Magazeti ya leo yamemnukuu Spika wa Bunge, Job Ndugai, akitaja mashtaka yanayomkabili CAG Assad. Ni kama ametaja hati ya mashtaka yenye tuhuma mbili, kama ifuatavyo:
Tuhuma ya kwanza: Huku ukijua kwamba, Bunge ni taasisi inayojumuisha Wabunge, Mawaziri na Rais, ambapo Rais ndiye mwajiri na mteuzi wa CAG Assad (1); na ukiwa unaelewa kwamba, Hati ya Majukumu ya CAG haisemi kuwa kutathmini utendaji wa taasisi ya Bunge ni kazi yake mojawapo, ulichukua hatua ya kufanya tathmini ya utendaji wa Bunge na kugundua kwamba Bunge ni dhaifu; na hivyo, kumdharau mteuzi wako kwa kufanya kazi iliyo nje ya majukumu yako rasmi. Mwenendo huu ni kinyume cha kifungu cha X kinachoongoza ajira yako kama CAG.
Tuhuma ya pili: Ukijua kwamba, wewe sio msemaji wa ofisi inayohusika na kutathmini utendaji wa Bunge; alibeba jukumu la kuitangazia dunia kwamba, Bunge la Tanzania ni dhaifu kwa mujibu wa Utafiti wako; na hivyo kulidhalilisha Bunge mbele ya Jumuiya ya KImataifa. Mwenendo huu ni kinyume cha kifungu cha Y kinachoongoza ajira yako kama CAG.
Wito: Hivyo, ndani ya masaa 48 baada ya kupata barua hii, unatakiwa kujitokeza mbele ya Mteuzi wako na kujieleza kwa mdomo na kwa maandishi kwa nini usichukuliwe hatua za kinidhamu.
Wako katika ujenzi wa Taifa,
Ayubu Ndugai.