Makengeza: Napeta nikitwanga

Msanii

Platinum Member
Jul 4, 2007
23,256
31,197
Posted Date::2/23/2008
WAHESHIMIWA wasomaji wangu,

Kwanza sina budi kusema kwamba mimi kweli naunga mkono mia kwa mia juhudi za serikali yetu tukufu kutulinda sisi Watanzania dhidi ya wazushi na wazishi ambao wanapenda kutumia mtandao kuanika ukweli mchafu unaozidi hata kashfa na hata kashfa zenyewe dhidi ya watukufu wetu nchini.


Naunga mkono na kusifu watawala wetu hata kama jitihada za watawala wetu hazitazaa matunda maana tovuti si kama gazeti la udaku, bali ni ni kama yale majini katika hadithi za mapokeo. Ukikata kichwa kimoja, vinaibuka vichwa vitano vikali zaidi. Kwa hiyo, bila shaka tayari zimeshaanzishwa tovuti zingine za kuwavutia wambea na washambenga wa nchi hii.


Na hata wambea wasiokuwa na dira sasa watadiriki kutafuta na wao pia wajue walikosa uhondo gani lakini bado nafurahi sana maana kazi ya serikali ni nini kama si kuhakikisha kwamba wananchi tunaweza kulala vizuri zaidi tukijua kwamba uhuru wa tovuti hatimaye umefinywa ili sisi tusifinywe na mawazo mabaya juu ya huyu au yule.


Ndipo hapo pia natambua kabisa kwamba methali ya ?mjumbe hauawi? ni methali ya uongo iliyopitwa na wakati. Kama mimi nina hasira na habari zote zinazotolewa dhidi yangu, na siwezi kuwafikia wale watoaji wa hizi habari, nitamaliza hasira zangu kwa nani kama si kwa mjumbe mwenyewe? Potelea mbali kama alikuja kwangu kwa nia njema au mbaya, linalobaki ni twanga pepeta tu, au twanga niendelee kupeta. Si ajabu ni ushambenga wake yule mjumbe kunikimbilia na kunipa story zake zile. Eti alitaka kuona kama nitanuna au kunona. Mwache nimtwange.


Ila tu ninaporejea zile hadithi za mapokeo, nakumbuka kwamba daima nilikuwa namsumbua bibi.


?Sasa bibi, haya majini yalitoka wapi? Na kwa nini yaliibuka kwa wakati ule??


?We mjukuu wangu, jini ni jini tu. Halina sababu linaibuka tu.?


Nilitaka kumbishia bibi lakini hata yeye alikuwa mtaalam wa twanga pepeta na sikutaka matako yawashe usiku kucha hivyo nilijinyamazia. Lakini bado nikajiuliza kwa nini shujaa yule hakutumia akili ya kujua chimbuko la jini na kulishughulikia badala ya kumaliza nguvu zake zote kupambana na vichwa visivyohesabika.
Na hata sasa, kwa nini majini ya kashfa yanatuandama na kila ukijaribu kukata kichwa kimoja kwa ushujaa, vitano zaidi vinaibuka? Kwa nini watu ambao kwa vyovyote wanajua mengi wanakimbilia tovuti na majina yasiyotambulika kutoa wanachotoa.
Chimbuko ni nini? Ni wivu wa madaraka? Au ni uovu wa wenye madaraka? Labda kuna kundi la watu ambalo limechoka kabisa ufisi uliokithiri. Haya maswali nawaachia watukufu na watukufuru wetu ambao wamevaa ngozi ya shujaa kutulinda sisi tusiojua na tusiotakiwa kujua kitu chochote.


Na nasema ni mashujaa kwelikweli. Maana ukishaanza kupambana na majini ya tovuti yabidi ufanye tovuti nikuvute hadi vichwa vyote vimekatwa. Watawala mashujaa duniani kote wanatoa jasho kwelikweli.


Sasa katika tovuti ambayo jina lake nisingependa kulitaja nisije nikafuatwa na mashujaa wenye mapanga yao, nikafuma blogu ya Bwana Kichaka mwenyewe ambaye alikuwa anawaandikia wandani wake.


Hiyaaa washikaji wangu,


Mliona nilivyocheza huko Afrika? Mliona? Yaani nawaambia kwamba safari ilikuwa raha sana. Ndiyo, ilibidi nikae mara mojamoja katika hospitali ambazo hazikuwa na kiyoyozi na kusikika harufu ya wagonjwa maskini lakini hali ya hewa haikuwa tofauti sana na Texas hivyo nilivumilia.


Nawaambieni Waafrika watu wazuri sana. Si kama wale wa nchi nyingine ambao wanaandamana na kuniandama kwa kuwaua watu wasiohesabika huko Iraq kwa kudanganya dunia nzima kuhusu silaha za maangamizi. Waafrika hawakuniuliza kwa nini napenda kuwapendelea matajiri wenzangu na kung?ang?ania mfumo wa dunia unaowapa pesa zaidi na zaidi wakati walio wengi wanazidi kufukarika.


Ingawa hata wao ni maskini hii ni dunia ya mwenye mali na kama hawana na wao basi waote ndoto tu. Hawakuniuliza, hawakunipinga, wakanichekelea tu. Na hawa wahuni wa vyombo vya habari vya nje walipojaribu kuniuliza maswali magumumagumu nilikingiwa kifua na mwenyeji wangu. Mungu akupe nini?


Hasa Tanzania nakuambia. Yaani... Nimepokelewa kwa shangwe. Hakuna aliyeniuliza ni milioni ngapi zinatumika kunifikisha nchi kama Tanzania na kuwa na gari langu na walinzi wangu na chakula changu, bila kumsahau mke wangu n.k. Walifurahi kuniona tu. Na eti walinipa heshima kubwa kwa kutaja majina yangu yote matatu.


Kidogo hata nisijitambue mwenyewe lakini niliambiwa kwamba kama wewe ni hohehahe, wastahili majina mawili tu lakini ukishapandishwa cheo basi lazima yatajwe majina yote kiasi kwamba rais hapa ana wasiwasi maana Waziri Mkuu wake mpya ana majina manne kwa hiyo anaweza kuonekana wa maana kuliko yeye mwenye majina matatu.


Anyway, tuache hayo. Kilichonifurahisha huko Tanzania ni kwamba hakuna wachambuzi kabisa. Nikitoa hela, samahani nikitoa ahadi ya hela, hakuna anayeniuliza kama ni ahadi ya kweli. Huko Washington, wenye vichwa vigumu wanahoji kama kweli nimeongeza hela kwa ajili ya ukimwi lakini hapa wananyoosha mikono tu kupokea chochote, iwe kweli, iwe feki.


Yaani nawaambia mimi nilikuwa najisikia kama wale wafalme wa zamani ambao wanabebwa na watu wavuja jasho huku natupa vihela vidogovidogo kwa wananchi ili wanisifu.


Hivi vihela vinawapofusha kiasi kwamba hawaoni kwamba nabebwa na wavujajasho wenzao, wala kwamba ulaji wangu umetokana na umaskini wao. La hasha! Wananishangilia na nikiamua kujitingishatingisha kama wao katika ngoma zao, wacha nipigiwe vigelegele. Wenye gele wa nchi nyingine kweli wanaweza kufanya hivyo? Afrika Bwana poa sana. Inapooza machungu yote niliyoyapata sehemu nyingine.


Of course, wale wapambe wangu walifanya kazi nzuri. Kila nilipopita mabango makubwamakubwa ya kupongeza na kuombea urafiki kati ya nchi yao na nchi yangu. Kidogo niwaulize kama wanajua mwisho wa urafiki kati ya simba na kondoo ni nini, lakini sikutaka kuwashtua. Aheri mashangilio ya ujinga kuliko shutuma za werevu!

Na unajua kidogo nisije hapa Tanzania? Maana wao bado wana doa ya yule rais wao wa kwanza ambaye alithubutu hata kumwumbua mtakatifu wetu wa uhafidhina, yaani RR. Na nilijua (au niliambiwa maana nitajua mangapi miye?) kwamba wale majirani wa Tanzania wamejua zaidi kujifunza kutoka kwetu.


Tabaka tawala tajiri kupita kiasi ambalo linazidi kujikita ili litajirike zaidi, utawala wa koo chache na mtoto kumrithi baba yake kisiasa, na of course, juzijuzi wizi wa kura wa waziwazi. Hawa kweli wanafunzi wazuri lakini waliniudhi maana hata ukiiba waziwazi, lazima utumie mazingaombwe ya kuwavuruga watu akili. Hamuoni kwetu watu walinyamaza? Lakini kwao ilikuwa vita ambayo inadidimiza vitegauchumi vya hao hao. Lazima uibe kwa akili bwana!


Lakini niliambiwa kwamba Tanzania nayo inajitahidi sana kuwafikia wenzao, hata kama wanafanya majaribio zaidi kwenye kisiwa kidogo tu.


Ni wajanja pia na huu utajiri wanaukoo tukufu zenye koo zao pana wanasaka kwa udi na uvumba lakini wamejifunza pia kwamba kama umeumbuka, bora ujiondokee kabla hujadondoshwa. Nasikia kulikuwa na mafisi waliokuwa wanangoja kwelikweli kuwahi mamilioni yangu lakini wakaumbuka dakika za mwisho.


Ndio mchezo wa siasa na walifuata sheria zake sawasawa. Au hivi ndivyo ninavyosema hadharani lakini sote twajua ni kwamba ukipatikana, unakana na kutukana hadi watu wafyate mkia. Nimepata kashfa ngapi wakati wa utawala wangu lakini nani anazikumbuka?


Kwa hiyo, nimemwaga pesa kama radi. Walivyokuwa wanazipigania, hakuna aliyehoji uhalali wa hizi pesa. Kwa mfano katika Ukimwi, hakuna aliyeuliza kwa nini napigania tuwe na mipango ya ubikira tu wakati hata mganga mkuu wa nchi yangu amesema waziwazi kwamba si mpango sahihi na kwamba inawahatarisha vijana zaidi na zaidi.


Lakini hayo ya baadaye. Ngoja nipumzike na kuangalia tena video vya mapokezi yangu. Raha tupu!

Source: Mwananchi Jumapili.

Aibu aibu tupu. Ni vyema viongozi wetu wakakubali kuwa JF ni kioo cha kujipima maana all dataz za mienendo yao tunazo na tutaendelea kuupasha umma yale ya maslahi yao kujua na si vinginevyo.
Mwandishi wa makala hiyo hapo juu ni R. Mabala anapatikana kwa upepe wa rmabala@gmail.com
 
Back
Top Bottom