Hatma ya kijana wa Kitanzania

Quartz360

Senior Member
Mar 27, 2023
124
302
Habari wana jukwaa.

Ni matumaini yangu mu wazima wa afya.

Leo ningependa tuangazie hatma ya kijana wa Kitanzania.

Nikiwa nimekaa zangu nimetulia nikiwaza ni namna gani naweza kuleta mchango wowote katika jamii yangu. Ghafla macho yangu yanajazwa na taswira ya mtu, aliyevalia mavazi yake maridadi, mathalani kumwita mtanashati ni haki yake.

Lakini napata kizuizi kuendelea kumnadi sifa zake mara baada ya kumdadisi kwa makini sura yake, ni kweli kijana alivalia mavazi nadhifu. Lakini sura ilizungumza zaidi, kwani alionekana ni mwenye kukosa matumaini, akiwa na moyo uliopondeka, huzuni na wasiwasi vilikua juu yake.

Dhahiri alivutia kwa yeyote kuweza kumdadisi kwa undani juu ya hari yake.

Kwa kufanya kama sina udadisi wowote juu yake, nikaendelea na mambo yangu, nikiwa na simu yangu, ghafla nikasikia sauti ikinisemesha nami kwa ujasiri mkubwa, nikainua macho kumtazama.

Kwa kweli ni mengi tuliyoongea siku hiyo, pasina shaka kuiita "Siku ya Kufikirisha" ni sahihi pia. Mengi juu ya yote, haya ndiyo niliyokusanya siku hiyo.

Kijana alisema ni mhitimu wa chuo kikuu akiwa na shahada yake kibindoni, mathalani kumwita msomi itakuwa sahihi zaidi. Aliongeza kwa kusema amehitimu na rafiki zake wengi kutoka vyuo mbalimbali kama vile UDOM, MUHAS, SUA, MZUMBE, UDSM, MIPANGO, SAUT, KIUT, ARDHI, MUM, JORDAN, NIT, CBE, IFM., kwa uchache aliweza kuvitaja.

Japo kwa sasa kila mtu na shughuli zake na hajui wanafanya nini kwa sasa.

Kijana aliongeza, tangu ahitimu chuo, maisha yamekuwa magumu, bashasha na matumaini makubwa aliyokuwa nayo pindi akiwa chuo alijua fika kwamba mafanikio yako upande wake, kwani hata familia yake ilitambua hilo.

Lakini ghafla hali ilibadirika kwa upande wake baada ya kuhitimu, kwani namna mtaa ulivyompokea ni tofauti kabisa na matarajio yake, kwani pesa imekua ngumu, hakuna ajira na gamba lake likiwa ndani na GPA yake.

Bahasha za kaki zimekuwa rafiki kwake kwani kila ofisi mjini hujitahidi kupita japo kujaribu bahati yake.

Mtaa unamzomea, jamii inamshangaa, familia haimwelewi hata kidogo, rafiki zake aliowacha kule mtaani wanamcheka, kuwa hakuna alichokipata chuoni, wanasema alikua anapoteza muda.

Nilipata huzuni moyoni, hadi machozi yalianza kunitoka, lakini kwa ujasiri mkubwa ilibidi nijikanze kwani kijana alikuwa na mengi ya kuniambia.

Moyoni nikawaza ni kwa nini anapitia changamoto zote hizi? Je hana ndugu wa kumsaidia? Lakini roho ikaniambia si kila ndugu ana moyo wa kusaidia wengine. Pia nikawaza je huyu kijana hana kile wanachokiita CONNECTION, lakini pia roho ikasita, huenda ndiye mtu wa kwanza kufika hapo alipo katika familia ama ukoo wao. Nikawaza pia, je? Huyu kijana nawezi hata kufanya biashara ndogo ndogo za kumpatia kipato, lakini pia roho ikaniambia vipi kuhusu mtaji? Nikawaza pia je huyu kijana alipokuwa chuo, hakutunza hata vijisenti vya boom? Au ndiyo wale waliokuwa wanaruka viwanja, na kubadili fashion, ama wapenzi? , napo nikasita kwani kuhukumu bila ushahidi sio sawa.

Nikiwa naendelea kuwaza, kijana alivuta pumzi na kuendelea,

Najuta kwa nini nilisoma, siamini kama GPA yangu si kitu tena, siamini kama shahada yangu haina thamani tena. Kijana machozi yalianza kumlenga nami nilimpa moyo aendelee na mazungumzo yale.

Lakini alishindwa kabisa kuendelea, nilimwonea huruma sana, niliwaza huenda akengua kaka yangu, dada yangu na hata mwanangu akipitia hali kama hiyo ingekuwaje? Alitoa kitambaa akapangusa machozi yale, akaniambia, naomba nikuache niwahi nyumbani ndugu yangu, tutaongea siku nyingine. Alinipa namba yake akaondoka, nami kwa moyo mkunjufu nilinakiri namba ile na nikimtakia kila lililo jema, huku akinithibitishia kuwa tungeonana tena siku nyingine.

Kwa uchovu na sonona isiyo kifani juu yangu, nilimsindikiza kwa macho kijana mpaka alipotoweka kwenye mboni za macho yangu.

Nami nilipata wasaa wa kushika simu yangu, na wazo lilinijia kichwani mwangu kuwa ujumbe ule ni mzito, na kuna mahali ulipaswa kufika. Hivyo nikapata nguvu ya kusimulia kisa hiki, ili kaka yangu, dada ama rafiki yangu apate la kujifunza, zaidi ya yote, jamii na serikali kwa ujumla iweze kulielewa hili.

Hivyo basi,

Serikali ilitambue hili:-
Pongezi kwako serikali, pongezi kwenu viongozi, ni kazi kubwa mnaifanya japo changamoto ni nyingi.
Mkumbukeni kijana wenu, mkumbukeni mtoto wenu, mkumbukeni shujaa wenu, ni yeye yule mliyemwambia ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA, ni yeye yule mliyemtengenezea mtaala wa Elimu, mathalani wazo lenu lilikuwa bora na dhima stahiki juu ya kijana wenu, ni yeye yule mliyemtaka akajiandikishe darasa la awali, ni yeye yule aliyesoma miaka saba kwa Elimu ya msingi, miaka minne kwa Elimu ya sekondari, miaka miwili kwa kidato cha Tano na Sita, na miaka mitatu, minne hadi mitano kwa Elimu ya chuo kikuu, ni yeye yule aliyetumia miaka zaidi ya kumi na sita shuleni, ni yeye yule aliyehitimu shahada yake, ni yeye yule aliyetoka chuoni, na ni yeye yule mliyemwambia AJIAJIRI, napata ukakasi kuunga mkono wazo lenu japo ni wazo zuri kwake pia, jamii na taifa pia, lakini kumbukeni ni yeye yule aliyefundishwa DICTATORSHIP IN GERMANY, ni yeye yule aliyefundishwa SOCIALISM IN RUSSIA, ni yeye yule aliyefundishwa TIMBER PRODUCTION IN NORWAY, ni yeye yule aliyefundishwa, AIRLINE TRANSPORT IN CANADA, ni yeye yule aliyefundishwa, RUBBER PRODUCTION IN SIR LANKA, ni yeye yule aliyefundishwa, HADITHI ZA SUNGURA NA FISI, ni yeye yule aliyefundishwa LOGARITHMS, ni yeye yule aliyefundishwa, THERMAL DYNAMICS, zaidi ya yote ni yeye yule aliyefundishwa PARTS OF THE BODY, PARTS OF FERN PLANT na PARTS OF THE GRASSHOPPER.

Napata ukakasi kuamini kama kijana wenu ataweza kupambana na kufanikiwa katika dunia hii ya sayansi na teknolojia. Napata wasiwasi juu ya kauli ya kujiajiri kwa kijana wenu. Kijana anahaha, aliyofundishwa shuleni hayakuti mtaani, hayatumii mtaani. Mtaa unamtaka awe na akili ya maisha, atafute pesa na aboreshe maisha yake. Kwa bahati mbaya kijana wenu hana huo uwezo, pengine hajaiva vilivyo, pengine hakuandaliwa vizuri ama ni tatizo lake, sijui. Tuachane na hayo vipi. Sasa hali ishakuwa mbaya, vijana wenu mnawafanyia nini kuwanusuru?

Jamii ilitambue hili:-
Kijana wenu kahitimu, katoka masomoni, ni dhahiri mna matumaini makubwa juu yake, hiyo ni haki yenu. Lakini kumbukeni dunia imebadilika, zama zimebadilika. Kama mliweza kuhitimu na kupata ajira enzi zenu, ni nyie. Msimcheke kijana wenu, msimlaumu ama kumkejeli, mtieni moyo, huyo ni wenu, mpeni mbinu bora za maisha, muwezesheni, mshikeni mkono, mtieni nguvu nae atafanikiwa.

Kijana litambue hili:-
Usione tunakutetea ukajua huna kosa, la hasha, tunajua ajira ni ngumu, tunajua pesa ni ngumu, lakini usomi wako usikufanye ubague kazi. Ukweli mchungu kijana wangu, kwa dunia ya sasa shahada yako na GPA yako kubwa inaweza isiwe chachu kuu ya wewe kufanikiwa katika maisha. Fikiria nje ya boksi, kama ulisoma ili uje ukae ofisini, siku hizi ni hamna, acha kulinganisha na elimu yako, ishi na watu vizuri, unaweza ukawa na elimu ya darasani ukazidiwa pesa na mtu uliyemwacha mtaani. Acha kuvimba na cheti chako, chapa kazi, usiseme huna connection, piga kazi, mfanye Mungu kuwa connection yako, usichague kazi, kwani ajira hakuna, acha uvivu kijana wangu, usiishie kuilaumu serikali, tumia muda huo kufanya kazi, weka juhudi, malengo na maono thabiti katika ndoto yako, acha kukesha mitandaoni, acha uzembe kabisa kijana wangu, maisha yako ni juu yako, jifunze kufanya biashara, kilimo na ufugaji.

  • Mtegemee Mungu.
  • Nidhamu katika kazi.
  • Acha starehe za dunia.
  • Jifunze maarifa ya Kifedha.
  • Heshimu kila mtu.
  • Usijikatie tamaa.
Wewe ni tunu ya taifa lako, acha kulia lia, wewe ni shujaa, kubali kubadili fikra zako, amua leo kupambania ndoto zako, familia yako na taifa lako. Daima Mungu atakuwa upande wako. 😍😍
"It's not over until it's over."

Keep on doing champion.
#MyCountryPeople 😁
 
Uzi bora kabisa hongera sana.

uzi usindikizwe na usomaji wa kitabu cha Money formula by joel nanauka.
 
Safari ya maisha ya kijana wakitanzania ni yakusikitisha na kutisha huzuni hofu upyeke manyanyoso hii ndio njia halisi
FB_IMG_1683587727930.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom