HADITHI YA KUSISIMUWA NCHI YA WACHAWI-22
Alilitaja jina la yule mzee niliyemfanyizia na binti yake mkubwa, akasema kuwa, hata alipokuwa anakubaliana aje kwangu alimuuliza uwezo wangu wa nguvu ya kichawi:
"Akasema nisikuogope, kwani huna lolote, na ni mgeni sana katika masuala ya kichawi. Lakini nilipokuona mambo yako nimekubali wewe ni mkongwe na tena uwezo wako ni mkubwa sana, nisamehe sana ndugu yangu."
Huruma iliniingia kwani kama kweli alidanganywa ina maana yule alitaka kumuua mwenzake, kwani ni kweli ni mtu nisiyewahi kumwona katika maisha yangu.
Nilimpa pole sana na kumwomba siku nyingine asikubali kuingia kwenye mambo ambayo hana uhakika nayo, yanaweza kumtokea mambo kama yale.
"Mimi nilishaamua kukuua moja kwa moja, kwani sikuwa na sababu ya kukushindwa, una nini wewe mpaka ushindane na mimi. Kwanini huyo mtu asikwambie sababu ya kukutuma wewe? Kwanini asije mwenyewe?" Nilimuuliza.
"Alisema mnafahamiana."
"Hata kama tunafahamiana, lakini si angekuja kwa sura nyingine, si inawezekana?"
"Ndiyo."
"Sasa? Alikwambia kama alishakuja nikamfanyia mambo makubwa?"
"Hapana, ila alisema aliwahi kuja usiku akakuchezea kama mpira."
"We uliamini?"
"Wakati anasema niliamini, lakini hali niliyoikuta hapa siamini hata kidogo."
Nilimshika kichwani, nikasema maneno fulani ya kichawi, mwanga mkubwa ukammulika pale alipo, hali ikawa shwari, akasimama huku akijipukuta vumbi ingawa hakukuwa na vumbi.
"Naweza kwenda?"
"Unaweza, ila kuwa makini na maisha yako, hayana kitu cha kubadilishana nayo," nilimwambia huku akifungua mlango na kutoka zake.
Huku nyuma nilibaki nimeduwaa, nilijiuliza maswali mengi, ni kwanini yule mzee aliamua kumtuma mtu dhaifu kuliko yeye ambaye kidogo ni mkongwe na anajua kupambana lakini bado nilimshinda.
Ile anaondoka tu na mimi nikiendelea kufikiria, mara upepo mkali ukavuma.
SASA ENDELEA…
Niliinua uso wangu kuangalia juu ulikotokea upepo, nikahisi ni jaribio tena, lakini nililipuuza kwa kusimama, nikaingia chumbani na kubadili nguo. Nilivaa shuka ya kaniki nikasimama katikati ya chumba, nikanyoosha mikono nikapotea.
Nilikwenda kutua kwenye genge la kukutania ambapo kwa mara ya kwanza toka niende na kurudi kwenye Nchi ya Wachawi.
Ngoma za kichawi zilikuwa zikiendelea, kutua kwangu kukazisitisha na kuibua kelele za kunilaki.
Mpaka hapo nataka kusema, nilikuwa mkubwa katika ngazi ya wachawi kuliko mwingine yeyote katika ukanda wa nchi. Na si kwamba nilitakiwa kudumu kwenye kundi langu, la hasha!
Moja ya majukumu yangu ilikuwa ni kuendelea kutembelea makundi yote ya kichawi na kuyapa nguvu na njia ya kuzidisha mapambano dhidi ya utaratibu sahihi wa Mungu.
Walipotulia, nilisimama katikati ya kundi kusalimia na kuwaambia mawili matatu:
"Hii ni nchi ya Tanzania, lakini kumbe kuna nchi mbalimbali duniani. Mungu aliposema ameumba vitu vinavyoonekana na visivyoonekana ni kweli.
"Pia, kumbe utaratibu unaotumiwa na shughuli za duniani na huko kwa wenzetu pia upo. Kila kitu kinakwenda sawasawa na huko. Kuna masekretari, kuna makarani, walinzi na mambo mbalaimbali."
Nikawaambia kuwa, mpambano uliopo sasa katika ya utawala bora wa Mungu duniani na ule wa chini ni kuhakikisha upotofu wa hali ya juu unafanyika katika maeneo mbalimbali ya haki.
Mfano, kuhamasisha viongozi wa dini kukubali matumizi ya kondom, kwa Mungu hata kama binadamu wote watakufa kwa Ukimwi kwa sababu hawakutumia kondom, ni sawa tu, yeye hana hasara.
Lakini pia uzazi, hakuna kitu kinachoshikiwa bango kwa Kiongozi Mkuu wa Nchi ya Wachawi kama kuvuruga uzazi, yaani wanawake wajawazito wasiwe wanazaa kwa usalama.
Haya niliyoyasema ukiyafuatilia kwa umakini utagundua ni kweli, kwani jamii sasa imekuwa ikikumbana na kauli ya baadhi ya viongozi wa dini au wanaharakati wanaotaka matumizi ya kondom ili kunusuru janga la Ukimwi au wengine wakisema mtu awe na mpenzi mmoja mwaminifu, hata kama hawako katika ndoa.
Lakini huko kwenye Nchi ya Wachawi wanajua na kuamini kuwa, uaminifu unaanzia kwenye ndoa tu na si nyuma ya hapo, yaani watu kama hawajaoana kwa ndoa uaminifu kwao wa nini, maana wanazini.
Hata wale wapenzi, anapotokea mmoja anamwomba mwenzake asimsaliti maana yake ni nini? Ni kwamba anaomba azini na yeye tu, asizini na mtu mwingine.
Wakati nawapa kwa ufupi kuhusu mambo ya duniani yanayojulikana kwenye nchi ile, walikuwa wametulia wakinisikiliza kwa umakini wa hali ya juu na mwisho wa yote, wachawi watatu walinyoosha vidole.
Nilimsimamisha mmoja ambaye aliuliza:
"Kwa maelezo yako, huko Nchi ya Wachawi wanajua usahihi wa jambo unaotakiwa kuwepo ni upi ila wao kazi yao kubwa ni kupotosha, si ndiyo?"
"Hawapotoshi, bali wanapambana na utaratibu sahihi wa Mungu."
Nikamsimamisha mwingine ambaye aliuliza:
"Kumbe kama ni hivyo hakuna haja ya kuwa wachawi maana tunakubaliana kuwa, tunaunga mkono wale wanaompiga Mungu ambapo siku ya mwisho, tutakwenda motoni."
Wakati huyu mchawi akiongea hivyo, upepo mkali ulitokea ukampaisha angani.
Je, nini kilitokea hapo? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kusisimua Jumapili..........