliwa na udini.

Semina hii haikuweza kufanyika kwa kuwa wahisani hawakupendezewanayo lakini walikuwa tayari kutoa fedha kiandikwe kitabu.

Prof. Haroub Othman akaniambia kuwa yeye amewaomba Dr. Khalfan na Dr. Sivalon wote kutoka Chuo Kikuu Cha Dar-es-Salaam kuratibu mradi huo na mimi niandike mmoja ya sura katika kitabu hicho.

Haya ndiyo niliyoandika tarehe 1 March.

Tarehe 2 March sentensi ya kwanza niliyoandika ni Adam Lusekelo akitangaza kupitia BBC Idhaa ya Kiswahili kuwa Augustino Mrema amejitoa CCM.

Tarehe 3 March Rais Mwinyi akizungumza katika Eid Baraza iliyoandaliwa na BAKWATA Ukumbi wa Diamond Jubilee aliwaonya Waislam kutosababisha kuvunjika kwa amani.

Rais Mwinyi kwa bahati mbaya sana kwa kutoijua historia ya uhuru wa Tanganyika alidhani kuwa kwa kuwafokea Waislam yeye atapendeza na kupendwa.

Haikuwa hivyo.
Augustino Mrema kwa mambo aliyokuwa akifanya alionekana ana nguvu kumshinda Rais Mwinyi.

Siku tatu kabla ya Mrema hajajitoa CCM, John Bwire mmoja wa wahariri wa Rai akihojiwa na BBC Idhaa ya Kiswahili alisema kuwa Mrema alikuwa kipenzi cha wananchi wa mji huo na wakimzunguka kwa mapenzi makubwa kila alipojitokeza hadharani.

Haya hayakuwa bure kulikuwa na ujumbe maalum katika yote haya na wenye macho waliona na wenye masikio walisikia.

Katika Sala ya Ijumaa Msikiti wa Mtoro siku hiyo hiyo Sheikh Khalifa Khamis alimshambulia sana Augustino Mrema.

Kila kukicha asubuhi kuna jipya.

Tarehe 4 March gazeti la Nipashe likaandika katika ukurasa wa mbele kuwa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Sheikh Hemed bin Jumaa amewaonya Waislam wasiwapigie kura Waislam wenzao katika uchaguzi utakaofanyika October.

Hii ndiyo hali ya siasa iliyokuwapo wakati nilipokutana na wazee wangu wale nyumbani kwa Balozi Abbas Sykes wakaniuliza Waislam wana lipi katika uchaguzi unaokuja mwezi October 1995.

Mazungumzo yetu yalikuwa marefu na nakumbuka Mzee Rashaad mbele yao alikuwa akiniambia, "Mohamed hapa uko ndani ya kambi ya adui haya yote unayowaeleza yatafika Makao Makuu Dodoma."

Si kama sikuyajua hayo lakini nilitaka kufikisha ujumbe.

Nilipomaliza kumsoma Dr. Salim nikajiuliza kwa nini ilikuwa lazima ielezwe au ienezwe na Rai kuwa Dr. Salim Ahmed Salim si mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM?

Je, hii ilikuwa moja ya njia ya kumsafishia njia Benjamin Mkapa?
Ieleweke kuwa Mkapa na Jenerali Ulimwengu walipata kuwa marafiki wakubwa.

Nikajiuliza tena kuna uwezekano kuwa yale ambayo niliwaeleza wazee wangu siku ile pale nyumbani kwa Balozi Sykes ndiyo huu ujumbe uliotoka kwa Balozi Khamis Suedi Genava kwenda kwa Dr. Salim Ahmed Salim Addis Ababa?

Dr. Salim hakusema ule ujumbe ulikuwa wa nini.

Kilichobakia ni dhana tu.
Labda ilikuwa kuhusu Uchaguzi Mkuu.

Kavazi la Dr. Salim lina mambo hapana mchezo.
Allah Ndiye Mjuzi.

1696193887899.png
1696193939019.png


1696193809094.png



 
Shukrani kwa kumbukizi hizi mzee mohamed nilitamani ungeeleza zaidi matukio yaliyotokea nyakati hizo, Mola azidi kukutunza mzee wetu.
 
Shukrani kwa kumbukizi hizi mzee mohamed nilitamani ungeeleza zaidi matukio yaliyotokea nyakati hizo, Mola azidi kukutunza mzee wetu.
Mla...
Amin kwa sote.
Mambo yako mengi na nia ni kuwafanya watu wakaisoma historia ya Dr. Salim Ahmed Salim.
 
HONGERA mzee Mohamed Said una hazina kubwa ya kumbukumbu nyingi ya HISTORIA ya siasa za TANGANYIKA/TANZANIA. ALLAH akujalie AFYA NJEMA na UMRI mrefu zaidi Ili tupate kunufaika na ELIMU ya HISTORIA HALISI YA SIASA ya TANGANYIKA/TANZANIA iliyofichwa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom