Hai: Aliyekuwa Diwani wa CHADEMA aachiwa huru kwa tuhuma za kumbaka Mwanafunzi baada ya DNA kuonesha Mtoto aliyezaliwa sio wake

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,501
9,280
Mahakama ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, imemwachia huru diwani wa zamani wa Masama Mashariki (CHADEMA), John Munisi, ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya kubaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Marire.

Akisoma hukumu hiyo Leo, Hakimu Mkazi wa Wilaya hiyo, Jasmin Abdul amesema mahakama hiyo haijamtia hatiani mshtakiwa huyo katika makosa mawili yanayomkabili, kwa kuwa vipimo vya sampuli za vinasaba (DNA), kuonyesha mtoto aliyezaliwa, hakuwa mtoto wa mshtakiwa.

Aidha, hakimu huyo amesema kwa kuwa mtoto aliyezaliwa si wa mshtakiwa, mahakama hiyo haioni sababu ya kuamini kwamba mshtakiwa alimbaka mwanafunzi huyo, hivyo inamwachia huru.

Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lebulu Mbise, kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti.

Anadaiwa alitenda kosa la kwanza katika Kijiji cha Ngira, Wilaya ya Hai, kwa kumbaka mwanafunzi huyo Aprili 4, mwaka 2019, kosa alilotenda akijua ni kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo, kinyume na kifungu 130 (1) (2) na kifungu 131 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16 ya Sheria iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2000.

Aidha, ilidaiwa pia mahakamani hapo kwamba, mshtakiwa alitenda kosa la pili katika kijiji hicho hicho, kwa kumpa ujauzito mwanafunzi huyo Aprili, kinyume na Sheria ya Elimu, kifungu cha 60 (A) (2) na (3) iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2002.

Katika ushahidi wa shahidi muhimu wa kesi hiyo ambaye ni mwanafunzi, alidai mahakamani hapo wakati akitoa ushahidi wake kwamba, hakuwahi kufanya ngono na mtu mwingine yoyote maishani mwake, tofauti na mshtakiwa huyo.

Wakati mshtakiwa Munisi, akitoa utetezi wake akiongozwa na Wakili Elia Kiwia, alidai hakuwahi kuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi na mwanafunzi huyo, wala hakuwahi kufanya ngono naye.

Mshtakiwa huyo alijitetea kwamba alibambikiziwa kesi hiyo, baada ya kiongozi mmoja, kumlazimisha ajiunge na Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipokataa, ndipo akambambikizia kesi hiyo namba 127 ya mwaka 2019.

Chanzo: IPP MEDIA
 
Si mchezo! Napongeza pande zote za kesi hii: Upande wa Mashtaka na Upande wa Utetezi. Kesi ya ubakaji ni kati ya kesi rahisi kuanzishwa lakini ngumu kuthibitishwa au kujitetea. Ni jambo jema kwenda mbele zaidi kwenye vipimo na kuoanisha na yamhusuyo mshtakiwa husika.
 
Wakati mshtakiwa Munisi, akitoa utetezi wake akiongozwa na Wakili Elia Kiwia, alidai hakuwahi kuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi na mwanafunzi huyo, wala hakuwahi kufanya ngono naye.

Mshtakiwa huyo alijitetea kwamba alibambikiziwa kesi hiyo, baada ya kiongozi mmoja, kumlazimisha ajiunge na Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipokataa, ndipo akambambikizia kesi hiyo namba 127 ya mwaka 2019.
 
Back
Top Bottom