1. Hakuna kwetu kwingine, kwanza nawasalimia,
Hakuna kwetu kwingine, ujumbe nawaambia,
Hakuna kwetu kwingine, wa Kijiji naingia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania.
2. Hakuna kwetu kwingine, hata tukiwa Asia
Hakuna kwetu kwingine, tukiwa na Arabia,
Hakuna kwetu kwingine, Na nchi za Yuropia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania.
3. Hakuna kwetu kwingine, na siye wa Amerikia,
Hakuna kwetu kwingine, na popote Afrikia,
Hakuna kwetu kwingine, katika hii dunia,
Hakuna kwetu kwingine ila kwetu Tanzania.
4. Hakuna kwetu kwingine, kwetu kwa kupigania
Hakuna kwetu kwingine, kwetu kwa kungangania,
Hakuna kwetu kwingine, kwetu tusikochukia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania
5. Hakuna kwetu kwingine, tunakokushabikia,
Hakuna kwetu kwingine, tunakokuulizia,
Hakuna kwetu kwingine, tunakokufuatilia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania.
6. Hakuna kwetu kwingine, kwingine kwetu na pia,
Hakuna kwetu kwingine, kwetu tusikogaia,
Hakuna kwetu kwingine, Ni Bongo nawaambia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania.
7. Hakuna kwetu kwingine, sababu ya kubishia,
Hakuna kwetu kwingine, hivyo twawangangania,
Hakuna kwetu kwingine, kamwe hatutaachia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania
8. Hakuna kwetu kwingine, kwetu kwa kushabikia,
Hakuna kwetu kwingine, kwingine kwa kuchangia,
Hakuna kwetu kwingine, chochote tukipatia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania.
9. Hakuna kwetu kwingine, utawalaye sikia!
Hakuna kwetu kwingine, ukweli tutakwambia,
Hakuna kwetu kwingine, na hata ukichukia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania,
10. Hakuna kwetu kwingine, hata mkitutishia,
Hakuna kwetu kwingine, hofu haitoingia,
Hakuna kwetu kwingine, bado tutawashukia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania
11. Hakuna kwetu kwingine, mafisadi mtalia,
Hakuna kwetu kwingine, vikaragosi vyenu pia,
Hakuna kwetu kwingine, hadi mje kukimbia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania
12. Hakuna kwetu kwingine, beti zangu zatimia,
Hakuna kwetu kwingine, ni dazeni siyo mia,
Hakuna kwetu kwingine, nafunga na kutulia,
Hakuna kwetu kwingine, ila kwetu Tanzania
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji a.k.a Tarumbeta ya Kijiji)