HADITHI YA KUSISIMUWA VITA YA WACHAWI-39
ILIPOISHIA:
"Dawa niliyompa mwenyeji wako kuondoa maumivu ya macho ulikuwa uwezo wangu wa mwisho lakini kupofuka ni kazi ya Mungu, sina uwezo huo, hakuna wa kuyaponya macho yako."
"Basi naomba msaada wa kunirudisha nyumbani."
"Atakurudisha aliyekuleta."
"Mmh! Sawa."
SASA ENDELEA...
"Sasa ndugu nina imani mmesikia jinsi wanadamu tulivyo wabaya, nataka kuwaambia hapa katika kundi la watu kuna wachawi wengi wakubwa na watoto. Hapa kuna dawa nitaweka kwenye maji kila mmoja atakuja kunawa uso mchawi atajulikana."
Mganga alifanya mambo yake kwa kuweka maji kwenye beseni kisha alisema kuwa kama kuna mtu anayejihusisha na mambo ya kichawi basi atoke mbele na kujipaka maji yale.
"Jamani nataka watu waje wanawe maji haya."
Katika umati uliokuwa pale uwanjani, walitoka wachache ambao walifika na kunawa maji, lakini wengi walibakia wamesimama walipokuwa wamesimama na kumfanya mganga aseme kwa sauti:
"Kwa hiyo hawa ndiyo wasafi na ninyi wote mliobaki ni wachawi?"
Watu wote walikaa kimya, alimwita mtoto mmoja wa miaka saba aliyekuwa amesimama kifua wazi. Yule mtoto alisogea mbele kwa mganga ambaye alimwambia anawe yale maji lakini alikataa na kufanya watu washangae. Mganga alimuuliza:
"Kwa nini hutaki kunawa?"
"Nitaungua."
"Mbona hakuna moto."
"Beseni lote linawaka moto na maji nayaona yanachemka nitaungua."
Aliitwa mtoto mwingine na kuombwa anawe, alinawa bila tatizo lakini alipoambiwa tena yule mtoto aligoma na kusema ataungua. Watu waliokuwa wakiona kama utani, mganga alimwita mzee mmoja ambaye aligoma na kuamua kuondoka.
"Ndugu zangu nataka niwaambie kitu kimoja kijijini kwetu uchawi umetawala, ni kweli anachosema mtoto kuwa ameona moto kwa vile ni mchawi.
Huyu mtoto anatumiwa na bibi yake usiku katika kuwanga na ndiye dereva wa ungo. Naweza kumwona mtoto mdogo lakini usiku anafanya kazi kubwa ya kuwabeba magwiji wa kijiji hiki akiwemo bibi yake.
"Kama mnabisha ngoja nimuulize, eti jana usiku mlikwenda wapi?"
"Nigeria."
"Kufanya nini?"
"Bibi aliniambia kulikuwa na mkutano."
"Nini kiliwapata?"
"Tulipofika sehemu wanasema Kameruni, ungo ulianza kuyumba nilijitahidi kuuweka sawa lakini mmoja wetu alianguka."
"Bibi yako alifanya nini?"
"Alipata presha."
"Yupo wapi?"
"Yupo ndani anaumwa."
"Mmesikia?" Aliwauliza watu waliokuwa wameshika mdomo wasiamini kilichokuwa kikisimuliwa na yule mtoto.
"Ndiyo," waliitikia wote.
"Mmeona, sasa hebu jiangalieni wote," aliwaeleza watu waliokuwepo pale.
Watu wote walitazamana bila kujua mganga alikusudia nini. Baada ya muda aliwauliza.
"Jamani kuna mtu hakuvaa nguo hapa?"
"Hapana wote tumevaa," walijibu kwa pamoja.
"Basi nataka kuwaeleza hapa kuna watu zaidi ya kumi hawana nguo na wamekuja kujaribu ninachokifanya. Nataka kuwaeleza kuwa wanajisumbua zaidi ni kuumbuka, ndugu zangu hakuna faida ya uchawi zaidi ya kuishi maisha magumu huku ukiingilia kazi ya Mungu kuua na kutesa.
"Watu wamefilisika kutokana na mchezo wa chuma ulete bila kujua wanawafanyia watu kazi. Nina imani baada ya tukio la leo nitahamishwa kijijini kwa vile wenye nguvu wameshasema, lakini nataka kuwaeleza nitakachokifanya leo wachawi wote wataanza upya kutumia nguvu za kichawi kwa vile nitaua nguvu zao zote.
Kwa muda mfupi kila mtu ataona mabadiliko ya mwili wake kama hutolewa usiku na kugeuzwa farasi wa kubeba wachawi bila kujua. "Wagonjwa wenye maradhi yasiyoonekana yatapata ufumbuzi, wenye uzito kwenye kazi na biashara baada ya zoezi langu watashangaa mabadiliko yatakayotokea.
"Kila mwenye tatizo la kichawi ataona mabadiliko ila mwenye tatizo la kudra ya Mungu aendelee kumuomba atapona. Nilisema kuna watu wapo uchi hawana nguo inawezekana mnaona natania, kwa hiyo mnataka kumuona?"
"Ndiyooo!" Waliitikia wote.
"Sasa nitamtoa mmoja mbele ambaye amekuja kunipima," baada ya kusema vile alitembeza macho kwenye kundi la watu na kusema:
"Namuomba mwanamke mmoja mwenye kanga ili mtu akiumbuka awahi kumfunika ili kumsitiri."
Mwanamke mmoja alitoka mbele na kanga mkononi, baada ya kupita alimwita bibi mmoja aliyekuwa amesimama pembeni mkono amekunja ngumi. Lakini yule bibi alikataa, mganga aliwatuma vijana kumleta mbele. Walimbeba juujuu na kumpeleka mbele.
Baada ya kufikishwa yule bibi aliweka mkono mdomoni kama mwanamwali na kuangalia chini kama mtu mwenye aibu. Baada ya kufikishwa mganga alimuomba mwanamke mwingine afike mbele, alitoka mwanamke mwingine mbele.
"Sasa ninataka kuwaonesha kitu mnamjua huyu bibi?
"Hatumjui."
"Huyu ni mgeni ila ameletwa kwa ajili ya kukabiliana na mimi ndiyo maana nikasema wapo zaidi ya kumi wote mtawajua."
Baada ya kusema vile aliweka maji mdomoni na kumpulizia mwanamke aliyeitwa mara ya mwisho. Kisha aliwageukia watu na kuwauliza:
"Mmeona nini?"
"Hatujaona kitu."
"Huyu mama amevaa hajavaa?"
"Amevaa."
"Mama simama hapo, bibi simama hapa."
Yule bibi alisimama alipokuwa amesimama mwenzake kisha mganga alijaza maji kinywani na kumpulizia. Ghafla kukawa na sinema ya bure na kuwafanya watu wote wapige kelele baada ya yule bibi kubakia mtupu. Alimuomba mama aliyekuja na nguo amfunge kisha aliwageukia watu na kuwauliza.
"Mmeona?"
"Ndiyo."
"Basi huyu ni mmoja wa wachawi waliopo hapa japokuwa wapo wengine wamevaa, tunakaa nao lakini ni viumbe wabaya ndugu zetu wanapotea kumbe wamegeuzwa misukule. Ndugu zetu wengine wanakufa katika mazingira tata kumbe wazazi wetu wanawatoa sadaka ya nyama kwa vile wanakula nyama za watu. Hii imefanya nyumba nyingi ziwe tupu kwa ajili ya tamaa ya wazazi.
Itaendelea Alkhmisi ijayo...........